UMEFUNULIWA AKILI?

UMEFUNULIWA AKILI?

Je! Umefunuliwa akili?..Baada ya Bwana Yesu kufufuka, tunasoma habari ya vijana wawili waliokuwa wanaenda kijiji kimoja kilichopo mbali kidogo na mji wa Yerusalemu, na walipokuwa njiani wakizungumza habari za kufufuka kwa Bwana biblia inatuambia Bwana wenyewe aliungana nao pasipo hata wao kujua, kwani  macho yao yalifumbwa wasimtambue lakini  baadaye mwisho wa safari yao walikuja  kumtambua..tunasoma habari hiyo katika..

Luka 24.13 “Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili.

14 Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia.

15 IKAWA KATIKA KUZUNGUMZA NA KUULIZANA KWAO, YESU MWENYEWE ALIKARIBIA, AKAANDAMANA NAO.

16 Macho yao yakafumbwa wasimtambue.

17 Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao.

18 Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi?

19 Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote;

20 tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha.

21 Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo;

22 tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema,

23 wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai.

24 Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona.

25 Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii!

26 Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake?

27 Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.

28 Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, NAYE ALIFANYA KAMA ANATAKA KUENDELEA MBELE.

29 Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao.

30 Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.

31 Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao.

32 Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko?”.

Wengi tunatamani Kristo atutokee siku moja, na kuanza kutembea nasi, ndipo tuamini Yupo na sisi, lakini hatujui kwamba Kristo yupo pamoja na sisi kila siku, akitufundisha na kutufunulia maandiko…kama Neno lake linavyosema “walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.”…Unaona hapo kwa wakati huo Macho yetu ya mwilini yanakuwa yamefumbwa yasimwone lakini macho yetu ya rohoni yanamwona.

Ndicho kilichowatokea hawa watu wawili waliokuwa wanaenda Emau..Bwana alipojiunga katikati yao Macho yao ya mwilini yalifumbwa wasimtambue lakini macho yao ya rohoni yalikuwa yanamwona Bwana, alipokuwa anawafunulia maandiko kumhusu yeye.

Ni kwanini Bwana alijiunga nao? Ni kwasababu “tayari walikuwa wameshakusanyika wawili kwa jina lake, wakizungumza habari zake” ..hivyo Kristo lazima atimize Neno lake “la kuwepo katikati yao”.

Sasa maana ya kuwepo katikati yao sio kumwona sura yake hapana! Bali kumwona yeye katika  Neno lake. Ndio maana wale watu wawili Bwana hakuwafumbua macho yao wamwone sura yake, bali alianza kwanza kuwafunulia maandiko wamwone yeye katika Neno lake.

Kwahiyo unaweza kuona Bwana havutiwi sana, na sisi kumwona yeye uso wake, bali anavutiwa sana na sisi kumwona yeye katika Neno lake. Ndio maana leo hatokei wengi, kwasababu anataka tumjue katika Neno lake, zaidi ya uso wake.

Ukiendelea kusoma habari za hawa vijana wawili, utagundua hata baada ya Bwana kumaliza kuwafunulia maandiko, hakutaka kuwafumbua macho ya mwili wamwone, badala yake utaona alitaka kuondoka kuwaacha katika hali ile ile ya kutomtambua, alitaka kuendelea mbele na safari yake, Ni kwanini alifanya vile? Ni kwasababu lengo lake halikuwa kuwaonyesha uso wake, bali lengo lake lilikuwa wamwelewe katika maandiko..Na baada ya kutimiza kusudi lake la kuwafunulia maandiko kazi ilikuwa imeshakwisha, alitaka kutengana nao… Lakini walipomshawishi sana ndipo akaamu kwenda  kula nao, na huko ndio akawafumbua macho yao ya mwilini wamwone.

28 Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, NAYE ALIFANYA KAMA ANATAKA KUENDELEA MBELE.

29 Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao”.

Na ndio maana tunakuja kusoma pia Bwana alimkemea Tomaso kwa kutokumwamini…yeye alitaka auone uso wa Bwana na majeraha yake ndipo aamini, lakini Bwana hakutaka amwamini kwa njia hiyo..alitaka Tomaso amwamini kwa njia ya maandiko?..alitaka Tomaso amwamini kwa ufunuo wa maandiko, sio kwa kumwona uso..alitaka Tomaso amtambue yeye kwa kuyajua yaliyotabiriwa kumhusu yeye kuanzia kwa Musa, zaburi na kwa manabii wote, na hayo mengine yawe baadaye sana kama yana umuhimu.

Ndugu sura ya Yesu haiwezi kutufanya tumwamini yeye hata kidogo, kitakachotufanya tumwamini Bwana Yesu ni ufunuo katika Neno lake, ni kumtambua kupitia Neno lake, kumwona ametabiriwa wapi katika maandiko, na nafasi yake ni ipi katika Roho sasa.

Wanafunzi hata baada ya kumwona Bwana YESU uso wake,akiwa amefufuka hawakumwamini, walimtilia mashaka, walidhani wanaona mizimu..Na hata kama Bwana angewatokea mara 100 kama asingewafunulia akili zao wayaelewe maandiko wasingemwamini…wangeendelea kumtilia mashaka tu!..Tunaona mtu kama  Yuda yeye sio kutokewa tu dakika chache halafu basi, hapana bali yeye aliishi, alikula, alilala na Yesu lakini mwisho wa siku akaja kumsaliti.

Luka 24.36 “Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu.

37 Wakashituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho.

38 Akawaambia, Mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu?

39 Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo.

40 Na baada ya kusema hayo aliwaonyesha mikono yake na miguu yake.

41 Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajabu, aliwaambia, Mna chakula cho chote hapa?

42 Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa.

43 Akakitwaa, akala mbele yao.

44 Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi.

45 NDIPO AKAWAFUNULIA AKILI ZAO WAPATE KUELEWA NA MAANDIKO.

46 Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu;

47 na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu”.

Je! na wewe leo amefunua akili zako, ili upate kuyaelewa maandiko??..ukiona huna hamu ndani yako ya kuyasoma maandiko, na hakuna msukumo wowote ndani yako wa kupenda kusoma Neno, mwombe Bwana leo hii akupe Neema…akupe hiyo nguvu, maana hawezi kukufunulia macho yako ya rohoni uyaelewe maandiko kama maandiko huyasomi… kuna hatari kubwa sana ya kukosa kulijua Neno la Mungu.. Kumbuka Kristo hakufungui macho uuone uso wake yeye, wala halitamani hilo…ingekuwa anataka tuuone uso wake, angeruhusu wakati ule picha yake ichorwe na iifadhiwe kwa vizazi vyetu hivi, kama neno lake limeweza kuhifadhiwa kwa vizazi vyote hivyo si zaidi picha? Ni kitu kidogo sana kuifanya picha yake ihifadhiwe kwa vizazi vyote lakini hakutaka… au angekuja kipindi hichi cha teknolojia ambapo kila mtu angeweza kumpiga picha na kuweka katika chumba chake cha ndani…Lakini hiyo sio njia anayoitumia ili sisi tumwamini yeye…yeye anataka tumwamini yeye, na tumjue, na tumfahamu sana kwa ufunuo wa Neno lake, biblia takatifu. Tukimtafuta katika nyuso tutamkosa hayupo huko…alimwambia Tomaso wana heri wale wasioona wakasadiki.

Je! na wewe ndugu unamtafuta Bwana leo kwa njia ipi? Kwa njia ya uso au maandiko?…Je Bwana amefunua akili zako uweze kumwona? Unasema unampenda Yesu wa kwenye picha au Yesu wa kwenye maandiko?..Na kama ni wa kwenye maandiko je! unayapenda maagizo yake yote aliyoyatoa?. Je! unajumuika na wengine wenye imani moja na wewe kwa maana alisema “wakusanyikapo wawili watatu kwa jina lake atakuwepo katikati yao”. Ni lazima tukusanyike kuanzia wawili na kuendelea ili Kristo, ajumuike pamoja nasi kutufunulia maandiko. Ni muhimu sana kuhudhuria bible study, au kukusanyika na mwenzetu kujifunza biblia kila iitwapo leo maadamu siku ile inakaribia, ndipo tutakapomwona Yesu.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine, Bwana akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

SAA YA KIAMA.

BIBLIA INAPOSEMA “HERI WALIO MASKINI WA ROHO MAANA UFALME WA MBINGUNI NI WAO”JE HATUNA RUHUSA YA KUWA MATAJIRI KATIKA ROHO?.

JE! NI KWELI KUNA VIUMBE VINAVYOISHI SAYARI NYINGINE (ALIENS)?

Mstari huu una maana gani? “Tupa chakula chako usoni pa maji; Maana utakiona baada ya siku nyingi”. (Mhubiri 11:1)


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments