JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

Jinsi Mungu anavyotuhudumia sisi ni tofauti na sisi tunavyoweza kufikiri, Sisi tunatazamia Mungu atatuhudumia kutoka mbinguni, lakini yeye yupo tofauti, msaada wake ameuweka sehemu ya chini sana, ambayo imedharauliwa na wengi, Leo hii ukimwomba Mungu jambo basi toa yale mawazo kwamba atakupa majibu kutoka katika mambo makubwa….Ni kweli matokeo ya majibu yatakuwa makubwa, lakini chanzo cha majibu yako kinaweza kisiwe huko unapokitazamia. Naamani alikuwa mkuu wa majeshi wa Taifa la Shamu, ambalo lilikuwa ni moja ya mataifa makubwa sana enzi zile za wafalme, lakini alisumbuliwa na ukoma kwa muda mrefu sana mpaka siku moja aliposikia kuna nabii wa Mungu Israeli, ambaye ni Elisha, tunaona lakini alipomfuata ili aponywe majibu yake yalikuwa ni tofauti na alivyotazamia. Tusome:

2Wafalme 5:9 “Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha.

10 Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema, Enenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia, nawe utakuwa safi.

11 Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nalidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la Bwana, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma.

12 Je! Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira.

13 Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi?

14 Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi.”

Unaona, hata leo watu wengi wamemwomba Mungu awafanyie mambo Fulani Fulani katika maisha yao, wengine wanayo magonjwa yanawasumbua wengine ni matatizo, lakini walipofika kwa Mungu waliposikia kuna maagizo Fulani ya kuzingatia, kwamba wanapaswa waokoke kwanza wao wanapuuzia, kwamfano biblia inaagiza kila mmoja anapaswa abatizwe kwa kuzamishwa katika maji mengi ili apate ondoleo la dhambi zake…

Lakini mtu akisikia hivyo utaona anaanza kutoa udhuru, wakitoa tafsiri zao, aah! Ubatizo haumpeleki mtu mbinguni!, Ubatizo hauondoi dhambi kinachoondoa dhambi ni damu ya YESU, wengine watasema, dini yetu haituagizi hivyo, wengine watasema batizo zote ni sawa za kunyunyiziwa na za kuzamwishwa ni sawa, wengine watasema nenda mto Yordani na wewe ukabatizwe kama Bwana Yesu ndio tujue kuwa kweli umebatizwa ipasavyo n.k Mtu huyo huyo pia atakuwa tayari kwenda kila mwisho wa wiki kuogelea baharini au kwenye mabwawa ya starehe kwa masaa mengi bila hata kukinai wala kuchoka, lakini kuingia katika yale maji kubatizwa mara moja tu katika jina la Bwana Yesu, ni vita! Ujue ni roho ya namna gani ipo ndani ya mtu wa namna hiyo!

Na mtu huyu huyu bado anasema ameokoka, na amekaa katika wokovu kwa miaka mingi..Nataka nikuambie kitendo cha kubatizwa kinaweza kisiwe na maana sana kwako, lakini kina maana kubwa sana kwa YESU aliyetoa maagizo hayo..

Unatazamia uwekewe mikono lakini Bwana anakwambia kashuke kwenye yale maji nawe utapona!….Unatazamia Bwana akwambie funga masaa mengi na uombe watu wakuombee au utoe sadaka nyingi….lakini Bwana anakupa maagizo marahisi tu, jishushe kafanye ibada ya kuwaosha miguu watakatifu nawe utaona matokeo makubwa tu!….wapo wengine wanasema kushiriki meza ya Bwana au kutawadhana miguu watakatifu havina maana yoyote, lakini Bwana Yesu alisema Heri ninyi mkiyafanya hayo.

Yohana 13:14 Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi.

15 Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.

16 Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka.

17 Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda”.

Wewe utajiona na hadhi yako, huwezi kushika miguu ya mwingine na kuiosha, Bwana Yesu aliyekuwa ni Mungu katika mwili lakini alifanya hivyo, mimi na wewe ni nani tusifanye?..yeye aliiosha miguu ya wavuvi, sisi ni nani tusioshane miguu?..

Sasa Maagizo ya msingi kama hayo mtu hataki kuzingatia anategemea vipi Mungu atampatia haja yake kwa haraka, kama anavyotaka yeye?..anatazamia aambiwe njoo nunua maji ya upako, au awekewe mikono na watumishi, au afunge na kuomba,..akidhani hayo ndio maagizo sahihi ya Mungu kama Naamani alivyofikiri kumbe sio. Wayahudi walimtazamia MASIHI wao atakuja kama mfalme mkuu sana, ambaye ataketi katika kiti cha enzi cha Daudi pale Israeli na kuwapigania dhidi ya maadui zao Warumi, lakini alipokuja katika familia ya kimaskini walipoteza shabaha, alipokuja hashiki silaha bali anahubiri upendo walimkosa, walipomuona amesulibiwa msalabani ndipo wakasema kabisa huyu amelaaniwa, lakini hawakujua kuwa Yule ndio Mungu mwenyewe aliyeuvaa mwili anaishi na sisi.

Vivyo hivyo na sisi tukitaka Mungu atuhudimie tunapaswa tujishushe, na kujishusha kwenyewe ni kuyatii maagizo yake mepesi aliyotupa, tusijione sisi ni wa rohoni sana, au tunajua zaidi yake mpaka tukadharau anachotuelekeza kufanya..Soma biblia ili ufahamu ukweli, na ukisha ujua ukweli basi uwe tayari kubadilika bila kujali dini yako au dhehebu lako linaamini vipi, na hiyo ndio dalili kubwa itakayokutambulisha kuwa ROHO WA MUNGU hajazimika bado ndani yako, ikiwa upo tayari kuyatii maagizo yake yote sawasawa na maandiko yanavyotulekeza.

Biblia inasema: “Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”. (Ufunuo 2:7)

Maran Atha.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

ALIYE MKUU KATIKA UFALME WA MBINGUNI.

JINSI YA KUITUMIA VYEMA NEEMA YA MUNGU ILIYO JUU YANGU.

NGUVU ZA ZAMANI ZIJAZO:

MWISHO WA HAO WAMSAHAUO MUNGU.

SIRI YA MUNGU.

BABA YANGU ANATENDA KAZI HATA SASA!


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Joseph Likare
Joseph Likare
2 years ago

AMEN