Sasa utajuaje kusudi la aliyekuleta hapa duniani (Yaani kusudi la Mungu)..juu yako?
1) Kwanza Ni lazima umpate huyo aliyekuleta duniani, na namna ya kumpata huyo ni kwa kupitia kitu kimoja kinachoitwa MSALABA..Kwa kupitia YESU KRISTO, Hakuna namna nyingine yoyote utakayoweza kumjua Mungu nje ya huyu YESU KRISTO, Huo ndio ukweli ndugu yangu, na huyu unampata tu kwa kumwamini na kwa kutubu dhambi zako na kumgeukia yeye kikweli kweli, na kwa kubatizwa na kwa kupokea Roho Mtakatifu. Hapo utakuwa umempata huyu aliyekuleta ulimwenguni.
2) Baada ya kumpata kwa kubatizwa na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu, sasa moja kwa moja ataanza kuongea na wewe na kukuongoza katika lile kusudi alilokuitia duniani, hajakuleta hapa duniani bure bure tu! Wala hajakuleta hapa ili uwe mfanyabiashara, au uwe maarufu, au uwe milionea, hapana lipo kusudi lingine ambalo ndilo alilokuletea hapa, na hilo kusudi linafanya kazi kwa silaha alizoziweka ndani yako tayari (yaani karama aliyoiweka ndani yako), kwa kupitia huyu Roho wake Mtakatifu atakufunulia hilo kusudi, na ukishalijua hilo kusudi ndipo amani ya ajabu ya kuishi duniani itakujia, kwasababu umeshajua dhumuni la wewe kuletwa duniani. Na kusudi hilo ndilo litakalokufanya uishi kama mpitaji tu katika hii dunia, ukijua kuwa hapa duniani, sio kwako, ni kama umetekwa tu na umeletwa ili utimize kusudi Fulani, na huku ukijua kabisa aliyekuleta sio mjinga kwamba akulete humu duniani na kisha ashindwe kukuhudumia mahitaji yako ya mwilini, kwahiyo utakuwa unaishi kwa bajeti ya aliyekuleta, sio bajeti yako wewe, huku ukiangalia na kulitazama kusudi lake. Na lolote utakalolifanya ndani yake utafanikiwa.