Ukisoma ule waraka wa pili ambao Paulo alimwandikia Timotheo kuanzia ile sura ya tatu mstari wa 1-9, utaona jinsi Paulo alivyoanza kumweleza Timotheo juu ya mambo yatakayotokea siku za mwisho..Lakini alianza kwa kumwambia neno hili “siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari”.. Jiulize ni kwa nini alimwambia hivyo?. Alimwambia hivyo kwasababu aliona jinsi wimbi kubwa la watu wenye mfano wa utauwa (wanaonekana kama ni watu wa Mungu), lakini wakizikana nguvu zake, watakavyonyanyuka na kuwapoteza wengi.
Hao watu hawakuwepo wakati mwingine wowote isipokuwa tu watatokea katika siku za mwisho, yaani watu wanaoonekana ni watumishi wa Mungu, wanaoonekana wanawaongoza watu katika njia za kweli, lakini kumbe nyuma ya mgongo wanazikana nguvu za Mungu..
Sasa hizi nguvu za Mungu ni zipi?..
Biblia inatueleza “Neno la msalaba” ndio nguvu ya Mungu..
1Wakorintho 1:18 “Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu”.
Sehemu nyingine inaiita injili kama “uweza wa Mungu (POWER)” Warumi 1:16.
Unaona Injili inayolenga ukombozi wa msalaba, inayowafanya watu wautazame msalabani, watubu dhambi , wakapate msamaha na ondoleo la dhambi zao, hapo ndipo nguvu za Mungu zilipo..
Hakuna mahali popote biblia inasema nguvu za Mungu zipo katika mali, au biashara na majumba..Hayo hayawezi kumfanya mtu apate uzima wa milele…Sasa watu wa namna hii ndio watanyanyuka sana katikati ya kanisa la Mungu, ambao watakuwa wanajifanya ni wanatangaza habari za wokovu, kumbe wanahubiri mambo yao mengine, hawana habari na injili ya toba, wala hata haiwavutii, wala hawajali kwamba mtu wanayemchunga na kuchukua sadaka zake anaweza kufa leo na kwenda kuzimu kutokana na dhambi zake, hilo hawalijali wao wapo radhi kuwasisitizia tu mafanikio ya miili yao, lakini si roho zao.
Wengine wapo radhi, kuwakaririsha mapokeo ya dini zao, ili watu wawe tu wa kidini, wajue litrujia, wasome rozari, na sala zote za marehemu, lakini hao hao watu ukiwauliza je umeokoka, watakauambia mimi si mlokole, ukiwauliza, Je! Unajua kuwa kuna kitu kinachoitwa Unyakuo, watakauambia..sijui unazungumzia kitu gani!!..Sasa embu fikiria mtu wa namna hiyo mbinguni atakwendaje?..Lakini hayo yote ni kiongozi wake hajawahi kumwambia hayo mambo, ni kiongozi ambaye anao mfano wa utauwa lakini anazikana nguvu za Mungu..
Sasa Paulo aliwafananisha watu hawa na Yane na Yambre ambao walinyanyuka wakati wa Musa..Jinsi walivyokuwa wanapingana naye..
2Timotheo 3:8 “Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani. 9 Lakini hawataendelea sana; maana upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama vile na upumbavu wa hao ulivyokuwa Dhahiri”.
2Timotheo 3:8 “Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani.
9 Lakini hawataendelea sana; maana upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama vile na upumbavu wa hao ulivyokuwa Dhahiri”.
Sasa kama uwafahamu Yane na Yambre ni wakina nani…
Walikuwa ni wale wachawi wa Farao ambao Musa alipokuwa anafanya miujiza na wao walikuwa wanafanya ili tu kumpinga Musa.
Unaona? Jambo pekee ambalo lilikuwa linawatofautisha hawa wachawi wawili (Yane na Yambre) na Musa, halikuwa miujiza..hapana, hata wao kwa sehemu fulani walipewa kufanya miujiza, jambo pekee lililowatofautisha na Musa, ni UJUMBE waliobeba.. Musa alikuja na ishara lakini alikuwa na Ujumbe nyuma ya ishara zile..Nao ndio huu “Bwana asema hivi! Waache watu wangu huru,waende kunitumikia”..Lakini Yane na Yambre hawakuwa na ujumbe wowote isipokuwa kupinga tu, na kuwaburudisha na kuwatumainisha wamisri kwa miujiza yao,..Ni wana-mazingaombwe tu!..Mtu anayefanya mazingaumbwe siku zote hana ujumbe wowote kwa mazingaombwe yake, anafanya tu kuburudisha watu, na wala wakati mwingine anaweza asiongee kuanzia anaanza mazingaombwe yake mpaka anamaliza. Na wakina Yane walikuwa hivyo hivyo.
