JE KUHUDUMU KWA NYIMBO ZA INJILI KUKOJE?

JE KUHUDUMU KWA NYIMBO ZA INJILI KUKOJE?

Nyimbo za Injili ni zipi?, waimbaji wanapaswa waitendeje huduma hiyo?..

Shalom. Karibu tuongeze maarifa kuhusu Neno la Mungu..Tukilijua Neno la Mungu vyema, tutayajua mapenzi ya Mungu na hivyo tutaishi kulingana na yeye anavyopenda na tutabarikiwa.

Moja ya karama ya muhimu sana katika Mwili wa Kristo ni karama ya uimbaji. Sasa ni wazi kuwa mtu yoyote anaweza kuimba, awe mwanamume au mwanamke..Lakini yupo ambaye akiimba nyimbo au akiimbisha basi kunaambatana na nguvu fulani za kipekee za Roho Mtakatifu. Sasa nguvu hizo sio za kuwafanya watu waanguke au walie..Hapana bali nguvu hizo ni zile zinazomfanya mtu apate badiliko fulani la rohoni, ageuke kutoka kuwa mwenye dhambi mpaka kuwa mtakatifu.

Mwimbaji huyu anapoimba au anapoimbisha, basi Roho yule yule anayeshuka juu ya watu wakati Mchungaji anahubiri ndio huyo huyo anayeshuka juu  ya watu wakati anaimbisha.

Sasa huduma ya uimbaji sio huduma ya kutafuta fedha, kama vile huduma nyingine yoyote katika mwili wa Kristo isivyo ya lengo la kutafuta fedha wala umaarufu. Mchungaji au Mwalimu anapohubiri katika kanisa lake, na anapoalikwa mahali pengine au Taifa lingine kwenda kuihubiri Injili, hapaswi kwenda kule kwa lengo la kutafuta fedha. Biblia inasema tumepewa bure tutoe bure..Hivyo atakwenda kule alikoalikwa na atahubiri bure..Ndio wale waliomwalika watamgharimia nauli, pamoja na malazi na makazi kwa huo wakati, lakini hapaswi kwenda kwa lengo la kutafuta malipo/mshahara. Kama waliomwalika watakuwa na moyo mwingine na kusema hatutapenda mtumishi huyu aondoke mikono mitupu, hivyo kwa kuguswa kwao wakampatia chochote kile iwe fedha, au mali..hapo sio dhambi kupokea..lakini Mchungaji, au mwalimu au mtu yoyote yule hapaswi kuomba chochote, wala kuonyesha dalili ya kuwa mhitaji.

Mungu anajua kuwahudumia watu wake, haihitaji yeye kusaidiwa, hivyo aliposema…”Tumepewa bure tutoe bure alimaanisha kabisa”..kwamba kwa namna yoyote ile atawafungulia watumishi wake mlango wa kula na kunywa hata njia hiyo.

Vivyo hivyo na uimbaji wa nyimbo za injili. Mtu yeyote aliyepewa karama hiyo hapaswi kuwa kama wasanii wa nyimbo za ulimwengu ambao wapo kwa lengo la kutafuta fedha kwa sanaa zao hizo. Mtu mwenye karama ya uimbaji atafanya kazi ya Mungu bure pasipo malipo..akifika mahali kaalikwa kwenda kuongoza nyimbo za kumsifu Mungu na kumwabudu, hapaswi kutazamia malipo kwa namna yoyote ile. Anapaswa afanye kazi yake ya uimbaji kwa uaminifu kama ya mchungaji aliyealikwa…aimbe nyimbo za injili na kuhakikisha neema ya Mungu imeshuka juu ya watu, hiyo ndio inapaswa iwe furaha yake ya kwanza, na lengo lake kuu la kwenda pale.

Hali kadhalika hapaswi kubadilika kimavazi na kufanana na wasanii wa kidunia..Kazi ya Mungu sio ya kuonyesha uanamitindo…kwamba leo umevaa hiki, kesho unavaa kile, ili watu wakuone jinsi unavyojua kuvaa…Vaa nguo za heshima, kama ni mwanamke vaa gauni refu haijalishi ni la gharama au sio la gharama, lakini lazima liwe la kujisitiri, hupaswi kwenda kufanya huduma huku umevaa suruali, huku mgongo upo wazi, huku umejichubua uso, huku umeweka make up mfano wa Mwanamke Yezebeli wa kwenye biblia..hali kadhalika mwanaume hupaswi kwenda kufanya huduma huku umenyoa kidunia, huku umevaa nguo za kubana, huku umejipamba mpaka unakaribia kufanana na wanawake.

Ukifanya hivyo na kwenda kufanya huduma na mambo hayo machafu utakuwa bado hujaelewa nini maana ya kumtumikia Mungu, utakuwa unamdharau Mungu na madhabahu yake, na utakapoambiwa ukweli utaona kama unaonewa WIVU, hakuna wivu hapo unaoonewa, ni kwa faida yako binafsi..Unakwenda kuzitafutia laana badala ya baraka ndugu…..Unapoacha kusimama katika Neno la Mungu na kujilinganisha na wasanii wa kidunia, ni sawa na mchungaji aliyeacha majukumu yake madhabahuni na kujilinganisha na wanasiasa waliopo bungeni.

Ndugu yangu, uliyejaliwa karama ya uimbaji..Utumie kwa utukufu wa Mungu, kama wachungaji ambao wamealikwa kutembea dunia yote kuhubiri hawabweteki na kwanini wewe unabweteka na kujiharibia huduma yako kwa kuwaiga hao wasanii wa kidunia au hata baadhi ya wanaojiita wasanii wa injili ambao hawajaelewa maana ya kumtumikia Mungu?

Sasa utauliza je! Sitakiwi kabisa kwenda kurekodi nyimbo zangu studio?

Hapana unapaswa ukazirekodi kabisa tena kwa bidii nyingi, kwa uongozo thabiti wa Roho Mtakatifu, ili injili ienee kwa wengi, na kuwa msaada na baraka kwa wengi..Lakini katika hiyo usiigeuze kuwa ndio sehemu ya kupatia fedha na utajiri. Weka bei ya bidhaa hiyo ambayo inalingana na gharama ulizoingia, na faida kidogo kwaajili ya msingi wa kazi zitakazofuata kama hizo na si kwaajili ya kupata fedha, wala kwaajili ya kujiandaa kuwa msanii maarufu. Na hupaswi kukasirika unaposikia watu wanabarikiwa kwa nyimbo ulizoimba, au wanaziimba nyimbo zilizotungwa na wewe pasipo kukutaja wewe wala kukupa malipo…Hupaswi kukasirika, zaidi ya yote unapaswa ufurahi kwasababu injili ya Kristo inakwenda mbele.

Kwasababu hata wachungaji ndio hivyo hivyo, wanapotengeneza kitabu..na mafunuo waliyoyapata na kuyaandika ndani ya kile kitabu yatakwenda kufundishwa huko na huko, kila mahali na hata kumrudia yeye mwenyewe…na wala hawasemi wala kuchukia kwamba ule ufunuo ni wa kwao na kwamba wana hati miliki nao, mtu mwingine hapaswi kuhubiri bila idhini yao. Kama yupo Mtumishi wa namna hiyo, basi huyo naye bado hajaelewa nini maana ya kuwa mtumishi,  kwasababu injili ya Kristo haihubiriwi kwa hati miliki. Lakini kama hujawahi kuona kwanini wewe muimbaji uchukie na kukwazika kuona mtu anaimba nyimbo uliyoiimba wewe bila hata kukutaja au kukutambua?.

Ukiona unasikia huo wivu basi fahamu kuwa bado kuna kasoro ndani yako, upo kutafuta umaarufu na faida kupitia kazi ya Mungu, na haupo kwa lengo la kuisambaza injili. Huna tofauti na Yuda Iskariote.

Hivyo zingatia hayo machache mtu wa Mungu, na Bwana atakusaidia, kama una huduma yoyote ndani yako ya kuhudumu kwa nyimbo za injili, tenga muda uilinganishe na huduma nyingine katika mwili wa Kristo jinsi zinavyofanya kazi, ili upate hekima na ufahamu jinsi ya kuitenda kazi ya Mungu katika shamba lake.

Bwaan akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

NYIMBO ZA WOKOVU

NINI TUNAJIFUNZA KWA MWANA MPOTEVU NA NDUGUYE?

KILEMBA CHA NEEMA, JE! UMEMVIKA MWANAO?

Maana ya huu mstari ni ipi? Mithali 14:4 ‘Zizi ni safi ambapo hapana ngombe;bali nguvu za ngombe zaleta faida nyingi’.

MATUMIZI YA DIVAI.

JE KUNA UISLAMU KATIKA BIBLIA?

KITABU CHA UZIMA

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments