JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Kuna tofauti kati ya UBATIZO wa Roho Mtakatifu na UPAKO wa Roho Mtakatifu.

Watu wanachanganyikiwa wakidhani kuwa na upako, au nguvu za Roho Mtakatifu, ndio Umebatizwa na Roho Mtakatifu. Lakini hii sio kweli, mtu anaweza kuwa na upako wa Roho Mtakatifu, akaponya magonjwa, akafufua wafu, akanena kwa lugha, akaona maono, akatabiri au kuota ndoto na ikaja kutokea, na bado asiwe amebatizwa na Roho Mtakatifu. Tunaona kabla ya Pentekoste wanafunzi wa Yesu ikiwemo Yuda aliyemsaliti Bwana walikuwa wanafanya ishara zote hizi na bado walikuwa hawajabatizwa na Roho wa Mungu..

Biblia inasema Mathayo 5:45

“…..maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.”

Hii ni SIRI kubwa sana inayozungumzwa hapo, Bwana anaachia nguvu zake kwa waovu na wema, anaachilia nguvu zake za uponyaji,miujiza, kwa wote waovu na wema n.k. Hivyo kigezo cha mtu kufanya ishara na miujiza si tiketi ya yeye kuwa mwana wa Mungu, Bwana aliwaambia wanafunzi wake..

Luka 10:20″ Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”

Unaona alituambia tusifurahi kwa sababu miujiza inatendeka na sisi bali kwasababu majina Yetu yameandikwa mbinguni hii ikiwa na maana,tunapaswa tufarahi tunapokuwa na mahusiano na Mungu na uhakika wa kwenda mbinguni na sio tunapokuwa na uwezo wa kutoa pepo au kufanya miujiza.

Katika kipindi hichi cha mwisho shetani amefanikiwa kuwadanganya wengi kwa njia hii, kwa kushindwa kutofautisha ubatizo halisi wa Roho Mtakatifu na Upako wa Roho Mtakatifu, si jambo la kushangaza kuona mtu anatoka kuvuta sigara na akaenda kunena kwa lugha, nabii katoka kuzini na bado akaenda kutoa unabii na huo unabii ukatimia kama ulivyo, mtu katoka kwenye ufisadi na akaenda kumwombea mtu akafufuka na bado anaota ndoto, ishara na miujiza vikifuatana naye, mtu katoka kutukana na bado akaenda kufundisha,na kutoa mapepo na bado nguvu za Mungu zikashuka na watu wakafunguliwa katika vifungo vyao..

lakini hiyo sio uthibitisho ya kwamba mtu huyo amepokea Roho Mtakatifu usidanganyike. Mungu anaweza kutumia chombo chochote kutenda kazi yake kama chombo cha kuazima tu, kazi ya hicho chombo ikiisha Mungu anaondoka. Kwa mfano tunaona katika biblia Mungu alimtumia Punda kuzungumza na Balaamu, lakini baada ya kuupeleka ujumbe yule punda akarudia katika hali yake ya mwanzo ya upunda.

Hivi ndivyo watu wanavyotumiwa na Mungu kama vyombo vya kuazima lakini wasiwe watu halisi wa Mungu, wamenyeshewa tu ile mvua ya upako ambayo inawanyeshea wote waovu na wema. Hii ni SIRI kubwa watu wanapaswa waijue.

Bwana Yesu alisema

Mathayo 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?
23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”.

Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”

Mstari huu unajieleza wazi kabisa juu ya watu wanaojidhani kuwa wanafanya miujiza na ishara ndio uthibitisho kuwa wao ni wana wa Mungu.

LAKINI UBATIZO WA ROHO MTAKATIFU NI UPI?

Uthibitisho wa Roho Mtakatifu pale anaposhuka juu yako anakufanya uwe kiumbe kipya (uzaliwe mara ya pili), anasafisha ile hali ya kutamani dhambi na kukufanya uwe mtakatifu na pia atakuongoza katika kuijua kweli yote tusome..

 Yohana 16:12 “Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa.
13 Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.
14 Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari”.

Jambo la kwanza Mkristo yeyote aliyepokea Roho Mtakatifu lazima Roho amuongoze katika kuijua ukweli, ikiwemo uelewa wa maandiko,kiu na shauku ya kumjua Mungu siku baada ya siku.na kufanywa ufanane na Yesu Kristo. Roho ya mafunuo itakuja juu yake, Hatafungwa na mambo ya dini bali na NENO la Mungu tu, na Roho atamweka mbali na ulimwengu, yaani kiu ya kuupenda mambo ya ulimwengu itaanza kufa ndani yake.

Jambo lingine ni Roho atashuhudia ndani yake kuwa yeye ni Mwana wa Mungu ( atakushuhudia katika maisha unayoishi)

Warumi 8:15 “Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.
16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu”;

Mtu huyo ataondokewa na hofu ya maisha kwa kuwa anajua anaye baba mbinguni, na Baba anamshuhudia ya kuwa yeye ni mtoto wake ndani yake. 

Kuna watu angali wakijidanganya kuwa wana Roho Mtakatifu lakini wamekosa haya mambo, ndani yao tamaa ya mambo ya ulimwengu imewavaa, Hawana uhusiano wowote  wao na Baba yao wa mbinguni, hofu na masumbufu ya maisha haya yamewasonga kana kwamba hawana Baba mbinguni, Wanalipinga siku zote NENO la Mungu, kuthibitisha dini zao na madhehebu yao(mfano wa mafarisayo na masadukayo), Hawapendi kuijua kweli halisi ya injili inayowapeleka watu mbinguni bali injili za pesa na mafanikio ya ulimwengu huu tu.

Sasa watu kama hao ni dhahiri kuwa hawajashukiwa na Roho wa Mungu bado, haijalishi wanafanya miujiza kiasi gani. Sio kwamba kuwa na hizo ishara ni mbaya, tofauti ni hii hawa wanakuwa wamenyeshewa mvua tu lakini hawana Roho, na wale waliobatizwa kweli kweli wanakuwa na vyote, 

Hivyo basi Roho wa Mungu anaposhuka juu ya mtu kwa mara ya kwanza huyo mtu anaweza akaanza kunena kwa lugha, au kuona maono, au kutabiri au akapata msisimko, au kushukiwa na nguvu za Mungu nyingi ndani yake,au akapata hisia ya tofauti ambayo hakuwahi kuisikia hapo kabla, wengine wakati Roho akishuka juu yao amani ya kipekee inawashukia,wengine hawasikii chochote lakini watafahamu kwa jinsi Roho wa Mungu anavyougua ndani yao, haya yote ni udhihirisho wa nje ambao hata wale wengine(magugu) wanaweza kuupata.

Lakini uthibitisho halisi ni jinsi maisha yako yatakavyokuwa yanaanza kubadilishwa na kufanywa kiumbe kipya siku baada ya siku kwa kutakaswa kwa Neno. na ubatizo wa Roho Mtakatifu unaambatana na karama za Mungu lakini kama tulivyosema mtu anaweza kuonyesha zile karama za Roho na asiwe amebatizwa na Roho Mtakatifu.

Na kuna mtazamo pia ya kuwa “kunena kwa lugha” kuwa ndio uthibitisho wa mtu kupokea Roho Mtakatifu, mtazamo huu si kweli mtu anaweza kunena kwa Lugha na asiwe amepokea Roho Mtakatifu kwasababu hichi ni kipawa cha Roho na kinamshukia yeyote kwa jinsi Roho alivyomjalia mtu, kumbuka hata mashetani wananena kwa lugha, Na kipawa hichi sio lazima kila mtu awe nacho,

kwasababu biblia inasema 

1wakoritho12:28 “Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha.
29 Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza?
30 Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri”?

Si unaona hapo sio wote wenye hicho kipawa cha kunena kwa Lugha. Kwahiyo mtu anaweza akabatizwa na Roho Mtakatifu na asinene kwa lugha, bali akaonyesha karama nyingine tofauti na hiyo, aidha unabii, au karama ya uponyaji, au neno la maarifa, au miujiza n.k. kwa jinsi Roho atakavyokujalia.. Mafundisho ya kwamba kila mtu lazima anene kwa lugha sio sahihi mwisho wa siku kama mtu hajapewa hicho kipawa anaishia kunena kwa akili zake tu, na kutakuwa hakuna kufasiri 1wakoritho 14.

Kwahiyo mpendwa kama haujabatizwa na Roho Mtakatifu mwombe Bwana naye atakupa Luka 11:9-13..”Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.

Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? Au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” 

Kumbuka kutoa zaka, kusaidia yatima, kuhudhuria ibada kila jumapili, hayo hayatoshi hata watu wasioamini wanafanya hayo na zaidi ya hayo(mfano mzuri ni waislamu)

soma….

Mathayo 5:20″ Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. “

Hii haki inakuja kwa kuzaliwa mara ya pili, hauwezi kuingia katika ufalme wa mbinguni pasipo hiyo, na ukishabatizwa na Roho Mtakatifu ndio kuzaliwa mara ya pili.

Matendo 2:38 “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.”

Kumbuka Roho mtakatifu ndiye MUHURI wa Mungu, (maana ya neno MUHURI ni kwamba “KAZI IMEKAMILIKA JUU YAKO”).waefeso 4:30 “Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi”. Pasipo huyo hauwezi kwenda mbinguni, kwa sababu biblia inasema warumi 8:9 “……….Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake”. 

Mungu akubariki!

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

HATUA ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA KUTUONGOZA

ACHENI MJUE YA KUWA MIMI NI MUNGU.

JE! KARAMA NI UTHIBITISHO WA KUWA NA MUNGU?

JIPE MOYO.

BWANA ALIPOSEMA “SIKUJA KUTANGUA TORATI BALI KUITIMILIZA” ALIKUWA ANAMAANISHA NINI?

rejeabiblia.com


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
6 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Lokiru Joseph
Lokiru Joseph
2 years ago

Ubarikiwe sana.

lucas mhula
lucas mhula
2 years ago

Amen, naomba kutumiwa hili somo kwenye namba yangu ya WhatsApp kama itawezekana, asante sana na mbarikiwe sana watumishi wa Mungu.

Silas
Silas
2 years ago

Je,mimi nilikua mkatholiki lakini vile lianza kujuwa kweli siendangi huko ilihali napambana kujuwa kweli tu kwa kusoma maandiko,
Sasa swali langu naezabatizwa mara ya pili?

Letcia Alphonce
Letcia Alphonce
3 years ago

Bwana Yesu asifiwe,Yesu alivyochomwa mkuki ubavuni damu na maji vilitoka,hiii inamanisha nini?