NGUVU ZA ZAMANI ZIJAZO:

NGUVU ZA ZAMANI ZIJAZO:

Waebrania 6:4 “Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu,

5 na kulionja neno zuri la Mungu, NA NGUVU ZA ZAMANI ZIJAZO.

6 wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri”.

Neno hili linatuonyesha kuwa kumbe licha ya mtu kuangaziwa nuru ya Mungu, yaani kupewa neema ya kumjua na kumwamini Yesu Kristo ambaye ndio Nuru yenyewe (Yohana 1:4-5), bado anaweza kuonja kitu kingine ndani yake, licha ya kuonja vipawa vya kimbinguni na kufanywa mshirika wa Roho Mtakatifu yaani kwa kuvuviwa karama za Roho kama vile Lugha, unabii, miujiza, utume, uchungaji, ualimu, uinjilisti n.k. mambo ambayo hapo kabla hayakuonekana kati ya watakatifu au kama yalionekana basi ni kwa sehemu ndogo sana, bado anaweza kuonja kitu kingine cha tofauti kabisa,.licha pia ya mtu kuliona Neno zuri la Mungu kama andiko hilo linavyotuambia, yaani Injili ya Yesu Kristo Bwana wetu ambayo kwa hiyo manabii wengi na wenye haki walitamani kuisikia lakini hawakupata neema kama sisi tunavyojua sasa, lakini bado lipo jambo lingine ambalo tunaambiwa mtu anaweza kulionja kwa wakati huu …Na jambo lenyewe KUONJA NGUVU ZA ZAMANI ZIJAZO..

Zamani zijazo ni nini?, Na nguvu zenyewe ndio zipi?

Biblia inapotumia Neno ZAMANI mara nyingi inamaanisha “nyakati fulani” au “kizazi fulani”..Na au kwa lugha rahisi ni “wakati wa Ulimwengu husika”..Hivyo inavyotumia Neno “Zamani hizi” inamaanisha kuwa wakati wa ulimwengu huu…Kwamfano pale Bwana Yesu alipowaambia wanafunzi wake.

“..Hakika nawaambia, hakuna mtu aliyeacha nyumba, au mke, au ndugu, au wazazi, au wana, kwa ajili ya ufalme wa Mungu,

30 asiyepokea zaidi mara nyingi katika ZAMANI HIZI, na katika ulimwengu ujao uzima wa milele. (Luka 18:29).”

Unaona, Hapo alimaanisha asiyepokea zaidi mara nyingi katika ulimwengu huu wa sasa, na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.

Vivyo hivyo inavyosema ZAMANI ZIJAZO..inamaanisha kuwa “nyakati za ulimwengu ujao”..Yaani ulimwengu baada ya huu mbovu tunaoishi kupita.

Sasa tukitazama mifano michache kwenye biblia itatusaidia kufahamu nini maana ya kuonja nguvu za zamani zijazo, embu tutazame ile habari moja ya yule mwanamke mkananayo ambaye Bwana Yesu alimfananisha na Mbwa.Tunasoma:

Mathayo 15: 21 “Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni.

22 Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.

23 Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu.

24 Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.

25 Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie.

26 Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.

27 Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.

28 Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile”.

Sasa katika habari hii sio kwamba Bwana alikuwa anamtukana kumfananisha na mbwa, au labda alikuwa anajaribu kumkatisha tamaa ili amwache, hapana bali kinyume chake alikuwa anamweleza uhalisia wa mambo jinsi yeye alivyo katika ulimwengu wa roho, na si yeye tu peke yake, bali pia watu wote ambao hawakuwa wayahudi kwa kuzaliwa. Na ndio maana hata ukisoma habari utaona japo yule mwanamke alitaka kuzungumza na Bwana lakini Bwana hakumjibu chochote, mpaka alipokuwa anasisitiza sana, ndipo Bwana akalazimika kufungua kinywa na kumkumbusha nafasi yake ni ipi katika majira aliyokuwa anaishi…

Sasa kumbuka hakukuwa na wakati wowote ambao watu wa mataifa walimtazamia Kristo aje kuwaokoa isipokuwa wayahudi tu peke yao. Japo unabii ulishatangulia zamani kwa vinywa vya manabii kuwa utafika wakati ambao mataifa nao watamtumainia huyo masihi, lakini sharti kwanza akataliwe na watu wake, na kuuawa ndipo damu ipatikane ya kuwasafisha watu wote mataifa ili nao wapokee kipawa cha neema kwa namna ile ile moja kama wayahudi, ni lazima kwanza dhabihu itolewe ili iondoe kile kiambazi cha kati kinachowatenga watu wa mataifa na wayahudi, hivyo wakati huo usingekuja kwanza kabla ya watu wake wenyewe kumkataa..

Lakini tunaona huyu mwanamke wa huko Tiro nchi ya mataifa ya kipagani, kwa sasa ni nchi ya LEBANONI kaskazini mwa Israeli, anakuja na kumfuata Bwana kabla ya majira yake na kumwomba ampe neema amponye mwanae ambaye alikuwa amepagawa na mapepo, lakini Bwana akamwambia asubiri kwanza watoto washibe (yaani wayahudi waipate hiyo neema kwanza),Bwana alimwambia sikutumwa ila kwa kondoo wa Israeli waliopotea, lakini yule mwanamke hakusikia badala yake aliendelea kung’ang’ania kana kwamba ni haki yake, mpaka mwisho wa siku baada ya Bwana kuiona imani yake jinsi ilivyokuwa kubwa akampatia alichokuwa anakitafuta kinyume na mipango iliyokuwa imewekwa kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, tunaona mtoto wake alipona saa ile ile na ule haukuwa tu uponyaji wa mwili wake bali pia hata wa roho yake… mbwa hajasubiria makombo

Sasa Jambo lililofanyika pale katika ulimwengu wa roho, ni kuwa imani ya yule mwanamke ilikwenda mpaka kipindi cha mbeleni kabisa Kalvari siku ambayo Bwana anasulibiwa, Imani ile ikaichukua ile damu iliyokuwa inamwagika katika mishipa ya Emanueli pale Kalvari, ikairudisha sasa mpaka wakati wa nyuma waliokuwepo pale Tiro katika mazungumzo, ikadai haki yake ya ukombozi ambayo ilishapata huko mbeleni kwa mateso yake..Na matokeo yake ikapokea sawasawa na ilivyotaka…

Ni sawa na mtu leo analazimisa alipwe sasa hivi mshahara ambao anapaswa aje kulipwa baada ya miaka 10 , na anang’ang’ania alipwe sasa mpaka analipwa.

Sasa kwa tukio hilo huyu mwanamke tunaweza kusema “Ameonja nguvu za zamani zijazo”..Nguvu za Wakati ambao bado haujafika lakini tayari kashaanza kuyafurahia matunda yake.

Na ndivyo ilivyo hata kwa wakati huu wa kipindi hichi cha mwisho tunachoishi, biblia inaweka wazi kabisa kuwa mtu anaweza kuonja nguvu za zamani zijazo au nguvu za ulimwengu ujao..

Sasa Nguvu za ulimwengu ujao ndio zipi?

Biblia inatueleza huko katika ulimwengu mpya, katika utawala wa amani wa miaka 1000 na Kristo hakutakuwa na magonjwa,wala shida, wala tabu wala vifo.

Isaya 33: 24 “Wala hapana mwenyeji atakayesema, MIMI MGONJWA; watu wakaao humo watasamehewa uovu wao.

Malaki 4: 2 Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, LENYE KUPONYA KATIKA MBAWA zake; nanyi mtatoka nje, na kucheza-cheza kama ndama wa mazizini”.

Unaona?, leo hii unapoumwa ugonjwa ambao hautibiki na Yesu anakuponya, hujui kuwa unaonja nguvu za zamani zijazo ambazo udhihirisho wake wote utaonekana katika ulimwengu ujao. Furaha na amani unayoipata sasa katika wokovu, hiyo ni kidokezo kidogo sana, kitakuja kujidhihirisha katika utimilifu wote kwenye huo ulimwengu ujao, Huna hofu ya mauti tena kama zamani kwasababu maisha yako yapo mikononi mwa Bwana, unatumaini sasa la uzima wa milele baada ya kifo, hapo umeonja uzima ambao unakuja huko mbeleni ambapo huko kutakuwa hakuna kufa.

Lakini kwa jinsi tunavyoukaribia mwisho basi fahamu kuwa ndivyo zile nguvu za ulimwengu ujao zitakavyozidi kuongezeka, na kuwa dhahiri katikati ya watu, unapoona wafu wanafufuliwa unadhani ni picha gani hapo Mungu anakuonyesha?,

Yapo mambo ambayo Mungu atakwenda kuyaachia siku hizi za mwisho yahusianayo na nguvu hizi za ulimwengu ujao ili kutimiza ule unabii wa Yoeli 2:28. Na jambo ambalo tutamalizia nalo ni kubadilishwa kwa miili yetu na kuvaa kutokuharibika yaani miili ya milele

1Wakorintho 15.53 “Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.

54 Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda”.

Hivyo Bwana anatazamia kuiona Imani thabiti ndani ya watu wake, Imani ya kumwamini Yeye mpaka kufika hatua ya mauti kumezwa na uzima, hayo ni mambo ya ulimwengu ujao lakini ni sharti yaonekane sasahivi,ni sharti yaanzie hapa kwanza..Na ndio maana Bwana Yesu alisema….Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;

26 naye KILA AISHIYE na kuniamini HATAKUFA KABISA hata milele. Je! Unayasadiki hayo? (Yohana 11:25).

Unaona hapo?, yeye aishiye, na sio yeye aliyekufa..Hivyo tunapaswa tufikie kimo cha kumwamini huyu Bwana wa uzima, sisi tunaoishi sasa mimi na wewe, mpaka tuvionje vipawa hivi vya kutokuonja mauti kabisa, Henoko alivifikia kabla ya wakati, Eliya alivifikia kabla ya watu, lakini sisi tulio karibu kabisa na zamani zijazo, ndio tunapaswa tuvifikie, na watakaofikia Imani hiyo ndio wale watakaokwenda na Bwana kwenye UNYAKUO.. Itafika wakati kanisa litafikia hicho kiwango cha mauti kutokuwa na nguvu, litakapofikia hicho kiwango ndio unyakuo utakuwa umefika.

Je! mimi na wewe tumejiandaje?. Tunasema tunangojea Bwana, je! imani yetu kwake ina nguvu ya kuvuta mambo yajayo?..je! na wewe utakuwa miongoni wa watakaokuwa na imani ya kunyakuliwa?

Luka 18: …walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?

Mungu atusaidie sote.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments