NGUVU YA HEKIMA NA AKILI

NGUVU YA HEKIMA NA AKILI

Shalom Mtu wa Mungu, karibu tujifunze Maneno ya Mungu, Uzima wetu na Taa yetu ituongozayo katika njia sahihi ya kufika mbinguni…

Sulemani Mfalme wa Israeli mwana wa Daudi, Ni mtu aliyempendeza Mungu sana hata kufikia hatua ya kuambiwa aombe lolote naye atapewa…Tunaona Mfalme akachagua kuomba Hekima badala ya Mali, na Maarifa badala ya Ufahari na nguvu za kijeshi…sio kwamba alichagua hivyo kwasababu alikuwa hapendi utajiri au ufahari, hapana alikuwa anaupenda na kuutamani, lakini alipiga hesabu awe na utajiri na nguvu za kijeshi kuliko wafalme wote duniani, halafu akose akili ya namna ya kuwaongoza na kutatua matatizo ya watu wake itamfaidia nini?..Kwahiyo akaona jambo la kwanza la kuchagua ni akili na hekima kwanza , na hayo mengine yatafuata mbele ya safari kama yatakuwa na ulazima.

Hebu leo tupewe na sisi nafasi kama hiyo, Mungu atuambie tuombe lolote naye atatupa…Utaona wengi wetu mambo tutakayoyakimbilia kwanza, tupewe mali nyingi na utajiri ili tuishi kwa raha sisi na familia zetu, na ndugu zetu na ukoo mzima…Lakini ni wachache sana watachagua Mungu awape Hekima na akili za kuwapenda wenzi wao na ndugu zao, na akili na maarifa ya kuwalea watoto wao katika njia inayopasa kutokujali kiwango cha utajiri au umaskini walichonacho…Hilo ndio lingetakiwa liwe jambo la kwanza la kuomba kisha hayo mengine ndio yafuate..

Kwasababu itakufaidia nini, uwe na fedha nyingi na utajiri mwingi na kuwatimizia watoto wako mahitaji yote na Mwisho wa siku wanakuja kuwa mashoga au makahaba? Si ni afadhali wale chakula cha kawaida kila siku lakini ni matajiri wa akili na hekima, walizozipata kutoka kwako na mwisho wa siku watakapokuja kuwa wakubwa watakuwa msaada kwako na kwa wengine?..au itakufaidia nini uwe na mali nyingi na fedha nyingi lakini mke wako au mume wako haoni raha ya kuishi na wewe?..unapata mali lakini unakosa hekima ya jinsi ya kuishi na mume/mke. Hiyo ni hatari sana…

Ndio maana biblia inasema katika Mithali 16:16 “ SI AFADHALI KUPATA HEKIMA KULIKO DHAHABU? NAAM, YAFAA KUCHAGUA UFAHAMU KULIKO FEDHA.” ..Hayo ni maneno ya mtu aliyekuwa tajiri kuliko wote duniani anakushauri hivyo, kwasababu yeye ameyapitia mengi na kuyaona mengi…Ni afadhali na Njiwa wanakaa kwenye viota vilivyotengenezwa na nyasi lakini upendo wao ni wa milele, kuliko kuishi kwenye kasri ambalo ni malumbano kutwa kuchwa.

Mhubiri 4:6 Heri konzi moja pamoja na utulivu, Kuliko konzi mbili pamoja na taabu; na kujilisha upepo.

Sulemani aliliona hilo akachagua Kuwa na Hekima, ambayo hekima hiyo biblia inasema ilizidi ikapita mpaka wana wote wa Mashariki,

1 Wafalme 4: 29 ‘Mungu akampa Sulemani hekima, na akili nyingi sana, na moyo mkuu, kama mchanga ulioko pwani.

30 Hekima ya Sulemani ikapita hekima ya wana wote wa mashariki, na hekima zote za Misri.

31 Kwa kuwa alikuwa na hekima kuliko watu wote; kuliko Ethani Mwezrahi, na Hemani, na Kalkoli, na Darda, wana wa Maholi; zikaenea sifa zake kati ya mataifa yote yaliyozunguka.

32 Naye akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano.

33 Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki.

34 Wakaja wa mataifa yote ili waisikie hekima ya Sulemani, toka wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamepata habari za hekima yake”.

Aliona kuliko awe tajiri kama baba yake na kuwa na nguvu nyingi za kijeshi kama baba yake halafu kila kukicha ni kutokuwa na maelewano ndani ya nchi yake, kila kukicha kupambana vita na maadui zake, aliona huo ni udhaifu mkubwa sana…akamwomba Mungu ampe hekima na akili ya namna ya kutawala, na Mungu akampa…Ndio maana utaona Sulemani hakukumbana na vita yoyote kama baba yake, lakini utawala wake ulikuwa na nguvu kuliko wa Daudi baba yake..hakushika upanga kwenda vitani lakini Maadui zake walikuwa wanamwogopa. Hakumuua Goliathi kwa upanga wala kwa kombeo, lakini Wafilisti walimwogopa. Kwa ufupi hakuna mtu aliyekuwa anadhubutu kupanga vita juu ya Sulemani kwasababu walikuwa wanamwogopa na wanamheshimu. Kwa hekima yake ya kutatua mambo. Alikuwa anao uwezo wa kusulihisha mambo mengi ikiwemo vita kabla hata halijafikia katika vilele vyake, kwa hiyo hekima ambayo Mungu alimpa.

Hivyo ndivyo Sulemani alivyokuwa anatawala, na kwasababu alikuwa hapambani vita, hakutumia gharama zozote vitani, na hivyo uchumi wake ulikuwa unakuwa kwa kasi, tofauti na Baba yake Daudi au Sauli, wao kukitokea ugomvi ni rahisi kuingia kwenye mapambano pasipo mazungumzo, kwasababu walikuwa wanaamini Mungu kuwa amewapa vyote na maadui zao watakuwa chini yao siku zote, kila watakapokanyaga kama ni mapenzi ya Mungu, Mungu atawamilikisha na kweli ndivyo ilivyo, Mungu alikuwa na Daudi kila mahali alishinda vita nyingi..Lakini walitumia gharama nyingi zisizokuwa na maana na muda mwingi vitani jambo ambalo lingeweza kusulihishwa kwa njia ya hekima au akili, ndio maana unaona haikuwa hivyo kwa Sulemani, Mungu alimshindia vita Sulemani pasipo kupambana vita, alimpa Hekima kama Silaha yake badala ya mapanga na nguvu. Haleluya!!.

Ndugu Hekima ni silaha kubwa sana…Ndio maana utaona ni kwanini mtu mmoja anakaa na mke wake au mume wake mwenzi mmoja au mwaka mmoja wameachana, na mwingine hana fedha wala si tajiri lakini wameishi na mwenzi wake miaka zaidi hata ya 40 na bado wanapendana na kuvumiliana, ni kwasababu ya hekima iliyopo ndani ya hao wawili..Sio kwamba hawajawaji kukosana kabisa, wanakosana lakini kila kukitokea kutokuelewana kidogo tu! Mmoja wao anatumia hekima ya kiMungu kutatua hilo tatizo kabla hawajafika mbali kabla hawajakwenda kumwambia mama mkwe au babamkwe au marafiki, hekima iliyo ndani yao inawapeleka kwenye unyenyekevu, upendo, uvumilivu, ustaarabu, kusitiriana, kuchunguza jambo kabla ya kuchukua hatua, kujaliana, kusameheana nk.

Lakini hao wengine waliokosa hekima utaona kukitokea tatizo kidogo tu! Moja kwa moja mguu wa kwanza ni kwa marafiki na mashosti kuwaelezea kinachoendelea kati yao na wenzi wao..Na ndio huko huko shetani anapata nafasi wanapata ushauri wa kipepo wa kuachana na kuaibishana wakati mwingine, na mwisho wa siku ndoa inavunjika. Na sio tu katika Nyanja ya ndoa, bali katika Nyanja zote za maisha Hekima ni silaha kubwa.

Ndugu kama haya yanaendelea kwako, achana na hayo maombi unayoomba au unayoombewa kila siku ya mafanikio ya biashara yako na kazi yako, anza kuomba hekima..Biblia inasema..

Mithali 16:16 “ SI AFADHALI KUPATA HEKIMA KULIKO DHAHABU? NAAM, YAFAA KUCHAGUA UFAHAMU KULIKO FEDHA.”

Ukiona matatizo kama hayo yamekutokea na unashindwa namna ya kuyatatua ni dhahiri kuwa umepungukiwa hekima na sio kingine..Na kupungukiwa hekima sio dhambi, ni udhaifu tu ambao kila mtu anazaliwa nao, na hivyo unaweza ukaondoka endapo mtu akitaka uondoke!..Kwahiyo unachotakiwa kufanya ni KUOMBA HEKIMA KWA MUNGU!.

➽Yakobo 1: 15 ‘’LAKINI MTU WA KWENU AKIPUNGUKIWA NA HEKIMA, NA AOMBE DUA KWA MUNGU, AWAPAYE WOTE, KWA UKARIMU, WALA HAKEMEI; NAYE ATAPEWA.

6 Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku.

7 Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.

8 Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote”.

Neno limetushauri kama tumepungukiwa na Hekima na tuombe, Sulemani aliomba hekima kwasababu aliona amepungukiwa..na sisi vivyo hivyo, tunapaswa tuombe! Kama tu nyimbo ya taifa letu TANZANIA, tunapoiimba tunamwambia Mungu aibariki nchi yetu, huku tukisema HEKIMA ni ngao yetu…yatupasaje sisi tunaoamini? Tunapaswa tuombe Ili tuongezewe hekima! Lakini tunapaswa tuombe kwa imani na pasipo kusitasita.

Sasa Maana ya kuomba kwa imani ni nini?.

Maana yake unapaswa uombe, ukiwa ndani ya IMANI ya YESU KRISTO, na ukiwa na uhakika kwamba Mungu unayemwomba anakusikia na anawapa thawabu watu wajinyenyekezao kwake!..ukiwa nje ya Imani ya Yesu Kristo ni ngumu kupokea hiyo hekima, kwasababu hiyo Hekima ndio Yesu Kristo mwenyewe. Na pia hutakiwi kusita sita..Maana ya kusitasita ni kuwa na mawazo mawili… “mawazo ya ..aa sijui itawezekana, sijui nimesikiwa?”..na mawazo ya kushika hili na lile kwa wakati mmoja!! Kwasasa lenga jambo moja tu! Kumwomba Mungu hekima, usianze kuomba; Bwana naomba hekima, unipe na utajiri nipate hela, unipe na magari matatu, nyumba, unipe maisha marefu, unipe na biashara kubwa ya kimataifa n.k

HUKO NI KUSITA-SITA KWENYE MAWAZO MAWILI na hakumpendezi Mungu, ni sawa na mwanajeshi anayekwenda vitani na kumwomba kamanda wake ampe bunduki tatu za kubeba, mabomu sita, ampe na ndege ya vita na kifaru cha kisasa, ampe na mboksi matatu ya risasi, visu ishirini, ampe na kombora moja la nyuklia..Ni wazi kuwa huyo mwanajeshi hajiamini na hafai kwenda vitani..Na sisi hatupaswi kuwa hivyo.Kusita sita kwa kushika mambo mawili kwa wakati mmoja, Tunatumia silaha MOJA YA HEKIMA KWANZA, hizo nyingine zitakuja baadaye. Kama Sulemani alivyofanya hakuanza kumwambia Mungu naomba hekima, unipe na watoto sita waje kuwa wafalme, unipe na maisha marefu, unipe na utajiri, unipe na umaarufu na ufahari dunia nzima wanijue…hapana hakufanya hivyo hakusitasita kwenye mawazo mawili aliomba jambo moja kuu kwanza HEKIMA, na hayo mengine Mungu atayafungua mbele ya safari.

Tunasoma..

1 Wafalme 3; 9 “Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?

10 Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili.

11 Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu;

12 basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe.

13 NA MAMBO YALE USIYOYAOMBA NIMEKUPA, MALI NA FAHARI, HATA HAPATAKUWA NA MTU KATIKA WAFALME KAMA WEWE, SIKU ZAKO ZOTE”.

Unaona Mungu anamwambia Sulemani nimekupa HATA YALE MAMBO USIYOYAOMBA! Tatizo kubwa lililopo katika Ukristo leo hii, ni kushindwa kuelewa kuwa Mungu anajua mahitaji yetu kabla hata ya sisi kumwomba, hata pasipo kumwambia anaweza kukutimizia mahitaji yako endapo utakuwa UMESHIKA JAMBO MOJA KUU NA LA MUHIMU.

Mungu si mwanadamu, au hana udhaifu wa kibinadamu wa kusahau kuwa hitaji moja linategemea lingine, umemwomba kiatu anajua kabisa utahitaji na soksi, kwasababu huwezi kuvaa kiatu bila soksi, kwahiyo siku atakapokujibu ombi la kiatu atakupa na soksi hapo hapo..atakutengenezea na mazingira ya kupata fedha ya kwenda kukisafisha na kukipiga rangi pia… Lakini tanguliza kwanza ombi la msingi la kuomba kiatu, ili hayo mengine Bwana akuongezee.

Na leo hii shika jambo hili moja kuu na la Muhimu “HEKIMA” Itafute hiyo na hayo mengine yote utazidishiwa, mali, maisha marefu, watoto, heshima,  n.k lakini la kwanza ni Hekima.

Mungu akubariki sana.Tafadhali “share” Ujumbe huu kwa wengine.

Kwa Maombezi, Ushauri, au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225789001312/ +225693036618

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?

UMEFUNULIWA AKILI?

KUNA TOFAUTI GANI KATI YA SALA NA DUA?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Kissinger mmbayi
Kissinger mmbayi
1 year ago

It is of benefits to my spirit.