UKIAMINI NA UKIMKIRI YESU KWA KINYWA CHAKO, UTAOKOKA.

UKIAMINI NA UKIMKIRI YESU KWA KINYWA CHAKO, UTAOKOKA.

Habari ya uzima wako mtu wa Mungu, Ni siku nyingine tena leo nakukaribisha tushiriki pamoja kujifunza Neno la Mungu, maji yaliyosafi yasafishayo roho zetu kila siku.

Sote tunafahamu kuwa biblia imetoa kanuni rahisi ya kuupata wokovu, nayo ni “kuamini” na “kukiri”. Lakini habari mbaya ni kuwa urahisi huu umechukuliwa kirahisi zaidi mpaka imefikia hatua imepoteza maana halisi ya andiko lenyewe lilivyomaanisha..Wengi wetu tunafundishwa au tunafahamu kuwa ukitaka kuokoka jambo la kwanza ni kuamini Yesu alifufuliwa katika wafu,halafu unazungumza kwa kinywa chako(Kukiri) kuwa yeye ni Bwana, basi hiyo inatosha kukufanya wewe kuwa mtoto wa Mungu na kuurithi ufalme wa mbinguni.

Na ndio maana imekuwa ni rahisi hata leo hii kusikia mlevi anakuambia nimeokoka, hata mtukanaji anakuambia nimeokoka, mwabudu sanamu anakwambia nimeokoka, mzinzi anakuambia nimeokoka, ni kwasababu gani?, ni kwasababu alishamkiri Yesu na kumwamini zamani.

Lakini je! hivyo ndivyo biblia inavyofundisha juu ya wokovu?.. Tukitazama hayo hayo mandiko yanatuambia hata mashetani nayo yanaamini na kutetemeka mbele za Yesu, na yaanamini kwamba alikufa akafufuka,(Yakobo 2:19) na vilevile yanakiri, kuwa yeye ni mwana wa Mungu..(Luka 4:41).

Kwa neema za Mungu leo tutatazama Neno kuamini na KUKIRI hasaa kwa kanisa ilikuwa ni ishara gani, na kulichukuliwa kwa uzito gani. Embu tupitia vifungu hivi:

Yohana 9:18 “Basi Wayahudi hawakusadiki habari zake, ya kuwa alikuwa kipofu, kisha akapata kuona; hata walipowaita wazazi wake yule aliyepata kuona.

19 Wakawauliza wakisema, Huyu ndiye mwana wenu, ambaye mnasema kwamba alizaliwa kipofu? Amepataje, basi, kuona sasa?

20 Wazazi wake wakawajibu, wakasema, Tunajua ya kuwa huyu ndiye mwana wetu, tena ya kuwa alizaliwa kipofu;

21 lakini jinsi aonavyo sasa hatujui; wala hatujui ni nani aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima; atajisemea mwenyewe.

22 Wazazi wake waliyasema hayo kwa sababu waliwaogopa Wayahudi; KWA MAANA WAYAHUDI WALIKUWA WAMEKWISHA KUAFIKIANA KWAMBA MTU AKIMKIRI KUWA NI KRISTO, atatengwa na sinagogi.

23 Ndiyo sababu wale wazazi wake walisema, Ni mtu mzima, mwulizeni yeye.”

Unaona zamani zile ilikuwa kabla hujafikiria kumkiri Yesu kwa namna yoyote ile, ilikuwa unapiga kwanza gharama ya mambo yatakayofuata baada ya hapo, Maana ilikuwa ukifikiria kuonyesha dalili za kumkiri tu moja kwa moja ulikuwa unatengwa na Sinagogi, kumbuka wayahudi walikuwa ni watu wa kidini, hivyo mtu ukitengwa na sinagogi ilimaanisha umetengwa na jamii nzima ikiwemo ndugu zako, na hivyo unajulikana kama kafiri, kama watu wa mataifa wasio na Mungu, hata siku ukifa hauzikwi pamoja na ndugu zako, hakuna sikukuu yoyote utakayoruhusiwa kushiriki, vilevile misaada ya kijamii haitakuhusu, unakuwa ni mtu wa kukataliwa siku zote hata katika mashauri yoyote hushirikishwi, unakuwa ni mtu wa kuudhiwa na kuvunjwa moyo kila siku.

Na ndio maana utaona wengi sana wakati Bwana Yesu yupo duniani walimwamini ikiwemo mafarisayo kama vile Nekodemo na wakuu wengine, lakini ki chini chini wakiogopa kumkiri hadharani kwasababu ya adhabu hiyo mbaya sana.

Yohana 12:42 “Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi.

43 Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu.”

Vile vile na baada ya Bwana Yesu kufa na kufufa,na kuondoka hali hiyo ndio ikazidi kuwa mbaya zaidi, ilikuwa sio tu kutengwa, lakini sasa mtu yoyote alikuwa akionekana anamkiri hadharani, ilikuwa ni mambo matatu yapo mbele yako, la kwanza lilikuwa ni kifo, na kama ukinusurika sana, basi ni kutupwa gerezani au kupigwa.. Hivyo mtu yoyote aliyeonekana anachukua uamuzi wa kumfuata Kristo au kumkiri alionekana ni mtu aliyechukua maamuzi ya kishujaa sana. Na ndio maana tunaona jinsi kanisa la kwanza lilivyokuwa linapitia dhiki nyingi sana, walikuwa kama wakimbizi, na wapitaji tu hiyo yote ni kwasababu ya Imani yao kwa Kristo.

Na ndio maana sasa hapa mtume Paulo aliliambia kanisa:

Warumi 10:9 “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. 10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.”.

Hili ni Neno lililochukuliwa kwa uzito sana kwa watu wa kipindi kile kuliko linavyochukuliwa sasa, lIlionyesha moja kwa moja njia ya MSALABA. Na mtu aliyefanya hivyo moja kwa moja alijua kuna dhiki na taabu anakwenda kukumbana nazo mbeleni, kuna kutengwa na kuchukiwa, na kukataliwa kwa ajili ya Yesu Kristo, kuna kuuawa na pengine hata kusulibishwa kwasababu ya imani yake tu kwa Yesu. Na kukiri kwenyewe sio mara moja tu kama wengi tunavyofanya sasa hivi hapana bali ilikuwa ni kila siku na ndio maana Paulo anasema, kwa kinywa mtu hukiri “HATA” kuupata wokovu, kuonyesha kuwa ni kitendo endelevu.

Lakini leo hii hili neno mkikiri Bwana Yesu linapewa tafsiri tofauti, Tunasema tumemkiri Yesu lakini hatupo tayari kujitwika misalaba yetu na kumfuata. Kiuhalisia hapo hatujamkiri Kristo maishani mwetu, yaani kwa lugha rahisi kumkiri Yesu kwa sasa sio kuzungumza tu mdomoni, kwasababu sasahivi hakuna dhiki yoyote utakayopitia kwa kusema YESU ni Bwana.

Kumkiri hasaa ni pale unapochukua uamuzi kama vile Kanisa la kwanza lilivyofanya kweli kwa vitendo, utamkiri kwa kuacha kuvaa vimini, na suruali, kwa kuacha kutembea na kampani zako mbaya za zamani, kuacha kwenda disco, na club, kukaa mbali na uasherati, kumtumikia Mungu, kuonyesha kuwa unamfauta KRISTO, huko ndiko kukiri kunakomaanishwa.

Lakini ikiwa mtu atasema nimemkiri, na bado unaipenda dunia kuliko Kristo, hapo haijalishi uliongozwa sala ya toba mara ngapi, bado utakuwa mbali tu na wokovu. Hivyo ndugu ikiwa hapo nyuma haukumaanisha, ulikiri tu, basi kama desturi na mazoeza basi leo hii maanisha kweli kweli mbele zake, Yeye anasema nikaribieni mimi, nami nitawakaribia nyinyi, hii ni kuonyesha kuwa ukionyesha Nia kweli kweli ya kumfuata Yesu, haihitaji hatua nyingi sana ili umfikie anachohitaji ni moyo wako wa kumaanisha kweli, na akishaona unamfuata bila kigugumizi basi na yeye atakufuata hapo ulipo kukushika mkono na kukupeleka pale anapotaka ufike..

Na ndio maana tuna kitu kinachoitwa neema, ambayo hiyo inatoka kwa Yesu Kristo pekee, hiyo kazi yake ni kukuchukua taratibu na kukusafisha bila kujalisha hali uliyonayo katika wakati huo, unakuvukisha viwango kidogo kidogo mpaka unajikuta ghafla umefika mahali mizizi ya wokovu imekita ndani yako, mahali ambapo shetani hawezi kukuchukua tena…Unakuwa tayari umeshatiwa MUHURI na Mungu mwenyewe kwa Yule Roho wake mtakatifu mpaka siku ya ukombozi wako(Waefeso 4:30).

Hivyo anza sasa Kumkiri Yesu kwa vitendo na Bwana atakuwepo nawe. Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Ubarikiwe sana.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasilianaa nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

MWAMBA WETU.

NINI TOFAUTI YA HAYA MANENO. 1) KUOKOKA, 2) WOKOVU, 3) KUONGOKA?

IKIWA MWENYE HAKI AKIOKOKA KWA SHIDA, MWENYE DHAMBI ATAONEKANA WAPI?

IKIWA MWENYE HAKI AKIOKOKA KWA SHIDA, MWENYE DHAMBI ATAONEKANA WAPI?

TUSIPOUTHAMINI WOKOVU TUTAPATAJE KUPONA?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Daud
Daud
2 years ago

Amen

Jina moja
Jina moja
3 years ago

Asante