TABIA ZA ROHONI.

TABIA ZA ROHONI.

Shalom! shalom!, karibu tuongeze maarifa katika mambo yetu yahusuyo wokovu wetu hapa duniani. Wengi wanadhani mtu akiingia tu katika wokovu basi, akili yake huwa inafutwa na kugeuzwa kuwa kitu kingine cha kimbinguni, Na hivyo vitu kama wivu, hasira, ghadhabu, visasi, vinyongo, chuki, huzuni, hofu, vinakuwa vimeondoka kabisa ndani ya huyo mtu, Na ikionekana kuwa havijaondoka basi huyo mtu bado hajafanyika kiumbe kipya.

Mimi hapo nyuma niliomuomba sana Mungu aniondolee hivyo vitu ndani yangu, kwasababu nilikuwa ninachukia ninapoona hasira inakuja ndani yangu na mimi ni mkristo, wakati mwingine hofu Fulani,.hayo yalinifanya nijione kama bado sijawa mkristo. Lakini baada ya kuona ninaomba sana viondoke bila ya kuona mafanikio yoyote, ndipo Mungu akanifumbua macho yangu ya ndani nikaona…

Nikaja kugundua kuwa nilikuwa ninamuomba Mungu aniondolee vitu ambavyo ameniumbia ndani yangu, na kama hiyo haitoshi, yeye mwenyewe anavyo…Nikafikiria nikasema ni kweli ukitafakari utaona Mungu anao wivu, amejitaja mwenyewe kuwa yeye ni Mungu mwenye wivu (Kutoka 20), amejitaja kuwa yeye ni Mungu mlipiza kisasi, amejitaja yeye ni Mungu mwenye hasira nyingi na ghadhabu, isitoshe amejionyesha sehemu nyingi kuwa anahuzunika wakati mwingine,..Sasa kama hivyo vitu vipo ndani yake kwanini mimi nimwombe aniondolee?..Na yeye katuumba sisi kwa mfano wake, biblia inasema hivyo.

Kiuhalisia vitu hivi Mungu hakuviumba kwa ubaya ndani yake na ndani ya watu wake, bali ni kwa nia njema kabisa na ya Upendo. Embu jaribu kufikiria kama mtu asingekuwa na wivu hata kidogo kwa mpenzi wake, inamaanisha kuwa hata angemwona mtu mwingine anam-baka mke wake, asingeshuhulika kufanya lolote angemwacha tu, kwasababu ndani yake hakuna chembe chembe za wivu, ambazo hizo zingemsaidia kumpigania mke wake asifanyiwe kitendo kama kile..

Jaribu pia kufikiria kama mtu asingekuwa na hofu ndani yake, angeweza hata kwenda kuchukua kisu na kumchoma mtu mwingine, au angeweza hata kwenda kusimama juu ya ghorofa refu na kujitupa chini, kwasababu ndani yake hakuna hofu ya kuogopa chochote, unadhani tungekuwa na madhara mengi na makubwa kiasi gani duniani?. Jamii zetu zingesimamaje?

Au fikiria ungekuwa hauna hasira hata kidogo ungekuwa wewe ni wa kuonewa au kuudhiwa tu kila saa, au unadhulumiwa haki yako, lakini kama mtu akiona umekasirika, ataogopa na kuacha kile alichokuwa anakifanya kwasababu anajua akiendelea madhara yoyote yanaweza kumtokea..Hivyo unaona hasira hapo inasimama kama ulinzi kwa mtu asionewe au asidhulumiwe au asiudhiwe.

Vivyo hivyo na vitu kama ukali, na vinginevyo. Ni mambo ambayo Mungu ametuumbia ndani yetu, ili yatumikie katika mahali papasapo,..Lakini leo hii ni kwanini tunaona , Wivu ni kitu kibaya, hasira ni kitu kibaya, kisasi ni kitu kibaya, chuki ni kitu kibaya, kinyongo ni kitu kibaya….Ni kwasababu tunavitumia mahali ambapo Mungu hakutaka vitumike na ndio hapo vinaonekana kuwa ni vitu vibaya visivyofaa kuonekana ndani ya mtu yeyote.

Embu tuangalie mfano wa wivu mzuri, Tuchukulie mfano wa Bwana wetu Yesu, yeye kuna wakati alishikwa na WIVU wa kushindwa kuvumilia mpaka kufikia hatua ya kuleta madhara na vurugu..Hayo yalitokea pale alipokwenda Hekaluni na kukuta watu wanafanya biashara mahali ambapo pangepaswa pawe mahali pa Ibada…ndipo tuona akapindua mezi zile na kuwachapa wale waliokuwa wanafanya biashara mule ndani. ..Mpaka wanafunzi wake wakakumbuka kuwa iliandikwa hivyo (Yohana 2:17 ….Wivu wa nyumba yako utanila.).

Unaona huo ni mfano mzuri jinsi wivu ulivyotumika jinsi ipasavyo. Lakini tujiulize ingekuwa na sisi tupo pale na yeye je! Tungeshirikiana naye kufanya kile kitendo? Ni rahisi kusema ndio. Lakini ikiwa leo hii tunaona Injili ya YESU KRISTO Bwana wetu inageuzwa na kuwa taasisi za kibiashara, na hakuna chochote kinachotukuna ndani yetu?..Badala yake wivu wetu unajidhihirisha katika mambo mengine yasiyokuwa na umuhimu sana, pale tunapoona wafanyakazi wenzetu wanatuibia ofisini, ndio tunakuwa na wivu, pale tunapoona mafisadi wanaaiibia  nchi, wanapitisha magendo, ndio tunazungumza mpaka mshipa ya shingo inatutoka, na kibaya zaidi pale tunapoona majirani zetu wanafanikiwa, ndipo tunatafuta namna zote juu chini za kuwashusha ili wasiendelee mbele …

Sasa kama wivu wa namna hii ndio Mungu kaukataa, kama upo ndani yetu basi tujue umetumika isipovyopasa na hivyo unahesabika kuwa ni dhambi mbele za Mungu..Nguvu hizo hizo unazotumia kuhakikisha adui yako hafanikiwi kwanini usizipeleke mbele za Mungu wako kuhakikisha adui yako MKUU shetani hafanikiwi na kazi zake mbovu?..Kwanini tunaona kazi ya Mungu inachezewa na sisi tunakaa kimya, wachekeshaji wameingia mpaka madhabahuni wanamfanyia Mungu dhihaka na sisi tunafurahi pamoja nao,..

Halikadhalika KISASI ni kitu chema ambacho kimeumbwa ndani yetu ili kitimize kusudi Fulani..Na kusudi hilo si lingine zaidi ya kumpiga shetani. Fikiria Ulipokuwa katika dhambi ulivyokuwa unateseka na magonjwa, ulivyokuwa unateswa na nguvu za giza au mapepo au wachawi au jinsi ulivyokuwa unakesha Disco na kupoteza muda mwingi na pesa nyingi, hata kwa wiki mara mbili ukimwabudu shetani kule..Lakini sasa umekuwa mkristo, kuna kitu Fulani ndani yako unapaswa ukihisi kitu kama kisasi kumlipizia shetani kukupotezea muda wako, na kukutesa na mambo mabaya, Hivyo sasa utahakikisha muda wako hata kwa wiki mara tatu unakesha katika kumsifu Mungu na na katika kuomba nakuziharibu kazi za shetani katika kuwavuta watu kwa Kristo..Hicho ndio kisasi Mungu anachokitafuta, ulikuwa unaimba nyimbo za kidunia, sasa umeokoka ni wakati wa kumwimbia na kumsifu Mungu kwa nguvu zaidi kulipiza kisasi kwa vile shetani alivyokutenda..

Ulikuwa ni msengenyaji na mmbea wa kupelekea taarifa za watu kwa watu wengine mpaka mtaa wa tatu sasa umeokoka ni wakati wa kutumia kipawa kilekile kumlipizia shetani kisasi kwa kusambaza habari za Yesu kwa nguvu wa watu wengine zaidi ya pale ili kumkomesha shetani. Hivyo ndio visasa ambavyo Mungu anavihitaji.

Vivyo hivyo tumeumbiwa hofu. Ulikuwa unamwogopa shetani na wachawi kiasi kwamba hata wewe mwenyewe ulikwenda huko huko kumwomba akupe hirizi kama kinga yako. Lakini sasa umeokoka, ile hofu imerudi mahali ipasapo, itumie hiyo kumwogopa Mungu wako na sio adui yako tena..kama Bwana Yesu alivyotuambia

Luka12:5 “Lakini nitawaonya mtakayemwogopa; mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo.”

Hofu yako ikiwa kwa Mungu utaogopa kwenda kuzini, utaogopa kutukutana, utaogopa kusema uongo, utaogopa kufanya mambo maovu, kama  haipo hautamjali Mungu n.k.

Chuki iliyopo ndani yako, ndugu hiyo Mungu hakukuumbia kwa ajili ya kuwachukia ndugu zako, ni wazi kuwa huwezi kumwekea chuki mdogo wako au kaka yako au mama yako aliyekuzaa, utakuwa na chuki sana na Yule ambaye uliyemwona akimchoma mdogo wako moto bila huruma., Vivyo hivyo chuki hasaa ya ki-Mungu ipo ndani yetu kumchukia SHETANI pamoja na mapepo yake yote, na kazi zake zote, na sio wanadamu wenzetu ambayo hayo ndiyo yamekuwa sababu ya ndugu zetu wengi mamilioni kuwepo kuzimu leo hii.. Na hivyo kama hiyo chuki itatumika ndani yetu kisawasawa leo hii tutaweka mikakati kabambe ya kumwangamiza shetani na kazi zake kwa KUHUBIRI INJILI YA YESU KRISTO kwa watu wote.

Hivyo kwa kumalizia, ni maombi yangu kuwa vipawa vyote na tabia zote Mungu alizoziweka ndani yako, usiruhusu shetani azitumie vibaya kwa faida zake, bali badala yake, tuziteke zikaleta manufaa makubwa katika ufalme wa mbinguni. Leo hii usimwombe Mungu akuondolee hasira ndani yako, haitaondoka hiyo, ili uwe mfano wa Mungu lazima uwe nayo, badala yake pale inapokuja basi ukumbuke lile Neno kuwa je! Mahali ninapoiachilia ni mahali pafaapo, kama hapafai, moja kwa moja ikatae hiyo hali na yenyewe itatulia,. Lakini ikiwa ni sehemu ifaayo yaani ni sehemu yenye manufaa kwa ajili ya ufalme wa mbinguni na kumkandamiza shetani..basi usiizuie kwani hiyo imevuviwa na Mungu kutimiza kusudi lake.

Ubarikiwe sana na Bwana Yesu.

Kwa Maombezi, Ushauri, au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

HISIA YA MUNGU ILIYO MBAYA KULIKO ZOTE.

TUSIPOUTHAMINI WOKOVU TUTAPATAJE KUPONA?

JE! NI KWELI UMEMFUATA YESU?

KIFAA BORA CHA MATUMIZI.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments