USIZITEGEMEE NGUVU ZAKO KUKUSAIDIA!

USIZITEGEMEE NGUVU ZAKO KUKUSAIDIA!

usizitegemee nguvu zako kukusaidia katika jambo lolote!

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze Biblia, Neno la Mungu ambalo ni Taa iongozayo miguu yetu na mwanga wa njia zetu (Zab.119:105).

Leo tutajifunza kwa ufupi, ni jinsi gani Bwana hapendezwi na sisi kuzitegemea nguvu zetu wenyewe, au kuwategemea wanadamu katika matatizo yanayotukabili. Au kutegemea vitu tulivyojiwekezea.

Tutajifunza kwa kumtazama Mtu anayeitwa Daudi. Ambaye wakati Fulani alikengeuka kidogo na kutaka kuzitegemea nguvu zake mwenyewe badala ya kumtegemea Mungu. Jambo ambalo lilimchukiza sana Mungu..Ingawa aliwahi kwenda kutubu lakini tayari lilikuwa limeshaleta madhara makubwa sana katika Taifa la Israeli.

Kama ni msomaji mzuri wa Biblia utakumbuka kuna wakati Mfalme Daudi wazo lilimwingia la kwenda kuwahesabu watu. Na kama utakumbuka jambo hilo lilimchukiza sana Mungu na kusababisha watu wengi kufa Israeli. Ingawa jambo hilo Mungu aliliruhusu makusudi ili kuwalipiza kisasi wana wa Israeli kwa makosa yao. Lakini bado halikuwa mpango kamili wa Mungu.

Tunasoma Daudi alikwenda kuwahesabu watu wote na kupata jumla ya mashujaa laki 8 wenye kufuta upanga katika Israeli na mashujaa laki 5 katika Yuda..Hivyo jumla ya mashujaa waliokuwa ni milioni moja na laki tatu.(1,300,000) Hiyo ni idadi kubwa sana ya watu.

Tusome.

2Samweli 24:1 “Tena hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, akamtia Daudi nia juu yao, akisema, Nenda, ukawahesabu Israeli na Yuda.

2 Basi mfalme akamwambia Yoabu, jemadari wa jeshi la askari, waliokuwa pamoja naye, Zunguka sasa katikati ya kabila zote za Israeli, tangu Dani mpaka Beer-sheba, mkawahesabu watu, nipate kujua jumla ya hao watu………..”

8 Nao walipokwisha kuzunguka nchi yote, wakaja Yerusalemu mwisho wa miezi kenda na siku ishirini.

9 Naye Yoabu akamtolea mfalme jumla ya hesabu ya watu; nao walikuwa wa Israeli mashujaa wenye kufuta panga mia nane elfu; nao wa Yuda walikuwa watu mia tano elfu.

10 Ndipo moyo wake Daudi ukamchoma baada ya kuwahesabu hao watu. Naye Daudi akamwambia Bwana, Nimekosa sana kwa haya niliyoyafanya; lakini sasa, Ee Bwana, nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.

11 Na Daudi alipoondoka asubuhi, neno la Bwana likamjia nabii Gadi, mwonaji wake Daudi, kusema,

12 Nenda, ukanene na Daudi, Bwana asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya uchague moja, nikutendee hilo.

13 Basi Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, miaka saba ya njaa ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Fanya shauri sasa, ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma.

14 Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na tuanguke katika mkono wa Bwana; kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu”.

Sasa ukichunguza Nia ya Daudi hasa haikuwa kujua idadi ya watu wote waliokuwemo Israeli, bali utagundua kuwa Nia yake kuu ilikuwa ni kujua idadi ya wanajeshi au mashujaa alionao wa vita waliokuwepo kwenye ufalme wake wote. Kumbuka Daudi alikuwa ni mtu wa Vita. Muda wote alikuwa amezungukwa na maadui hivyo alitaka kwenda kuwahesabu wanajeshi wake ili ajiwekee matumaini katika jeshi hilo.

Hapo kabla Daudi alikuwa hajui anao idadi ya wanajeshi wangapi, alikuwa anamtegemea tu Mungu asilimia 100, ikitokea vita anaita idadi ya wanajeshi waliopo, bila kujali watakuwa ni wachache kiasi gani ukilinganisha na maadui zao kwasababu Bwana ndiye aliyekuwa jemedari wake.

Ndio maana utaona karibia kila mahali Daudi alikuwa anasema..

Zaburi 20: 7 “Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la Bwana, Mungu wetu.

8 Wao wameinama na kuanguka, Bali sisi tumeinuka na kusimama.

9 Bwana, umwokoe mfalme, Utuitikie siku tuitayo”.

1Samweli 17: 45 “Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.

46 Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli.

47 Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi”

Lakini Daudi Mtu ambaye alikuwa hategemei majeshi kumwokoa. Sasa hapa anaanza kujitumainisha katika hayo. Alikuwa hategemei mikuki, panga wala fumo sasa anaanza kuvitegemea kwa kutaka kujua idadi ya wanajeshi walioshika upanga. Amesahau kuwa miaka yote Mungu hakuwahi kumwokoa kwa wingi wa jeshi au silaha alizonazo.

Hiyo ikawa ni dhambi kubwa sana ikasababishia Mungu kuyapunguza hayo majeshi yake aliyoyahesabu, kwa kuleta Tauni, wakafa watu elfu 70. Na tena hapo ni kwasababu tu ya Rehema za Mungu kuwa nyingi, endapo Bwana asingeachilia Rehema zake. Watu milioni kadhaa wangekufa. Na hayo majeshi aliyojitumainia nayo yatakuwa wapi?…Usizitegemee nguvu zako.

Ndio maana Bwana Yesu alisema mfano huu katika kitabu cha Luka.

Luka 12:19 “Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi.

20 Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?

21 Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu”.

Je! Tumaini lako liko wapi? Kwenye mali ulizo nazo?. Au hazina ulizo nazo, au vitega uchumi vyako?. Au watoto wako?, au idadi ya wafanyakazi ulio nao? Au Bwana?. Usianze kusema sasa nina mali nyingi au fedha nyingi au salio kubwa kwenye akaunti yangu basi kesho yangu itakuwa safi, kesho yangu itakuwa ya ushindi, bali useme Ninaye Bwana moyoni mwangu kesho yangu itakuwa safi, kesho yangu itakuwa ya Baraka na ya mafanikio haijalishi niacho hiki au sina, kwasababu Bwana ndiye ngome yangu na jabali langu.

Kama ni Bwana ndiye tegemeo lako, basi umechagua fungu jema ambalo hutakuja kujutia kamwe! usizitegemee nguvu zako..Wakati wengine wanataja hazina zao wewe utalitaja jina la Bwana wa Majeshi, wakati wengine wanatumaini vitu vya ulimwengu huu, wewe unamtumainia Bwana.

Lakini kama humtumainii Bwana na unajitumainisha katika vitu ulivyowekeza hapa duniani. Kumbuka Yaliyompata Daudi yanaweza kukupata na wewe. Watu aliojitumainia Daudi kwa kwenda kuwahesabu walipunguzwa kwa Tauni ya siku tatu tu. Kadhalika Bwana atasambaratisha kila kitu unachojitumainisha kwacho leo hii. Atapunguza mali ulizonazo, atapunguza hata kile kidogo ambacho ulikuwa umeshakianza. Kwasababu yeye anasema ni Mungu mwenye wivu. Hawezi kuruhusu Vitu vya Ulimwengu huu vichukue nafasi yake yeye. Usizitegemee nguvu zako.

Bwana akubariki sana. Kama hujampa Yesu Kristo maisha yako, ni vyema ukafanya hivyo leo. Kwasababu saa ya wokovu ni sasa na si Kesho. Tubu kwa kumaanisha kuacha dhambi na Bwana atakusamehe na kukuokoa.

Maran atha! jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

Ni sahihi kumuita Mariamu mama wa Mungu?

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

TIMAZI NI NINI

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Devis Julius administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Magesa
Magesa
2 years ago

Nabarikiwa Sana na masomo mnayotoa