JINSI YA KUITUMIA VYEMA NEEMA YA MUNGU ILIYO JUU YANGU.

JINSI YA KUITUMIA VYEMA NEEMA YA MUNGU ILIYO JUU YANGU.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze neno la Mungu, ambalo litatutoa sehemu moja hadi nyingine kiroho..Kama Daudi anavyosema..“Neno lako limesafika sana, Kwa hiyo mtumishi wako amelipenda. (Zaburi 119:140)”..Neno la Mungu ndio chakula chetu, ndio silaha yetu na ndio ngao yetu. Biblia inasema Neno la Mungu ni kama upanga wenye makali pande zote mbili, sio upande mmoja kama haya mapanga tunayoyajua sisi, bali una makali pande zote mbili mfano wa SIME, linakata kuwili.

Waebrania 4: 12 “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote UKATAO KUWILI, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.

13 Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu”.

Mtu akichomwa na kisu cha kawaida tumboni au kifuani kitaishia kwenye utumbo tu au mapafu, lakini Neno la Mungu ambalo ni kama upanga, biblia inasema linachoma na kuingia mpaka kwenye viungo vyote vya mwili…na mafuta yaliyo ndani yake, mafuta yaliyozungumziwa hapo ni mafuta yanayotengenezwa ndani ya mifupa (bone marrows), katikati kabisa ya mifupa mikubwa panapotengenezwa chembechembe hai za damu nyeupe, ndipo mafuta hayo yanapotengenezwa, Neno la Mungu kote huko linapita..Na aliishii kupenya huko tu…biblia inazidi kutuambia linapenya hata kizifikia nafsi na roho mahali siri za moyo zinapositirika, na linakata kata na tenganisha na kuharibu kabisa.

Kwahiyo unaweza ukaona Neno la Mungu ni silaha kubwa kiasi gani kama tukiweza kulitumia…

Lakini leo hatutaingia sana huko, bali tutajifunza somo la JINSI YA KUITUMIA VYEMA NEEMA YA MUNGU ILIYO JUU YAKO.

Kwanza ni muhimu kufahamu nini maana ya Neema, NEEMA ni kitu mtu anachopewa ambacho hakustahili kuwa nacho..tafsiri yake inakaribia sana kufanana na ZAWADI lakini sio zawadi..Neema tafsiri yake ni ya ndani kabisa..kwasababu zawadi mtu anapewa kwasababu kafanya kitu fulani kizuri…lakini Neema haiko hivyo, neema ni kitu mtu anapewa pasipo kustahili…kwamfano mtu anaweza kupewa nafasi ya kusomeshwa bure na serikali au mtu binafsi kwasababu pengine huyo mtu hana uwezo wa kujisomesha, au pengine amefaulu sana hivyo anapewa kama offer fulani ya kusomeshwa bure…Lakini Neema haipo hivyo, neema ni pale mtu anapewa nafasi ya kusomeshwa bure pasipo kuangaliwa yeye ni tajiri au ni maskini, au ana uwezo fulani au hana uwezo, amekidhi vigezo au hajakidhi. Hiyo ndiyo tunaweza kusema ni NEEMA.

Na kipawa cha Neema sisi wanadamu hatuwezi kuvitoa, ni ngumu sana kuvitoa kwasababu mara nyingi tunaangalia hali ya mtu ndipo tunamsaidia…Ni nani leo anaweza kwenda kutoa shamba lake na kumpa bure tajiri namba moja duniani? Kwa nia ya dhati kabisa na sio ya kujipendekeza?.. na baada ya kumpa anasahau?..utagundua hakuna au ni wachache sana wanaoweza kufanya hivyo wengi watakwambia..aa kama ni wema si afadhali ningeenda kumpa hilo shamba maskini fulani, kuliko  kumpa huyu mtu ambaye tayari ana mamilioni ya fedha, ndivyo mioyo yetu ilivyo sisi wanadamu. Lakini kwa Mungu haipo hivyo, NEEMA yake haina mipaka…haiangalii huyu ni tajiri au ni maskini, haiangalii huyu ni anacho au hana, anastahili kuwa nacho au hastahili.

Ndio maana wokovu na wenyewe ni NEEMA. Ingekuwa Mungu anaangalia hali fulani mtu aliyonayo ndio ampe wokovu, watu wengi wangeukosa..Tunaokolewa kwa NEEMA. Hakuna hali fulani tuliyonayo iliyomshawishi Mungu kutuokoa sisi zaidi ya NEEMA YAKE, …Ni buree kabisa tumeokolewa pasipo sababu. Sio kwa matendo yetu mema tumeokolewa, si kwa kusali kwetu sana tumeokolewa. Hapana.

Waefeso 2:8 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;

9 wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu”.

Kwahiyo kama NEEMA ipo hivyo basi sio kitu cha kujisifia, kwasababu hakuna mtu kwa ajili ya sababu ndio amestahili au hakustahili kupewa.

Sasa Neema ya wokovu tumepewa wote, lakini pia kuna neema ya VIPAWA AU KARAMA, hii nayo ni vile vile, mtu hapewi kwasababu fulani fulani hivi..kwamba ni mtakatifu sana au kwamba si mtakatifu sana hapana! hii Mungu anampa mtu kama anavyotaka bila sababu yoyote na kama ni hivyo basi haipaswi kuwa ni ya kujisifia kwa namna yoyote, ukiona mtu anajisifia karama au kipawa, ujue huyo mtu bado hajauelewa UKRISTO hata kidogo, au ni mchanga sana kiroho.

Ukiona mtu anajisifia mimi ni mtu wa kusali sana, au mtakatifu sana, au nilimfanyia kitu fulani Mungu ndio maana naweza kufundisha, au ndio maana naona maono, au ndio maana ninaweza kunena kwa lugha, au ndio maana nina upako, nikimwekea tu mtu mikono anapona, tambua huyo mtu bado hajaelewa nini maana ya NEEMA, pengine atakuja kuelewa baadaye lakini kwa wakati huo anaojisifia bado hajaelewa maana ya neema.

Kwa ufupi Vipawa vya Mungu havitokani na juhudi zetu, baada ya kuamini tu na kubatizwa mtu unajikuta tu unapata uwezo wa kipekee katika kufanya jambo fulani la kimungu ndio hapo alikuwa hajui kama ana karama ya uponyaji, hivyo anapomwekea tu mtu mikono anapokea uponyaji n.k lakini sio jambo la kusema ni kwasababu fulani ndio maana ninao huu uwezo sasa..karama za Mungu sio zawadi kwamba tumefanya jambo fulani ndipo Mungu anatuzawadia kama pongezi, haiko hivyo karama za Mungu ni NEEMA unapewa pasipo sababu yoyote. Na Mungu anatoa jinsi anavyotaka yeye, huyu hivi yule vile.

Ukishindwa kuelewa hili, utajikuta unatamani kuwa kama mtu fulani ukidhani kuwa alifanya kajuhudi fulani mpaka kuwa vile, na unajikuta unashindwa kukaa katika nafasi yako, na kuanza kusifia watu, badala ya Mungu.

Sasa tukirudi kwenye kiini cha somo letu linalosema NAMNA YA KUITUMIA VYEMA NEEMA YA MUNGU ILIYO JUU YANGU, tutajifunza namna ya kuitumia vyema neema tulizopewa na kutuletea matokeo makubwa katika viwango vya kimbinguni.

Hebu tusome kwanza mistari ifuatayo na kisha tuendelee..

Luka 21 : 1-4

“1 Akainua macho yake akawaona matajiri wakitia sadaka zao katika sanduku la hazina.

2 Akamwona mjane mmoja maskini akitia mle senti mbili.

3 Akasema, Hakika nawaambia, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote;

4 maana, hao wote walitia sadakani katika mali iliyowazidi, bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo”.

Katika habari hiyo Bwana aliona makundi mawili ya watu: la kwanza ni yule mwanamke mmoja MASKINI, ambaye kwa NEEMA, Mungu aliyompa hakuwa na kingi, lakini alitoa vyote Na kundi la pili aliloliona ni MATAJIRI ambao walitoa sadaka katika sehemu iliyowazidia.

 

Katika mfano huu, tunaweza tukamfananisha yule mwanamke mjane na wale watu ambao Bwana amewapa vipawa vinavyoonekana kama ni vya chini kabisa katika kazi ya Mungu, ambapo kiuhalisia hakuna kipawa chochote kisichokuwa na umuhimu katika mwili wa Kristo kwamfano kuna wengine hawana kitu lakini utakuta siku zote kanisa lipo katika hali ya usafi, wanahakikisha usafi wa kanisa katika viwango vyote, wanajitoa katika viwango vyote…wengine kazi yao ni kusambaza nakala tu za Neno la Mungu ingawa hawana kitu, lakini kwa bidii zote wanajitahidi..Sasa hawa wanafananishwa na huyu mwanamke ambaye alitoa vyote alivyo navyo kwa Mungu.

Lakini kundi lingine linalojiona lenyewe ndilo la muhimu sana, pengine mchungaji, au nabii au mwalimu ambaye kila siku anaonekana pale madhabahuni akifundisha lakini haitumii karama yake inavyopaswa anaangukia katika hili kundi la pili la matajiri waliotoa katika sehemu ya mali iliyowazidi, kwasababu wao wanadhani kukaa kuonekana na kusifiwa na watu ndio hivyo hivyo ilivyo hata mbele za Mungu.

Sasa siku ya mwisho wale wa mwisho watakuwa wakwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho. Kwasababu katika utajiri wao hawakutoa vyote.

Na mimi leo nakwambia wewe unayesoma ujumbe huu USINIE MAKUU bali jishughulishe na mambo madogo, usitamani yaliyo makubwa wakati haya madogo huyafanyi yanavyopasa…katika haya haya madogo, fanya kwa bidii, toa vyote ulivyonavyo kwa ajili ya Bwana, toa muda wako wote kuhakikisha injili inakwenda mbele hata kama huna fedha, hiyo ndio thawabu yenyewe, usijilinganishe na wale wengine kwasababu Macho ya Mungu sio kama ya kwetu sisi wanadamu.

Usidanganyike na INJILI Kutoka kuzimu zinazosema, utafute kwanza mali ndipo umtumikie Mungu, ndugu yangu Mungu hakuhurumii umaskini wa mwili wako!! Ana uhurumia kwanza umaskini wa roho yako….Ingekuwa anauhurumia kwanza umaskini wa miili yetu, yule mwanamke mjane aliyetoa senti mbili pale pale angeanza kumuhurumia na kusemaa ooo maskini yule mwanamke asitoe chochote maana ni mjane na ni kile tu alichobakiwa nacho…lakini badala yake unaona Bwana alimwacha atoe vyote alivyo navyo kwa ajili ya roho yake, pingine hata chakula cha mchana bibi yule hakupata, ilimradi tu ahakikishe nyumba ya Mungu ipo katika hali nzuri…Bwana hakuuangalia umaskini wake wa pale…Bali aliuangalia UTAJIRI WAKE KATIKA MBINGU MPYA NA NCHI MPYA…Si ajabu tunaweza kwenda kumkuta kule mbinguni ameketi na Bwana katika kiti chake cha enzi.

Kwahiyo hiyo achana na INJILI ZA MAFANIKIO YA KUZIMU!!... injili za kuonyeshwa milki zote za dunia ndani ya dakika moja, Zile shetani alizomuhubiria Bwana Yesu na kumwambia NITAKUPA VITU VYOTE UKIANGUKA KUNISUJUDIA!!. Biblia inasema Bwana hatatupungukia kabisa,

Waebrania 13: 5 “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.

6 Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?”

Bwana atatupa utajiri kwa wakati wake na kwa kuchuma kidogo kidogo, sio za leo na kesho! Mithali 13:11.

Ni matumaini yangu kuwa NEEMA iliyo juu yako utaitumia inavyopaswa, utaitumia yote..pasipo kuangalia mazingira yoyote ya nje, kwasababu Bwana pia alikupa pasipo kuangalia hali yako. Na Mungu akubariki.

Kama hujampa Bwana maisha yako ayatawale, usipoteze muda, mlango wa Neema upo wazi, ila hautakuwa hivi siku zote, ni vyema ukafanya hivyo sasa, kwasababu saa ya wokovu ni sasa…usidanganyike kuwa watu hawaokoki leo, wokovu unaanzia hapa hapa duniani..hivyo kama Roho anakuhimiza kufanya hivyo sasa usikawie, unachopaswa kufanya ni kutubu dhambi zako zote kwa kudhamiria kuziacha, na baada ya kutubu kwako, basi haraka sana nenda katafute mahali utakapoweza kubatizwa ubatizo sahihi wa kimaandiko, yaani wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO, na Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi na kuielewa biblia, na hapo utakuwa umezaliwa mara ya pili.

Mungu akubariki sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine, print ikiwezekana na Bwana akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPPMada Zinazoendana:

USIMFANYIE JEURI ROHO WA NEEMA.

UMEIZALIA MATUNDA MIAKA 4 YA NEEMA ULIYOPEWA?

JIWE LA KUKWAZA

TABIA ZA ROHONI.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
John
John
11 months ago

John ntine

Imani Ruzamuka
Imani Ruzamuka
4 years ago

Asante sana