Kuna tofauti gani kati ya SALA na DUA?

Kuna tofauti gani kati ya SALA na DUA?

JIBU: SALA ni neno la ujumla linalojumuisha maombi yote, iwe ya shukrani, mahitaji, ibada, sifa, toba,ulinzi, Baraka n.k…Kwamfano yale maombi ya Baba yetu uliye mbinguni Yesu aliyowafundisha wanafunzi wake….Ni mfano wa SALA.

Kwahiyo unaposhukurau ni sala, unapoomba toba ni sala, unapomba hitaji lolote Kwa Mungu kama chakula, mavazi, nyumba n.k. hizo zote ni sala, unapomshukuru Mungu kwa maombi ni sala, na pia unapomwimbia Mungu sifa kama Daudi alivyokuwa anafanya kadhalika ni sala.

Lakini maombi ya Dua ni tofauti kidogo na sala, kwasababu sala ni Neno la ujumla kama tulivyosema lakini DUA imeegemea sana katika maombi ya MAHITAJI..

Kumbuka pia kuna maombi ya kawaida ya mahitaji haya ni yale ambayo unamwomba Mungu akufanyie jambo Fulani, kama tulivyosema hapo juu kuomba riziki, chakula, pesa, n.k. lakini Dua ni maombi ya hitaji isipokuwa haya yanakwenda ndani zaidi, (na ya masafa marefu) ndiyo yanayohusisha na kuomba rehema, kumsihi Mungu akutendee jambo Fulani ambalo pengine usingestahili kulipata, na dua huwa inaambatana na kujinyenyekeza kwa hali ya juu, na wakati mwingine inahusisha pia na kufunga kwa muda mrefu. Kwamfano unapoomba toba juu ya Kanisa, nchi au familia yako, au ndoa yako kwamba Mungu airehemu kwa makosa Fulani yaliyofanyika, huwezi kwenda kwa maombi ya kawaida tu kama unavyokwenda kumwomba akupe chakula, au pesa, au mavazi, au kazi, hapana hapo utamwendea kwa unyenyekevu, kwa kuomboleza, wakati mwingine kufunga kumsihi Mungu juu ya uovu wa kanisa, au nchi au familia yako ausamehe, sasa hiyo ndio inayoitwa Dua.

Mfano ulio hai tunaweza kuuona kwa Danieli, pale alipoomba DUA juu ya makosa na uovu wa watu wake uliowasababishia mpaka kupelekwa Babeli,

Danieli 9: 2 katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini.

3 Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa MAOMBI NA DUA, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu.

4 Nikamwomba Bwana, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake;

5 tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako…………; )

Maombi ya namna hii tunaona pia yalifanyika kwa Nehemia, pale alipopata taarifa juu ya uharibifu wa Yerusalemu na maovu ya watu wake yaliyokuwa yametendeka Yerusalemu, aliomba Dua kwa Mungu kwa kuomboleza na kufunga kama Danieli alivyofanya. Soma (Nehemia 1).

Tunaona pia kwa malkia Esta na wayahudi wote walipotangaziwa kuuawa, walijinyenyekeza mbele za Mungu kwa kufunga na kuomboleza kwa ajili ya maangamizi yao, Mungu akasikia dua zako, akawaokoa na maangamizi.

Kadhalika na Daudi mara nyingi alipokuwa akipitia shida, aliingia katika maombi ya Dua kwa ajili yake mwenyewe na Mungu amwepushe na adui zake.(Zaburi 28:2, zaburi 30:8).

Bwana wetu Yesu Kristo pia alikuwa anaomba Dua. Waebrania 5: 7 “Yeye [YESU], siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, MAOMBI NA DUA pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu;” Unaona hapo?

Hata sisi pia tunapaswa tuwe watu wa SALA na DUA kwa ajili yetu wenyewe kuomba rehema mbele za Mungu, na kwa ajili ya Kanisa, na kwa ajili ya Nchi ili Mungu aweze kufungua mambo mengine yaliyofungwa mbele yetu. Kwasababu biblia pia imetukumbusha hilo katika:

1Timotheo 2: 1 “Basi, kabla ya mambo yote, nataka DUA, na SALA, na MAOMBEZI, na SHUKRANI, zifanyike kwa ajili ya watu wote;

2 kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu.

3 Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu;”


Mada zinazoendana:

FAIDA ZA MAOMBI.

MAOMBI KWA WENYE MAMLAKA.

MAOMBI YA YABESI.

ELIYA ALIOMBA KWA BIDII, JE! KUOMBA KWA BIDII KUKOJE?

OKOA BADALA YA KUANGAMIZA!

MKUU WA GIZA.

MJI WENYE MISINGI.


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Steward
Steward
3 years ago

Dua nine no la kiswahili!

Anonymous
Anonymous
2 years ago
Reply to  Steward

Ndio, dua ni neno la katika lugha ya kiswahili.