MARIAMU

MARIAMU

Inaaminiwa na wengi wetu kuwa Mariamu, mama, aliyemzaa Bwana wetu Yesu Kristo, alikuwa ni mwanamke wa kipekee sana, na aliyebarikiwa zaidi ya wanawake wengine wote, na kabla hajapata Neema ya kumzaa Bwana wetu Yesu Kristo alikuwa ni mtu mkuu sana, na anayependwa sana na aliyeheshimika sana…Lakini je! ni kweli maandiko yanasema hivyo?

Tukisoma maandiko kitabu cha Luka 1: 1.42 inasema  “akapaza sauti kwa nguvu akasema, UMEBARIKIWA WEWE KATIKA WANAWAKE, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa”.

Maneno hayo yalizungumzwa na Elizabeth, mama yake Yohana Mbatizaji baada ya kukutana na Mariamu, Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu akambariki na kumwambia UMEBARIKIWA WEWE KATIKA WANAWAKE.

Sasa jambo la muhimu la kuzingatia hapo ni hilo neno “KATIKA” Hakusema “kuliko wanawake wote” hapana bali “katika

Ikiwa na maana kuwa katika wanawake waliobarikiwa na yeye (Mariamu) ni mmoja wapo..na sio kwamba yeye kabarikiwa kuliko wote..

Wakati Fulani mwanamke mmoja alimtaja Mariamu kuwa kabarikiwa sana, mbele ya umati mkubwa wa watu na mbele ya Bwana Yesu, lakini Bwana alimrekebisha pale pale na kumwambia HERI walisikiao Neno la Mungu na kulishika..

Sasa maana ya neno heri ni  amebarikiwa yeye

Luka 11:27 “Ikawa alipokuwa akisema maneno hayo, mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia, Heri {limebarikiwa} tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya. Lakini yeye alisema, Afadhali, heri{wamebarikiwa} walisikiao neno la Mungu na kulishika”.

Kwa lugha nyepesi katika mstari huo tunaweza kusema “…Mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake akamwambia; amebarikiwa mwanamke Mariamu aliyekuzaa, lakini Bwana akasema amebarikiwa zaidi mwanamke Yule alisikiaye Neno la Mungu na kulishika”

Kwahiyo unaweza ukaona hapo ingekuwa Mariamu amebarikiwa kuliko wanawake wote, Bwana Yesu asingemkosoa huyu mwanamke aliyekuja Kumtangaza Mariamu hadharani kuwa ni mbarikiwa.

Na pia kumbuka Bwana  Yesu hakutabiriwa kutokea katika ukoo wa Mariamu, bali ukoo wa Yusufu Mumewe Mariamu..ndio maana ukisoma pale mwanzo wa kitabu cha Mathayo utaona ukoo wa Bwana Yesu Ulianzia kwa Ibrahimu na ukaishia kwa Yusufu mumewe Mariamu, na haukuanzia kwa Ibrahimu na kuishia kwa wazazi wake Mariamu. Hivyo unaweza ukaona ni neema tu Mariamu kumzaa Bwana.

Kwahiyo ni muhimu kufahamu hilo ili tusije tukamwona Mtu Fulani ni wa kipekee sana katika maandiko zaidi ya mwingine, Imefikia wakati watu wanamaabudu Marimu, bila hata hofu ya Mungu, mwanamuhisisha katika ibada zao na kumtolea shukrani kana kwamba yeye ni Kristo. Hata Nabii Eliya biblia inatuambia alikuwa ni mtu mwenye tabia moja na sisi (Yakobo 5:17). Mfano kama  biblia isingeandika vile leo hii si ajabu tungewaona watu wamemfanya leo kuwa ni mtu wa nne katika uungu wa  Mungu.

Ni YESU KRISTO,  peke yake aliye Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana ndiye aliyekuwa wa kipekee zaidi ya wengine wote duniani…

Sasa tukirudi kwenye kiini cha somo ambacho tutaona  ni jambo gani lililomfanya Mariamu, apate neema ya kumzaa Mwokozi wa Ulimwengu Yesu Kristo.

Awali ya yote Biblia takatifu haijaelezea maisha ya nyuma ya Mariamu kabla ya kumzaa  Bwana wetu Yesu Kristo..Lakini tukiyachunguza maandiko  kwa undani tunaweza tukapata dondoo chache za maisha yake ya nyuma jinsi yalivyokuwa..

Sasa kabla ya kumsoma Mariamu hebu tuwasome kidogo Wanawake wachache kwenye maandiko waliopewa neema ya kuzaa baadhi ya MASHUJAA..

Tukianza na mwanamke wa Kwanza wakati wa kipindi cha Waamuzi, aliyekuwa (Mke wa mtu mmoja aliyeitwa Manoa) Tunasoma hivi..

Waamuzi 13: 2 “Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; NA MKEWE ALIKUWA TASA, hakuzaa watoto.

3 Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini UTACHUKUA MIMBA, NAWE UTAMZAA MTOTO MWANAMUME.

4 Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi;

5 kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti”.

Mwanamke huyu ndiye aliyemzaa shujaa Samsoni…Sasa ukiyachunguza kwa makini maisha yake utagundua alikuwa ni Mwanamke aliyekuwa MNYONGE kwa sababu alikuwa tasa..wakati  wanawake wengine wana watoto yeye hakuwa na mtoto hata mmoja na umri wake umeshakwenda…Na inaelekea alikuwa katika hali hiyo kwa muda mrefu akimwomba Mungu usiku na mchana, na pengine alimwekea nadhiri Bwana kwamba endapo atapata mtoto wa kiume atampatia Bwana kama sadaka.  Hivyo aliendelea kubakia katika hali hiyo hiyo paka siku malaika wa Bwana alipomtokea na kumwambia atazaa mtoto wa kiume (Samsoni) ambaye atawaokoa watu wake Israeli na maadui zao. Huyu Samsoni biblia inasema alikuwa ni Mnadhiri wa Bwana tangu tumboni mwa mama yake.

Tukirudi tena kwenye maandiko tunamwona mwanamke mwingine aliyezaa Shujaa..Na huyu si mwingine zaidi ya Hana mke wa Helkana. Huyu naye hakuwa na mtoto kwa muda mrefu na zaidi ya yote, mke mwenza alikuwa akimtesa na kumchokoza mara kwa mara kutokana na hali yake ya utasa..Hivyo kwasababu ni mcha Mungu na alikuwa mwenye haki alimwekea Bwana nadhiri kwamba endapo atapata Mtoto wa kiume atamweka wakfu kwa Bwana maisha yake yote…na Bwana alimkumbuka akampa Neema ya kumzaa Nabii Samweli, aliyekuja kuwa nabii mkubwa sana Israeli na Mwamuzi. Na hivyo Bwana akautoa UNYONGE wake akampatia Faraja yake dhidi ya dhiki na mateso aliyokuwa anayapitia kwa muda mrefu.

Hivyo Hana alifurahi sana mpaka akazungumza maneno haya..

1 Samweli 2: 1 “Naye Hana akaomba, akasema, Moyo wangu wamshangilia Bwana, Pembe yangu imetukuka katika Bwana, Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu; Kwa kuwa naufurahia wokovu wako;

2 Hakuna aliye mtakatifu kama Bwana; Kwa maana hakuna ye yote ila wewe, Wala hakuna mwamba kama Mungu wetu.

2 Samwli 2:3 “Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani.

4 Pinde zao mashujaa zimevunjika, Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu.

5 Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula, Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha. Naam, huyo aliyekua tasa amezaa watoto saba, Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika.

6 Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu.

7 Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu.

8 HUMWINUA MNYONGE KUTOKA MAVUMBINI, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake”.

Ukisoma mstari wa 8 unasema “HUMWINUA MNYONGE KUTOKA MAVUMBINI Ikifunua kuwa hapo kwanza Hana alikuwa mnyonge lakini Bwana alimwinua kutoka mavumbini, alikuwa chini na sasa  Bwana kamwinua juu sana..alikuwa hana mtoto lakini sasa kamzaa shujaa Samweli n.k

Tukimtazama mwanamke wa Mwisho katika maandiko ambaye naye pia alizaa Shujaa…alikuwa ni Elizabethi aliyekuwa ndugu yake Mariamu. Huyu Elizabeth naye alikuwa ni Tasa, hakuwa na Mtoto mpaka alipokuwa mzee, yeye pamoja na Mume wake Zakaria walikuwa ni wacha Mungu.. Na zaidi ya yote mume wake alikuwa ni Kuhani hivyo walikuwa wakiomba dua usiku na mchana kuhusu hali yao..Siku moja malaika alimtoke Zakaria na kumwambia mkewe aliye Tasa atachukua Mimba, na atazaa mtoto ambaye atawarejesha wengi kwa Bwana.. Na huyu mtoto tunakuja kumwona si mwingine zaidi ya YOHANA MBATIZAJI, ambaye alitabiriwa kuja kwa roho ya Eliya..Shujaa wa Bwana aliyetabiriwa kuitengeneza njia ya Bwana. Habari yake inapatikana katika (Luka mlango wa kwanza wote).

Sasa tabia za wanawake wote hawa watatu,: Yaani Mke wa Manoa, Hana, pamoja na Elizabethi utaona kuwa walikuwa ni wanawake wanyonge na wacha Mungu, na watulivu, na waliodharaulika… Hakuna hata mmoja aliyekuwa na heshima katika jamii ya watu wake wanaowazunguka, walikuwa ni wanawake wasio na uzao, kwa mfano Hana, hakuwa na watoto lakini bado alikuwa anamcha Mungu, alikuwa hakosi zamu za kwenda kuabudu Yerusalemu…Hivyo kwa mienendo yao inayompendeza Bwana na ya utulivu, na ya kusubiri kwa muda mrefu, Bwana akawapa neema ya Kuzaa MASHUJAA..

Na sio hao tu, tazama maisha ya Sara ambaye alikuwa mgumba kwa miaka mingi, mwanamke aliyemcha Mungu na mume wake mpaka kufikia hatua ya kumwita mumewe bwana. Mwanamke aliyedharauliwa na wanawake wengine wote lakini yeye ndiye alikuyekuja kumzaa Isaka. Vivyo hivyo tunaowaona akina Rebeka mambo yale yale, Raheli ambaye alikuja kumzaa Yusufu, mambo yale yale n.k.

Sasa mpaka hapo tumeshaanza kupata picha ya MWANAMKE MARIAMU jinsi alivyokuwa naye alikuwa ni mwanamke wa dizaini gani?? Kwa kuwasoma maisha ya hao wanawake watatu waliotangulia unaweza ukapata picha kuwa Mariamu naye sio kwamba alikuwa ni mwanamke aliyekuwa na kila kitu, au aliyekuwa na heshima…Hapana! Utaona tabia yake na maisha yake ni lazima itakuwa yanafanana na hao wanawake watatu waliomtangulia… Inawezekana yeye hakuwa Tasa kwasababu alikuwa ni Bikira lakini alikuwa ni mjonge mahali Fulani.. alikuwa ni mwanamke aliyedharaulika…pengine familia yao ilikuwa inajulikana ni duni tu, na pengine ilikuwa haina jina…Pengine wabinti wenzake walikuwa wanafanikiwa na kuzaa watoto wenye sifa, yeye alijitunza tu! Alikuwa anachekwa kama Hana, alikuwa ni mdhaifu, na alikuwa hana umaarufu wowote, pengine alikuwa hana uzuri sana wa kuvutia kama mmojawapo ya wanawake wa kidunia waliokuwepo kipindi kile, lakini alikuwa mcha Mungu…

Lakini ulipofika wakati. Bwana akautazama unyonge wake..akamkirimia kumzaa SHUJAA WA MASHUJAA, na MFALME WA WAFALME haleluya!! Malaika wa Bwana akatumwa kama alivyotumwa kwa mke wa Manoa, akatumwa kama alivyotumwa kwa Zekaria Mume wa Elizabethi, akaambiwa atachukua mimba kwa uwezo wa Roho na kumzaa Bwana Yesu. Hivyo Bwana akawa amemwondolea unyonge wake, na yeye akajihisi ni mwanamke kati ya wanawake waliobarikiwa..ndio maana utakuja kuona akisema…

Luka 1: 46 “Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,

47 Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu;

48 Kwa kuwa ameutazama UNYONGE WA MJAKAZI WAKE. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa;

49 Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu.

50 Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi Kwa hao wanaomcha.

51 Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

52 Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; NA WANYONGE AMEWAKWEZA.

53 WENYE NJAA AMEWASHIBISHA MEMA, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu”.

Unaona anasema hapo “wanyonge amewakweza” ikiwa na maana kuwa hapo kwanza naye pia alikuwa mnyonge.

Ni jambo gani la kujifunza kwa Mariamu na wanawake hawa wengine?

Katika hali zao za Unyonge walimngojea Bwana na kumtumainia kwa saburi, na pili walijua Bwana ndiye anayeshusha na ndiye anayepandisha…Walipoona tabu nje! Bwana ndiye aliyekuwa kimbilio lao, Hana hakuzunguka kwa wapunga pepo kupata utatuzi wa tatizo lake, wala Elizabethi hakuwatafuta waganga wamtatulie tatizo lake la kukosa mtoto, walijua ni Bwana ndiye aliyewafunga matumbo yao na ipo siku yatafunguka..hivyo waliendelea kukaa katika njia zake..

Hakuna hata mmoja unaona akimlaumu Mungu katika hali yake ya unyonge aliyokuwa anapitia, wote walikuwa katika hali ya utulivu mpaka ulipofikia wakati wa Ahadi zao kutimia wote walizaa mashujaa..Ukimsoma pia Sara na Rebeka na Raheli na Ruthu aliyekuwa bibi yake Daudi..utaona jambo hilo hilo, wote walikuwa ni wanawake wavumilvu na hawakuiacha njia yao ya haki na mwisho wakazaa mashujaa.

Hivyo Dada/Kaka unayesoma ujumbe huu, ukitaka kuzaa Shujaa katika maisha yako epuka manunguniko, epuka njia za mkato, kubali kudharauliwa na kuwa mnyonge, kubali kuonekana sasa wewe ni mshamba katika Kristo,kubali kuonekana tasa usiyeweza kufanya chochote maadamu unamcha Mungu usiogope. kwasababu utafika wakati Bwana atalikumbuka teso la kijakazi wake kama Mariamu alivyosema.

Unapokosa kitu sasa usiwalaani waliokuwa nacho, wabariki,ukikosa mtoto sasa usiwalaani wanaokulaani, usizunguke kwa waganga, wala usiuache UTAKATIFU wako, ishi maisha yanayompendeza Mungu kila siku,ukijiepusha na mambo yote mabaya ya ulimwengu, kwasababu Mungu anao wakati wake na majira yake, na ukifika wakati Bwana atakufurahisha kama alivyomfurahisha Mariamu , atautoa unyonge wako kama alivyoutoa wa Mariamu na wengine.

Isaya 54: 1 “Imba, wewe uliye tasa, wewe usiyezaa; paza sauti yako kwa kuimba, piga kelele, wewe usiyekuwa na utungu; maana watoto wake aliyeachwa ni wengi kuliko watoto wake yeye aliyeolewa, asema Bwana”.

Bwana akubariki.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

MIRIAMU NI NANI

DHAMBI ILIYOMKOSESHA SHETANI:

JINSI MWISHO ULIVYOKARIBIA.

MANA ILIYOSHUSHWA KUTOKA MBINGUNI.

VIGEZO VYA KUWA KARIBU NA YESU KRISTO KATIKA ULIMWENGU UJAO.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
4 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Getrude Charles
Getrude Charles
1 year ago

Amina Mtumishi wa Mungu, zidi kubarikiwa kwa kututia moyo watumishi wa Kristo Yesu.

Agnes Richard
Agnes Richard
3 years ago

Nimebarikiwa na maandiko haya

Mohamed kassim
Mohamed kassim
3 years ago

Be blessed bro.
Samahani unakijua kile kitabu kinachohusu namna au historia kuhusu mateso waliyopata kanisa la mwanzo????