Yearly Archive 2023

Biblia inasema tujihadhari na “Mbwa” hawa mbwa ni akina nani? (Wafilipi 3:2)

Jibu: Tusome..

Wafilipi 3:2  “Jihadharini na mbwa, jihadharini na watendao mabaya, jihadharini na wajikatao”

Hapa kuna makundi matatu yaliyotajwa ambayo tunapaswa tujihadhari nayo, kundi la Kwanza ni “MBWA” kundi la Pili ni “WATU WAJIKATAO” na kundi la tatu ni “WATU WATENDAO MABAYA”.

Sasa kabla ya kwenda kuangalia Mbwa ni watu wa namna gani, kwanza tuyatazame haya makundi mawili ya mwisho, ambayo ni watu wajikatao na watenda mabaya..

Watu “watendao mabaya” wanaozungumziwa hapo, ni watu walio ndani ya imani lakini wanatenda mabaya.. watu hawa biblia imetuonya tujihadhari nao, yaani tusichangamane.. Mtume Paulo alizidi kuliweka hili vizuri katika kitabu cha 1Wakorintho 5:9-11.

1Wakorintho 5:9  “Naliwaandikia katika waraka wangu, kwamba msichangamane na wazinzi.

10  Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang’anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia.

11  Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang’anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye”.

Lengo la kutochangamana na makundi haya ya watu walio ndani ya kanisa lakini ni watenda mabaya, ni ili wajisikie aibu kwa wanayoyafanya na hatimaye wageuke na kutubu.

Kundi la Pili: Ni “Watu Wajikatao”.. kumbuka hapa anasema “watu wajikatao” na sio “watu wajikataao” kuna tofauti ya kujikata na kujikataa.. hapa wanazungumziwa watu wanaojikata!.. Sasa ni watu gani hao wanaojikata?.. si wengine bali walikuwa ni wayahudi ambao walikuwa wanashinikiza tohara, kuwa ndio dalili ya kukubaliwa na Mungu..

Lilikuwepo kundi la walioamini, ambao hata sasa lipo lililokuwa linasisitiza tohara kuwa ni jambo la lazima, na kwamba mtu asipotahiriwa hawezi kukubaliwa na Mungu. Watu hawa walikuwa kweli wamemwamini Yesu lakini sheria za torati bado zilikuwa zinawaendesha, ambazo kimsingi hizo haziwezi kumkamilisha mtu, bali Neema ya Yesu pekee… kushika mwezi, mwaka, siku, sabato haya yote hayafai katika kumkamilisha mtu.

1Wakorintho 7:19  “Kutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu bali kuzihifadhi amri za Mungu.

20  Kila mtu na akae katika hali ile ile ambayo alikuwa nayo alipoitwa”

Kwa maelezo mengine marefu kuhusiana na watu wajikatao unaweza kufungua hapa >>> WATU WAJIKATAO

Na kundi la Tatu na la Mwisho, ambalo biblia imetaja tujihadhari nalo ni kundi la “MBWA”.

 Sasa utajiuliza hawa “Mbwa” ni akina nani?

Bwana Yesu aliwataja wazi kabisa hawa Mbwa ni wakina nani.. Tusome..

Mathayo 7:15  “Jihadharini na MANABII WA UONGO, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni MBWA-MWITU WAKALI.

16  Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti”

Umeona?… Kumbe Mbwa wanaozungumziwa hapo ni “Manabii wa Uongo” na tena hawajatwi kama Mbwa tu!, bali kama “Mbwa-Mwitu” tena wakali!.. maana yake wasiohurumia kundi.. Na hatutawatambua kwa mionekano yao, kwasababu kwa nje wamevaa mavazi ya kondoo, (wanafanana na watumishi wa kweli wa Mungu) lakini tutawatambua kwa matunda yao, maana yake kwa yale wanayoyafundisha na wanayoyaishi.

Na manabii wa uongo ni mjumuisho wa Mitume wa Uongo, wachungaji wa uongo, waalimu wa Uongo, pamoja na waimbaji wa Uongo. Kwaufupi watu wote wanaosimama kutangaza injili kwa wengine! Lakini maisha yao ya ndani si wakristo, ila kwa nje wanasifika kama watumishi wa Mungu.

Ikiwa mtu atasimama na kuhubiri injili nyingine tofauti na ile iliyoandikwa katika biblia, basi huyo kibiblia ni “Mbwa”, ikiwa mtu atahubiri injili isiyo ya wokovu, badala yake ya kumpoteza mtu au kumfanya afurahie dhambi..mtu huyo kibiblia ni Mbwa, na tumetahadharishwa kukaa mbali naye.

Nabii wa Kweli wa Mungu atakuwa kama Musa!, Mpole kuliko wote, na mwenye kuwaelekeza watu kwa Mungu na si kwake wala kwa shetani.

Kumbukumbu 13: 1 “Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,

 2 ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;

 3 wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.

4 Tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye”

Je! Unaongozwa na nani?.. Manabii wa Uongo, Miujiza na Ishara au NENO LA MUNGU?.

Kumbukumbu 6:4 “Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. 

5 Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote”.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Watu wajikatao ni watu wa namna gani? (Wafilipi3:1).

Mstari huu una maana gani? “Tupa chakula chako usoni pa maji; Maana utakiona baada ya siku nyingi”. (Mhubiri 11:1)Kutekewa maana yake nini?(Mathayo 22:12)

Mungu anatufundisha kusamehe mara saba sabini, ila Kwanini yeye hakumsamehe Adamu alipoasi?.

HAKUONA MAHALI PA KUTUA KWA WAYO WA MGUU WAKE.

VICHEKESHO NA UTANI MADHABAHUNI

Rudi nyumbani

Print this post

Kutekewa maana yake nini?(Mathayo 22:12)

Jibu: Tusome kuanzia mstari wa 8 ili tuweze kuelewa vizuri..


Mathayo 22:8 “Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili.
9 Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini.
10 Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni.
11 Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi.
12 Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? NAYE AKATEKEWA”.


“Kutekewa” kunakozungumziwa hapo si Kutekewa maji au kinywaji fulani, hapana!…Bali maana yake Ni “KUKOSA MANENO”


Mtu anayekosa Neno la kujibu pale anapoulizwa, mtu huyo Ndio katekewa..
Katika habari hiyo Bwana Yesu anatoa mfano wa mtu aliyeishiwa maneno baada ya kukutwa hana vazi la harusi.


Hali itakayokuwa kwa wengi katika Ile siku ya mwisho. Maandiko yanaonyesha kuwa katika siku ya mwisho, Bwana atawakataa watu wengi, ambao hawakuwa na vazi la Harusi walipokuwa duniani.
Na vazi la harusi maandiko yameweka wazi kuwa Ni “Matendo ya haki ya watakatifu”.


Ufunuo 19:8 “Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu”


Katika siku ile wengi watadhani Ni dini zao zintakazowapa kibali Cha kuingia uzimani, wengine watadhani Ni Imani zao n.k. pasipo kujua kuwa bila utakatifu hakuna mtu atakayemwona Mungu.


Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao”


Na Utakatifu hatuupati kwa nguvu zetu, Bali kwa msaada wa Bwana.


Tunapotubu kwa kudhamiria kabisa kuacha dhambi zetu, na kubatizwa katika ubatizo sahihi Kama bado hatujabatizwa Basi Bwana anatupa Roho wake mtakatifu ambaye huyo ndiye atakayetusaidia sisi kuweza kuwa wakamilifu na watakatifu.


Hivyo tukiupata utakatifu katika maisha yetu, Basi katika Roho tutaonekana mbele zake tumevaa vazi la harusi na hivyo siku Ile hatutatekewa mbele zake, hatutaishiwa maneno.


Lakini tukiyakosa hayo, huku tukitumainia dini zetu, na madhehebu yetu, na theologia zetu… basi tujue kuwa tutakosa cha kujibu mbele zake siku Ile..


Mathayo 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?
23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

BALI WANA WA UFALME WATATUPWA NJE!.

TAFUTA KWA BIDII KUWA MTAKATIFU.

MATUNDA 9 YA ROHO MTAKATIFU

Je! Ni halali kuoa/kuolewa na mtu ambaye tayari anao watoto?

Kwanini wanawake wengi huwa wanalipuka mapepo?

Rudi nyumbani

Print this post

Shetani anaishi wapi, Je! Amefungwa au yupo kuzimu?

JIBU: Wapo wanaofikiri kwamba shetani amefungwa, atakuja kufunguliwa kipindi Fulani huko mbele, lakini pia wapo wanaodhani, shetani anaishi mahali Fulani kuzimu( aidha chini ya bahari, au kwenye sayari fulani), ambapo huko kuna amesimika utawala wake unaofanana na huu wa duniani.

Lakini ukweli ni kwamba shetani hajafungwa, wala hayupo katika eneo Fulani rasmi la mwilini, ambalo unaweza kwenda ukakutana naye.

Ikumbukwe kuwa ibilisi anafanya kazi katika ulimwengu wa roho, alipoasi mbinguni, alitupwa chini duniani, akaanza kazi yake ya kuudanganya ulimwengu mpaka akafanikiwa kuuteka ukawa chini ya milki yake, Tunalithibitisha hilo katika maneno aliyomwambia Bwana Yesu.

  Luka 4:5 Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja.

6  Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo.

7  Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako. 8  Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke

Hivyo shetani yupo anazunguka zunguka duniani hana makao rasmi, Alimwambia hivyo Mungu.

Ayubu 1:6 “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao.  7 Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo”.

Atakuja kufungwa kipindi ambacho utawala wa miaka 1000 wa amani wa Yesu Kristo kuanza, na baadaye atafunguliwa kidogo, lakini kwasasa hajafungwa yupo duniani ndio chanzo cha maovu yote, wala hana eneo Fulani rasmi kwamba amejijengea  anaishi huko na mapepo yake, hapana bali wanafanya kazi katika ulimwengu wa roho, wakijigawanya tu katika vitengo mbalimbali, wengine katika anga, wengine, katika mataifa, wengine katika familia moja moja, na wengine katika kila huduma/au kanisa la Kristo lilipo, wengine katika uchawi n.k.

Hivyo, sisi tutamshinda na kumpinga tu kwa kulishika Neno la Mungu, na kudumu katika maombi daima.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MBINGUNI YUPO NANI SASA?

ZIFAHAMU HUDUMA KUU (10) ZA SHETANI DUNIANI.

POPOBAWA NI KWELI YUPO?

ZIFAHAMU KAZI TATU ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA ULIMWENGU.

MATESO YA KUZIMU.

HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?

Rudi nyumbani

Print this post

MAGONJWA YAKUPATAYO MARA KWA MARA.

1Timotheo 5:23  “Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara”

Haya ni maneno ya mtume Paulo kwa mtoto wake wa kiroho Timotheo, Ni rahisi kuyachukulia juu juu, lakini ukitazama kwa undani utaona jinsi watu wa kale walivyojitoa kwa Bwana,bila kuruhusu hali zao za mwilini kuwakwamisha.

Kama tunavyosoma, Timotheo alikuwa ni kijana mwenye bidii sana, aliyetumika na Mtume Paulo katika kuineza injili sehemu kubwa ya dunia, lakini kijana huyu hakuwa vizuri sana kiafya kama tunavyodhani, alikuwa anasumbuliwa na tumbo, lakini kama hilo halitoshi, alikuwa pia anapatwa na magonjwa ya MARA KWA MARA, tena katika ujana na sio uzee. Ni heri magonjwa hayo yangekuwa ni ya siku moja, bali ya mara kwa mara. Paulo aliishi naye kwa muda mrefu hivyo alikuwa anamwelewa sana, anashangaa leo yupo sawa, kesho, ni mgonjwa, wiki hii yupo sawa, wiki ijayo tumbo linamsumbua sana.

Lakini katika yote hayo, hakuwa kama Dema ambaye alimwacha Paulo, akaurudia ulimwengu, yeye aliendelea kuitenda kazi ya Bwana katika madhaifu yake ya mwili,  Ni mtu tu pekee ambaye Paulo alijiona amani kumwachia hata huduma yake aiendeleza duniani. Alikuwa kama Elisha kwa Eliya.

Hivyo mwishoni kabisa mwa huduma, tunaona hapa Paulo anamwandikia waraka huu na kumsisitiza, asinywe maji tu peke yake, bali na mvinyo kidogo kwa ajili ya magonjwa hayo ya mara kwa mara, Paulo hapa anampa ushauri wa kitabibu, zaidi ya ule wa kiroho, kwani zamani mvinyo , ulitumika kwa ajili ya baadhi ya magonjwa, lakini sasa kwa wakati wetu tunazo dawa za hospitalini. Unaweza kujiuliza Paulo ambaye Mungu alimtumia kwa ishara na miujiza ya kupita kawaida, angepaswa amweke, mikono, na kukemea magonjwa hayo ya mara kwa mara yamwachie, lakini alitambua kuwa si kila wakati hali itakuwa hivyo, mambo mengine Mungu anayaruhusu yatokee kwa sababu zake.

Ni kama Elisha, ambaye, alisumbuliwa na ugonjwa ambao ulikuja kumuua, lakini hakumwacha Bwana, na kusema Mungu gani huyu hanioni, aliendelea kuwa nabii wa Mungu,

2Wafalme 13:14 “Basi Elisha alikuwa ameshikwa na ugonjwa wake uliomwua; naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatelemka amtazame, akamlilia mbele yake, akasema, Baba yangu! Baba yangu! Gari la Israeli na wapanda farasi wake!”

Ni nini Bwana anataka tujifunze?

Katika madhaifu yetu, kamwe tusipunguze spidi ya kumtumikia Mungu, kwasababu mambo tunayoyapitia sisi walishayapitia watakatifu wengine waliotutangulia. Kijana Timotheo, alikuwa ni mdhaifu sana kimwili, lakini aliichapa injili ya Kristo, bila kujali yamsibuyo. Alisafiri huko na huko.

Yawezekana na wewe, ni mhubiri au mtumishi wa Bwana, lakini vidonda vya tumbo, haviishi ndani yako ijapokuwa umemwomba sana Bwana aviondoe lakini bado huoni matokeo yoyote, endelea hivyo hivyo kutumika usisubiri upone, una magonjwa Fulani ya kichwa ambayo yanakuja na kuondoka, yanakuja na kuondoka, yasikukwamishe, mkumbuke Timotheo, kunywa dawa za hospitalini, songa mbele, unasumbuliwa na saratani, unasumbuliwa na sukari, inapanda, inashuka, kila siku ni kuchoma sindani, Usingoje kwanza Bwana akuponye, endelea, kwani huzijui njia za Bwana, hujui ni kwanini leo upo hivyo, huwenda amekusudia, uishi maisha marefu kuliko zaidi ya wengine katika hali hiyo hiyo ili jina lake litukuzwe, na uwaponye wengi wanaosumbuliwa na maradhi kama hayo, Elisha baada ya kufa katika ule ugonjwa wake, tunaona bado mifupa yake ilifufua wafu, Hivyo kuugua si kikwazo cha Mungu kutokututumia sisi.

Tujipe moyo tusonge mbele, Bwana anatupenda, kwani yeye mwenyewe alisema, pale tuwapo dhaifu ndipo tulipo na nguvu.

2Wakorintho12:9  “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 12.10  Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu”.

Bwana akubariki

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

UWEPO WA BWANA HATA KATIKATI YA MATESO.

USIKATE TAMAA UNAPOPITIA MAGONJWA.

Nini maana ya..“wakiwazuia watu wasioe” (1Timotheo 4:1)

AMEFANYIKA BORA KUPITA MALAIKA!

MAUMIVU  NYUMA-YA-HUDUMA.

NINI TOFAUTI KATI YA KARAMA, UTENDAJI KAZI NA HUDUMA.

KANSA/SARATANI INATIBIKA.

Rudi nyumbani

Print this post

Mungu anatufundisha kusamehe mara saba sabini, ila Kwanini yeye hakumsamehe Adamu alipoasi?.

Jibu:  Adhabu iliyompata Adamu na Hawa, haikutokana na hasira ya Mungu!.. bali ilikuwa ni matokeo ya walichokifanya.

Hebu tafakari mfano huu…. “unamwonya mtu asile kitu Fulani kwasababu unajua madhara ya hicho kitu kwamba endapo akikila basi kitamsababishia apofuke macho na hata kufa huko baadaye, kwasababu kina sumu mbaya ndani yake”.

Lakini huyo mtu ambaye ulimtahadharisha asifanya hivyo, hakukusikiliza wewe badala yake akaenda kula hicho kitu ambacho madhara yake ni kupofuka macho na hata kufa. Na siku alipokula wewe ukajua na kwa huzuni  ukaenda kumwuliza kwanini ulikula?..yeye akatoa sababu zake anazozijua yeye, kisha wewe ukamwambia kwamba.. “kwasababu umekula hicho kitu basi macho yako yatapofuka siku si nyingi  na pia utakufa!.

Sasa swali ni je!, kwa wewe kumwambia hivyo kwamba “atapofuka macho na kufa” je umemhukumu, au umemwambia tu mambo yatakayompata kutokana na kitu alichokifanya?.. Au je kwa wewe kumwambia hivyo, kuna uhusiano wowote wa wewe kumsamehe au kutomsamehe?.. Jibu ni la!, wewe umemwambia tu madhara ya alichokifanya na kuanzia pale utaanza kumhurumia na kumtafutia suluhisho ili ile sumu iliyoingia ndani yake iweze kutoka….

Ndicho kilichotokea pale Edeni, adhabu aliyoipata Adamu na Hawa ni kwasababu ya matokeo ya walichokifanya na si kwasababu ya hasira ya Mungu!!. Na Mungu kwa huruma zake, kuanzia pale ndio akaanza mpango wa kumponya mwanadamu kwa madhara aliyoyaingiza katika maisha yake.

Na ndipo akapata mpango bora, ambao huo utaondoa moja kwa moja madhara yaliyoingia ndani ya Mwanadamu, na mpango huo si mwingine zaidi ya ule wa kumtoa Mwanawe wa pekee YESU KRISTO, aje kufa kwa ajili ya dhambi zetu, na kutukomboa, kuanzia hapo Mungu akamtoa Adamu pale Edeni ili amweke katika mpango mpya na ulio kamili, utakaomkamilisha.

Yesu Kristo pekee ndiye tiba ya KIFO  ambacho kilikuwa kimeingia katika maisha yetu tangu siku ile wazazi wetu, Adamu na Hawa walipoasi.

Yohana 11:25  “Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi”

Yesu Kristo ndiye tiba ya mambo yote, ndiye suluhisho la matatizo yote ya maisha, na pasipo yeye sisi hatuwezi kufanya lolote.

Yohana 15:5  “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote”.

Na nje ya Yesu Kristo hapana wokovu..

Matendo 4:12 “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo”

Je! Umempokea Yesu katika maisha yako?.. je umebatizwa katika ubatizo sahihi? Je umepokea Roho Mtakatifu wa kweli?. Kama bado unasubiri nini?

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JUMA LA SABINI (70) LA DANIELI

KWANINI YESU NI ADAMU WA PILI?

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA

JINA LAKO NI LA NANI?

BASI TUENDELEE KUMJUA MUNGU,NAYE ATATUJILIA KAMA MVUA YA VULI.

KWANINI TUNAPASWA KWENDA KUIHUBIRI INJILI KWA UJASIRI WOTE?

Rudi nyumbani

Print this post

AKAPITA KATIKA LILE SHAMBA AMBALO YAKOBO ALIMPA YUSUFU MWANAWE

Kuna wakati Bwana Yesu alianza safari ya kuchosha ya kutembea kutoka Yerusalemu kuelekea Galilaya..lakini maandiko yanatuonyesha katika safari yake yote hiyo hakuona mahali papote pa kupumzika, japo alikatiza katika vijiji na miji midogo midogo.

Lakini alipofika Samaria mahali ambapo hapakai wayahudi, aliingia katika eneo ambalo, huwenda alihisi amani  nyingi ya Mungu ikibubujika ndani yake, na hapo hapo akaona kisima cha maji akatulia apumzike kidogo.

Lakini maandiko yanatupa uelewa eneo hilo lilikuwa ni la namna gani mpaka likamfanya Yesu avutiwe nalo…yanasema..mahali pale palikuwa ni karibu na Shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe..

Yohana 4:3-8

[3]aliacha Uyahudi, akaenda zake tena mpaka Galilaya.

[4]Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria.

[5]Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe.

[6]Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita.

[7]Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe.

[8]Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula.

Yesu aliiiona ardhi ile katika roho, aliona mbaraka ule wa Yakobo kwa mwanawe Yusufu unavyomkaribisha pale, hivyo hakuweza kupita hivi hivi bila kutenda jambo…aliiona haki ya Yusufu inamlilia shambani kwake.. Kumbuka Israeli yote ilikuwa ni Milki ya wana wote wa 12 wa Yakobo, lakini si kila shamba la mwana wa Yakobo Yesu alipumzika.

Hivyo kitendo cha Yesu tu kutulia pale, kama tunavyojua habari watu wengi wa Samaria wakapokea wokovu akawaokoa watu ambao hawakustahili wokovu kabisa (yaani wasamaria).

Unaweza kujiuliza ni wakati gani Yakobo alimpa Yusufu shamba hilo? Waweza kusoma habari hiyo katika..Mwanzo 48:21-22

Utaona akipewa sehemu mara dufu ya wenzake.. Na hiyo yote ni kwasababu Yakobo alimpenda Yusufu kwa tabia zake njema.

Ile Tabia ya Yusufu ya kumcha Bwana alipokea thawabu sio tu za wakati ule alipofanyika kuwa waziri mkuu wa Misri.. Lakini tunaona pia hadi kipindi cha Bwana Yesu baraka zake bado zilitembea.

Leo hii ukimcha Mungu wewe kama kijana, utawasababishia wengine kupokea neema ya wokovu  hata wakati ambapo haupo hapa duniani.. Kumcha Mungu ni uwekezaji mkubwa sana zaidi ya mali.

Bwana akikubariki uzao, basi huwenda vitukuu vyako vikawa majesho hodari ya Kristo, kwasababu Yesu anapita kuangalia ni wapi mbaraka wa Yusufu upo  ili apumzike?akakuona wewe.

Akikubariki mashamba au mali, siku za mbeleni aidha uwapo hai au ufapo, Kristo atapita hapo na patakuwa kitovu cha madhabahu nyingi za Mungu.

Chochote kile ukiachacho duniani, kama sio mali, kama sio shamba, kama sio vitu..basi Mungu atatumia hata mifupa yako kuwaponya wengine.. Ndivyo Mungu alivyovyafanya kwa Elisha baada ya kufa na miaka mingi kupita ameshasahaulika, amebakia tu mifupa,kaburini, lakini maiti ilipoangukia mifupa yake, ile maiti ikafufuka.

Je ni tabia gani unaionyesha kwa Mungu sasa, hadi akupe shamba lake spesheli ambalo Kristo atakuja kupumzikia hapo siku za mbeleni? Watoto wako, vijukuu vyako, vitabrikiwaje kama wewe hutamcha Mungu sasa?

Tafakari maisha ya Yusufu, kisha fananisha na yako utapata majibu. Yatupasa tuichukie dhambi, tuchukie uasherati, tuchukie wizi, tuwe waaminifu, tuishi maisha yanayompendeza Mungu sikuzote. 

Na hatimaye na sisi tutakuwa wokovu kwa vizazi vyajavyo. 

Bwana atuponye..Bwana atusaidie.

Shalom

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

WALA HAKUSIMAMA MTU PAMOJA NAYE, YUSUFU ALIPOJITAMBULISHA KWA NDUGUZE

Je! habari ya Yusufu, inabeba ujumbe gani kwa agano jipya?

UVUMILIVU NA MIKAKATI YA ABSALOMU, INA FUNZA NYUMA YAKE.

Kuiaua Nchi ni kufanya nini? (Waamuzi 18:2).

Injili iliyopo kwa Samaki aina ya Eeli.

Rudi nyumbani

Print this post

HAKUONA MAHALI PA KUTUA KWA WAYO WA MGUU WAKE.

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze biblia, Neno La Mungu wetu.

Mwanzo 8:6 “Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya; 

7 akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huko na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi.

 8 Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi; 

9 bali YULE NJIWA HAKUONA MAHALI PA KUTUA KWA WAYO WA MGUU WAKE, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani”

Tunaona wakati wa Nuhu kutoka safinani… Aliwaachia ndege wawili ili kupima hali ya mazingira ya nje. Na ndege wa kwanza ambaye ni “KUNGURU” aliondoka lakini hakumrudia Nuhu.. lakini ndege wa pili ambaye ni “NJIWA” Alipoondoka na kukuta nje maji yamejaa kila mahali, alirudi safinani..

Sasa ni kwanini Njiwa arudi na kunguru asirudi?.

Siri ipo katika ile sura ya Saba, kuhusiana na wanyama Najisi na wasio Najisi.

Mwanzo 7:1 “Bwana akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki.

 2 Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, mume na mke; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mume na mke. 

3 Tena katika ndege wa angani saba saba, mume na mke; ili kuhifadhi hai mbegu juu ya uso wa nchi yote”

Sasa Kunguru yupo katika kundi la Ndege Najisi,

Walawi 11:13 “Kisha katika ndege hawa watakuwa ni machukizo kwenu; hawataliwa, ndio machukizo; tai, na furukombe, na kipungu;

14 na mwewe, na kozi kwa aina zake,

15 na kila kunguru kwa aina zake”

Na njiwa yupo katika kundi la ndege Safi (yaani wasio najisi) ndio maana alikuwa anatumika katika matoleo.

Sasa tabia ya ndege/wanyama najisi ni za tofauti na zile za wasio najisi. Wanyama najisi wanakula chochote na wanaweza kuishi popote.. lakini Wanyama/ndege wasio najisi wanachagua vitu vya kula, vile vile wanachagua mazingira ya kuishi, si kila mahali wanaweza kuishi.

Ndio maana tunaona huyu kunguru alipoachiwa, alienda kuzunguka zunguka huko nje, lakini njiwa aliona mazingira ya nje si salama, bado wakati wake, na hatimaye akarudi safinani.

Sasa wanyama najisi kiroho wanafananishwa na watu wa ulimwengu huu, walio mbali na MUNGU, na wanyama Safi (yaani wasio najisi) wanafananishwa na watu wa Mungu, waliookolewa kwa damu ya thamani ya YESU KRISTO, ambao hawajitii unajisi na mambo ya dunia.

Kama vile njiwa alivyozunguka huko na huko na kuona safinani ni mahali salama katika dunia iliyoharibika.. vile vile watu wa Mungu, kamwe hawawezi kuona hii dunia ipo salama, au ni mahali pa kustarehe kuliko safinani. Na safina ni BWANA YESU!.

Ukiona unaifurahia dunia iliyochafuka, dunia iliyojaa anasa, dunia iliyo mabaya basi katika roho wewe ni najisi.. Ukiona unaufurahia uasherati, ulevi, wizi unaoendelea duniani, na hata wewe mwenyewe kuwa mshirika wa hayo, basi fahamu kuwa unafanana na Yule kunguru! Na hivyo ni najisi mbele za Mungu kulingana na biblia.

Mathayo 15:18 “….vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi.

19  Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano;

20  hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi…”

Je! wewe ni miongoni mwa walio najisi au safi? Kama bado dhambi inatawala maisha yako basi upo hatarini hivyo suluhisho ni kumgeukia Yesu kwa kutubu na kumaanisha kuacha dhambi, na Yesu atakupokea na kukupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu, ambaye kupitia huyo atakutakasa kwa kukupa uwezo wa kufanya yale mema ambayo ulikuwa unashindwa kuyafanya kwa nguvu zako.

Kataa ukunguru!

Bwana akubariki

maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Kwanini Mungu aliwaita Adamu na Hawa jina moja?

JIHADHARI NA ROHO ZIDANGANYAZO.

Je mwanamke anaruhusiwa kupanda madhabahuni akiwa katika siku zake?

Mahali pa juu palikuwa ni wapi kama tunavyosoma katika biblia?

HUJAPEWA MBAWA ZA KUKIMBIA MATATIZO

Rudi nyumbani

Print this post

Je Yesu ni Mungu au Nabii?

Maandiko yanaonyesha kuwa YESU ni Mungu na pia ni NABII.  Ni sawa na mkuu wa nchi anaweza kuwa RAISI kwa wananchi, lakini pia anaweza kuwa BABA au MAMA kwa watoto wake. Hivyo mtu mmoja anaweza kuwa na vyeo zaidi ya kimoja kufuatana na mazingira aliyopo. Raisi akiwa ofisini ataitwa Raisi, akiwa nyumbani kwake na watoto wake ataitwa Baba/mama.

Vile vile Kristo akiwa mbinguni ni Mungu, akiwa duniani ni Mwana wa Adamu na Nabii na Mwokozi, na akiwa ndani yetu ni Roho Mtakatifu.

Sasa ni wapi maandiko yanatuonyesha kuwa Yesu alikuwa ni Nabii?

Luka 24:19  “Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, ALIYEKUWA MTU NABII, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote”

Kumbukumbu 18:15 “Bwana, Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni yeye”.

Vile vile ni wapi maandiko yanatuonyesha kuwa Yesu alikuwa Mwana wa Mungu?

Mathayo 16:15  “Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?

16  Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.

17  Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni”

Na ni wapi maandiko yanatuonyesha kuwa YESU alikuwa Mungu?

Tito 2:13  “tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu”

Soma pia 1Timotheo 3:16 na Yohana 1:1.

Kwahiyo Yesu ni yote katika vyote, na ndio Mwokozi wa Ulimwengu, na ndiye Njia ya kufika mbinguni. Hakuna mwanadamu yeyote atakayefika mbinguni isipokuwa kwa njia yake yeye.

Je umempokea Yesu?.. Kama bado unasubiri nini?

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Bwana Yesu alikufa akiwa na umri gani?

Je shetani anaweza kushusha moto kutoka mbinguni?

Tofauti kati ya maandiko na Neno ni ipi?

KUMBE MUNGU ANAWEZA KUKULIPA KWA USICHOSTAHILI!

AKAZIDI KUENDELEA KATIKA HEKIMA NA KIMO.

Rudi nyumbani

Print this post

Kalibu maana yake nini? (Mathayo 6:30).

Mathayo 6:30 “Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba?”

Neno hili “kalibu” limerudiwa pia kutajwa katika Luka 12:28, na maana ya neno hili ni “TANURU LA MOTO”. Kwa kawaida baada ya kusafisha mazingira, kwa kuondoa Nyasi au takataka huwa zinatupwa katika tanuru la moto, sasa tanuru hilo ndilo linaloitwa “Kalibu”, Na Bwana Yesu alitoa mfano huo kuonyesha maisha yetu jinsi yalivyo na thamani mara nyingi zaidi kuliko maua ya kondeni.

Kwani kama Mungu anavyoyavika utukufu maua ya kondeni, kwa rangi zangi zake za kuvutia, basi sisi ni zaidi sana mbele zake kuliko hayo MAUA ya kondeni, ambayo leo yapo lakini kesho yanatupwa motoni.. Sisi tuna thamani mbele zake kuliko maua, maana yake sisi atatuvisha zaidi kuliko Maua, atatulisha zaidi kuliko ndege, atatubariki kuliko viumbe vyote vya asili. Huo ni upendeleo wa kipekee sana.

Tunachopaswa kufanya ni kuutafuta tu ufalme wake na haki yake, halafu hayo  mengine ya chakula, mavazi tumwachie yeye, kasema atatuzidishia, na yeye kamwe hawezi kusema uongo.

Luka 12:29 “Ninyi msitafute mtakavyokula wala mtakavyokunywa; wala msifanye wasiwasi,

30  kwa maana, hayo yote ndiyo watafutayo mataifa ya duniani, lakini Baba yenu anajua ya kuwa mna haja na hayo.

31  Bali utafuteni ufalme wa Mungu, na hayo mtaongezewa.

32  Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme”

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Je suruali ni vazi la kiume tu?

Wakati wakina Shadraka wanatupwa katika tanuru la moto, Danieli alikuwa wapi?

JINA LA MUNGU NI LIPI?

Nyinyoro ni nini?

MWIMBIE BWANA ZABURI KATIKA NYAKATI ZA FURAHA.

Rudi nyumbani

Print this post

RUHUSU TOHARA IPITE JUU YA KARAMA YAKO.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo mwokozi wetu. Karibu tujifunze maneno yake ya uzima.

Ni wazi kuwa kila mmoja wetu anatamani kumzalia Mungu matunda mengi, anatamani kuona karama yake ikifanyika Baraka kwa watu wengi, anatamani kuona watu wakiokoka, watu wakijengeka, watu wakiinuliwa. Lakini anapoona haoni matokeo haya, katika hatua za awali za utumishi, anaishia kuvunjika moyo na kusema nachofanya ni kama sio huduma yake.

Lakini hajui kanuni za Mungu anazozitumia ili kutufikisha katika viwango vya uzaaji wa matunda. Bwana Yesu alisema, tukikaa ndani yake, na yeye ndani yetu, tutazaa sana,(Yohana 15:1-8)  Lakini bado wengi tunadhani kukaa ndani ya Bwana, ni kusema nimeokoka..hilo tu!. Jambo ambalo si kweli, wapo waliokaa kwa muda mrefu lakini hawazai matunda yoyote. Kukaa ndani ya Kristo sio tu kuokoka bali  ni kujua kanuni za Kristo za uzaaji wa matunda.

Tusome, maandiko haya, yatusaidie kuona jambo hili kwa undani.  Haya ni maagizo ambayo Bwana aliwapa wana wa Israeli kuhusiana na miti yao ya matunda watakayoipanda wafikapo Kaanani.

Walawi 19:23 “Nanyi hapo mtakapoingia nchi ile, mkiwa mmepanda miti ya namna zote kwa ajili ya chakula, ndipo mtayahesabu matunda yake kama ni KUTOTAHIRIWA; muda wa miaka mitatu miti hiyo itakuwa kwenu kama kutotahiriwa; matunda yake hayataliwa. 

24 Lakini mwaka wa nne matunda yake yote yatakuwa ni MATAKATIFU, kwa ajili ya kumpa Bwana shukrani.

25 Na katika mwaka wa tano mtakula katika matunda yake, ili ipate kuwapa MAONGEO YAKE; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu”.

Mungu anawaonyesha kanuni ya uzaaji matunda, ambayo imegawanyika katika hatua kuu tatu.

Hatua ya kwanza, ni ile miaka mitatu ya kwanza(Kutokutahiriwa):

Katika hii miaka miti huwa inazaa matunda, lakini matunda yale, huhesabiwa kama ni najisi: Wakulima wanaelewa vema kuwa sikuzote matunda ya kwanza, huwa ni dhaifu, hayana ladha nzuri, hivyo  wameapo, hukatwa na kutupwa, ili kupisha ukuaji mwingine, na umeaji mzuri wa matunda mapya kwa msimu ujao.

Kufunua karama zetu, pindi uokokapo, huna budi kuzaa matunda haya ya awali. Ambayo ki-msingi huwa hayana matokeo yoyote makubwa,  unaweza ukafanya kazi  ya Mungu ambayo ni kama vile haina matunda yoyote, utajiona haustahili, au haujui, lakini ni sharti uendelee kuzaa, kwa kipindi ulichowekewa mbele yako. Ukishavuta hatua hii,ndipo unaingia ya pili. Huwezi pelekwa nyingine kama hii ya kwanza hujapitia.

Hatua ya pili: Kuyafanya  matakatifu kwa Bwana.

Wana wa Israeli, bado hawakuruhusiwa, kuyala matunda yao, hata katika mwaka wanne, japo  matunda yanakuwa yameshakomaa na kukidhi kuliwa kabisa, lakini hawakuruhusiwa kuyala, bali waliagizwa wayatoe wakfu kwa Bwana. Hii maana yake ni nini, karama au huduma uliyopewa, wapaswa uigharimie wewe, hapa ni kukubali kujitoa kikamilifu katika wito huo uliopewa na Mungu. Nguvu zako, akili zako zote, hata mali zako ziwekeze kwa Bwana. Watu wengi,wafikapo hatua hii,wanasema huku ni kugumu, uzalendo umenishinda, tena nimpe Mungu, badala yeye ndio anipe mimi. Ndivyo hata huyu mkulima anavyowaza, nimesubiria miaka yote hii mitatu ‘matunda yanakuja na kuanguka tu’, halafu mwaka huu wa nne, badala  nifaidi, nashangaa, kuambiwa nimtolee tena Bwana. Ndugu hiyo ndiyo kanuni ya Ki-Mungu. Kutoa! Hakuepukiki kwa Bwana.

Hatua ya tatu: Maongeo.

Maongeo ni maongezeko, yaani Baraka. Au kuzaa kupita kiasi.

Katika mwaka wa Tano, ndio mkulima anaanza kuona faida ya kazi yake yote. Miti ya waisraeli ilibarikiwa kipekee tofauti na ile ya mataifa mengine,kwasababu ilifuata  kanuni hii ya Mungu. Walikuwa wanavuna kupita kiasi, kila mwaka mizeituni, mizabibu, tini, ilitoa matunda mengi kupita miti yote ya matunda ulimwenguni.

Nasi pia, tufikie hatua ya kuona maongeo katika huduma zetu. Hatuna budi, kwanza kutumika kwa uaminifu na kwa uvumilivu kwa kipindi Fulani,bila kuona faida yoyote inayoeleweka katika huduma/karama zetu, hatuna budi kupitia kukosea sana, unamuhubiria mtu, unadhani atasimama, kesho anarudi nyuma, matunda yako ni kama kazi bure. Lakini hilo halina budi lifanyike, kamwe mambo hayaji ndani ya siku moja, fanyia kazi kwanza kile ulichopewa,bila kujali matokeo ya nje.

Vilevile Baada ya kipindi Fulani. Utagharimika, ujitoe, haswaa, katika huduma/karama  hiyo. Hapa usizuie chochote ulichonacho, unampa Mungu vyote, kama malimbuko kwake, hii ni kuonyesha upendo wako kwa hicho unachotaka umzalie Mungu matunda.

Na mwisho. Bwana anabariki.  Matunda yanakuja, katika utimilifu wote. Maono yako yanatimia, karama yako  inakuwa sababu ya wengi kumgeukia Mungu.

.Lakini kumbuka “Kamwe usikae tu na kusema siku moja nitafikia pale” bila kuonyesha bidii sasa. Utamaliza miaka 20 katika wokovu, hujamzalia Mungu tunda lolote. Bwana atusaidie kulitambua hili.

Njia mojawapo ya kutambua hicho ulichopewa ni karama yako, ni kusikia msukumo wa kukifanya kwa Mungu. Huo msukumo utendee kazi sana. Utakuwa msaada mkubwa sana mbeleni.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NITAIFAHAMU VIPI KARAMA YANGU?.

ICHOCHEE KARAMA YAKO.

Maongeo ni nini?(Wakolosai 2:19)

NENO LA MUNGU NI UFUNUO MKAMILIFU.

NI KWA NAMNA GANI ROHO HUTUTAMANI KIASI CHA KUONA WIVU?

TWAENENDA KWA IMANI NA SI KWA KUONA.

NI KWASABABU YA YESU KRISTO.

Rudi nyumbani

Print this post