JUMA LA SABINI (70) LA DANIELI

JUMA LA SABINI (70) LA DANIELI

Kabla hatujaliangalia juma la 70 hebu tufahamu kwa ufupi haya majuma 70 ni yapi?

Tukisoma Danieli

9:24-27 “24 Muda wa majuma sabini umeamriwa juu ya watu wako, na juu ya mji wako mtakatifu, ili kukomesha makosa, na kuishiliza dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, na kuleta haki ya milele, na kutia muhuri maono na unabii, na kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu.

25 Basi ujue na kufahamu, ya kuwa tangu kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hata zamani zake masihi aliye mkuu; kutakuwa na majuma saba; na katika majuma sitini na mawili utajengwa tena pamoja na njia kuu zake na handaki, naam, katika nyakati za taabu. 

26 Na baada ya yale majuma sitini na mawili, masihi atakatiliwa mbali, naye atakuwa hana kitu; na watu wa mkuu atakayekuja watauangamiza mji, na patakatifu; na mwisho wake utakuwa pamoja na gharika, na hata mwisho ule vita vitakuwapo; ukiwa umekwisha kukusudiwa.

27 Naye atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja; na kwa nusu ya juma hiyo ataikomesha sadaka na dhabihu; na mahali pake litasimama chukizo la uharibifu; na hivyo, hata ukomo, na ghadhabu iliyokusudiwa imemwagwa juu yake mwenye kuharibu”

Katika lugha ya biblia juma moja linawakilisha miaka 7.Hivyo majuma 70 ni sawasawa na 7*70=490

kwahiyo miaka 490 imeamuriwa kwa watu wake,sasa hawa watu wake wanaozungumziwa hapa ni wayahudi na sio watu wa mataifa. Majuma haya sabini yalianza kuhesabiwa baada tu ya danieli kupokea hayo maono.

MAJUMA 7 YA KWANZA:

Majuma 7 ya kwanza ambayo ni miaka 49 Danieli aliambiwa Yerusalemu utajengwa tena upya na njia zake kuu katika kipindi cha taabu na shida. katika hichi kipindi Hekalu la pili lilijengwa upya na kumalizika ndani ya hii miaka 49 ya kwanza baada ya kutoka uamishoni babeli.

MAJUMA 62:

Haya yalianza kuhesabiwa pale tu baada ya hekalu kumalizika kujengwa ndani ya yale majuma 7 ya kwanza. katika haya majuma 62 yaani miaka 434 ikishakwisha masihi yaani YESU KRISTO atakatiliwa mbali. Mpaka hapo majuma 69 yatakuwa yameisha. kwahiyo masihi yaani Yesu Kristo atakuwa ameshazaliwa na mwisho wa hilo juma la 69 yaani 62+7=69, atakatiliwa mbali, hili lilitokea pale alipopelekwa kalvari.AD 33

JUMA 1 LA MWISHO:

Majuma 69 yalipoisha Mungu aliacha kushughulika na wayahudi na neema ikahamia kwa mataifa kwasababu wayahudi walimkataa Masihi wao,kwahiyo kikaanza kipindi cha mataifa ambacho mpaka sasa tunaendelea nacho takribani miaka 2000 sasa. Na Neema itakaporudi Israeli ndipo juma moja la mwisho litakapoanza kuhesabiwa tena yaani miaka 7 ya mwisho, kutimiza majuma sabini.  majuma haya 70 yaliamuriwa kwa watu wa Daniel yaani wayahudi na sio pamoja na watu wa mataifa. Na katikati ya hili juma la mwisho yaani miaka mitatu na nusu ya kwanza injili itapelekwa Israeli, na katika miaka mitatu na nusu ya mwisho mpinga kristo atavunja agano atakaloingia na wayahudi na kukomesha sadaka na dhabihu na ndipo ile dhiki kuu itakapoanza.

MTAZAMO AMBAO SIO SAHIHI 

Kuhusu juma la mwisho la 70, watu wengi waaminio wa ujumbe wa William Branham wananukuu baadhi ya sehemu alizohubiri katika vitabu vya ujumbe, mfano katika kitabu cha “ufunuo wa mihuri saba” katika zamu ya maswali na majibu, alisema  kuwa lile juma la 70 lilishaanza na BWANA YESU alishalitimiza nusu ya juma hilo alipokuwa duniani katika ile miaka mitatu na nusu ya kwanza aliyohubiri ulimwenguni.na miaka mitatu na nusu iliyobaki itatimizwa baada tu ya kanisa kunyakuliwa.

Lakini pia tukinukuu ndugu William Branhama alichofundisha katika kitabu cha “LILE JUMA LA 70 LA DANIELI”  agosti 6 mwaka 1961 alisema kuwa lile juma la sabini litaanza baada tu ya utimilifu wa mataifa(yaani kanisa kwenda kwenye unyakuo) na itabaki miaka 7 ambapo  miaka mitatu na nusu ya kwanza injili itapelekwa Israeli na wale manabii wawili wa ufunuo 11 na mitatu na nusu ya mwisho itakuwa ni wakati wa ile dhiki kuu baada ya mpinga kristo kulivunja lile agano atakaloingia na wayahudi.

Hapa tunaona kuwa ndugu Branham alizungumza vitu viwili tofauti vinavyoonekana kama kupingana..sasa tuchukue lipi tuache lipi?. Je! ni ujumbe unashida?? hapana ni watu wasioulewa ujumbe na kushikilia vipengele vya vitabu tuu pasipo kuomba msaada wa Roho Mtakatifu ndio wanaoufanya ujumbe usieleweke, Hata ndugu William Branham alisema  mwenyewe “biblia ndio muongozo wangu” na pia alisema “hata mimi nikizungumza neno lolote kinyume na biblia usilichukue” Mambo mengi aliyoyazungumza nabii alipewa na BWANA ila sio yote aliyokuwa anazungumza yalikuwa ni “HIVI ASEMA BWANA”.. ni mara ngapi tuliona akikiri kuwa mambo mengine hafahamu, anayefahamu kila kitu na asiyekosea ni BWANA YESU KRISTO peke yake. Aleluya.!

.Ni dhahiri kabisa tunajua kuwa NENO LA MUNGU haliwezi kujichanganya Mungu aliyaruhusu haya makusudi ili kutupima sisi kama tumelielewa NENO na kama kweli tunampenda BWANA YESU, na kurejeza kila kitu kwenye NENO lake 

Sasa ili kuondoa huo mkanganyiko inatupasa kurudi kwenye biblia tuangalie inasemaje na sio kuangalia vitabu vinasemaje, vitabu vinapaswa kuturudisha kwenye NENO na sio NENO liturudishe kwenye vitabu. Ni jukumu letu sisi kuhakiki kila neno linalosemwa na mtu yeyote kwa NENO na nabii mwenyewe ndivyo alivyotufundisha wote. Nabii hakumvumilia wala kumuonea haya mtu yeyote anayetoa mapokeo yake nje ya neno.

Biblia inasema danieli 9:26 ” Na baada ya yale majuma sitini na mawili, masihi atakatiliwa mbali, naye atakuwa hana kitu; na watu wa mkuu atakayekuja watauangamiza mji” Hapa tunaona dhahiri Masihi atakatiliwa mbali mara baada ya majuma 62  kukamilika, kukamilisha majuma 69 yaani (7+62=69) kuisha, na sio baada ya majuma 62.5 yaani(7+62.5=69.5).unaona biblia inasema baada ya yale majuma 69 kuisha ndipo masihi atakapokatiliwa mbali.

 Na huyo mkuu atakayekuja baada ya Masihi kukatiliwa mbali atakuwa ni mpinga kristo naye atafanya agano na watu wengi katika juma moja yaani miaka 7. na nusu ya juma hilo atalivunja hilo agano na kuikomesha sadaka na dhabihu, kumbuka Masihi na mkuu atakayekuja ni watu wawili tofauti.chukizo la uharibifu ni mpinga kristo atakapoingia lile agano na israeli.

Tukisema masihi ni sawa na mkuu wa watu atakayekuja tutakuwa hatujaielewa biblia vizuri kwasababu, maandiko yanasema watu wa huyo mkuu atakayekuja ndio watakoutekeza mji, na tunafahamu katika historia warumi ndio waliouteketeza mji 70AD kutimiza ule unabii Bwana Yesu aliousema mtakapouna mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi mjue uharibifu wake umefika.(luka 21:20).

Hivyo sio watu wa Yesu Kristo(yaani wayahudi) walioteketeza mji bali ni watu(warumi), wa yule “mkuu atakayekuja” yaani mpinga kristo. ambaye kwa kipindi hicho alikuwa bado hajaja lakini baadaye atakuja na kuingia agano na wayahudi katika lile juma moja la mwisho lililobaki.

Kwahiyo kulingana na NENO juma la sabini litaanza baada tu ya injili kumalizika kwa mataifa na ndivyo hata nabii alivyohubiri katika ujumbe aliofundisha agosti 6 mwaka 1961″LILE JUMA LA SABINI LA DANIELI”. Hivyo mtazamo unaosema kuwa Bwana Yesu alishakamilisha nusu ya juma akiwa hapa duniani sio sahihi.

2 petro 1:10 “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe. Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo.” 

Mungu akubariki!

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

MZEITUNI HALISI UTAKAPOPACHIKWA.

MUNGU MWENYE HAKI.

MWISHO WA HAO WAMSAHAUO MUNGU

MANABII WALISEMA “NENO LA MUNGU LIKANIJIA” ..MAANA YA HILI NENO NI NINI?.

NINI MAANA YA HILI ANDIKO “USHUHUDA WA YESU NDIO ROHO YA UNABII” (UFUNUO 19:10)?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Mashibe Elias
Mashibe Elias
4 years ago

Nilikuwa naomba kujua hizo hesabu za majuma 70. Yaani kutoka 455 B.C hadi pale 33.A.D. tafadhali.