JE UNATAMANI KUMJUA MUNGU, NA HUJUI PA KUANZIA?

JE UNATAMANI KUMJUA MUNGU, NA HUJUI PA KUANZIA?

Ukiwasimamisha watu wawili mbele yako, mmoja daktari na mwingine mtu wa kawaida ambaye hajasoma, halafu ukawaonyesha wote wawili ndege ya kivita inayopaa hewani, kisha ukawauliza swali moja jepesi “ Je! Ile mnayoiona juu ni kazi ya nani”….moja kwa moja Yule mtu ambaye hajasoma atakuambia bila shaka ile ni kazi ya mtu,.. lakini Yule daktari si rahisi kwake kutoa jibu la kiwepesi wepesi hivyo, kulingana na kiwango chake cha elimu kumuhusu mwanadamu, atakuambia “mimi ninaona kazi ya ubongo wa mwanadamu”

Sasa ikiwa wewe ndio umeweka utoe alama hapo, ni nani kapata na nani kakosa, utatoa jibu gani?..Ni wazi kuwa Utagundua kuwa wote wawili wapo sahihi, isipokuwa tu Yule daktari kwa kuwa ameshamsoma sana mwanadamu katika fani yake ya utabibu aliyoipitia na kujua kuwa kilichondani ya mwanadamu ndicho kilichofanya kazi ile, hakuishia tu juu juu kumtaja mtu, bali aliingia ndani zaidi mahali huo uutu wake unaomfanya kuwa mtu unapotokea na hapo si pengine zaidi ya kwenye ubongo..hapo ndipo panapomtofauti kuwa huyu ni nyani na huyu ni mtu.

Vivyo hivyo, kwa mtu wa kawaida tu akiulizwa hii unayoiona duniani ni kazi ya nani, asilimia 99 watakuambia tunaona kazi ya Mungu, lakini ni wachache sana watakuambia tunaona kazi ya Neno la Mungu, ambapo huo ndio ubongo wa Mungu wenyewe. Kwa hilo ulimwengu mzima uliumbwa kwalo.

Webrania 11:3 “Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo Dhahiri”.

Lakini watu wengi wanachanganyikiwa wakidhani kuwa Neno la Mungu ni tofauti na Mungu..Kwamba ile ni nafsi nyingine ya tatu ya Mungu..Embu turudi pale kwenye ule mstari wa

Yohana 1:1 inaposema:

“1 Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.

2 Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.

3 Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika”.

Sasa embu tumfananishe Yohana na Yule daktari mwenye elimu, ni wazi kuwa angesema maneno yake hivi “tangu zamani ubongo ulikuwepo, na huo ubongo ulikuwepo ndani ya mtu, na huo ubongo ndio mtu mwenyewe, vyote vimefanyika kwa huo, wala pasipo huo hakuna ndege yoyote ya kivita ingeweza kuumbwa au kitu chochote kile”..

Umeona hapo, Ndivyo ilivyo kwa hata katika habari za Neno la Mungu ndio Ubongo wa Mungu, huwezi kulitenga Neno lake na yeye, kwasababu yeye ndio Neno lenyewe..

Tunajua kabisa taarifa zote zimuhusuzo mwanadamu, na ufahamu wake wote upo kwenye ubongo kibaolojia, kwamba ukitaka kujua siri zake basi cheza na ubongo wake, ukitaka kujua uwezo wake wa kufikiri au kufanya mambo, au kuamua, basi cheza na ubongo wake, lakini kama ukijifanya unaweza kumfahamu Mtu kwa kumwangalia tu sura yake au urefu wake, au uzuri wake, au kazi zake, utapotea na usiambulie chochote ..

Vivyo hivyo na leo hii, ili umwelewe Mungu, huna budi kuusoma ubongo wake, na ubongo wake ni Neno lake, hutakaa umjue Mungu kwa vitu alivyoviumba, hutakaa umjue Mungu kwa maajabu anayoyafanya, utamjua Mungu kwa Neno lake tu..basi..

Kama ni hivyo basi? Je hili Neno lake likoje likoje na tutalipata wapi?.

Mungu alijua shida itakuja hapo kwa wanadamu, hivyo akatugawia ofa kubwa sana, ambayo hakuna mtu angeweza kufiki kama Mungu angekaa afanye kitu kama hicho, na ofa hiyo si nyingine zaidi ya kuliundia Neno lake mwili kama ule ule wa binadamu, na kulifanya liishi na wanadamu, liongee, lizungumze nao, liulizwe maswali, litufundishe sisi namna ya kumjua Mungu, na kumfikia yeye..na huo mwili ndio ule ulioitwa YESU KRISTO, mwana wa Mungu aliye hai, Haleluya!! (1Timotheo 3:16)

1Yohana 1:1 “Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima;

2 (na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena twashuhudia, na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu);”

Sasa unaweza kuona kazi imerahisishwa, tunaweza kujua siri zote na ufahamu wote wa Mungu kama tutaweza kumfahamu vizuri YESU KRISTO na kuyafuata maagizo yake yote aliyotuagiza. Yeye ndio huo Ubongo wa Mungu unaozungumza na sisi kila siku..Tukiyashika maneno yake basi hakuna kitu chochote kitakachoshindikana kwetu.

Hivyo, ikiwa unahitaji kumjua Mungu au kumkaribia na kuzungumza naye, au kuzijua siri zake zote, hatua ya awali kabisa ya kuanzana nayo ni kumwamini YESU KRISTO, na kumpa maisha yako ayaongoze..Na hiyo inakuja kwa kutubu kwanza dhambi zako zote mbele zake kwa kumaanisha kabisa kuziacha, na kutokuzifanya tena, kisha ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi kwa jina la Yesu Kristo kulingana na Matendo 2:38 kama hukuwahi kubatizwa, nawe utakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu. Na kuanzia huo wakati na kuendelea ataanza kukupa uelewa wa kumjua Mungu, kwa namna ambayo hukuwahi kuijua.

Lakini ukitafuta kumjua Mungu kwa nje nyingine mbali na YESU KRISTO,..Hesabu kuwa umepotea. Kwasababu maandiko yanasema katika

Yohana 14:6 “ Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”

Ubarikiwe sana. Tafadhali “Share” ujumbe huu Na kwa wengine.

Na Bwana atakubariki.

Mada Nyinginezo:

KWANINI YESU KRISTO ALIKUJA DUNIANI?

TABIA YA KIPEKEE USIYOIJUA KUHUSU NENO LA MUNGU.

NENO LA MUNGU KATIKA UTIMILIFU WOTE.

MZEITUNI HALISI UTAKAPOPACHIKWA.

SADAKA ILIYOKUBALIKA.

NI WAKATI GANI SHETANI ANAPENDA KUMSHAMBULIA MWAMINI?


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
M
M
1 year ago

Amina