HISIA YA MUNGU ILIYO MBAYA KULIKO ZOTE.

HISIA YA MUNGU ILIYO MBAYA KULIKO ZOTE.

Tabia hizi zote tunazozionyesha zitokazo ndani yetu kwa mfano, furaha, amani, upendo, hasira, ghadhabu, wivu, uchungu, huruma, n.k. asili yake sio sisi bali ni Mungu, kwasababu sisi tumeumbwa kwa mfano wa Mungu kama maandiko yasemavyo, hivyo hizi ni baadhi tu ya tabia ambazo Mungu mwenyewe alikuwa nazo kabla hata ya ulimwengu kuwako.

Sababu ya Mungu kuviruhusu vitu kama hivi vitokee ndani yetu, ni kutufundisha sisi kwa vitendo ili tuyajue mapenzi yake ni nini. Pale tunapoweza kuuhisi upendo au kuutoa upendo kwa wengine, basi tunafahamu kuwa yupo ambaye anayeitwa Upendo mwenyewe, na hivyo hiyo inatufanya sisi kuilewa vizuri asili ya Mungu tofauti na kama tungekuwa tumehadithiwa tu kuwa Mungu anatupenda halafu hatujawahi kuhisi upendo wowote ndani yetu, au hatujui upendo ni kitu gani. Ni wazi kabisa kuwa tusingemwelewa Mungu vizuri, na vivyo hivyo katika mambo mengine mema kama vile huruma, furaha, amani, faraja,fadhili, upole, unyenyekevu n.k. Yote hayo tusingeweza kuyapokea kutoka kwa Mungu kama asingetuonjesha mambo hayo ndani yetu sisi wenyewe pale tunapohudumiana sisi kwa sisi.

Lakini pia upo upande wa pili wa hisia hizo, ambao huo sio mzuri sana, na kila mwanadamu amepewa, kwamfano hasira sio jambo jema, na hasira huja kwa kuudhiwa, na tunajua hakuna mtu hata mmoja anayependa kuudhiwa, lakini hasira hutokea yenyewe ndani pale mambo kama hayo yanapokuja, si kwamba mtu anaitengeneza hapana, bali ni jambo ambalo linatokea lenyewe pale vitu kama maudhi au makwazo vinapozuka kinyume na matarajio yake, kadhalika na mambo mengine kama ghadhabu, uchungu, huzuni, sononeko n.k.

Lakini lipo jambo ambalo linafunika vyote katika hisia mbaya, kama vile UPENDO unavyofunika hisia zote nzuri, kadhalika katika upande wa hisia mbaya lipo jambo linalofunika hisia zote kwa ubaya na hili si lingine zaidi ya WIVU. Wivu nao unaweza kuja kwa sababu nyingi lakini wivu ulio wa kiwango cha juu ni ule wivu unaokuja kwasababu ya mpenzi (mke au mume).

Kwasababu kiwango cha juu kabisa cha hisia nzuri (yaani upendo) huwa kinatoka kwa mpenzi, kadhalika na kiwango cha juu kabisa cha hisia mbaya (yaani wivu), huwa kinatoka kwa huyo huyo mpenzi. Hasira inaweza kuleta madhara ya hasira, ghadhabu inaweza kuletea madhara ya ghadhabu peke yake, uchungu unaweza kuleta madhara ya uchungu pekee yake,lakini kitu kinachoitwa WIVU ni mbali sana na hivi vingine hicho kinajumuisha vyote humo humo, ni kiwango cha juu kabisa cha hisia mbaya kwa mwanadamu, na ndivyo ilivyo hata kwa Mungu, na sababu kubwa ya wivu ni USALITI.

Leo hii ni wazi kabisa kuona watu wakijiua, watu wakiua wengine, watu wakisaliti hata wazazi wao ndugu zao,kwa ajili ya wivu wa mpenzi, watu wakimkosea Mungu wakienda hata kwa waganga, watu wakilipiza visasi vibaya kwa sababu ya jambo dogo tu la wivu wa mapenzi, watu wanapigana kila siku kwa ajili ya jambo hilo, wengine wanafanya uhalifu n.k. Kwa ufupi pale mtu anapofikia kiwango cha juu sana cha wivu basi mtu huyo huwa anaamua kufanya jambo lolote lile bila kujali ni madhara mangapi anaweza kuleta katika jamii yake au kwake mwenyewe kwa tukio hilo. Kwasababu ni jambo ambalo limechanganyikana na hasira humo humo, uchungu humo humo, ghadhabu humo humo, huzuni humo humo na kila kitu, Hivyo ili watu kuepuka na hilo mapema kabisa kabla hawajingia katika vifungo vya ndoa, huwa wanaingia kabisa katika mapatano kuwa huko mbele hawataumizana kwa kusalitiana.

Na ndio maana biblia inasema katika:

Mithali 27: 4 “Ghadhabu ni kali, na hasira ni gharika; LAKINI NI NANI AWEZAYE KUSIMAMA MBELE YA WIVU”.

Mungu ameziweka hizo hisia makusudi ndani ya wanadamu ili waweze nao kumwelewa pale anaposema jambo Fulani ni chukizo kwake, wajue alimaanisha linamchukiza kweli kweli , anaposema MIMI NI MUNGU MWENYE WIVU (Kutoka 20:5). Wajue kuwa kwa jinsi ile ile wivu unavyokula ndani yao ndivyo unavyokula ndani ya moyo wa Mungu, Na hivyo inawapasa wachukue sana tahadhari kujiepusha nayo, kwasababu wasipofanya hivyo basi wao wenyewe watakuwa wamejiweka katika hatari ya kupatwa na madhara makubwa sana yatokanayo na wivu wake.

Katika agano la kale Mungu alikuwa anatiwa wivu pale anapokuwa anaona watu wake wanaacha kumwabudu yeye, wanageukia masanamu na kuyafanya kuwa ndio miungu yao, jambo ambalo alishawaonya tangu zamani kwenye zile amri kuu 10 akisema:

Kutoka 20: 2 “Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.

3 Usiwe na miungu mingine ila mimi.

4 Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini

duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.

5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, NI MUNGU MWENYE WIVU; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao”,.

Unaona lakini wengi wao hawakuijali hiyo hisia mbaya ya Mungu wakaendelea kufanya hivyo angali wanajua kabisa waliyokuwa wanayafanya sio sahihi. Matokeo yake ikawapelekea Mungu kuwapiga kwa mapigo ya kila namna, wanyama wakali, njaa, upanga,magonjwa ya kila namna, na mwisho wa siku wakaondolewa katika nchi ambayo Mungu aliwaambia itakuwa urithi wao milele, nchi ambayo Mungu aliwaapia itawazaliwa wenyewe, nchi ibubujikayo maziwa na asali. Lakini sasa imebalika na kuwa kinyume chake, kutokana na njia zao mbaya mbele zake.

Vivyo hivyo na katika agano jipya, kumbuka agano la kale ni kivuli cha agano jipya, mambo yale ambayo Mungu alikuwa anayachukia wakati ule ndiyo hayo hayo anaendelea kuyachukia hata wakati huu, na tena sasa hivi tunapaswa tuwe makini zaidi kwasababu Mungu ameuweka wivu wake kwa uwazi zaidi kuliko ilivyokuwa ameuweka katika agano la kale.

Kwani kipindi kile Wivu wale aliufunua tu katika mambo ya nje, kwenye ibada za sanamu za nje, lakini sasa sio tu zile za nje, bali pia na zile zinazotoka rohoni. Embu tuzitamaze kwa ufupi sanamu hizo.

1.SANAMU ZA NJE! ZA SASA.

1Wakorintho 10: 14 “Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.

15 Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo.

16 Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo?

17Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.

18Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu?

19 Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu?

20 Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani.

21 Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani.

22 AU TWAMTIA BWANA WIVU? Je! Tuna nguvu zaidi ya yeye?”.

Unaona hapo?, matambiko, na mila mtu asizozijua maana yake, unakuta mtu anakwenda kufanya huko kijijini kwake, hajui kuwa unafanya ushirika na mashetani badala ya Mungu, anakwenda kwenye ngoma na hivyo anamtia Mungu wivu kwa ibada hizo za masanamu anazozifanya, anakwenda kwa waganga, anakwenda kwa wasoma nyota. anaabudu sanamu za watakatifu waliokufa zamani (sanamu za bikira Maria, Mt Petro n.k), anafanya kazi katika makampuni ya pombe, au sigara, au ya biashara haramu au anauza hivyo vitu. Hizo zote ni ibada za sanamu na kibaya zaidi bado mtu huyo anajiita mkristo hujui kuwa anamtia Mungu wivu ambao huo hauzimwi kwa namna yoyote ile, isipokuwa mauti, biblia inasema ni NI NANI AWEZAJE KUSIMAMA MBELE YA WIVU?

2. SANAMU ZA NDANI.

Wakolosai 3:5-9

“5 Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, NDIYO IBADA YA SANAMU;

6 kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu.

7 Katika hayo ninyi nanyi mlitembea zamani, mlipoishi katika hayo.

8 Lakini sasa yawekeni mbali nanyi haya yote, hasira, na ghadhabu, na uovu, na matukano, na matusi vinywani mwenu.

9 Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake;”

Unaona hapo?, hata uasherati mtu anaoufanya ni ibada za sanamu, pornography ni ibada za sanamu, ushoga, usagaji, mustarbation, uasherati yote hayo ni ibada za sanamu mbele za Mungu, biblia inaendelea kusema matusi midomoni na lugha chafu, uovu, n.k. yote hayo ni ibada za sanamu na hivyo kwa hayo mtu anamtia wivu Mungu kila siku anavyozidi kuendelea kufanya. Na ghadhabu ya Mungu, inaujilia ulimwengu mzima kwasababu ya hayo.

Hivyo ndugu, tuikwepe ghadhabu ijayo kutokana na wivu wake, Kwasababu wivu huleta visasi hivyo tukae mbali na kisasi cha Mungu kila siku tuishi maisha ya kujitakasa ikiwa sisi ni wakristo.. Lakini kama upo nje ya ukristo (yaani hujampa Bwana maisha yako). Mungu pia hapendezwi na njia zako, ni heri ukageuka sasa, na kutubu angali muda upo, ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa na kwa jina la YESU upate ondoleo la dhambi zako, kisha Bwana atakupa Roho wake mtakatifu kukulinda na kukufundisha. Ni maombi yangu utafanya hivyo na Bwana akuangazie Nuru yake.

“Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu.( 1Yohana 5:21)”

Ubarikiwe.

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments