TABIA YA KIPEKEE USIYOIJUA KUHUSU NENO LA MUNGU.

TABIA YA KIPEKEE USIYOIJUA KUHUSU NENO LA MUNGU.

Ukisoma vitabu vya Injili utaona mfano wa kwanza kabisa BWANA YESU alioutoa ni ule mfano wa Mpanzi, utaona jinsi mpanzi alivyotoka na kwenda kupanda mbegu zake, ukiendelea kusoma pale utagundua kuwa ule mfano haukueleweka kwa wengi, sio tu kwa makutano bali pia kwa wanafunzi wake..Lakini walipomfuata na kumwomba awafafanulie kuna kauli Bwana Yesu aliitoa pale nataka tuione; nayo ni hii:

Marko 4.13 ‘Akawaambia, Hamjui mfano huu? BASI MIFANO YOTE MTAITAMBUAJE?’.

Tafakari hilo Neno, BASI MIFANO YOTE MTAITAMBUAJE?..Kumbe Mfano huo ni msingi wa kuielewa na mifano mingine yote iliyobakia, kwa watu wanaofahamu somo la Hisabati vizuri wanaelewa kuwa kanuni ya PAI π..Ni kiungo kikuu cha Hisabati, ukitaka kutafuata Eneo la kitu chochote kile iwe ni duara au tufe, pipa, n.k. basi PAI ni lazima itumike.

Vivyo hivyo tukirudi kwenye maandiko ili kuielewa mifano yote Yesu aliyokuwa anaifundisha kuhusiana na ufalme wa mbinguni basi tafsiri ya mfano ule wa Mpanzi ni lazima kuulewa vinginevyo hutaambulia chochote.

Sasa tukirudi katika huo mfano kwa kuwa unajulikana hatutaweza kuuleza wote hapa, lakini mpanzi Yule alipotoka kwenda shambani malengo yake yalikuwa ni mbegu zake zote zimee vizuri na kuzaa nyingine 30, nyingine 60, nyingine 100. Lakini tunasoma zilikumbana na changamoto kadhaa kabla ya kufikia hatua ya kuzaa matunda.

Sasa kabla hatujafika mbali nataka tuone mifano miwili iliyofuata mbele yake baada ya huo..Ili itusaidie kuunga kiini cha somo letu la leo vizuri ..

Tusome..

Marko 4:26 ‘Akasema, Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi;

27 akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye.

28 Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke.

29 Hata matunda yakiiva, mara atapeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika.

30 Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie katika mfano gani?

31 Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi,

32 lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake.

33 Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia’.

AMEN.

Sasa Nataka tuichukue kwa pamoja mifano hii mitatu, tuunde kitu ambacho kitatusaidia wote,..Mifano hii, yote inaonyesha historia ya mbegu, jinsi zilipotoka na jinsi zilivyoishia isipokuwa katika TABIA tofauti tofauti na mapito tofauti tofauti.

Kumbuka kule nyumba kabisa kwenye mfano wa mpanzi Bwana Yesu alitoa tafsiri ya Ile mbegu kuwa lile ni NENO LA Mungu (Luka 8:11) lililopandwa ndani ya moyo wa mtu. Hivyo Neno la Mungu linapopandwa katika moyo wa mtu katika hatua za awali penda lisipende litapita katika nyakati TATU kulingana na mifano hiyo mitatu.

1) ⏩Kwanza ni lazima lipitie changamoto: Mtu aliyepandwa atakumbana na udhia, na misongo ya hapa na pale, kulingana na ule mfano wa mpanzi, Hili ni jukumu la mhusika mwenyewe kuhakikisha kuwa haling’olewi na Yule adui, wala halisongwi.

2)⏩ Pili Litakuwa linamea lenyewe: Hili sio jukumu tena la mtu, bali ni jukumu la Mungu mwenyewe, wakati linavumilia vipindi vigumu vya hatihati ya kung’olewa au kusongwa, huku kwa nyuma siku baada ya siku linakuwa lenyewe taratibu.

3) ⏩Na Tatu japo litaanzia katika udogo sana, likishafikia ukomavu litakuwa kubwa kuliko miti mingine yote. Hivyo mwisho wa safari ya utunzaji wa mbegu ile. Basi litakuwa baraka kubwa sana kuliko chochote kile duniani.

Hivyo ndugu, ndio maana sasa baada ya mifano ya namna hiyo kuisha YESU akaanza kuwafundisha watu mifano inayoelezea thamani ya mbegu hiyo akiifananisha na Hazina kubwa sana na lulu za thamani ..utaona anasema, ufalme wa mbinguni umefanana na mfanyabiashara aliyekuwa anatafuta Lulu ya thamani kubwa, na alipoina akaenda kuuza vyote alivyonavyo na kwenda kuinunua lulu ile, anasema tena ni sawa na mtu aliyeona hazina iliyositirika katika shamba, alipoiona akaificha na kwa furaha akaenda kuuza vyote alivyonavyo na kwenda kulinunua shamba lile.

Hiyo yote ni kuonyesha kuwa ana AKILI sana mtu yule anayelisikia Neno la Mungu na kuzingatia kuliweka moyoni mwake, na kwenda kufanyia kazi kile anachofundishwa, anafanya bidii kulifakari Neno la Mungu, analiona kama almasi, anatafuta huku na kule huku akilinganisha na maandiko, akivulimilia dhiki zote zinazokuja kutokana na ukristo wake na itikadi zake kali za kuliishi Neno, na shutuma na kuchekwa, na kudharauliwa, na kutengwa, na kuchukiwa, akivumilia yote bila kuliacha hilo Neno lililopandwa moyoni mwake kudondoka, akihakikisha shughuli za ulimwengu huu hazimsongi mpaka anakosa muda wa kuwa karibu na Mungu wake, akihakikisha anapata muda mrefu wa kulitafakari Neno la Mungu kuliko kuchati..

Sasa Biblia inaeleza mtu huyo kuna faida kubwa inamngoja mbeleni yake.. Yeye kwa wakati huo hatajua chochote, wala hatafahamu kama kuna kitu kinakuwa ndani yake, anaweza kuona kama anafanya kitu ambacho hakimletei faida yoyote katika mwili, hakimwingizii pesa, hakimpi umaarufu, lakini kumbe kidogo kidogo, ile mbegu inamea, kutoka KUWA MBEGU MPAKA JANI MPAKA SUKE.. Na japo ilianza ndogo sana kama chembe ya haradali itakuwa yenyewe, kumbuka haihitaji msaada wowote kukuzwa na mtu, itakuwa na kuwa kubwa kuliko miti yote, na ndipo hapo watu watakuja kushangaa, kumetokea nini kwa mtu huyu tusiyemtazamia amekuwa hivi ghafla…Ndipo kama mfano unavyosema ndege watakuja kukaa chini ya huo mti, ndivyo itakavyokuwa kwa mtu huyo, atakuja kuwa msaada mkubwa kwa watu wengi kwa kila kitu. Kwa vitu vya rohoni na mwilini.

Hiyo ilimtokea kiongozi wetu mkuu YESU KRISTO, Biblia inasema alikuwa ni mtu wa kudharauliwa, wa kutokuaminiwa siku zote, lakini yeye alilitunza Neno la Mungu tangu utoto wake, mpaka utu uzima, mpaka alipofikia kilele sasa cha Neno lenyewe kutaka kuanza kuzaa matunda, ndipo walipomtambua kuwa Yule hakuwa mwanadamu wa kawaida..Utasoma pale walianza kujiuliza huyu sio Yule seremala, na ndugu zake tunao wote hapa? Sasa katolea wapi hekima yote hii ambayo hajasoma, na miujiza yote hii, ulimwengu mzima ulimfuata kumsikiliza, yeye ni nani hasa? Ukisoma biblia utaona kuna watu walitoka mpaka Uyunani huko kuja kutaka kumwona Bwana Yesu…Hayo ndio maajabu ya Neno la Mungu likitunzwa vizuri ndani ya mtu…Linafanya mambo makubwa, na ndio maana shetani katika hatua za kwanza atahakikisha kwa bidii zote analiondoa ndani yako.

Hizi ni siri kutoka kwa MKUU wetu YESU KRISTO, Kwamba kama na sisi tukizitumia, tutafika pale alipo yeye. Leo hii, mbegu nyingi zinatupwa ndani yako, unazidharau, kwasababu labda mtu huyo anayekuhubiria hajulikani, ni mtu tu wa mtaani unayemfahamu, lakini kumbuka ufalme wa Mungu ndani ya mtu unaanza kama chembe ya haradali, ndogo sana, maneno ambayo mtumishi yoyote yule wa kawaida anaweza akayabeba ndani yake, inaanza kwa maneno machache sana ya wokovu, ambayo baadaye yakiisha kukua ndani ya mtu yanaweza kuupindia ulimwengu mzima.. Usipuuzie Neno la Mungu leo unapolisikia, embu chukua hatua ya kuanza kulitunza, anza kulifanyia kazi, hakikisha shetani hakichukui hichi ulichokisia moyoni mwako, na dalili zitakazoonyesha hiyo mbegu inakuwa ni maadui kutokea, shetani atafanya juu chini kuing’oa lakini wewe zingatia kanuni hizo, UVUMILIE yote, iwe ni dhiki, iwe ni misongo ya mambo ya ulimwengu huu..Fanya bidii kulitunza Neno la Mungu, faida yake utaiona baada ya muda Fulani.

Ni matumaini yangu, utatubu leo na kumkabidhi Bwana maisha yako. Huo ndio mwanzo wa kuitunza mbegu yao.

Ubarikiwe sana.

Amen.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Kwa Maombezi, Ushauri, au Ratiba za Ibada wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312


Mada Zinazoendana:

JE! WEWE NI MBEGU HALISI?

USIACHE KUJIFUNZA NENO LA MUNGU

NENO LA MUNGU KATIKA UTIMILIFU WOTE.

TUNAPOSEMA TUISHI KWA NENO, INAMAANISHA TUISHI MAISHA YA NAMNA GANI?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
1 year ago

Amina