TOA SADAKA ISIYO NA KASORO KWA BWANA.

TOA SADAKA ISIYO NA KASORO KWA BWANA.

Toa sadaka isiyo na kasoro kwa bwana.


Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo, libarikiwe!. Karibu tena tujifunze biblia..Hatuna budi kufanya hivyo kila siku..maadamu tumepewa uhai.

Leo tutaendelea kujifunza umuhimu wa kumtolea Mungu kitu kilicho bora..kama hujapita somo lililotangulia lenye kichwa kinachosema “TUPENDE KUMTOLEA MUNGU VILE VINAVYOTUGHARIMU ZAIDI.”..Naomba ulipitie kwanza ili tuweze kwenda pamoja katika masomo haya yanayofuata.

Kuna umuhimu mkubwa sana kumtolea Mungu vitu vinavyotugharimu. Tusipende kutoa tu ilimradi tumetoa, kwasababu Mungu wetu ana hekima kuliko sisi na anaitazama mioyo yetu kwa undani sana. Mtu akija na kukupa wewe zawadi..na ile zawadi aliyokupa ukaja kugundua haikuwa imekusudiwa uipokee wewe..Ilikuwa ni ya mtu mwingine lakini kwasababu mtu huyo hakuwepo, na hakuna wa kumpa ukapewa wewe, hutaichukulia kwa moyo wa furaha sana kama kama ingekuwa imelengwa kwako moja kwa moja, Sasa ni kweli umepewa zawadi..jambo jema na la kushukuru, hata hicho umekipata, lakini zawadi ile ingekuwa na nguvu kwako kama ingekuwa wewe ndio mlengwa wa kwanza. Kama sisi wanadamu tuna hisia kama hizo..basi Mungu naye hapendezwi na sadaka za masalia.

Anapenda tumtolee kitu ambacho tulikuwa tumekipanga kumtolea yeye na si makombo, hapendi kuwekwa wa pili…Kumweka wa pili ni kumdharau…Haangalii wingi bali anaangalia ubora wa ile sadaka. Sadaka unayomtolea ina ubora kiasi gani..inaugusa moyo wake kiasi gani, umeigharimikia kiasi gani, hata kama ni sh.100 lakini haikuwa chenji ya kiatu ulichokwenda kununua..

Katika Agano la kale ambapo utoaji wa sadaka ulihusisha kafara za Wanyama…Wanyama ambao walitumika kwa kafara hizo kama ng’ombe, mbuzi, kondoo, njiwa n.k Mungu alitoa amri kwamba kamwe wasitolewe wakiwa na kilema, udhaifu, ugonjwa wala wenye lawama yoyote..

Ilikuwa kumtolea Mungu ng’ombe aliye na chongo ni dhambi, kumtolea mwanakondoo aliye mlemavu ni dhambi…kadhalika kumtolea ng’ombe mwenye kumbukumbu yoyote mbaya huko nyuma kama kuua mtu, au kuua ng’ombe mwenzake au kufanya jambo lolote baya ilikuwa ni dhambi kumtoa kama sadaka ya kuteketezwa kwa Mungu. Ng’ombe wa sadaka alikuwa ni lazima asiwe na hatia.

Walawi 22: 20 “Lakini mnyama ye yote aliye na kilema msimtoe; kwa kuwa hatakubaliwa kwa ajili yenu”

Kumbukumbu 17:1“Usimchinjie Bwana, Mungu wako, ng’ombe wala kondoo aliye na kilema, wala neno ovu lo lote; kwa kuwa hayo ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako”

Malaki 1:13 “Tena mwasema, Tazama, jambo hili linatuchokesha namna gani! Nanyi mmelidharau, asema Bwana wa majeshi; nanyi mmeleta kitu kilichopatikana kwa udhalimu, na kilema, na kilicho kigonjwa; ndivyo mnavyoleta sadaka; je! Niikubali hii mikononi mwenu? Asema Bwana.

14 Lakini na alaaniwe mtu mwenye kudanganya, ambaye katika kundi lake ana mume, akaweka nadhiri, ila amtolea Bwana kitu kilicho na kilema; kwa maana mimi ni Mfalme mkuu, asema Bwana wa majeshi, na jina langu latisha katika Mataifa”.

Katika agano la kale ilikuwa hairuhusiwi hata kwenda kununua ng’ombe wa mtu usiyemjua..kwasababu hujui huyo ng’ombe au kondoo alikuwa na kasoro gani huko nyuma..labda alishaua mtu utajuaje!..au alishapigana na mwenzake na kumuua utajuaje?..kwahiyo ilikuwa ni lazima mnyama aidha atoke kwenye zizi lako mwenyewe au kwa mtu unayemjua ambaye ni mwaminifu sana au anayeaminika na watu..Ili kuepuka kumtolea Mungu kitu chenye kasoro.

Umewahi kujiuliza ni kwanini siku ile Bwana Yesu alipoingia hekaluni alikuta watu wanauza njiwa, ng’ombe na mbuzi na hakukuta wanauza mashati, nguo, viatu au vyakula?.

Yohana 2:13 “Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu.

14 Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi”

Unajua ni kwanini?..Ni kwasababu watu walikuwa wanatoka mbali..wengine mataifa ya mbali na hivyo wengi wanaona uvivu kutenga muda kwenda kutafuta ng’ombe asiye na lawama wala kilema wala kasoro yoyote…walikuwa wanaona ni jambo linalochukua muda sana na linalogharimu fedha nyingi mpaka umpate huyo mnyama wa viwango hivyo…na bado ni gharama kumsafirisha yule mnyama kutoka huko waliko mpaka hekaluni kwa makuhani ili atolewe kama sadaka ya kuteketezwa..

Sasa ili kulikwepa hilo wakawa wanatafuta njia mbadala ya kuwapata wale Wanyama mahali karibu na hekalu lilipo..sasa watu wa mataifa wakaona hiyo ni fursa..wakaanza kupeleka ng’ombe zao zilizonona kwenda kuziuza karibu na hekalu, wengine wakawa wanauza ng’ombe waliowaiba, wengine wanauza ng’ombe ambao wanamagonjwa ambayo hayajaanza kujidhihirisha bado…lengo lao wapate fedha..wengine mbuzi wanaowauza wamelala na wanadamu huko nyuma…nani anajali ilimradi tu wapate fedha..wapo radhi hata kudanganya kwamba mbuzi yule au kondoo huyu hana hatia kabisa alikuwa msafi na mpole tangu anazaliwa ili wamuuze tu wapate fedha na Kesho walete wengine..wetengeneze pesa nyingi..wakaikoleza biashara mpaka pakageuka kuwa soko na vibaka wakawemo humo humo ndani pengine hata na kamari zilichezeshwa humo.

Na kwasababu wayahudi wanaokuja pale wanaotoka mbali huko na huko hawapendi kujisumbua kutafuta kilicho bora mbele za Mungu…wanauziwa pale pale hakaluni Wanyama ambao ni machakizo kuwatoa mbele za Mungu, ambao hawajui hata wametoka wapi..…Wanatoka nyumbani bila chochote..wanafika hekaluni wananua mbuzi, wanawapa makuhani wanatolewa sadaka mbele za Mungu, wanarudi nyumbani..na kuamini kwamba wametoka kubarikiwa…kumbe wametoka KULAANIWA!..Wakidhani kwamba wametoka kumheshimu Mungu kumbe wametoka kumdharau..Ndio maana Bwana aliwafukuza wote wanaouza hao wanyama mule hekaluni..kwasababu yalikuwa ni machukizo yanayoendela mule..

Je na unaithamini sadaka yako unayomtolea Mungu kila siku?..je ina kasoro yoyote?..Kama umeipata kwa njia ya wizi usiende kumtolea Mungu hiyo tayari ina dosari kadhalika kama sadaka uliyoipata umeipata kwa njia ya ukahaba usimtolee,.. kama umeipata kwa njia ya kuuza bar, au sigara, au madawa ya kulevya au kamari, au ufisadi, au rushwa au wizi ni heri usimtolee Mungu…kama ni vimasalia salia ndio umepanga umtolee Mungu..usivitoe…Kwasababu Biblia inasema..

Mithali 15: 8 “Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana..”

Ni masuala ya sadaka haya haya ndio yaliyoutoa uhai wa Anania na mkewe Safira…Anania kauza kiwanja kapanga kumtolea Mungu fedha yote aliyouzia kiwanja..lakini yeye akawa anakwenda kumtolea Mungu chenji huku fedha nyingine kaizuia..matokeo yake akafa yeye na mkewe..na hiyo ni agano jipya sio agano la kale.

Kwahiyo ukitaka kumtolea Mungu tafuta donge nono..ambalo huwezi kumwambia hata mtu kwasababu atakushangaa na kukuona wa ajabu..Unapomtolea Mungu mtolee kwa fedha iliyopatikana kihalali na kiwango cha juu ili sadaka yako isiwe na kasoro..Na njia nyingine bora ambayo Mungu atakuongoza umtolee yeye ambayo haitakuwa ni ya kumdharau..mtolee yeye ili ubarikiwe.

Bwana akubariki sana.

Shalom

Kama hujaokoka..Okoka sasahivi na kama hujabatizwa katafute ubatizo sahihi haraka sana..kwasababu mambo hayo mawili yanakwenda pamoja..

Mada Nyinginezo:

USILETE UJIRA WA KAHABA, NYUMBANI KWA MUNGU.

Tofauti katika ya zaka na sadaka ni ipi?

TUMTOLEE MUNGU VILE VINAVYOTUGHARIMU ZAIDI.

KIJITO CHA UTAKASO.

UWEPO WA BWANA HATA KATIKATI YA MATESO.

TUMAINI NI NINI?

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments