Na unafahamu zamani zile mfano mtu akipewa jina ni lazima libebe maana kubwa sana juu ya maisha yake ya baadaye. Hivyo Yabesi kuitwa lile jina iliashiria kuwa maisha yake yote yatakuja kuwa ni maisha ya huzuni, uchungu, mtu wa kulemea wengine, mtu wa nuksi na mikosi, tabu, majonzi n.k. Hakuna mtu aliyeweka tumaini lolote jema la Yabesi mbeleni.. Lakini Yabesi aliendelea kukua na hilo jina akiona kuwa hakuna mtu mtaani kwao aliyeitwa kwa jina kama hilo. wakati watoto wengine wanaitwa majina mazuri kama Furaha, Amani, Upendo, Tumaini, Faraja, Godbless, Neema, Rehema n.k. yeye anaitwa, huzuni, msiba, Matatizo, masumbuko, shida, tabu, majuto. Hilo lilimwingia sana moyoni mwake, pengine lilimpa mawazo mengi maishani kufikiri juu ya hatma yake itakavyokuwa, kuwa atakuwa mtu wa huzuni siku zote za maisha yake.