ESTA: Mlango wa 8, 9 & 10. (SIKU KUU YA PURIMU)

ESTA: Mlango wa 8, 9 & 10. (SIKU KUU YA PURIMU)

Jina la YESU KRISTO BWANA wetu lisifiwe.

Karibu kwenye mwendelezo wa kitabu cha Esta, leo tukiwa katika sura za mwisho, yapo mambo mengi ya kujifunza yahusuyo safari yetu ya ukristo tunapopitia kitabu hichi, tunaona mara baada ya Hamani adui wa watu wa Mungu kuuawa, Malkia Esta ananyanyuka tena kumwomba mfalme ayaondoe madhara aliyokusudia juu ya wayahudi wote waliandikiwa kuuawa, tunasoma;

Mlango 8

“ 1 Siku ile mfalme Ahasuero alimpa malkia Esta nyumba yake Hamani, yule adui ya Wayahudi. Mordekai naye akahudhuria mbele ya mfalme; kwa maana Esta alikuwa amedhihirisha alivyomhusu.

2 Basi mfalme akaivua pete yake, aliyompokonya Hamani, akampa Mordekai. Naye Esta akamweka Mordekai kuwa juu ya mlango wake Hamani.

3 Tena Esta akasema na mfalme mara ya pili, akaanguka miguuni pake, akamsihi kwa machozi ayaondoe madhara ya Hamani, Mwagagi, na shauri alilowafanyia Wayahudi.

4 Ndipo mfalme alipomnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu. Basi Esta akaondoka, akasimama mbele ya mfalme.

5 Akasema, Mfalme akiona vema, nami nikiwa nimepata kibali machoni pake, na neno likionekana jema mbele ya mfalme, nami nikimpendeza machoni pake, iandikwe kuzitangua barua za Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, alizotunga na kuziandika ili kuwaangamiza Wayahudi walioko katika majimbo yote ya mfalme.

6 Kwa maana niwezeje kuyaona mabaya yatakayowajia watu wangu? Au niwezeje kuyatazama maangamizo ya jamaa zangu?

7 Mfalme Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, Myahudi, kusema, Tazama, nimekwisha kumpa Esta nyumba yake Hamani, naye mwenyewe wamekwisha kumtundika juu ya mti, kwa sababu aliwatia mikono Wayahudi.

8 Basi waandikieni Wayahudi pia vyo vyote mpendavyo, kwa jina la mfalme, mkatie muhuri kwa pete ya mfalme; kwa kuwa andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme hakuna awezaye kulitangua.

9 Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa pale pale, siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani; na kama vile Mordekai alivyoamuru, Wayahudi wakaandikiwa, pamoja na maakida na maliwali, na wakuu wa majimbo toka Bara Hindi mpaka Kushi, majimbo mia na ishirini na saba, kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; na Wayahudi kwa mwandiko wao na kwa lugha yao”.

Kama tunavyosoma ule msiba mkuu na uchungu ambao ulikuwa juu ya wayahudi wote duniani Bwana aliugeuza na kuwa furaha na shangwe kwao, ile nyumba ya Hamani pamoja na cheo chake walipewa Mordekai na watu wake, wale walioonekana hawana heshima katikati ya mataifa Bwana aliwapa heshima kuliko jamii za watu wote duniani. wale walioonekana wadogo wakawa wakuu katikati ya mataifa. Biblia inasema kukawa nuru na furaha kwao;

Hata ile siku waliyopanga kuwaangamiza wayahudi wote tarehe 13 mwezi wa 12, ndio ikawa tarehe hiyo hiyo ya wayahudi wote duniani kuwaangamiza maadui zao waliowazunguka na kuwatawala. Hivyo tarehe 14. na 15 ya mwezi huo huo wa 12 wakaifanya kuwa sikukuu yao ya ushindi Bwana aliowapa dhidi ya maadui zao, wakaifanya kuwa sikukuu ya kupelekeana zawadi, pamoja na karamu na furaha waliyoiita sikukuu ya PURIMU.

Esta 8: 15 “Naye Mordekai akatoka usoni pa mfalme, amevaa mavazi ya kifalme, ya rangi ya samawi na nyeupe, mwenye taji kubwa ya dhahabu, na joho ya kitani safi na rangi ya zambarau. Mji wa Shushani wakapaza sauti, wakashangilia.

16 IKAWA NURU na FURAHA na SHANGWE na HESHIMA kwa Wayahudi.

17 Na katika kila jimbo, na kila mji, po pote palipowasili amri ya mfalme na mbiu yake, Wayahudi wakapata FURAHA, na SHANGWE, KARAMU na SIKUKUU. HATA WENGI WA WATU WA NCHI WAKAJIFANYA WAYAHUDI, KWA KUWA HOFU YA WAYAHUDI IMEWAANGUKIA. “

Hivyo Bwana akawapa wayahudi wote kustarehe na kufurahi siku zote za ufalme wa Ahasuero.

Kumbuka habari yoyote tunayoisoma katika agano la kale ni kivuli cha mambo yatakayokuja kutokea mbeleni. Wakati wote shetani alipojaribu kuwaletea mateso na dhiki watu wa Mungu, Bwana alitolea wokovu na ushindi mkuu kwao, tunasoma habari ya wana wa Israeli jinsi walivyopiganiwa na Bwana dhidi ya maadui zao walipokuwa wanatoka Misri, wakati wa-Misri walipoona njia pekee iliyosalia ni kuwateketezea katika zile kingo za bahari ya shamu, kinyume chake, wao ndio walioteketezwa katika ile habari, ikawa shangwe kwa wayahudi, huo ulikuwa ni mfano wa PURIMU kwao.

Vivyo hivyo na sehemu nyingine zote, tunaona wakati wa wafilisti walipokuja kupigana na Israeli, wakati wa akina Shedraki, Meshaka, na Abadnego walipotupwa katika tanuru la moto, wakati wa Danieli alipotupwa katika tundu la simba, n.k. hata kwa Bwana wetu Yesu, tunaona jambo lile lile shetani alijaribu kumuua akidhani ameshinda, lakini ufufuo ulidhihirisha ushindi wake, wote hawa maangamizi yao yaligeuka kuwa wokovu mkubwa kwao…ikawa kama mfano wa PURIMU kwao.

Vivyo hivyo katika siku za mwisho shetani anashindana na UZAO wa Mungu, yaani wayahudi wa mwilini na wayahudi wa rohoni (wakristo), kama alivyofanya katika siku za kale, kumbuka HAMANI ni mfano wa mpinga-kristo atakayekuja, na Esta ni mfano wa BIBI-ARUSI wa Kristo. Kama vile HAMANI alivyokusudia kuwaangamiza wayahudi wote duniani, isipokuwa Esta kwasababu yeye alikuwa ni malkia..Vivyo hivyo na mpinga-kristo atakapotafuta kuwaua wayahudi wote (wa-mwilini na wa-rohoni) hatoweza kwa BIBI-ARUSI wa Kristo kwasababu wakati huo atakuwa ameshakwenda katika unyakuo yupo kwenye Jumba la kifalme mbinguni mfano wa Esta. Hivyo hayo madhara hayatamkuta yeye.

Mpinga-kristo (ambaye atakuwa ni PAPA wa wakati huo), atakusudia kuundoa uzao wote wa Mungu duniani kwa njia ya hila, kwa kisingizio cha kuleta amani duniani kama Hamani alivyofanya kuwasingizia wayahudi kwamba wamefarakana na watu wote wa dunia nzima, jambo ambalo si kweli. Hivyo katika siku hizo wayahudi wote, na wale wakristo wote waliokuwa vuguvugu waliokosa unyakuo watagharimika kuingia katika ile dhiki kuu Bwana aliyoizungumzia.

Japokuwa mpinga-kristo atafanikiwa kuua watu wengi, lakini haitakuwa kwa wote, kwasababu biblia inasema wapo watakaofichwa mbali naye,(Ufunuo 12) mpaka siku ile MFALME WA WAFALME NA BWANA WA MABWANA, YESU KRISTO Atakapokuja na mawingu pamoja na bibi-arusi wake, kuwaokoa wateule wake walioko duniani, na kila jicho litamwona, atakaposhuka na kukusanya watu wake(wayahudi) toka pembe nne za dunia, hapo ndipo mataifa yote yatakapoomboleza kwa maana atakuja na upanga kinywani mwake, kama vile maadui wa wayahudi walivyoomboleza siku yao ilipofika, mbele ya Mordekai na Esta ndivyo itakavyokuwa siku ile mbele ya Bwana Yesu na watakatifu wake. Mataifa yaliyowatesa watu wa Mungu yataomboleza sana mbele zake.

Ufunuo 19:11 “Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita.

12 Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe.

13 Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.

14 NA MAJESHI YALIYO MBINGUNI WAKAMFUATA, WAMEPANDA FARASI WEUPE, NA KUVIKWA KITANI NZURI, NYEUPE, SAFI.

15 Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi.

16 Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA”.

Umeona hapo, ukirudi kwenye..
 Mathayo 24: 29 inasema….; Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika;
30 ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi.
31 Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu”.

PURIMU KWA WATU WA MUNGU.

Katika sura ya tisa ya kitabu cha Esta, kama vile tulivyoona jinsi wayahudi walivyosheherekea sikukuu ya PURIMU baada ya ushindi dhidi ya maadui zao, mpaka wale wasiokuwa wayahudi walijifanya kuwa kama wayahudi, kadhalika na katika siku hizo mpinga-kristo na mifumo yake yote mibovu pamoja na mataifa yote yaliyosalia wataangamizwa kwa maangamizo makuu katika vita vya Har-Magedoni. Wakati huo wengi watatamani kuwa kama watu wa Mungu lakini haitawezekana tena, kwao itakuwa ni MSIBA mkuu, wakati huo watoto wa Mungu kwao itakuwa ni KARAMU ya PURIMU. Kufarijiwa na kuburudishwa milele, na kufutwa machozi. Pale watakapomwona BWANA wao uso kwa uso akija kuwapigania na kuleta utawala mpya wa AMANI wa miaka 1000 usio wa shida wala uchungu.

Ufunuo 19:17 “Kisha nikaona malaika mmoja amesimama katika jua; akalia kwa sauti kuu, akiwaambia ndege wote warukao katikati ya mbingu, Njoni mkutane KWA KARAMU YA MUNGU ILIYO KUU;

18 mpate kula nyama ya wafalme, na nyama ya majemadari, na nyama ya watu hodari, na nyama ya farasi na ya watu wawapandao, na nyama ya watu wote, waungwana kwa watumwa, wadogo kwa wakubwa.

19 Kisha nikamwona huyo mnyama, na wafalme wa nchi, na majeshi yao, wamekutana kufanya vita na yeye aketiye juu ya farasi yule, tena na majeshi yake.

20 Yule mnyama akakamatwa, na yule nabii wa uongo pamoja naye, yeye aliyezifanya hizo ishara mbele yake, ambazo kwa hizo aliwadanganya watu wale walioipokea ile chapa ya huyo mnyama, nao walioisujudia sanamu yake; hao wawili wakatupwa wangali hai katika lile ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti;

21 NA WALE WALIOSALIA WALIUAWA KWA UPANGA WAKE YEYE ALIYEKETI JUU YA YULE FARASI, upanga utokao katika kinywa chake. Na ndege wote wakashiba kwa nyama zao.”

Unaona hapo ndugu hii roho ya mpinga-kristo ilishaanza kutenda kazi tangu zamani, na shabaha yake si kwa kila mtu duniani bali ni kwa wale walio uzao wa Mungu tu.Iliwauwa wakristo wengi wakati wa zama za giza zaidi ya milioni 68, Na chombo chake teule anachotumia na atakachokuja kutumia kuyalaghai mataifa yote ulimwenguni ni dini na madhehebu huku akihubiri injili yake bandia yenye kivuli cha amani lakini nia yake sio kuleta amani bali kuangamiza uzao mteule wa Mungu. Hivyo ndugu ni wakati wa kujitathimini, je! Wewe ni mfuasi wa kweli wa Kristo au mfuasi wa dini au dhehebu?, je! Wewe ni mtakatifu au vuguvugu,.je! unahuakika wa kwenda mbinguni au unahisi tu?. Je! Wewe ni bibi-arusi wa kweli kama Esta au kama Vashti. Jibu lipo moyoni mwako. Kumbuka ndani ya kanisa yapo magugu na ngano, wapo wanawali wapumbavu na werevu..Je! wewe ni yupi kati ya hayo?.

Bwana wetu yuaja.

Mungu akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Kwa maombezi/ Ushauri/ Ratiba za Ibada/Maswali/ Whatsapp/ Piga namba hizi: +255693036618/ +255789001312


Mada Nyinginezo:

NIFANYE NINI ILI NIIKWEPE HUKUMU.

NITASHINDAJE HALI YA KUUMIZWA NA MANENO YA WATU!

UPUMBAVU WA MUNGU.

JE! MUNGU ATAIANGAMIZA DUNIA TENA BAADA YA GHARIKA YA NUHU?

MANENO HAYA YANA MAANA GANI? “..KWA SABABU HAMTOI ROHO KWA KIPIMO. (YOHANA3:34)”


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments