Ni miaka mingapi ya njaa Daudi aliyoambiwa achague? Ni miaka 7 au miaka 3?

Ni miaka mingapi ya njaa Daudi aliyoambiwa achague? Ni miaka 7 au miaka 3?

 Tukisoma 2Samweli 24:13, tunaona biblia imesema ni miaka 7 imewekwa mbele ya Dauidi, Lakini tukienda kusoma tena habari hiyo hiyo katika kitabu cha 1Nyakati 21:12, tunaona biblia inataja miaka 3 ya njaa na si 7 tena. Je! Ipi ni ipi?


Labda tuanze kusoma habari hiyo katika kitabu cha 2 Samweli..

2Samweli 24:11 “Na Daudi alipoondoka asubuhi, neno la Bwana likamjia nabii Gadi, mwonaji wake Daudi, kusema,

12 Nenda, ukanene na Daudi, Bwana asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya uchague moja, nikutendee hilo.

13 Basi Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, MIAKA SABA YA NJAA ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Fanya shauri sasa, ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma”.

Hapo tunaona kweli ni miaka 7, Lakini tusome tena habari hiyo katika Mambo ya Nyakati.

1Nyakati 21:11 “Basi Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Bwana asema hivi, Kubali upendavyo;

12 MIAKA MITATU YA NJAA; au miezi mitatu kuangamia mbele ya adui zako, ukipatwa na upanga wa watesi wako; au siku tatu upanga wa Bwana, yaani tauni katika nchi, na malaika wa Bwana akiharibu kati ya mipaka yote ya Israeli. Haya basi ufikiri ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma”.

Kwa mistari hiyo ni rahisi kusema biblia inajichanganya.. Lakini kiuhalisia, biblia haijichanganyi mahali popote, wala haijakosewa mahali popote.

Katika habari hiyo, waandishi wote wawili wa vitabu hivyo, walikuwa wapo sahihi.. hakuna ambaye hakuwa sahihi, kwasababu wote walikuwa wanaongozwa na Roho Mtakatifu katika kuandika. Isipokuwa kila mmoja aliandika katika mazingira tofauti na mwenzake, na hawakunakiliana hivyo, ushuhuda wa mmoja hauwezi kufanana asilimia mia na wa mwingine.

Hebu chukua mfano, umefungua taarifa ya habari katika vyombo viwili tofauti, ni wazi kuwa unaweza kusikia habari moja lakini imefafanuliwa tofauti katika vyombo vyote viwili lakini habari ni ile ile moja.

Habari hizo haziwezi kufanana asilimia mia, vinginevyo kimoja kitakuwa kimenakili habari ya mwingine kama ilivyo.

Kadhalika kitabu cha Samweli sio nakala ya kitabu cha Mambo ya Nyakati, kadhalika kitabu cha Luka sio nakala ya kitabu cha Mathayo..ingawa vyote vinaweza kuwa vinaelezea matukio yanayofanana, lakini haviwezi kufanana asilimia mia, kwasababu ni mashahidi wawili tofauti. Ndio maana unaona Ushuhuda wa Luka haifananini asilimia mia na wa Mathayo au Marko.

Sasa labda turudi katika habari hiyo ya Daudi..

Tukianza na kitabu hicho cha 2Samweli 24, labda turudi sura mbili nyuma, tuone ni tukio gani lilitokea.. kisha tutaanza kuelewa ni kwasababu gani Mwandishi hapa kataja miaka 7 badala ya 3..

Tusome,

2Samweli 21:1 “Kulikuwa na njaa siku za Daudi MUDA WA MIAKA MITATU, MWAKA KWA MWAKA; naye Daudi akautafuta uso wa Bwana. Bwana akasema, Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni”.

Umeona hapo? Kabla Daudi kutaka kwenda kuwahesabu watu, kulitangulia njaa miaka 3, ambapo njaa hiyo ilisababishwa na Sauli kuwaua wagibeoni.

Sasa baada ya Daudi kutafuta utatuzi wa njaa hiyo, maandiko yanatuambia alifanya kosa lingine la kwenda kuwahesabu Israeli, jambo ambalo lingeiingiza tena Israeli katika baa la njaa kwa miaka mingine 3 mbele. Na kama ukisoma pale, Sensa ya kuwahesabu Israeli ilichukua miezi kama 9 na siku 20 (2Samweli 24:8).

Kwahiyo ukichukua Miaka 3 ya njaa iliyosababishwa na Sauli,  ukijumlisha na hiyo miezi 9.. utaona ni kipindi cha takribani Miaka 4. Na maandiko yanasema baada ya Daudi kuwahesabu Israeli ndipo Neno la Bwana likamjia..kwahiyo inawezekana ikawa siku ile ile alipomaliza kuwahesabu au wiki moja baadaye au mwezi mmoja baadaye ndipo Neno la Bwana likamjia.. Lakini yote katika yote miaka 4 iliisha ambayo ilikuwa ya njaa..kabla ya kuja mingine 3 kwaajili ya kosa hilo la kwenda kuwahesabu.

Kwahiyo ukichukua hiyo miaka 3 ya Sauli, ukajumlisha KIPINDI CHA MWAKA MZIMA cha SENSA, Pamoja na Neno la Bwana kumjia Daudi, Ukajumlisha na MIAKA HIYO 3 Daudi aliyoambiwa achague, Jumla yake utapata ni miaka 7.

Kwahiyo Mwandishi wa katika kitabu hicho cha Samweli alichokuwa anakimaanisha ni kwamba Endapo Daudi atachagua janga la miaka 3 ya njaa.. atakuwa amefanya JUMLA ya miaka ya njaa katika Israeli kuwa SABA.

Lakini tukirudi kwa mwandishi wa kitabu cha Mambo ya Nyakati, yeye alikwenda moja kwa moja kwenye hiyo miaka 3 ya mwisho, pasipo kuhesabu ile 3 ya kwanza iliyotangulia, pamoja na ule mmoja wa Sensa. Na ndio maana utaona katika kitabu hicho cha Mambo ya Nyakati hajaeleza popote kuhusu Njaa hiyo ya kwanza iliyosababishwa na Sauli…kama alivyoeleza mwandishi wa kitabu cha Samweli.

Kwahiyo hakuna utata wowote katika hiyo mistari.

Sasa ilikuwepo sababu kwanini Mungu achukizwe na Daudi katika kwenda kuwahesabu Israeli..Sababu hiyo kwa urefu unaweza kuisoma hapa>> USIZITEGEMEE NGUVU ZAKO KUKUSAIDIA

Mwisho, tukumbuke kuwa Kristo yupo mlangoni kurudi kulinyakua kanisa lake.. na atakuja kama mwivi, Je! umejiandaa?. Kama bado mwamini Yesu leo, na kubatizwa, upate ondoleo la dhambi.

Bwana atubariki.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

NJAA ILIYOPO SASA.

HUYU MELKIZEDEKI NI NANI?

HUYU MELKIZEDEKI NI NANI?

RUDIA, TENA NA TENA KUMWOMBA MUNGU USIKATE TAMAA.

KUJIPAMBA NI DHAMBI?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments