JIHADHARI NA DHAMBI YA WIVU/HUSUDA.

JIHADHARI NA DHAMBI YA WIVU/HUSUDA.

Jiepusha na dhambi ya wivu/husuda ambayo mwisho wake ni mauaji.

Silaha moja kubwa shetani anayoitumia kuwadhuru watu ni wivu…mtu mwenye wivu ni rahisi kutumiwa na shetani kwa viwango vikubwa sana… Mauaji mengi yanasababishwa na wivu, uchawi mwingi unatokana na wivu, hila nyingi zinatokana na wivu..na mambo yote mabaya yanatokana na wivu.

Hivyo ni muhimu kujifunza kutokuwa na wivu ili tusiwe kifaa cha kutumiwa na shetani kuwadhuru wengine.

 Roho ya wivu ndiyo iliyowafanya  Mafarisayo na Masadukayo wamchukie Bwana, pale walipoona Bwana anatenda miujiza ambayo wao hawawezi kuitenda, pale walipoona Bwana anawarejeza watu wengi kwa Mungu kuliko wao…Na mioyoni Roho Mtakatifu alikuwa akiwashuhudia kabisa kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu…na walikuwa wanajua kabisa katumwa na Mungu lakini kwasababu ya wivu..wakawa wanajitoa ufahamu na kumkufuru.. Soma..

Mathayo 22:15 “Ndipo Mafarisayo wakaenda zao, wakafanya shauri, jinsi ya kumtega kwa maneno.

16 Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu”.

Unaona, walijua kabisa Kristo alikuwa mtu wa kweli aliyetumwa na Mungu..

Soma tena.. Yohana  3:1-3 utalithibitisha hilo…

Yohana 3:1 “Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi.

2 Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye”.

Lakini pamoja na hayo yote nguvu ya wivu ilikuwa kubwa ndani yao ikazidi nguvu ya kumpenda..na hatimaye wakafanya hila mpaka za kutaka kwenda kumsulubisha mfalme wao..Walimsulubisha moyoni wakijua kabisa huyu ni mwana wa Mungu aliyetumwa kutoka mbinguni…Hilo halikuwa na shaka mioyoni mwao. Walijua kabisa ndiye mfalme aliyetabiriwa kuja ulimwenguni.

Na hata walipompeleka kwa Pilato..Haraka sana Pilato ambaye hakuwa Myahudi akajua kuwa hakukuwa na kosa lolote alilolifanya Bwana Yesu ambalo linastahili yeye kusulubiwa lakini ni kwasababu tu ya wivu…Hawa wayahudi wamesikia tu wivu alivyojiita yeye ni mwana wa Mungu..Hilo tu! Wala hakuna lingine…walimwonea wivu kwa miujiza aliyokuwa anaitenda ambayo wao walishindwa kuitenda na wala hakuna lingine, na jinsi anavyowajalia watu wengi kupata wokovu…Kwahiyo hata Pilato aliliona hilo kama biblia inavyosema katika..

Marko 15:9 “Pilato akawajibu, akisema, Je! Mnataka niwafungulie mfalme wa Wayahudi?

10 Kwa maana alitambua ya kuwa wakuu wa makuhani wamemtoa kwa HUSUDA.

11 Lakini wakuu wa makuhani wakawataharakisha makutano, kwamba afadhali awafungulie Baraba”.

Sasa neno ‘HUSUDA’ maana yake ni ‘WIVU’ soma tena (Mathayo 27:17-18)..Kwahiyo unaona Pilato alishawajua kabisa hawa watu ni wivu ndio uliowafanya watake kumwua Yesu na wala hakuna lingine..alijua kabisa mioyoni mwako wanamwamini Yesu na kwamba “Yesu katoka kwa Mungu, na ni mfalme wao” lakini kwa kuwa wamemwonea wivu ndio maana wanataka afe…Ndio maana Pilato alikuwa akiwauliza kwa kurudia rudia.. “kama kweli wamemaanisha kumuua mfalme wao”

Yohana 19:13 “Basi Pilato, aliposikia maneno hayo, akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au kwa Kiebrania, Gabatha.

14 Nayo ilikuwa Maandalio ya pasaka, yapata saa sita. Akawaambia Wayahudi, TAZAMA, MFALME WENU!

15 Basi wale wakapiga kelele, Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe! Pilato akawaambia, JE! NIMSULIBISHE MFALME WENU! Wakuu wa makuhani wakamjibu, Sisi hatuna mfalme ila Kaisari”.

Wivu ni mbaya sana unakufanya umkane Mtu, hata kama unamwamini na kumpenda…

Na ndio maana mwishoni kabisa baada ya kusulubishwa Bwana Yesu, Pilato aliandika anwani juu ya msalaba wa Bwana Yesu kwa lazima.. “Yesu Mnazareti, Mfalme wa Wayahudi”

Yohana 19:19 “Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI.

20 Basi anwani hiyo waliisoma wengi katika Wayahudi; maana mahali pale aliposulibiwa Yesu palikuwa karibu na mji; nayo iliandikwa kwa Kiebrania, na Kirumi, na Kiyunani.

21 Basi wakuu wa makuhani na Wayahudi wakamwambia Pilato, Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi.

22 PILATO AKAJIBU, NILIYOANDIKA NIMEYAANDIKA”.

Unaona hapo?..Pilato aling’ang’ania kuandika anwani ile kwa lazima?…kwanini?..ni kwasababu anaujua unafiki wa mafarisayo..mioyoni mwao walimwamini lakini mdomoni walimkana na kumtukana na kumsulubisha na hiyo yote ni kwasababu ya wivu tu!. Na ndio maana Pilato akaandika anwani ile.

Yohana 12:42 “Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi”.

Sasa sio wote kabisa waliomwamini, Bwana Yesu…wapo ambao ni kweli hawakumwamini kabisa pamoja na ishara zote zile alizozifanya…lakini asilimia kubwa ya mafarisayo na wakuu wa makuhani walimwamini Bwana mioyoni mwao lakini WIVU ukawasababisha kumsulubisha Bwana, na sio Bwana tu bali hata mitume wake walisumbuliwa na mafarisayo hao hao..na yote hiyo ni kutokana na wivu tu.

Matendo 5:16 “Nayo makutano ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa.

17 Akaondoka Kuhani Mkuu na wote waliokuwa pamoja naye, (hao ndio walio wa madhehebu ya Masadukayo), WAMEJAA WIVU,

18 wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza;”

Hiyo ndiyo silaha shetani aliyotumia kumpeleka Bwana msalabani…Na silaha hiyo hiyo anaitumia leo kuangamiza watu..Je! na wewe una wivu?…kama unaingiwa na wivu ndugu yako akipata jambo Fulani ambalo wewe huna ujue unakaribia kufanyika chombo cha shetani kumwangamiza, kama unasikia wivu jambo Fulani zuri ndugu yako, au jamii yako, au rafiki yako analolifanya, kama unasikia wivu, mwingine anapooa, au anapoolewa au anapofanya hiki au kile..au anapotoka hatua moja mpaka  nyingine…kuna hatari kubwa ya kufanyika chombo cha shetani. Na wivu ukizidi sana unakuwa huna tena huruma..unakuwa unatamani kifo kwa huyo ndugu yako kama vile Kaini, alivyomwonea wivu ndugu yake mpaka akaenda kumwua.

Hivyo ni kwa namna gani utashinda Wivu?

Kwanza ni kwa kumpa Yesu Kristo maisha yako?..Unapookoka Bwana anakufanya kuwa kiumbe kipya, na ya kale yote yanakuwa yamepita, unakuwa umefanyika kiumbe kipya…Ule utu wa zamani, Bwana anauzika, Nia yako Bwana anaigueza kutoka kutazama vitu vya ulimwengu huu vinavyopita na kutazama mambo ya ulimwengu ujao ya milele yasiyoharibika..Hivyo kunakuwa hakuna shughuli yoyote ya kidunia ambayo itaweza kukupa wivu ndani ya moyo wako kwasababu nia yako imeshageuzwa na kuutazama ulimwengu ujao ambao utajiri wake na hazina yako hauna mwisho.

Pili baada ya kuokoka unapaswa uanze kujiwekea hazina yako mbinguni, Biblia inasema hazina yako ilipo ndipo na moyo wako utakapokuwepo…Hazina yako ikiwa kubwa katika mambo ya ulimwengu huu na moyo wako lazima utakuwa huko huko, hilo haliepukiki, kama ndoto zako kubwa kuliko zote ni wewe kupata mali nyingi sana ili hatimaye watu wote waje kukuona na kukuangukia na kukuheshimu, hapo roho ya wivu hauwezi kuiepuka, kwasababu atakapotokea mtu kakuzidi kidogo tu au unamwona ananyanyuka utamwonea wivu. Ndicho kilichowakuta mafarisayo na masadukayo, walikuwa na ndoto kubwa za wao waonekane wapo juu ya watu wote, na alipotokea mwingine mwenye nguvu kuliko wao wakaishia kumwonea wivu.

Lakini kama hazina yako ipo mbinguni, kwamba ndoto yako kubwa ni siku ile uirithi mbingu kwa daraja la kwanza, na kuwa na thawabu kubwa kule, kamwe hutakaa umwonee mtu wivu kwa vitu vya kidunia vinavyopita…Hazina yako inapoongezeka mbinguni, mawazo yako, akili yako, na moyo wako wote unakuwa kule, unakuwa kila siku unatafakari utukufu na thawabu zinazokungoja kule, na hivyo habari ya kuanza kuona wivu kwa vitu vya kidunia unakuwa huna..

Na hazina ya mbinguni unaitengeneza kwa kumpendeza Mungu na kwa kuifanya kazi yake…Na kazi yake sio kuhubiri tu, bali hata ile ya kuosha choo cha nyumba ya Mungu ni kazi yake yenye thawabu kubwa kule, hata ile ya kuwaombea watakatifu ni kazi yake yenye thawabu kubwa sana…n.k Unapofanya hayo bila ulegevu Roho Mtakatifu kila siku atakuwa anakushuhudia ndani yako kwamba thawabu yako ni kubwa mbinguni, na inazidi kuongezeka siku baada ya siku, hivyo kamwe huwezi kumwonea wivu mtu aliyeoa/ kuolewa na wewe hujaolewa, au jirani yako ambaye ni bilionea..

Ufunuo 2:17 “Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea………

26 Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa,

27 naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyanzi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu”……

Ufunuo 3:5 “Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake”………..

12 Yeye ashindaye, nitamfanya kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo tena kabisa, nami nitaandika juu yake jina la Mungu wangu, na jina la mji wa Mungu wangu, huo Yerusalemu mpya, ushukao kutoka mbinguni kwa Mungu wangu, na jina langu mwenyewe, lile jipya…….

21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi”.N.k

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

NI NANI ALIYEWALOGA?

JE NI DHAMBI KUWA NA MAHUSIANO KABLA YA NDOA?

Kwanini kila nikitaka kusali naingiwa na uvivu?

NINI TOFAUTI KATI YA KARAMA, UTENDAJI KAZI NA HUDUMA.

MSIJISUMBUE KWA NENO LOLOTE.

TOA SADAKA ISIYO NA KASORO KWA BWANA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Rehema Mwasampeta
Rehema Mwasampeta
3 years ago

Napenda mafundisho nitumie kila mnavyoweza