MADHARA YA KUTAFUTA ISHARA.

MADHARA YA KUTAFUTA ISHARA.

Ni kweli kitendo cha Kufa na kufufuka kwa Bwana Yesu kilikuwa kimeshatabiriwa hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote na kufufuka, Lakini pia tujiulize kwanini kufufuka kwake kulikawia kidogo, mpaka zikafika siku tatu, au kwanini zisiendelee na kuwa 10 au 20, kwanini ziwe ni zile tatu tu. Ndio tunaweza kusema hiyo ilikuwa ni kupisha muda wa kwenda kuzimu, lakini huko kuzimu kwanini kusingechukua siku moja au wiki, Ukweli ni kwamba siku ile ile aliyokufa, angepaswa afufuke siku hiyo hiyo, na angekuwa hajayatangua maandiko yoyote yale. Lakini kukaa kwake kaburini siku tatu, kulisababishwa na baadhi ya watu, ambao leo tutawaona, tunaweza kudhani kitendo kile ni kizuri sana kama watu wanavyodhani..Lakini nataka nikuambie ndugu tunapaswa tujitathimini sana.

Kumbuka wale watu Bwana aliokuwa nao (Wayahudi) sikuzote walikuwa ni watu wa kutokuamini, japo Mungu alijidhihirisha kwao kwa namna nyingi kwa kupitia manabii wake wengi huko nyuma lakini bado walikuwa hawataki kuamini mpaka waone ishara Fulani, sio kwamba Mungu alikuwa hawapi ishara alikuwa anawapa ishara nyingi njema lakini bado wakipewa walikuwa hawasadiki vile vile, mpaka ilipofikia wakati Mungu anakaribia kumleta Yesu duniani, Mungu aliwatangulizia Yohana mbatizaji kwanza kwa roho ya Eliya, lakini bado hawakutaka kuamini. Yaani kwa ufupi ni watu ambao walikuwa hawaeleweki wanataka kitu gani, au waone ishara ya aina gani ili waamini..Na ndio maana Bwana Yesu alisema..

Mathayo 11:16 ‘Lakini nitakifananisha na nini kizazi hiki? Kimefanana na watoto wanaokaa sokoni, wanaowaita wenzao, wakisema,

17 Tuliwapigia filimbi, wala hamkucheza; tuliomboleza, wala hamkulia.18 Maana Yohanaalikuja, hali wala hanywi, wakasema, Yuna pepo.

19 Mwana wa Adamu alikuja, akila na kunywa, wakasema, Mlafi huyu, na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi! Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwakazi zake.

20 Ndipo akaanza kuikemea miji ile ambamo ndani yake ilifanyika miujiza yake iliyo mingi, kwa sababu haikutubu.

21 Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu.

22 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi.

23 Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujizailiyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.

24 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe”.

Pamoja na Kwamba Bwana Yesu alikuwa anawafanyia miujiza mikubwa kama ile, na ishara nyingi kiasi kile, lakini bado walikuwa wanataka waonyeshwe ISHARA nyingine zitakazowashawishi wamwamini

Hilo tunalithibitisha kwenye vifungu hivi vya maandiko:

Yohana 6:30 “Wakamwambia, Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani? 31 Baba zetu waliila mana jangwani kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale.

32 Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni.

33 Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima”.

Unaona? ni watu wa kupenda ishara tu, na hata walipopewa walikuwa bado hawaamini.Jiulize dakika chache tu nyuma Yesu aliwavunjia ile mikate 5 wakala maelfu ya watu, hilo hawakuliona kama ni ishara kwao inayofanana na ile ile ya Musa..hilo hawakuliona, Watu wa namna hiyo unadhani wataonyeshwa jambo gani waridhike?

Biblia imeweka wazi kabisa Wayahudi ni watu wa kupenda Ishara, soma (1Wakorintho 1.22) kwasababu Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima;

Sasa mambo hayo yalipozidi Bwana hakupendezwa nao kabisa, Na ndio akawaambia maneno haya.

Luka 11:29 “Na makutano walipokuwa wakimkusanyikia, alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ILA ISHARA YA YONA.

30 Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki”.

Sasa wakati mwingine tunapaswa tujiulize ni kwanini Bwana hakuwachagulia ishara ya aina nyingine bali ile ya Yona?, kwanini asingewapa ishara kama ya Eliya kushusha moto, au ya Joshua kusimamisha jua, bali kawapa ile ya Yona?.

 

Embu turudi kumchunguza Yona kidogo, kumbuka Yona hakutumwa kwenda kuwaokoa wana wa Israeli, wala hakutumwa kwenda kutoa tu unabii na kuondoka kama alivyokuwa anafanya huko nyuma katika Taifa la Israeli, hapana bali alitumwa Ninawi kwenda kutangaza hukumu. Kwamba baada ya siku 40 Ninawi inaangamizwa kama wasipotubu..Sasa Hekima ya Mungu ilivyokuwa kubwa aliruhusu Yona akengeuke, ili amezwe na Yule samaki, ili akae siku tatu usiku na mchana kwenye tumbo lile. Na siku atakapotapikwa aende kuwahadithia watu wa Ninawi mambo yote yaliyomkuta…kwamba wale watu watathimini wenyewe kama yeye kwa kosa moja tu! La kutokuisikiliza sauti ya Mungu yamemkuta hayo, itakuwaje wao ambao maisha yao yote yapo kwenye dhambi watapataje kupona kama wasipotubu?.

Unaona Vivyo hivyo Mungu aruhusu Kristo amalize siku tatu kaburi, mfano wa Yona, ili somo lieleweke vizuri, kama ISHARA kwa WAYAHUDI. Lakini onyo haliendi kwao Bali linakuja kwetu sisi watu wa mataifa. Kama vile Yona hapo mwanzo alikuwa ni nabii wa Israeli tu, lakini ili afikie mataifa ilimpasa siku tatu zipotelee kwenye tumbo la samaki. Sasa leo hii tunafurahia Yona katapikwa na Yule samaki, lakini hatufahamu ujumbe Yona anaotuletea sisi, kuwa TUTUBU, kwani baada ya siku 40 mataifa yote yataangamizwa.

Upo usemi unaosema siku za mwizi ni 40, hiyo haimaanishi kuwa ni siku 40 kweli kweli hapana, bali ni lugha tu iliyopenda kutumia neno 40 kama kiashiria cha neema. Vivyo hivyo zile siku 40 za watu wa Ninawi walizopewa watubu ndio siku 40 zetu sisi katika roho watu wa mataifa..

Injili inahubiriwa miaka 2000 sasa, unaopoona kufa kwa Yesu na kukaa kwake kaburini siku tatu unaona ISHARA GANI NZURI HIYO?, Amefufuka na kutoka Kaburini ili kukuhubiria kuwa yapo mabaya mbeleni yanakuja kama hutatubu.

Ndugu hizi ni nyakati za mwisho, UNYAKUO upo karibu sana kutokea, vile vile na maangamizi ya dunia hii yapo karibu sana kutokea Biblia imesema hivyo. Tumepewa kipindi kirefu hichi cha kutubu, tusipofanya hivyo kama unyakuo hautatukuta basi kifo ni lazima, sasa tutawezaje kupona siku ile. Tutajitetea vipi mbele za Mungu kuwa hatukuwa na muda. Na ndio maana Bwana alimalizia na kuwaambia wale watu maneno haya.

“……32 WATU WA NINAWI WATASIMAMA SIKU YA HUKUMU PAMOJA NA KIZAZI HIKI, NAO WATAKIHUKUMU KUWA NA HATIA; KWA SABABU WAO WALITUBU KWA MAHUBIRI YA YONA, NA HAPA PANA MKUBWA KULIKO YONA”.

Yona alihubiri siku tatu akaenda kukaa kule mlimani akisubiria maangamizi, lakini Sisi tumekuwa tukiisikia injili ya Yesu Kristo kila siku na bado tunaendelea kusikia injili masikioni mwetu kwa njia mbalimbali kuonyesha ni jinsi gani Kristo anavyotuhurumia tusiangamie kwa hayo mambo mabaya yanayokuja huko mbele.

Ni maombi yangu, ikiwa bado upo katika dhambi utatubu leo, kwa kumaanisha kabisa kuacha dhambi zako, na hakika Bwana atakupokea na kukufanya kuwa kiumbe kipya..Na ikiwa pia wokovu wako ni wa kusua sua, mguu moja huku mwingine kule, ni vizuri leo ukafanya maamuzi ya kusimama imara, Hakikisha pia baada ya kutubu kwako, tafuta mahali ukabatizwe katika ubatizo ulio sahihi wa kimaandiko kukamilisha wokovu wako. Na ubatizo sahihi ni ule wa kuzamishwa katika maji tele na uwe katika Jina la YESU KRISTO.

Nakutakia kila la heri katika safari yako ya wokovu hapa duniani. Na Bwana akubariki.

Pia kwa Maombezi, Ushauri au Ratiba za Ibada basi Wasiliana nasi kwa namba

+225789001312/ +225693036618

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

SAUTI NYUMA YA ISHARA.

INJILI KULINGANA NA TEKNOLOJIA

MWEZI NI ISHARA GANI KWETU?

TOBA IGUSAYO MOYO WA BWANA.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Aman Ernest
Aman Ernest
1 year ago

Amina! Asante Kwa ujumbe mzuri!

Joseph
Joseph
2 years ago

Ujumbe Mzuri Sana, Asante kwa Neno la Uzima.