Musa alikuwa na ujumbe wa ukombozi, wa kuwatangazia watu uhuru watoke katika utumwa mgumu wa Farao, Ambao kwa sasa sisi tuliookolewa tunafananishwa na wana wa Israeli pale tunapomwamini Kristo, tunaokolewa kutoka katika utumwa wa dhambi wa Ibilisi.
Sasa ukiona, mtu anakujia na miujiza na ishara hizi au zile, lakini hana ujumbe wowote wa kukutoa Misri (kukutoa kwenye utumwa wa dhambi), Basi ujue kuwa unaongozwa na Yane na Yambre(wana mazingaombwe), watumishi wa shetani.. Haijalishi watashika biblia, haijilishi watakuombea upone kiasi gani, Yane na Yambre waliweza kuyafanya hayo yote, haijalishi watafanya miujiza mingi vipi, kama hawana ujumbe wa kukurudisha msalabani upate ukombozi wa roho yako, Ujue hao ni Yane na Yambre tu wanakuongoza…
Ndio hao sasa mtume Paulo anaowazungumzia kuwa “wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake”…..Hizi ndio nyakati zenyewe za hatari zinazozungumziwa hapo. Mahali popote unapoongozwa embu jipime nafsi yako, je tangu umekuwa hapo ni kitu gani kimeongezeka katika Maisha yako ya rohoni kwa ujumla, Je! Mahusiano yako na Mungu yameongezeka au yapo pale pale?, Kama sivyo basi ujue upo chini ya Yane na Yambre wa siku za mwisho.
Na kibaya Zaidi kama hujui, watu waliochangia kuufanya moyo wa Farao kuwa mgumu ni hawa wachawi wawili..Kama sio wao basi pengine Farao angeshatubu zamani..(Ingawa ni Mungu mwenyewe ndiye aliyeruhsu). Vivyo hivyo leo hutaki kumgeukia Kristo na kutaka kutubu dhambi zako na kutafuta utakatifu kwasababu tayari wapo akina Yane na Yambre wanaokupumbaza na miujiza, ukikumbushwa habari ya utakatifu na kwenda mbinguni, unasema nabii wetu/kiongozi wetu wa kidini mbona hajawahi kutufundisha hayo, na miujiza mbona inafanyika mingi tu..
Ndugu siku ukifa na kujikuta upo kuzimu, hutakuwa na la kujitetea, kwasababu biblia inatuambia..mtu akifa matendo yake yanafuatana naye (Ufunuo 14:13)..Haisema majumba yake, au magari yake, au bishara yake, au dhehebu lake, inasema matendo yake..Sasa kama nabii wako au mchungaji wako, anakutumaisha na mambo ya ulimwengu huu na wewe unaona raha, nataka nikuambie siku ile vyote pamoja na mali zako, pamoja na huyo kiongozi wako wa imani, aliyekuwa anakufundisha kujiwekea hazina duniani badala ya mbinguni, wote watakuaga pale makaburini, utakuwa umebakia wewe mwenyewe, utashangaa ni matendo yako tu yapo na wewe..hayo ndiyo yatakayoeleza hatma yako ni nini..
kwasababu biblia imeshatuonya jinsi ya kuendana na watu wa namna hii, hivyo ni wajibu wako wewe binafsi kutumia akili, kwa kuutafuta uhusiano wako binafsi na Mungu wako…Kuupima wokovu wako kama upo sawasawa au la, na kama haupo! Basi ndio ufanye bidii kumtafuta Kristo kwa moyo wako wote na kwa nguvu zako zote, katika hichi kipindi kifupi tulichobakiwa nacho, maadamu muda unao..
2Wakorintho 13:5 “Jijaribuni wenyewe kwamba mmekuwa katika imani; jithibitisheni wenyewe. Au hamjijui wenyewe, kwamba Yesu Kristo yu ndani yenu? Isipokuwa mmekataliwa”
Usisubiri ufe ndipo ujue kuwa ulikuwa kwenye njia isiyo sahihi, amka usingizi, anza kuyatengeneza Maisha yako.
Waefeso 5:14 “Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza”.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group
Mada Nyinginezo:
HUDUMA YA (ELIFAZI, SOFARI, NA BILDADI).
Je! hizi roho saba za Mungu ni zipi? na je zinatofautiana na Roho Mtakatifu?
HATUTAACHA KUJIFUNZA NENO KILA INAPOITWA LEO.
Utii ni nini? na ni nani tunayepaswa kumtii au kutokumtii?
HERI YULE ATAKAYEKULA MKATE KATIKA UFALME WA MUNGU.
Rudi Nyumbani:
Print this post
Nimebarikiwa na somo. Mungu awatie nguvu watumishi ya kuendelea kufundisha Neno la Mungu.
napenda masomo yenu mnitumie,amina
Hakika Bwana Yesu ni mkuu,kutokana na mafundisho haya naona uponyaji wa roho yangu.Amina
Amen utukufu kwa Bwana Yesu..
Asanteni sana na Mungu awabatiki
Amen nawe pia