JE UMEOKOKA?

JE UMEOKOKA?

Shalom, mtu wa Mungu karibu tujifunze Biblia pamoja..

Wapo wanaodhani kuwa hakuna kuokoka duniani! lakini nataka nikuambie wokovu ni hapa hapa duniani..Mbinguni ni matokeo ya wokovu wetu.

Biblia inasema kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku za kuja kwake mwana wa Adamu, Na kama ilivyokuwa katika siku za Lutu ndivyo itakavyokuwa katika siku za kuja kwake mwana wa Adamu..Hivyo tukijifunza ni vitu gani vilikuwa vinaendelea muda mchache kabla ya Matukio hayo mawili ya kuangamizwa dunia, tunaweza kuelewa ni mambo gani yatatokea katika siku za kuja kwa Kristo mara ya pili.

Tukio la kipekee tunaloweza kuliona kabla ya Moto kushuka sodoma na gomora ni namna watu walivyookoka…Yapo matukio mengi lakini leo tutalizungumzia hili moja.

Biblia inasema.

Mwanzo 19: 12 “Basi wale watu wakamwambia Lutu, Je! Unaye mtu hapa zaidi? Mkwe, wanao, na binti zako, na wo wote ulio nao katika mji, uwatoe katika mahali hapa;

13 maana tutapaharibu sisi mahali hapa, kwa kuwa kilio chake kimezidi mbele za Bwana; naye Bwana ametupeleka tupaharibu.

14 Lutu akatoka akasema na wakweze, waliowaposa binti zake, akasema, Ondokeni mtoke katika mahali hapa kwa sababu Bwana atauharibu mji huu. LAKINI AKAWA KAMA ACHEZAYE MACHONI PA WAKWEZE.

15 Hata alfajiri ndipo malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, Ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili waliopo hapa, usipotee katika maovu ya mji huu”.

Tunasoma hapo, kabla ya gharika, kuna injili ya haraka haraka ilipita…Lutu aliambiwa akawaambie ndugu zake watoke mjini kwasababu mji unakwenda kuangamizwa, na laiti kama hao ndugu zake wangesikia, kila mmoja angeogopa na kwenda mbio kuwaambia ndugu zao wengine wa mahali pengine…na hao ndugu wengine wangewaambia wengine…Hivyo kwa kipindi kifupi watu wengi sana wangeokoka…laiti watu wangekuwa na masikio ya kusikia maonyo na kuwa hofu ya Mungu, hata baada ya hukumu ile kutamkwa bado kungekuwepo na nafasi ya KUOKOKA!..Lakini hata huo mlango mdogo wa Neema watu waliupuuzia na hivyo kusababisha kuangamizwa wote.

Na kama pia ukichunguza wakati wa Gharika, Nuhu hakuokoka peke yake, bali aliambiwa akawakusanye watu wa jamaa yake yote…Ni wazi kuwa naye pia alikwenda kuwaambia mambo yale yale…lakini inawezekana naye pia alionekana kama anacheza! Ndio maana akaishia kuingia safinani yeye na wanawe tu, kama Lutu alivyookoka yeye na wanawe!

Mwanzo 7:1 “Bwana akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki”.

Mwanzo 7: 5 “Nuhu akafanya kama vile Bwana alivyomwamuru.

6 Naye Nuhu alikuwa mtu wa miaka mia sita hapo hiyo gharika ya maji ilipokuwa juu ya nchi.

7 Nuhu akaingia katika safina, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye; kwa sababu ya maji ya gharika”

Ndugu nafasi hii ndogo Mungu anayoitoa baada ya hukumu kutamkwa sio ya kwenda kutenda mema, hapana! ni nafasi ya kuokoka!! Hukumu imeshatamkwa..haiwezi kugeuzwa ni lazima ije tu kama ilivyotamkwa! Ni nafasi ya kuukimbia ulimwengu na kuingia safinani, hivyo hivyo kama ulivyo….Ni wakati wa kuikimbia sodoma na gomora ukiwa hivyo hivyo ulivyo…Usiende kumuaga mtu! Wala usiende kumwuliza baba yako au mama yako je! Natakiwa kuokoka? Ondoka sodoma kama ulivyo! Wewe kama wewe…wokovu unaanzia hapo hapo sodoma ulipo! kwasababu hukumu imeshatamkwa…Watoto wa Nuhu haikuhitaji utakatifu mwingi kupata nafasi ya kuingia safinani?..hawakuwa wakamilifu na ndio maana unaona baada ya kutoka safinani, Hamu aliuona uchi wa Baba yake…Lakini walitii injili ndio maana wakaokoka! tu Injili ya Nuhu ya mwisho ya kuokoka! Basi! Kulikuwa hakuna muda tena wa Mungu kusikiliza maombi ya watu…kulikuwa na mambo mawili tu! Aidha kuingia safinani uokoke au kubaki duniani uangamie.

Ukishaingia safinani tayari umeokoka! Hata kama mafuriko hayajaja!

Na siku za mwisho karibia na kuja kwa Yesu ndio injili ndio hiyo inahubiriwa na Roho Mtakatifu, hatuwezi kukaa na kumwomba Mungu kwamba asiiangamize dunia! Alishasema siku ya maangamizi itakuja ni kweli itakuja! Hakuna atakayeweza kubadilisha hilo… Na hivyo zipo chaguzi mbili tu mbele yetu! Kubaki ulimwenguni kuangamia au kuingia safinani kupona! Safina ni Bwana Yesu.

Kama unataka kuokoka na maangamizi..unamfuata Bwana Yesu ukiwa mwenye dhambi kama ulivyo wokovu ni hapa hapa duniani…haihitaji utakatifu kumwamini Yesu…Kwasababu kilichopo mbele ni kifo..Ukimwamini Yesu na kutubu moja kwa moja unapata nafasi ya kuingia safinani..na utakuwa umeokoka na maangamizi, kwasababu huwezi kuokoka mahali ambapo hakuna maangamizi!..Kisha baada ya hapo wewe mwenyewe atakuongoza katika utakatifu na ukamilifu wote,..wewe unachopaswa kufanya ni kuanzia huo wakati kutokuangalia nyuma tu,

Je! Upo safinani?…Umeitii Injili ya Roho Mtakatifu inayotuonya tujiepushe na ulimwengu?

Bwana akubariki

Mada Nyinginezo:

UKIAMINI NA UKIMKIRI YESU KWA KINYWA CHAKO, UTAOKOKA.

TOBA IGUSAYO MOYO WA BWANA.

MATUNDA YAPATANAYO NA TOBA!

NYOTA ZIPOTEAZO.

SAA YA KIAMA.

FREEMASONS NI NINI? NA MTU ATATOKAJE HUKO?


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments