ROHO HUTUOMBEA KWA KUUGUA KUSIKOWEZA KUTAMKWA!

ROHO HUTUOMBEA KWA KUUGUA KUSIKOWEZA KUTAMKWA!

Warumi 8:26 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.

27 Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.

28 Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake”

Haijalishi tuna ujuzi wa kuongea kiasi gani?, haijalishi tuna vipaji vya kuongea na vya kupangilia maneno kiasi gani, haijalishi tunayajua maandiko kiasi gani…Mbele za Mungu watu wote ulimwenguni hatujui kuomba jinsi ipasavyo! Hata kama tunaweza kujiona tumeomba vizuri kiasi gani au tumebobea kiasi gani…bado hatujui kuomba jinsi ipasavyo…

Utauliza hata mchungaji, au Nabii, au Mwalimu, au Askofu aliyekaa kwenye wokovu miaka mingi, bado atakuwa hajui kuomba jinsi ipasavyo?..Jibu ni ndio! Hata kama atakuwa amekaa miaka mia katika wokovu, na kila siku anasali, na anajua maandiko yote na kuyanukuu kisahihi wakati wa kuomba…Bado pasipo Roho Mtakatifu atakuwa hajui kuomba jinsi ipasavyo, na hivyo maombi yake huwa hewa mbele za Mungu.

Leo tutajifunza Umuhimu wa Kuwa na Roho Mtakatifu katika kuomba! Kwa maana yeye ndiye atusaidiaye kuomba!…Sasa Utauliza Roho Mtakatifu anatuombeaje? Je yupo huko mbinguni amekaa akituombea kwa Baba muda wote akipeleka mahitaji yetu hata kama wakati tukiwa tumelala au vipi?..Na swali lingine ni kwamba je! Kama anatuombea sisi tuna haja gani tena ya kuomba..maana yeye ndiye anayetuombea vizuri Zaidi.

Ili kupata majibu ya maswali hayo, tujifunze kwanza kidogo jinsi Roho Mtakatifu anavyotenda kazi katika kuwavuta watu kwake..

Mtu aliyejaa Roho Mtakatifu, anapokwenda kuhubiri kwa watu walio nje ya Kristo, yule Roho aliyeko ndani yake, anaingia ndani ya wale watu ambao wapo nje ya Kristo, na kumsaidia kuhubiri ndani ya mioyo yao…Kwahiyo huyu mhubiri mwenye kigugumizi na asiyejua kuongea vizuri, labda pengine atazungumza maneno machache tu lakini kwasababu anaye Roho Mtakatifu anayemsaidia kuhubiri katika mioyo ya wale wenye dhambi upande wa pili…unakuta wale wenye dhambi kuna nguvu ndani yao inayowashawishi mara mbili zaidi watubu waache dhambi, watajikuta hata hawategemei tena maneno ya yule mhubiri, lakini ile nguvu ndani yao inaanza kuwahubiria dhambi na kuhukumu maisha yao ya dhambi……

Sasa hicho kitendo cha wenye dhambi kusikia kama wanahubiriwa kwa nguvu mara mbili Zaidi katika mioyo yao zaidi ya wanavyosikia katika masikio ya nje…Huo ndio unaoitwa Msaada wa Roho Mtakatifu kwa yule Mhubiri..Hivyo kitendo hicho tunaweza kukiweka katika sentensi hii..

“Roho Mtakatifu amemsaidia yule Mhubiri, kuwahubiria wale wenye dhambi mioyoni mwao kwa kuugua kusikoweza kutamkika” Matokeo yake wale wenye dhambi wakawahi kukubali kumpa Yesu Maisha yao kuliko yule Mhubiri angekosa huo msaada.

Yohana 16:7 Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.

8 Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.

Sasa endapo huyo Mhubiri angekuwa hana Roho Mtakatifu ndani yake, wale watu mioyoni mwao wasingesikia chochote kinachowahubiria hivyo wangemsikiliza yule mhubiri na kigugumizi chake, na mwisho wa siku wangeishia kumcheka na kumwona anapoteza muda..na wangemwona hajui kuongea wala kujieleza na wasingetubu!..Au hata kama ungekuwa unajua kuongea vizuri na kupangilia maneno na kunukuuu, wangekusifia tu kwamba unajua kuongea vizuri na kwamba ni mhubiri mzuri lakini ndani ya mioyo yao wasingesikia chochote kinachowasukuma wao kutubu dhambi, na hivyo kuishia kupata hasara badala ya faida.

Sasa kwa formula hiyo hiyo, ndiyo Roho Mtakatifu anayotusaidia kuomba mbele za Mungu…Unapoingia magotini kumwomba Mungu, hoja zako wewe zina madhaifu mengi, na wala hazieleweki mbele za Mungu, hata kama umejiona umezipangilia kiasi gani, hata kama umejiona umenukuu maandiko kiasi gani…Lakini kwasababu tu hunaye Roho Mtakatifu, Unakuwa una msaada wa anayekusaidia kuomba upande wa pili, katika moyo wa Mungu.

Sasa Roho Mtakatifu anakusaidia kuzipeleka zile hoja zako mbele za Moyo wa Mungu, kiasi kwamba unanena maneno machache, lakini huku nyuma Roho anayahubiri yale maneno uliyoyanena moyoni mwa Baba mbinguni kwa ufasaha Zaidi, na hivyo kuuchoma na kuugusa moyo wa Mungu kwa namna isiyoweza kutamkika mpaka kufikia kuleta majibu yanayotakiwa. Haleluya!

Huo ndio umuhimu wa Roho Mtakatifu kwa mwaminio yeyote! Tunamhitaji sana Roho Mtakatifu katika mambo yote maana pasipo yeye sisi hatuwezi, ndio maana biblia imemwita “MSAIDIZI” Msaidizi maana yake anatusaidia pale tunapokwama..

Tunaposali tunamhitaji huyu msaidizi, hakuna chuo chochote cha kwenda kusomea jinsi ya kuomba! Roho Mtakatifu pekee yake ndiye anayeweza kutuombea jinsi ipasavyo…Na anatuombea pale tunapoomba! Sio wakati tumelala…hapana! Hata mhubiri anamsaidia kuhubiri pale anapohubiri, sio wakati ambao hahubiri.

Hivyo kama mtu hana Roho Mtakatifu basi umekosa kitu kikubwa sana na cha maana sana, ni heri angekosa utajiri wote wa ulimwengu huu au kukosa kila kitu kuliko kumkosa Roho Mtakatifu..kwasababu Biblia imesema katika Warumi 8:9 kuwa “Mtu yeyote asiye na Roho huyo sio wa Mungu”

Je! Umepokea Roho Mtakatifu?…Au bado unaomba tu bila msaada wake?..Lakini Utauliza nitampokeaje? Jibu lipo ndani ya Biblia Takatifu katika Mstari ufuatao…

Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”

Fomula ya kumpokea ndiyo hiyo, kutubu kwanza kwa kumaanisha kuacha Maisha ya dhambi kama ulevi, anasa, uasherati, uvutaji sigara, chuki, visasi, utazamaji picha chafu, utukanaji, ulawiti, usagaji, ushoga, ushirikina, uchawi, n.k Kisha ukishatubu kutoka moyoni kabisa na Bwana akiiona Toba yako na Imani yako kuwa ni ya dhati kabisa…ATAKUSAMEHE KABISA! Na baada ya msamaha huo wa Bure utakaoupata hatua inayofuata ni kwenda kutafuta ubatizo sahihi, ambao huo ni wa kuzamishwa mwili wote kwenye maji na kwa JINA LA YESU KRISTO, Kisha baada ya huo Roho Ataingia ndani yako, Msaidizi wetu ambaye ni Zawadi kutoka kwa Baba, ambayo tumepewa sisi na Watoto wetu na wote tutakaowahubiria kumjua yeye.

Hakuna mfariji wa kweli kama ROHO MTAKATIFU.

Bwana akubariki.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

MATUNDA 9 YA ROHO MTAKATIFU.

HATUA ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA KUTUONGOZA.

JE! KARAMA NI UTHIBITISHO WA KUWA NA MUNGU?

NGURUMO SABA

UNYAKUO.


 

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
6 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
11 months ago

Ubatizo ni ubatizo, haijalishi umebatizwa kwa maji mengi au maji kidogo, mwingi atabatizwa kwenye habari ya Hindi, mwingineziwa Victoria na mwingine mto Mara, wote hawa watakuwa wamebatizwa pasipo kujali wingi wa maji!

Sephania
Sephania
1 year ago

MUNGU YEYE AKUONAE SIRINI NA AKUJAZE

Benard wamalwa
Benard wamalwa
1 year ago

Nitumie maana ya fungu la kumi.

Japhet ladislaus mkai
Japhet ladislaus mkai
3 years ago

Amen ubarikiwe sana ,Mungu akutendee sawasawa na unachostaili