Watu wengi wanajiuliza Roho Mtakatifu ni nani? Jibu rahisi ni kuwa Roho Mtakatifu ni Roho ya Mungu, Mungu anayo Roho kama vile mwanadamu alivyo na roho, hakuna mwanadamu yeyote asiye na roho.
Na Biblia inasema katika Mwanzo 1:26 kwamba Mwanadamu aliumbwa kwa mfano na sura ya Mungu. Ikiwa na maana kuwa kama mwanadamu ana nafsi halikadhalika Mungu naye anayo nafsi, na kama mwanadamu anayo roho vilevile na Mungu naye anayo Roho. Kwasababu tumeumbwa kwa sura yake na kwa mfano wake. Na kama vile mwanadamu anao mwili halikadhalika Mungu naye anao mwili.
Na Mwili wa Mungu si mwingine zaidi ya ule uliodhihirishwa pale Kalvari miaka 2000 iliyopita. Nao ni mwili wa Bwana Yesu Kristo, hivyo Yesu Kristo ndiye Mungu mwenyewe aliyedhihirishwa katika Mwili. Hivyo aliyemwona Yesu amemwona Mungu (Yohana 14:8-10)
1Timotheo 3:16 “Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu”.
Huyo ni Yesu anayezungumziwa hapo.
Na kadhalika roho iliyokuwepo ndani ya Mwili wa Bwana Yesu Kristo ndio Roho ya Mungu na ndiye ROHO MTAKATIFU MWENYEWE. Tunalithibitisha hilo katika kitabu cha.
Matendo 16:6 “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. 7 Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, 8 wakapita Misia wakatelemkia Troa”.
Matendo 16:6 “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia.
7 Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa,
8 wakapita Misia wakatelemkia Troa”.
Sasa utauliza kama Roho wa Yesu ndiye Roho Mtakatifu iweje mahali pengine Bwana Yesu anaonekana amejaa Roho Mtakatifu?. Na mahali pengine anaonekana Roho Mtakatifu akishuka juu yake?
Jibu ni kwamba, Roho wa Mungu hana mipaka kama roho zetu sisi wanadamu zilivyo na mipaka, sisi wanadamu Mungu alivyotuumba roho zetu mipaka yake ni katika miili yetu.
Haziwezi kutenda kazi nje ya fahamu zetu au miili yetu.Haiwezekani niongee na wewe hapa na wakati huo huo roho yangu ipo China. Hilo haliwezekani kwetu sisi wanadamu, isipokuwa kwa Mungu linawezekana. Roho wake anauwezo wa kuwa kila mahali, ndio maana wewe uliopo Tanzania utasali muda huu na mwingine aliyepo China atasali na mwingine aliyeko Amerika atakuwa anamwabudu Mungu muda huo huo na wote Roho Mtakatifu akawasikia na kuwahudumia kila mtu kivyake. Huyo huyo anao uwezo wa kuwepo mbinguni, na duniani ndani ya Mwili wa Bwana Yesu na wakati huo huo kuzimu, hakuna mahali asipofika.
Ndio maana utaona alikuwa ndani ya Kristo, na bado akashuka juu ya Kristo, na akaachiliwa juu yetu siku ile ya Pentekoste.
Hiyo ndiyo tofauti ya Roho wa Mungu na roho ya mwanadamu. Roho zetu zina mipaka lakini Roho wa Yesu hana mipaka.
Na ni kwanini Roho wa Yesu anajulikana kama Roho Mtakatifu?
Ni kwasababu yeye ni Roho Takatifu, hiyo ndio sifa kubwa na ya kipekee Roho wa Yesu aliyoibeba..Yeye ni mtakatifu na hachangamani na uchafu.
Na ndio maana uthibitisho wa Kwanza kabisa wa Mtu aliyempokea Roho Mtakatifu ni kuwa Mtakatifu. Umepokea uwezo wa kufanyika mwana wa Mungu, unakuwa kama YESU. Naamini mpaka hapo utakuwa umeshafahamu Roho Mtakatifu ni nani?
Je! Umepokea moyoni mwako? kama bado ni kwanini? Biblia imesema ahadi hiyo ni ya bure na tunapewa bila malipo, kwa yeyote atakayemwamini.
Matendo 2:39 “Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”.
Gharama za kumpata huyo Roho si fedha bali ni Uamuzi tu! Ukimtafuta Mungu kwa bidii utampata Neno lake linasema hivyo..
Hivyo kanuni rahisi sana ya kumpata ni KUTUBU kwanza: Yaani unamaanisha kuacha dhambi kwa vitendo, kisha kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji tele (Yohana 3:23) na kwa jina la Yesu kwaajili ya ondoleo la dhambi kulingana na Matendo 2:38 ili kuukamilisha wokovu wako. Na Roho Mtakatifu ataingia ndani yako, atakayekupa uwezo wa kuwa kama yeye alivyo yaani Mtakatifu. Vilevile atakushushia na karama zake za Roho kwa jinsi apendavyo yeye juu yako. Hapo ndipo utakapopokea uwezo wa kuwa shahidi wake
Kumbuka biblia inasema wote wasio na Roho Mtakatifu hao sio wake (Soma Warumi 8:9), Hivyo ni wajibu wetu sote kumtafuta Roho Mtakatifu kwa bidii sana. Kwasababu hutaweza kumjua Mungu, wala kupokea uwezo wa kuishinda dhambi kama huna Roho Mtakatifu ndani yako.
Bwana akubariki.
Maran Atha !jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
KWANINI YESU KRISTO ALIKUJA DUNIANI?
JE UNATAMANI KUMJUA MUNGU, NA HUJUI PA KUANZIA?
KWANINI YESU KRISTO NI MWANA WA DAUDI?
ROHO HUTUOMBEA KWA KUUGUA KUSIKOWEZA KUTAMKWA!
KAMA MUNGU ANABORESHA KAZI ZAKE, KWANINI WEWE USIBORESHE ZA KWAKO?.
Rudi Nyumbani:
Print this post