Nini tofauti ya haya maneno. 1) KUOKOKA, 2) WOKOVU, 3) KUONGOKA.?

Nini tofauti ya haya maneno. 1) KUOKOKA, 2) WOKOVU, 3) KUONGOKA.?

JIBU: Shalom! Maana ya Neno ongoka ni KUGUEUKA.

Hivyo biblia inaposema mtu ni mwongofu inamaanisha kuwa ni mtu aliyegeuka na kuacha mienendo aliyokuwa anaiendea hapo mwanzo. Embu tutazame baadhi ya vifungu kwa kupitia hivyo tutajifunza kwa uelewa mrahisi zaidi:  

Mathayo 18.3 “akasema, Amin, nawaambia, MSIPOONGOKA na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni”.

Hapo Bwana alikuwa anamaanisha MSIPOGEUKA na kuwa kama vitoto, yaani wasipogeuzwa fikra zao na kuwa kama watoto wadogo hawawezi kuuingia katika ufalme wa mbinguni.   Kadhalika tukisoma..

Marko 4: 11 “Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje yote hufanywa kwa mifano,

12 ili wakitazama watazame, wasione; Na wakisikia wasikie, wasielewe; Wasije WAKAONGOKA, na kusamehewa.”  

Tunaona hapo Bwana alimaanisha wale watu wasije WAKAGEUKA na kuacha njia zao mbaya, ambapo kama wakifanya hivyo Mungu atawasemehe, na kuwaachilia neema ya kusamehewa dhambi zao.   Tukisoma pia..

1Timotheo 3.6 “Wala asiwe mtu ALIYEONGOKA karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.”

Hapo Mtume Paulo aliposema mtu aliyeongoka hivi karibuni, alimaanisha kuwa mtu Yule aliyegeuka na kuacha njia zake mbovu, hivi karibuni, asije akapewa kazi ya uaskofu kwasababu mtu kama huyo bado hajaweza kuijua imani vizuri, na kuweza kuzitambua hila za shetani kwani bado ni mchanga wa imani.  

Hivyo ukitazama na vifungu vingine utaliona jambo hilo kwa muda wako unaweza ukavipitia baadhi ninavyokuorodheshea hapa (Mathayo 13:15,Luka 22:32, Matendo 15:3).  

Kwa hiyo tunaweza kusema mtu anaweza akawa ni mwongofu, lakini bado hajaokoka. Tutalitazama hilo kwa undani tutakapojua kwanza maana ya kuokoa pia.

KUOKOKA/WOKOVU.  (Nini Maana ya kuokoka/ kuokoka ni nini?)

Kuokoka na wokovu ni kitu kile kile..Kuokoka ni kitenzi cha nomino Wokovu. Hivyo mtu mpaka awe ameokoka ni lazima kwanza awe amehusishwa na anayemwokoa mwenyewe (yaani mwokozi). Katika ukristo huwezi kusema umeokoka mwenyewe kama Yesu Kristo hajayageuza maisha yako, kama maisha yako hajahusianishwa na Kristo moja kwa moja, basi utakuwa umepokea wokovu mwingine tofauti na ule unaozungumzwa kwenye biblia.  

Biblia inasema.

Warumi 10:9 “ Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, “”utaokoka””.

10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu”.

  Na pia inasema: “AAMINIYE na KUBATIZWA “ataokoka”; asiyeamini, atahukumiwa.(Marko 16:16)”. Zingatia hivyo vifungu viwili vya mistari, vitakuja kutusaidia huko mbeleni. Kwasababu vyote viwili vinahusianishwa na suala la wokovu kwa mwanadamu.   Kama tulivyosema suala la kuokoka ni jambo la kuingia moja kwa moja katika mahusiano ya karibu na Yule anayekuokoa. Upo udanganyifu mkubwa unaoendelea duniani sasahivi, watu wadhaniao kuwa wokovu ni jambo la Kuzungumza tu kwenye kinywa halafu basi wewe tayari utakuwa umeokoka. Hivyo imepelekea kila mtu duniani anasema ameokoka hata kama ni mlevi kisa tu tayari alishakiri yale maneno alipokuwa anaangozwa sala ya toba.  

Watumishi wa Mungu wameyaacha na yale mwengine na kuona kuwa hayana umuhimu wowote. Hii ni kutokana na kwamba Kushindwa kuelewa maana ya Neno KUKIRI, ndiyo inayopelekea wokovu kuonekana ni kitu cha ajabu sasa duniani. Ndiyo inayopelekea watu kutoona nguvu za wokovu zikitenda kazi ndani yako. Wanakiri wameookoa, wameokoka.. lakini ukweli ni kwamba Wapo mbali na wokovu kuliko wao wanavyodhani.   Biblia inaposema kwa kinywa mtu Hukiri “HATA” kupata wokovu..zingatia hilo Neno “HATA”..Ikiwa na maana kuwa ni tendo ENDELEVU. Sio kuzungumza tu siku moja halafu basi, Pia ili neno KIRI liwe na uweza na nguvu ni lazima pia neno KANA liwepo..

Kwa Watakatifu wa kale ilikuwa mtu akionyesha tu kumkiri Yesu kuwa ni mwokozi ilikuwa adhabu yake ni kufa au kutengwa na jamii pamoja na sinagogi. (Soma Yohana 3&9). Hivyo watu wa wakati ule ilikuwa kukiri tu vile, basi wewe ulikuwa umeshajihalalisha si wa kwao, na hivyo unawekwa mbali na watu wote wanamchukia Kristo. Lakini kukiri kwetu sisi mazingira tuliyopo mazingira ya kukana hayapo basi hilo neno halina nguvu kwa kinywa pekee.

Kama ndio hivyo basi sisi tunamkirije Kristo?.

  Tunamkiri Kristo kwa maisha yetu na matendo yetu kuonyesha kuwa ni kweli Kristo alikufa, na kufufuka pamoja na sisi, kwanza kwa kubatizwa katika maji mengi na katika jina la YESU KRISTO kama maandiko yasemavyo pindi tu tuaminipo kama ishara ya kuamini kuwa alikufa akafufuka pamoja na sisi kuuonyesha ulimwengu tumekuwa milki halali ya Bwana. Na Pili ni kukubali kuishi maisha yanayomkiri Kristo kila siku.

  Hapo ndio mtu anakuwa tayari kuingia gharama zote ikiwemo kuwa tayari kutengwa, kuchukiwa, kuachwa, kudharauliwa kwa ajili ya KRISTO, kwa ajili ya kumfuata Kristo.   Sasa hapo ndipo mtu amemkiri Kristo. Na wokovu kwake ni jambo la lazima.   Fananisha maneno hayo na vifungu hivi Bwana Yesu alivyowaambia makutano:  

Mathayo 10:32 “Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni.

33 Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.

34 Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga.

35 Kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu; 36 na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.

37 Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.

38 Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili.”  

Pia ni vizuri kufahamu kuwa wapo watu wanaosema kuwa tukiwa hapa duniani hatuwezi kukoka mpaka tutakapokwenda mbinguni. Huo nao ni uongo. Biblia inasema 2 Wakoritho 6: 2 “Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia;tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama SIKU YA WOKOVU NI SASA)”.

  Unaona hapo?

Siku ya wokovu ni sasa. Tunaokolewa tukiwa hapa duniani hivyo mtu kusema nimeokoka ikiwa kweli amezingatia vigezo vyote vilivyotelewa na huyo amwokoaye.

  Hana budi kujithibitishia hilo kuwa tayari ameshaokoka. Na hivyo siku ile ya kwenda mbinguni ni kukamilishwa tu kwa wokovu wake. Kumbuka raha ya wokovu inaanzia hapa hapa duniani pindi tu pale mtu anapomwamini Yesu Kristo, matunda ya wokovu yanaanzia duniani mbinguni ni kukamilishwa tu.   Hivyo, kwa kuhitimisha tunaweza kusema mtu aliyeongoka ni tofauti na aliyeokoka. Japo aliyeokoka tayari alishaongoka ndani yake, lakini aliyeongoka haitupi uhakika kuwa ameokoka, kwasababu Neno lenyewe kuongoka ni KUGEUKA na sio KUOKOLEWA.   Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Ubarikiwe sana.


 

Mada zinazoendana:

JE! UMECHAGULIWA KABLA YA KUWEKWA MISINGI YA ULIMWENGU?

KAMA MHUBIRI NI WOKOVU UPI UNAUPELEKA KWA WATU?

UKIAMINI NA UKIMKIRI YESU KWA KINYWA CHAKO, UTAOKOKA.

MELKIZEDEKI NI NANI?

DANIELI: MLANGO WA 1

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

KANUNI RAHISI YA KUFANIKIWA.


 

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments