NENO LA MUNGU KATIKA UTIMILIFU WOTE.

NENO LA MUNGU KATIKA UTIMILIFU WOTE.

Kitabu kinachoitwa BIBLIA, ambacho tunakifahamu kama Neno la Mungu, kiuhalisia sio Neno la Mungu katika utimilifu wote, hapana bali ni muhtasari au mwongozo wa sisi kulifahamu NENO LA MUNGU katika utimilifu wote. Kwasababu injili inasema katika Yohana 21: 25 “ Kuna na mambo mengi aliyoyafanya YESU; Ambayo yakiandikwa moja moja nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa.”….Pia Sulemani aliandika katika Mhubiri 12: 12 “ Tena zaidi ya hayo mwanangu kubali maonyo; hakuna mwisho wowote wa kutunga vitabu vingi…”

Unaona hapo kwahiyo Neno lote la Mungu likiandikwa katika vitabu biblia haisemi uongo ni kweli ulimwengu usingetosha kwa wingi wa vitabu ambavyo vingeandikwa, ni mabilioni kwa mabilioni ya vitabu, kungekuwa na milima ya vitabu ulimwenguni kote kulielezea Neno la Mungu.

Hivyo biblia ni kama ufupisho tu! (summary), wa Neno la Mungu. Kwahiyo ili tuweze kulielewa Neno la Mungu kwa namna ambayo Mungu anataka tulielewe, hatupaswi kuishia hapo kwenye summary peke yake, bali tunapaswa tuzame katika kina na mapana kwa kupitia muhstari ule (Biblia) ili tupate picha yote ya kusudi la Mungu katika maisha yetu kwa ujumla.

Biblia iliposema “UTAFUTENI KWANZA UFALME WAKE NA HAKI YAKE” (Mathayo 6:33)… haikumaanisha kumaliza kusoma vitabu 66 vya biblia, na kukariri mistari yote iliyomo kule, Hapana, wazia hili, mpaka mtu anakuambia utafute kitu Fulani, inamaanisha kuwa hicho kitu anachokuambia ukitafute hakipatikani kiwepesi, ni kitu kilichojificha na ndio maana anakuambia ukitafute, hivyo utahitaji jitihada ya ziada kukipata. Na ndivyo ulivyo ufalme wa mbinguni, upo katika SIRI.

Tuchukulie tu mfano mwepesi katika biblia pale Bwana YESU aliposema “WATAFAKARINI/WAANGALIENI NDEGE, hawapandi wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao je! Ninyi si bora mara nyingi kupita hao?” (Mathayo 6:25, Luka 12:24)..

Bwana Yesu alimtumia kunguru kama mmojawapo wa ndege hao kutupa siri mojawapo ya ufalme wa mbinguni inayohusianishwa na kanuni za kuishi kwa watoto wa Mungu, namna Mungu anavyowahudumia watoto wake. Akatoa mfano wa kunguru ambao tunao kila siku katikati ya jamii yetu, tunawaona maisha yao ni kweli hawapandi wala hawavuni lakini wanakula na kunywa,hawana hazina lakini kesho yake ni lazima wale. Sasa Bwana akasema sisi ni bora mara nyingi zaidi kuliko hao.

Pia tazama..

1 Hawa ndege katika Walawi 11:13-19 ndio ndege gani kwasasa?
2 Unyenyekevu ni nini?
3 Uru ya Ukaldayo ni nini?
4 NINI KINATOKEA BAADA YA KIFO?
5 Je Malaika Mikaeli ndiye Yesu mwenyewe?
6 Kwanini Bwana Yesu alivikwa taji ya miiba?
7 Kitanga/Vitanga ni nini?
8 Baali alikuwa nani?
9 Maana Ya Maneno Katika Biblia.
10 Upole ni nini?

Lakini tusiishie tu hapo, alisema Neno hili “WATAFAKARINI hao”, ikiwa na maana tusiwatafakari tu jinsi wanavyokula na wanavyokula, bali pia tuende zaidi ya hapo, tuwachunguze na jinsi wanavyoishi, wanavyozaliana wanavyojihudumia n.k ili tupate hekima nyingine ya ziada ndani yake…

Ni wazi kuwa kama Bwana angekuwa na muda wa kutosha angeendelea na kusema “watazameni kunguru jinsi wanavyoishi, hawali vyakula vizuri sana, lakini hawamezi vidonge wala hawana hospitali…” Je! Unahabari kuwa kunguru ni ndege anayeishi muda mrefu sana kuliko wanyama wengi mwituni na ndege wengi?.. Kunguru ni ndege anayekadiriwa kuishi zaidi ya miaka 80, hivyo wapo kunguru wenye umri mkubwa zaidi hata ya wa kwako na wanaishi mijini, lakini katika siku zote za maisha yao, hawajawahi kumeza kidonge wala kulazwa, japokuwa hawali vizuri kama wewe….

Sasa hapo ndio NENO LINAKUAMBIA JE! WEWE SI BORA KULIKO WAO?..kwa namna nyingine kama ukiamini kuwa Mungu anaweza kukufanyia zaidi ya wao, na kukujali zaidi ya wao unaweza kuishi maisha marefu pasipo kumeza vidonge, wala kwenda hospitali, wala pasipo kutazama sana ulaji bora kama ndio tiketi ya wewe kuishi muda mrefu..

Hapo tumetumia tu mfano wa kunguru, Lakini pale mwanzo Bwana alisema WATAZAMENI NDEGE.. Ikiwa na maana tutazame na jamii nyingine zote za ndege kwa jinsi tuwezavyo ili tupate hekima ya NENO LA MUNGU ndani ya maisha ya hivyo viumbe, kisha kwa IMANI tumwesabie Mungu anaweza kututendea sisi mara nyingi zaidi ya hao kwasababu yeye mwenyewe alishasema sisi ni bora mara nyingi zaidi ya hao.

(shomoro)

Tukianza kuchambua ndege mmoja mmoja hatutamaliza, lakini unaweza kumtafakari hata kuku ukapata hekima ya NENO LA MUNGU ndani yake, unaweza ukamtazama, mbuni, tai, njiwa, bundi, popo, mashomoro, Yesu aliwatolea mfano katika

Luka 12:6-7 “Je! Mashomoro watano hawauzwi kwa senti mbili? Wala hasahauliwi hata mmojawapo mbele za Mungu.

7 Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi bora ninyi kuliko mashomoro wengi”)

Kuna ndege wengine ukitafakari hekima Mungu alizoweka ndani yao utashangaa, wapo ndege ambao wao mara baada ya kutaga mayai yao, badala ya kuanza kuyaahatamia kama kuku au bata wafanyavyo, wao badala yake wanakwenda sehemu zenye milima ya volkano mahali palipo na joto Fulani, na kuyaacha mayai yao huko yapate lile joto, na baada ya muda Fulani kupita yale mayai yanajiangua vifaranga yenyewe kisha mama zao wanakuja kuchukua vifaranga vyao na kuondoka.. Neno la Mungu ni lile lile “Je! Ninyi si bora mara nyingi zaidi ya hao..? Inatufundisha nini hapo? kwamba zipo njia zilizozoelewa na watu wengi katika kufanikisha jambo Fulani, lakini ukimwamini tu Mungu kwamba anaouwezo wa kukufanyia na wewe kukutokezea njia Fulani pasipo kutumia nguvu nyingi kuzipata kama wengine…. Sasa hilo ni Neno la Mungu lililofichwa ambalo huwezi kulikuta moja kwa moja kwenye kitabu.

Alisema pia yatafakarini “MAUA YA KONDENI” hayafanyi kazi wala hayasokoti, nami nawaambia hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo.Basi ikiwa Mungu huyavika majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba?.

Tunayafahamu maua, hayajitaabikii kupata uzuri wake, jaribu kifikira zile harufu nzuri zinazotoka kwenye maua yale, je! Kuna mwanadamu yoyote anaweza kutoa harufu nzuri vile?. Lakini Mungu anatuonyesha nini? Anatuonyesha kwamba tukimwamini yeye, hata yale yaliyo mazuri zaidi ya hayo atatukirimia katika miili yetu ya udhaifu kwasababu sisi ni bora kuliko maua yote na miti yote kondeni.

