CHAKULA CHA ROHONI.

CHAKULA CHA ROHONI.

Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze Maneno ya uzima, Leo hii ukimwuliza mtu yeyote aliye mkristo swali.. ‘chakula cha rohoni ni nini?’….atakujibu pasipo kusita sita kuwa ni NENO LA MUNGU. Na ndivyo ilivyo Neno la Mungu ndio chakula cha Roho zetu. Ni swali ambalo jibu lake linajulikana na watu wote.

Wapo wengi wanaofahamu umuhimu wa Neno la Mungu, lakini vile vile si wengi wanaofahamu kazi ya Neno la Mungu katika maisha yao ya hapa duniani na huko wanakokwenda.

Leo tutatazama kwa ufupi kazi ya Neno la Mungu juu ya maisha yetu ya kikristo.

Kwanza kabisa kama tunavyojua wengi wetu kuwa Neno la Mungu linafananishwa na chakula, na pia kama tunavyojua mtu hawezi kukua vizuri au kuongezeka kimo au unene pasipo kula vizuri..Moja ya kazi ya chakula ni kutufanya tukue kimwili na kuwa na afya njema.

Kadhalika katika roho, ili tusitawi katika roho vile ipasavyo ni lazima tule vizuri rohoni, na chakula hakiliwi mara moja kwa mwaka, vinginevyo utakufa, bali kinaliwa mara tatu kwa siku, angalau huo ndio tunaweza kusema ni mlo ulio sahihi.

Lakini licha ya faida mojawapo ya chakula ambayo ni ya kuukuza mwili, ipo pia faida nyingine ya muhimu sana ambayo wengi wetu hatuifahamu, au kama tunaifahamu basi hatuitilii maanani.

Na faida hiyo ni kuupa MWILI NGUVU.

Mtu anapokula chakula, kile chakula kinaingia tumboni, na kuchanganyikana na baadhi ya vimeng’enyo na kisha kuna baadhi ya hatua zinaendelea pale, kile chakula kinavunjwa vunjwa na hatimaye kunapatikana virutubisho ambavyo vinaweza kuupa mwili nguvu, ndio hapo mtu anapata nguvu ya kuweza kusimama, kutembea, kufanya kazi, kukimbia, kuongea, kuona n.k. kama alikuwa ni mtu wa mapambano vitani anapata nguvu ya kupambana vizuri zaidi na kushinda.

Na Neno la Mungu ni hivyo hivyo, halitusaidii tu kukua kiroho, kama wengi wetu tunavyojua, bali pia linatupa nguvu za kila siku zinazoweza kutusaidia kufanya kazi za kiroho, kusimama katika roho, kukimbia katika roho, kushindana katika roho na kushinda. Ndio maana mtu mwenye afya njema utakuta anakula mara tatu kwa siku na anakula mlo kamili. Na mtu wa namna hiyo ni ngumu kuwa mdhaifu au kushambuliwa na magonjwa.

Kadhalika ni wajibu wetu hata sisi kulitafakari Neno si mara moja tu kwa siku au kwa wiki, hapana hata ikiwezekana mara tatu au mara nne kwa siku, ili kujiweka katika hali ya kuwa na afya njema katika roho. Kwasababu nguvu za rohoni kila siku zinapungua na zinahitaji kuongezwa chaji kwa kula chakula kizuri cha roho…Mtu asikudanganye eti! Kuwa nguvu za rohoni, hazipungui au haziishi,!! Huo ni uongo ndugu!! Watu wote nguvu zao zinaisha kila siku kwasababu zinatumika katika roho kufanya shughuli nyingi..hivyo ni lazima kila siku ziongezwe na zinaongezwa kwa kula chakula cha rohoni (Neno la Mungu).

Ndio maana biblia inatuambie “yeye ajidhaniaye kuwa amesimama aangalie asianguke 1Wakorintho 10:12”..Ikiwa na maana kuwa tunajukumu kila siku la kujiongeza nguvu za rohoni. Hata vyombo vya elektroniki kama simu, hakuna kifaa kinachokaa na charge muda wote ni lazima kuna wakati kinakwenda kuongezewa nguvu kwa kuchajiwa…Watu tu wa imani nyingine katika mambo yao wanaweza kufanya dua mara tano kwa siku, lakini wakristo hatuwezi kufanya lolote.

Ni kwanini wakati mwingine mtu anashambuliwa na nguvu za giza?..Ni kwasababu nguvu zake za rohoni ni chache, kila kukicha wachawi wanakusumbua, na magonjwa ya ajabu ajabu yasiyofahamika chanzo chake..mengi ya hayo (ingawa sio yote) yanasababishwa na roho yako kutokula vyema. Mara ya mwisho ulikula wiki iliyopita unategemea vipi usiwe dhaifu?, usishambuliwe na wachawi?.

Nguvu za rohoni hazipatikani kwa kulisoma Neno siku moja na kwenda zako?, haiko hivyo kabisa, Tunahitaji kujifunza Maandiko kila siku ili tuishi. Hata kama tutarudia chakula kile kile kila siku ni afadhali kufanya hivyo kuliko kutokula kabisa.

Ni afadhali kurudia kile kile nilichojifunza jana na juzi kuliko kutoshika kabisa Biblia na kujifunza maandiko, ndugu zipo hatari nyingi sana za kutolitafakari Neno la Mungu.

Na dalili moja wapo ya kufa kiroho ni kutokusikia kabisa kiu ya KUSOMA NENO. Hiyo ni dalili kubwa sana ya kufa kiroho, kwasababu maiti siku zote haili, wala haisikii njaa. Lakini mtu ambaye yupo hai katika roho ni lazima kila siku asikie njaa ya kulitafakari Neno la Mungu kichwani mwake..Haiwezi ikapita siku au yakapita masaa kadhaa hajalitafakari kabisa Neno la Mungu kichwani mwake…hiyo haiwezekani…Ni lazima njaa itamsumbua tu! Na ataenda kutafuta njia ya kuishibisha roho yake kwa kuyasoma maneno ya Mungu ya Uzima.

Ili siku yako, mwezi wako, mwaka wako uende vizuri unahitaji Neno la Mungu rohoni mwako, ili roho yako iwe salama unahitaji kujifunza Neno la Mungu kila siku, ili ukue katika maarifa ya ki-Mungu na ili umjue yeye zaidi, Kujifunza Neno lake kila siku hakukwepeki. Hiyo ndio siri ya kuishi pasipo kusumbuliwa na shetani na kuendelea mbele, Ni kwa kula tu chakula kilicho sahihi.

Zaburi 119: 105 “Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu”.

Sikiliza maneno haya ya YEHOVA…

Kumbukumbu 11:18 “Kwa hiyo yawekeni maneno yangu mioyoni mwenu na rohoni mwenu; yafungeni yawe dalili juu ya mikono yenu, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yenu.

19 Nayo wafunzeni vijana vyenu kwa kuyazungumza uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.

20 Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako;

21 ili siku zenu zifanywe nyingi, na za vijana vyenu nao, juu ya nchi Bwana aliyowaapia baba zenu kuwa atawapa, kama zilivyo siku za mbingu juu ya nchi”. 

Wakolosai 3: 16 “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu”.

Ubarikiwe!

Kwa Maombezi, Ushauri, au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036613/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

NJAA IPO!, USIACHE KULA ASALI.

MANA ILIYOSHUSHWA KUTOKA MBINGUNI.

CHAKULA CHA ROHONI.

MAJI YA UZIMA.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Stany ndume
Stany ndume
1 year ago

Amen Mungu ni mwema Sana ,,,na website iyi ninzuri mnoh kwakujifunza Mambo yakiroho ,,,imenisaidiya Sana kukua kiroho ambayo sikujuwa nilifahamu kupitia website yenu Mungu awapendelee sanaaaa.

James Bwata
James Bwata
2 years ago

NABALIIWA SANA NA PAGE HII YA WINGU LA MASHAHIDI NA NAJIFUNZA MAMBO MENGI MAZURI SANA SANA BY PASTOR JAMES BWATA