Mashonde ni nini? (Ezekieli 4:15).

by Admin | 21 December 2023 08:46 am12

Swali: Mashonde ni kitu gani kama tunavyosoma katika Ezekieli 4:15, na yamebeba ufunuo gani?

Jibu: Turejee..

Ezekieli 4:12“Nawe utakila kama mkate wa shayiri, nawe utakioka mbele ya macho yao juu ya MASHONDE YATOKAYO KATIKA MWANADAMU”.

“Mashonde” ni jina lingine la “kinyesi kikavu” aidha cha mwanadamu au mnyama.

Zamani na hata sasa katika maeneo baadhi, kinyesi kikavu kimetumika kama chanzo cha nishati, kwasababu kinawaka kwa haraka zaidi hata ya kuni, Hivyo kinaweza kutumika kama mbadala wa kuni kama kikiwa kwa wingi.

Katika maeneo ya mashariki ya kati, vinyesi vikavu vya ngamia na ng’ombe vilitumika kwa sana kama chanzo cha nishati, na nyakati chache chache sana (hususani vipindi vya ukame na dhiki), na vilitumika hata vya wanadamu lakini vyote vilikuwa ni vikavu….lakini sasa vinatumika hata vibichi kutokana na kukuwa kwa teknolojia.

Sasa tukirejea katika biblia, tunasoma Nabii Ezekieli akipewa maagizo na Mungu kuwa aoke mkate aina ya shayiri juu ya Mashonde (yaani kinyesi) cha mwanadamu, maana yake atumie kinyesi cha mwanadamu kama chanzo cha nishati, badala ya cha Wanyama. Sasa changamoto ya kutumia vinyesi, aidha vya mwanadamu au mnyama kama nishati ni “harufu”.

Maana yake kile kitakachopikwa juu ya mashonde (kinyesi) fulani kitabeba harufu ya kile kinyesi husika, kwahiyo kama mkate utaokwa juu ya kinyesi cha ngamia, basi ule mkate kwa sehemu utatoa harufu ya kinyesi cha ngamia, vile vile kama umeokwa juu ya kinyesi cha mwanadamu basi utatoa harufu ya kinyesi cha mwanadamu.

Hivyo Mungu alimwambia Ezekieli atumie kinyesi cha Mtu, kutengeneza huo mkate na kisha aule!.. Lengo la kumwambia vile si kumwadhibu Ezekieli, la! Kwani Ezekieli alikuwa ni nabii wa Mungu mwaminifu sana, hivyo aliambiwa afanye vile ili awe ishara kwa Taifa la Israeli kama Hosea alivyokuwa ishara kwa Taifa la Israeli alipoambia akaoe mwanamke wa uzinzi.

Maana yake kwa Ezekieli kula mkate uliookwa juu ya kinyesi cha mtu, ni ujumbe kwa wana wa Israeli kuwa na wao watakwenda utumwani mahali pa dhiki nyingi, na watapitia shida na njaa kali hata kufikia hatua ya kukosa chanzo bora cha nishati na hivyo kuona hata kinyesi chao wenyewe chaweza kufaa kwa nishati ya kuokea mikate ili tu waweze kuzishibisha nafsi zao wasife kwa njaa.

Hivyo Bwana Mungu alimchagulia Ezekieli hiyo ishara, lakini tunasoma Ezekieli alimsihi Bwana ambadilishie hiyo ishara kwani hakuwahi kula kitu najisi tangu amezaliwa, (kwasababu kulingana na desturi za kiyahudi kitu chochote kilichookwa juu ya kinyesi ni najisi), Hivyo akamsikia kwa ombi hilo, na Bwana Mungu akambadilishia, badala ya kutumia kinyesi cha mtu, basi atumie cha Ng’ombe, na ndivyo Ezekieli alivyofanya kama tunavyosoma…

Ezekieli 4:13 “Bwana akasema, Hivyo ndivyo wana wa Israeli watakavyokula chakula chao, hali kimetiwa unajisi, kati ya mataifa nitakakowafukuza

14 Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, tazama, roho yangu haikutiwa unajisi; maana tangu ujana wangu hata sasa sijala nyamafu, wala iliyoraruliwa na hayawani; wala nyama ichukizayo haikuingia kinywani mwangu.

15 Ndipo akaniambia, Tazama, NIMEKUPA MASHONDE YA NG’OMBE badala ya mashonde ya mwanadamu, nawe utakipika chakula chako juu ya hayo.

16 Tena akaniambia, Mwanadamu, tazama, nitalivunja tegemeo la chakula katika Yerusalemu; nao watakula mkate kwa kuupima, na kwa kuutunza sana; nao watakunywa maji kwa kuyapima, na kwa kushangaa;

17 wapate kupungukiwa na mkate na maji, na kustaajabiana, na kukonda kwa sababu ya uovu wao”.

Ni nini tunajifunza katika Habari hiyo?

Kikubwa tunachoweza kujifunza ni kuwa “tunapomwacha Mungu na kufuata mambo yetu, tunajiweka katika hatari ya kuharibu Maisha yetu kuanzia ya rohoni mpaka ya mwilini”.  Wana wa Israeli hapa walimwacha Mungu na matokeo yake Maisha yao yaliharibika kwa njaa na umasikini na utumwa mpaka kufikia hatua ya kula mikate iliyookwa juu ya vinyesi vyao wenyewe, na ni hivyo hivyo hata leo, (kwasababu Mungu ni yule yule hajabadilika)… kama tukigeuka na kufuata mambo yetu, basi Maisha yetu yataharibika hata zaidi ya hayo ya wana wa Israeli nyakati hizo.

Je umempokea YESU KRISTO, kama Bwana na Mwokozi wa Maisha yako?

Bwana atusaidie.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

EZEKIELI, ITABIRIE MIFUPA MIKAVU.

HERI YULE ATAKAYEKULA MKATE KATIKA UFALME WA MUNGU.

Roho Mtakatifu ni nani?.

Kuna tofauti gani kati ya  “Edeni” na “Adeni”?

Bawa la mbuni hufurahi; Lakini mabawa yake na manyoya yake, je! Yana huruma? 

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/12/21/mashonde-ni-nini-ezekieli-415/