Kadhalika mahali pengine Bwana Yesu alisema Ufalme wa mbinguni umefanana na “MFANYA BIASHARA” mwenye kutafuta lulu nzuri naye alipoiona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyonavyo vyote akainunua (Mathayo 13:45-46)

Hapo tunamwona Bwana Yesu akitufunulia siri nyingine ya ufalme wa Mungu iliyopo katikati ya wafanya biashara, kwanamna nyingine ili tuweze kulielewa neno la Mungu kwa mapana tunaweza kuwatafakari wafanya biashara wengi tulionao katika maisha yetu ya kawaida, wapo wafanyabiashara wa madini (ambao kwa hapa ndio Bwana Yesu aliowatolea mfano), Kwa namna ya kawaida mfanyabiashara wa madini akiona dini lolote linauzwa mahali kwa bei ya chini, na dini hilo hilo linanunulika kwa bei kubwa sehemu nyingine, ikiwa fedha aliyonayo haimtoshi kulinunua lile jiwe, atafanya sio tu kwenda kuuza mali zake bali pia hata kukopa, ataenda kukopa popote pale ili afikishe kile kiwango cha fedha kwasababu anajua akishalipata atakwenda kuliuza kwa bei ya juu hata mara mbili ya ile aliyonunulia na hivyo kufidia gharama zake zote alizoingia pamoja na faida yake juu.

Vivyo hivyo na katika mambo ya ufalme wa mbinguni.. faida yake na thamani yake mtu akishaiona hapa duniani na katika ulimwengu unaokuja..mtu bila shuruti anajikuta anagharimika kutii maagizo yote ya kuupata, ataacha kila kitu, ataacha mambo ya dunia, fasheni, anasa, wizi, ulevi, usengenyaji,rushwa n.k. ili tu aupate kwasababu anajua faida yake ni kubwa sana mbeleni.

Na sio tu wafanyabiashara wa madini peke yake, huo ni mfano mmojawapo tu Bwana Yesu alitupa ili sisi tupate hekima ya kuwatazama na wengine tujifunze zaidi.. wapo wafanyabiashara wa mazao, mafuta, simu, nguo, n.k.wanaotuzunguka, Ambao kila mmoja ukimchunguza utaona SIRI ZA UFALME WA MBINGUNI zimejificha ndani yao..Hilo ndio Neno la Mungu ambalo huwezi kuliona kwa utimilifu wote kwenye kitabu cha biblia.

Kadhalika Bwana aliwaangalia wakulima, akatoa mfano wa Yule mpanzi aliyekwenda kupanda mbegu zake nyingine zikaangukia kwenye miiba, nyingine kwenye miamba n.k. Ikifundisha jinsi Neno la Mungu linavyopandwa ndani ya mioyo ya watu, na umeaji wake. Hapo ulikuwa ni ukulima wa kale wa kutupa mbegu lakini sasahivi tunao ukulima wa aina nyingi. Kwamfano tunaweza kuitafakari hekima ya ukulima wa sasa..

Kuna wakulima wawili wamenunua mashamba mawili kila mmoja hekari 1000, mmoja akasema nitatumia nguvu zangu kulima shamba langu la hekari 1000 kwa jembe la mkono mpaka liishe, na mwingine akasema hii kazi ni kubwa sana, hivyo nahitaji kutafuta kitu cha ziada kunirahisishia kazi, yeye akaamua ule muda wa asubuhi kuamka na kwenda kulima autumie karakana kubuni nyenzo mbadala itakayomrahisishia yeye kufanya kazi ile kubwa.

Hivyo ilimchukua kweli muda wa mamiezi ya utafiti hatimaye akagundua chombo kinachoitwa TREKTA kulimia..Na wakati mwenzake yupo katika heka ya 600 ambayo kailima kwa miezi kadhaa yeye ndio analeta kifaa chake shambani kianze kazi..Na kilipoanza kazi kwa muda mfupi tu labda wiki moja tu kilikuwa kimeshamaliza kulima hekari zote 1000, lakini yule mwingine alitumia nguvu nyingi mwilini pasipo akili.

Vivyo hivyo inatufundisha nini kwa wakati huu?, utendaji kazi shambani kwa Mungu kwa wakati huu sio sawa na ule wa zamani, ilimchukua Mtume Paulo miaka mingi ya kuzunguka sehemu kubwa ya dunia kupeleka injili kutokana na kwamba nyenzo zilikuwa hafifu.

Lakini kwasasahivi tukitumia njia hiyo tutapata matokeo madogo na kutugharimu muda mrefu, hatuwezi tukategemea sauti zetu tu na wakati kuna vipaza sauti, hatuwezi tukategemea usafiri wa farasi wakati vipo vyombo vya moto, vitakavyokufikisha kwa muda mfupi na haraka, na kufikisha ujumbe ule ule. Hivyo hili ni Neno la Mungu pia ambalo huwezi kulikuta kwenye kitabu cha biblia moja kwa moja japokuwa lipo.

Mahali pengine Bwana alialikwa karamuni, huko huko akauona ufalme wa mbinguni ndani yake. Akatumia hiyo hiyo karamu ya kidunia kufananisha na karamu ya mwanakondoo, alisema Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyeandaa karamu yake, akaalika watu waliostahili waje lakini wakakataa kuja kila mmoja akatoa udhuru, hivyo yule mtu akaaagiza waitwe viwete, vipofu na viziwi kufidia nafasi za wale waliokataa kuja, na mwisho Bwana akasema ufalme wa mbinguni upo hivyo hivyo “walio alikwa ni wengi lakini wateule ni wachache”…Kwa namna ile ile tunaweza kujifunza kwa harusi na karamu za wakati huu wa sasa na kupata hekima nyingi kupitia hizo…

Kwamfano katika harusi za sasahivi ambazo nyingi ni za kipagani, sio kama zamani ambapo mtu yeyote tu alikuwa anaweza kujichomeka kwenye harusi, hapana siku hizi hauingii pasipo kadi, na kadi yenyewe hupewi pasipo mchango.. na mchango wenyewe sio tu ilimradi mchango, hapana ni kiwango Fulani kimewekwa, hata kama umechangia lakini hujafikia hicho kiwango, haupewi kadi..Inafunua siri za ufalme wa mbinguni, mtoto yeyote wa Mungu anapaswa ajue hilo ni NENO LA MUNGU..

Katika karamu ya Mungu hawataingia watu ambao hawajaalikwa, na kualikwa tu haitoshi unapaswa uchangie kitu katika karamu hiyo ili upewe kadi ya mwaliko, na kuchangia huko maana yake ni kuchangia kitu katika injili, mfano kuhubiri habari njema kwa wengine, kuchangia kazi ya Mungu kwa mali zako kwa sadaka na zaka, n.k. Hivyo tusidhani kama kumkabidhi Bwana maisha yetu tu! inatosha, la! Kuna kufanya zaidi, ili tujiweke katika nafasi nzuri ya kuingia katika ile karamu ya mwanakondoo, ambayo itafanyika mbinguni mara baada ya unyakuo.

Kadhalika Bwana alipokwenda kuwachagua wengi wa mitume wake aliwakuta katika kazi ya uvuvi, huko huko akawafunulia SIRI za ufalme wa mbinguni zilizokuwa zimejificha katikati ya shughuli zao za kila siku akawaambia:

Mathayo 13:47 “Tena ufalme wa mbinguni umefanana na JUYA, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna, 48 hata lilipojaa wakalivuta pwani, wakaketi wakakusanya walio wema vyomboni bali waliowabaya wakawatupa, ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; Malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki.”

Bwana Yesu alizungumza kwa mifano ya namna hiyo mingi na ndio maana akawaambia wanafunzi wake. NINYI MMEJALIWA KUZIFAHAMU SIRI ZA UFALME WA MBINGUNI, lakini wengine sivyo..Kwahiyo sisi wakristo tunapaswa tujifunze Neno la Mungu zaidi ya ule mwongozo tuliopewa. Na ndio hapo wengi wanakwama kwasababu wanategemea mwongozo kupata moja kwa moja majibu yao ya kila kitu…

Ndio hapo utakuta mtu anakuambia ni wapi kwenye biblia pameandikwa mtu asivute sigara, au asitoe mimba, au asitumie madawa ya kulevya, au asipake wanja, au asicheze kamari, asifanye mustarbation n.k….Hawafahamu kuwa biblia ilishazungumza juu ya hayo mambo lakini kwasababu hawajajaliwa kuzifahamu siri za ufalme wa mbinguni wanakuwa vipofu…

Lakini biblia ilishasema katika

Wagalatia 5:19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndio haya, uasherati, uchafu, ufisadi.

20 Ibada za sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitna, faraka, uzushi.

21 Husuda, ulevi, ulafi, NA MAMBO YANAYOFANANA NA HAYO,

katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.

Unaona hapo? Kitabu cha biblia kisingeweza kutaja mambo yote, na ndio maana ikafupisha kwa kusema NA MAMBO YANAYOFANANA NA HAYO…mambo yenyewe ndio hayo, uvutaji sigara, kamari, utoaji mimba, mustarbation, miziki ya kidunia, pornography, kupaka wanja kama Yezebeli, nk.

Hivyo ndugu, Neno la Mungu unalo hapo ulipo, ukisoma BIBLIA kwa kujifunza utaliona NENO LA MUNGU, lakini ukisoma Biblia kama kitabu tu, utaishia kujiona umefahamu kila habari iliyoandikwa na kuona hakuna jipya la kujifunza.

Bwana anasema UTAFUTENI KWANZA UFALME WAKE…Na yeye anasema ni mkuu kuliko Sulemani (yaani anayo hekima kuliko Sulemani) lakini Sulemani Biblia inamtaja aliitafuta tafuta hekima kwa bidii nyingi mpaka akaiona katikati ya wanyama wote, na miti yote.

1Wafalme 4: 32 Naye [Sulemani] akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano.

33 Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama na za ndege, na vitambaavyo, na samaki.

Unaona hapo,? Unaweza kujenga picha sasa Mfalme Mkuu, Mungu wetu YESU KRISTO yeye ambaye ni mkuu zaidi ya Sulemani alitoa mifano mingapi ihusuyo ufalme wa mbinguni kwa kutazama tu mambo yanayotuzunguka?. Hakika Vitabu visingetosha kuandika kila kitu alichokifanya na kusema.

Alituachia tu mwongozo katika kitabu kile kidogo (biblia) vingine sisi kwa msaada wa Roho Mtakatifu tunapaswa tufahamu na kuelewa kwa msaada wa kile..Hivyo ndugu fahamu kuwa hizi ni nyakati za mwisho, Ni wakati wa kuutafuta ufalme wa mbinguni kwa bidii..Leo hii tunajua shule zinazofaulisha huwa zinazingatia vigezo Fulani, utagundua kuwa nyingi zinakuwa ni za Bweni, na zina sheria kali katika masomo na katika ustaarabu, wanafunzi hawaruhusiwi kujihusisha na jambo lolote nje ya masomo, kama vile mapenzi, kazi, n.k.

Utakuta shule inazingatia uvaaji wa sare, kuweka usawa wa wanafunzi wote, kadhalika na waalimu nao wanazingatia kutimiza wajibu wao kufundisha wanafunzi kulingana na muhamala na kuwafauatilia..Hivyo mwisho wa siku shule hiyo unakuta inaleta matokeo mazuri kwa wanafunzi, kuliko shule nyingine ambazo hazizingatii hivyo vigezo…

Vivyo hivyo katika ukristo, Kanisa linafananishwa na shule, mwanafunzi bora ni yule atakayechagua shule itakayomletea matokeo mazuri mwishoni, atakuwa tayari kujizuia na mambo mengine ili kusudi kwamba apate kilicho bora, Mkristo kama mwanafunzi wa Kristo na mshirika wa kanisa hatojali gharama za kuwa mwanafunzi wa Kristo, atakapoambiwa aache kila kitu cha kidunia, ajitenge na uovu hatauliza mara mbili kwasababu anajua faida ya kufanya hivyo huko mbeleni, atakapoambiwa avae mavazi ya kujisitiri hatachukia, atakapoambiwa aache kuabudu sanamu hatachukia, atakapoonywa juu ya dhambi zake hatokwazika, kwasababu anataka kupata cheti bora. 

Bwana Yesu akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments