UHURU WA ROHO.

UHURU WA ROHO.

Kama tunavyosoma biblia baada ya wana wa Israeli kuingia katika nchi ya Ahadi, hawakuwa na Mfalme, kila mtu alifanya jambo aliloliona ni jema machoni pake, ndivyo Biblia inavyosema katika…

Waamuzi 17: 6 “Siku hizo hapakuwa na mfalme katika israeli; kila mtu alifanya hayo aliyoyaona kuwa ni mema machoni pake mwenyewe”.

Lakini tunasoma pamoja na kuwa hawakuwa na Mfalme wala serikali yoyote inayotawala juu yao, waliishi kwa amani na Furaha, hakukuwa na mtu aliyemtawala mwenzake, wala aliyekuwa juu ya mwenzake, wote walikuwa sawa. Na walikaa katika hali hiyo kwa mamia ya miaka kwasababu ndivyo Bwana Mungu alivyopenda waishi katika hali hiyo, kwamba asiwepo aliye mkuu zaidi ya mwingine, yeye Bwana ndiye atakayekuwa Mkuu kwao na Mfalme wao.

Unaweza ukajiuliza leo hii mfano Taifa lisiwe na Raisi, wala mawaziri, wala serikali ya uongozi, litakuwaje!! kwamba kila mtu anafanya kile akionacho kuwa ni chema machoni pake, Ni wazi kuwa Taifa la namna haliwezi kusimama, ni taifa litakalo jaa vurugu, mauaji, dhuluma, uonevu, ubeberu, na mambo mengine mabaya yataonekana tu, kwasababu hakuna viongozi juu yao..

Lakini haikuwa hivyo kwa Wana wa Israeli, baada ya kutoka Misri, hawakuwa na Mfalme wala Raisi, wala mawaziri, lakini walikaa kwa utulivu na kwa utaratibu.. Kwasababu Mungu mwenyewe alikuwa katikati yao kama Roho Mtakatifu (Mfalme wao asiyeonekana kwa Macho). Akiwaamua na kuwaongoza katika utulivu na uhuru..kwa namna isiyoweza kuelezeka na kuchunguzika Ndio maana biblia inasema katika…

2 Wakoritho 3:17 Basi “BWANA” ndiye Roho; walakini ALIPO ROHO WA BWANA, hapo ndipo PENYE UHURU.”

Nataka uone hapo maandiko yanaposema kuwa “BWANA NDIYE ROHO”…Ikimaanisha kuwa Roho Mtakatifu ndiye Bwana Yule Yule, sio nafsi nyingine ya tatu hapana ni Yule Yule Bwana..Hata katika hali ya kawaida huwezi kumtenganisha mtu na Roho yake, wewe na Roho yako ni kitu kimoja, Roho yako sio nafsi yako ya tatu hapana! Roho yako ni wewe mwenyewe! Ndio maana na hapa maandiko yanasema “BWANA NDIYE ROHO” Na hakuna mahali popote katika maandiko matakatifu yamemtaja kuwa Mungu ana nafsi tatu. Hapana Mungu ni mmoja ana nafsi moja na Roho yake ni moja..Ndio maana na sisi wanadamu hatuna nafsi tatu, bali tuna nafsi moja, na Roho moja na mwili mmoja kwasababu katuumba kwa mfano wake na sura yeke yeye mwenyewe mwenye nafsi moja na Roho moja na mwili mmoja.

Sasa Kumbuka “BWANA NDIYE ROHO”… Roho Mtakatifu ndiye Yule Yule Yesu Kristo akifanya kazi katika Roho,..alipokuwa hapa duniani alikuwa anafanya kazi katika mwili, lakini ili kwamba ajiletee faida kubwa zaidi ilimpasa aondoke ili aje tena katika roho..ndio maana utaona alisema “bado kitambo kidogo hamnioni na tena bado kitambo kidogo mtaniona”, akimaanisha kuwa atakuja tena kwetu kwa njia nyingine bora zaidi itakayomfanya aingie ndani yetu, na ndio hiyo njia ya Roho, ambayo ndio ukamilifu wake kwetu sisi .

Na tukisoma pia kitabu cha Ufunuo mlango wa pili na wa tatu, tunaona Bwana Yesu Kristo akitoa ujumbe kwa Yale makanisa saba, Lakini mwanzo wa kila kanisa utaona anajitambulisha kuwa ni Bwana Yesu ndiye anayezungumza maneno yale lakini mwisho wa ujumbe utaona anasema “Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.”.. Hebu tuchukue mfano wa kanisa moja la Thiatira.

Mwanzoni mwa ujumbe anasema Ufunuo 2:18-19 “Haya ndiyo anenayo Mwana wa Mungu,[YESU KRISTO] yeye aliye na macho yake kama mwali wa moto, na miguu yake mfano wa shaba iliyosuguliwa sana. Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza.”..

Sasa huyu ni Bwana Yesu ndiye anayeyazungumza maneno hayo, lakini mwishoni mwa Barua hatuoni akimalizia kama alivyoanza, kwamba badala ya kusema “mwenye masikio na asikie neno hili ambalo Mwana wa Mungu anayaambia makanisa” badala yake anasema “mwenye masikio na asikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”.. Kwahiyo ni dhahiri kuwa “BWANA NDIYE ROHO” kama MTUME PAULO alivyosema.Hivyo ni muhimu kufahamu haya, ili kujiwekea vizuri msingi wa kumwelewa Bwana wetu Yesu Kristo na uweza wake, na utendaji kazi wake sasa katikati ya kanisa.

Lakini tukiendelea kwenye kile kipengele cha pili cha ule mstari kinachosema ““BWANA” ndiye Roho; walakini ALIPO ROHO WA BWANA, hapo ndipo PENYE UHURU.”

Nataka tukiangalie hicho kipengele kinachosema “ALIPO ROHO WA BWANA HAPO NDIPO PENYE UHURU”

Kwa kulinganisha na habari ile ya wana wa Israeli baada ya kutoka Misri, tunaona Bwana hakuwaweka chini ya Utumwa mwingine walipoingia kaanani, hakuwaweka tena chini ya wafalme kama farao, wala chini ya majemedari, wala hakuruhusu tena warudie maisha ya kiutumwa katika nchi ya Ahadi waliyokuwa wanaiendea. Bwana alikuwa Mfalme wao wa Amani, alikuwa katikati yao kama Roho. Akiwaweka katika utulivu, na uhuru wa hali ya juu. Bwana aliwalinda na roho mbaya za ugomvi, mateso, chuki, visasi, ubeberu, na maadui wote, fitina, dhiki, mashindano, ubinafsi…waliishi wote kama ndugu wa familia moja, na mataifa yote duniani yaliwaogopa kwa umoja huo uliokuwa katikati yao,..

Bwana aliwalinda kwa ile Hekima ya NZIGE, kama Mfalme Sulemani alivyoizungumza katika Mithali zake..Akisema nzige ni wadudu walio na akili nyingi sana.

Mithali 30: 27 “NZIGE HAWANA MFALME; Lakini huenda wote pamoja VIKOSI VIKOSI”.

Bwana aliwapa uhuru wa hali ya juu, kiasi kwamba kila mtu aliweza kufanya alilolitaka. Kulikuwa hakuna Taifa lingine duniani lililojiendesha bila mfalme, mataifa yote ya ulimwengu yalilishangaa Taifa la Israeli lenye mamilioni ya watu kipindi hicho linajiendesha pasipo mfalme na bado linafanikiwa kuliko mataifa yote, linapigana na maadui zake na kuwashinda.

Lakini tunaona maandiko yanasema baada ya miaka mingi kupita, kikainuka kizazi kingine ambacho hakikuutaka uhuru ule Bwana aliowapa na badala yake wakataka kuwa na Mfalme kama mataifa mengine, Na kwasababu walilisisitiza hilo jambo kwa nguvu Bwana akawapa haja ya mioyo yao, lakini hawakujua kuwa wamemkataa Bwana mwenyewe ambaye alikuwa katikati yao kama Roho awapaye uhuru, amani, furaha,upendo, raha na heri katika ile nchi ya Ahadi, wao wakataka uongozi wa kibinadamu…Japo Bwana aliwaonya kuwa mfalme watakayemchagua atatwaa binti zao na kuwafanya wajakazi wake, atatwaa mali zao na kuzifanya zake, atawalipisha kodi na atawashurutisha waishi kama wanavyotaka wao, lakini wao bado walimkataa Roho mtakatifu na kutaka uongozo wa wanadamu.

1Samweli 8:1-22

“1 Hata Samweli alipokuwa mzee, aliwafanya wanawe wawe waamuzi juu ya Israeli.

2 Na jina la mwanawe mzaliwa wa kwanza aliitwa Yoeli; na jina la wa pili Abiya; walikuwa waamuzi katika Beer-sheba.

3 Ila wanawe hawakuenda katika njia zake, bali waliziacha, ili wapate faida; wakapokea rushwa, na kupotosha hukumu.

4 Ndipo wazee wote wa Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama;

5 wakamwambia, Angalia, wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tufanyie mfalme atuamue, mfano wa mataifa yote.

6 Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba Bwana.

7 Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao.

8 Kwa kadiri ya matendo yote waliyonitenda tokea siku ile nilipowatoa katika Misri hata leo, kwa kuniacha mimi, na kwa kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokutenda wewe.

9 Basi sasa, isikilize sauti yao; walakini, uwaonye sana, na kuwaonyesha desturi ya mfalme atakayewamiliki.

10 Naye Samweli akawaambia wale watu waliotaka mfalme maneno yote ya Bwana.

11 Akasema, Mfalme atakayewamiliki ninyi atakuwa na desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka kwake, kwa magari yake, na kuwa wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya magari yake.

12 Naye atawaweka kwake kuwa maakida juu ya elfu, na maakida juu ya hamsini; na wengine atawaweka walime shamba lake, na kuvuna mavuno yake, na kufanyiza zana zake za vita, na vyombo vya magari yake.

13 Na binti zenu atawatwaa kuwa wafanyaji wa marhamu, na wapishi, na waokaji.

14 Atatwaa makonde yenu, na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni, yale yaliyo mazuri sana, ili awape watumishi wake.

15 Naye atawatoza ushuru wa mbegu zenu na wa mizabibu yenu, awape maakida wake, na watumishi Wake.

16 Atawatwaa watumishi wenu na wajakazi wenu, na ng’ombe zenu walio wazuri sana, na punda zenu, naye atawatia katika kazi zake mwenyewe”.

17 Atawatoza fungu la kumi la makundi yenu; nanyi mtakuwa watumwa wake.

18 NANYI MTALIA SIKU ILE KWA SABABU YA MFALME WENU MLIYEJICHAGULIA; BWANA ASIWAJIBU SIKU ILE.

19 Walakini hao watu wakakataa kuisikiliza sauti ya Samweli; wakasema, Sivyo hivyo; lakini tunataka kuwa na mfalme juu yetu;

20 ili sisi nasi tufanane na mataifa yote; tena ili mfalme wetu atuamue, tena atoke mbele yetu na kutupigia vita vyetu.

21 Samweli akayasikia maneno yote ya watu, akayanena masikioni mwa Bwana.

22 Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti yao, ukawafanyie mfalme. Kisha Samweli akawaambia watu wa Israeli, Enendeni kila mtu mjini kwake”.

Mstari wa 18 unasema ..“NANYI MTALIA SIKU ILE KWA SABABU YA MFALME WENU MLIYEJICHAGULIA; BWANA ASIWAJIBU SIKU ILE.

Unaona hapo?. Baada ya Israeli kujitwalia mfalme ndio ulikuwa mwanzo wa matatizo kwa taifa lile, tunakuja kusoma baadaye hao hao wafalme ndio waliokuwa wakwanza kuweka vinyago tena Israeli kama walivyokuwa kule Misri. Israeli ikaanza kudhoofika kidogo kidogo mpaka kufikia hatua ya Mungu kuchukizwa nao kwa sanamu zao na kutawanywa katika mataifa yote ulimwenguni.

Mambo hayo ni kivuli cha mambo yanayoendelea sasa, Mfalme wetu ni YESU KRISTO, ambaye hapo kwanza alikuja katika mwili, akatufundisha katika mwili, lakini sasa yupo katikati yetu katika ROHO anatuonya katika roho, anatuita kutoka katika utumwa wa dhambi na kutuingiza katika Uhuru wa Roho. Kwasababu BWANA NDIYE ROHO, na alipo Roho hapo ndipo penye uhuru.

Na kanisa leo limetoka katika kutawaliwa na ROHO MTAKATIFU na kuzama katika utawala wa kibinadamu, Sio Roho tena anaamua bali ni mitazamo ya wanadamu, sio tena karama za Roho zinazoongoza kanisa bali ni vyeo vinavyoongoza kanisa, kiasi kwamba ukiwa mchungaji mkuu, au kasisi, au padre, papa au shemasi, au askofu basi wewe unaweza ukasimama badala ya YESU KRISTO DUNIANI, Unaweza ukasamehe dhambi, unaweza ukawabariki watu katika dhambi zao, n.k..ndio maana hakuna, uhuru, umoja,wala amani, wala usafi,wala utakatifu ndani ya kanisa, kwasababu Kristo katupwa nje! Haiwezekani kupaa kama nzige, wakati kuna uongozi mwingine zaidi ya ROHO MTAKATIFU, Wana wa Israeli baada ya kumkataa Bwana kama Mfalme wao, ndio vyanzo vya matatizo yote ndani ya Taifa la Israeli vilipoanzia, wakaanza kujiweka watumwa wao kwa wao.

Kwahiyo Biblia inatuonya tutuoke huko, kwenye kamba za dini na udhehebu, zilizoacha uongozi wa Roho Mtakatifu (Yesu Kristo) na kuingiza uongozi wa wanadamu, Tumgeukie Mfalme wetu Yesu Kristo ambaye leo hii katika mwisho wa nyakati anatuonya “yeye aliye na sikio alisikie Neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”..Toka katika dhambi, rudi katika Neno, toka katika uvuguvugu ambao Bwana kasema atakutapika, toka katika ulevi, toka katika anasa za ulimwengu huu, rushwa, uasherati, usengenyaji, utukanaji, uuaji, ushirikina na mambo mengine yote yanayofanana na hayo..

2 Wakorintho 6 : 14 “…kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?

15 Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?

16 Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.

17 Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.

18 Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,”

Rudi katika kamba za kimadhehebu kwasababu hayo yote yameshahukumiwa. Tafuta Roho Mtakatifu kwasababu huo ndio MUHURI WA MUNGU. Biblia inasema hivyo katika waefeso 4:30, ikiwa na maana kuwa ukipokea Roho Mtakatifu ndani yako, basi wewe tayari ni kazi iliyokamilika. Mungu kashakutia alamu kuwa wewe ni wa kwake. Na pasipo Roho Mtakatifu hakuna uhuru wala hakuna unyakuo. Dini wala udhehebu havikuhakikishii hilo isipokuwa Yesu Kristo peke yake. Tubu leo uoshwe dhambi zako na Bwana atakupa Roho wake.

Bwana akabariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

SIRI YA KUASI KATIKA KANISA LA MUNGU.

UTAMBUE UJUMBE WA SAA UNAYOISHI.

ROHO ZILIZO CHINI YA MADHABAHU:

MWANZI ULIOPONDEKA.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments