Lakini kwa Ibrahimu haikuwa hivyo, alikuwa na jicho la mbali zaidi, hakutazama Baraka hizo Mungu alizomwahidia za kitambo tu, hakutazama wingi wa uzao atakaokuwa nao duniani, hakutazama ukuu wa taifa atakalolizaa duniani, hakutazama utajiri wa kimwilini, kwa hili jicho la kimwilini, bali aliyatafakari maisha yake kwa utulivu sana, akiangalia jinsi Mungu alivyomtoa Nchi ya Ulkadayo na kumleta pale Kaanani, na jinsi Mungu alivyomwepusha katika taabu zote zile, za kungojea nchi ambayo Mungu amemwahidia, akajiuliza kama Mungu anao uwezo wa kunifanya taifa kubwa ndani ya dakika moja, kwanini anakawia hivi kunipa mwana? Sababu nini?..Ibrahimu alitaka kujua kusudi la maisha, nyuma ya haya yote kuna nini?.. Na ndipo akafahamu kuwa maisha yake ni picha ya mambo yatarajiwayo mbeleni yajayo baada ya ulimwengu huu kupita. Alifahamu kuwa maisha yake ni somo, maisha yake ni sauti Mungu anayozungumza naye juu ya mambo ya mbeleni sana..ng’ambo ya pazia..