UWEPO WA BWANA HATA KATIKATI YA MATESO.

UWEPO WA BWANA HATA KATIKATI YA MATESO.

Shalom…Jina la Bwana, libarikiwe..Karibu tuzidi kujifunza Neno la Mungu…Ambalo ni Taa iongozayo miguu yetu na mwanga wa njia zetu. (Zaburi 119:105).

Leo tutajikumbusha namna Mungu anavyotenda kazi ili tusijikute tunaingia kwenye manung’uniko pale tunapojikuta tunapitia hali fulani tofauti na vile tulivyoitegemea…Kama wengi wetu tujuavyo Maisha ya Yusufu kwenye Biblia yamebeba funzo kubwa sana ya jinsi gani Mungu anaweza kumtoa mtu aliyekata tamaa katika mateso na kumnyanyua juu tena.

Lakini pamoja na hayo kuna jambo la Muhimu la kujifunza juu ya Yusufu…Ukitazama katika hatua zote Yusufu alizopitia utagundua kuwa Mungu alikuwa naye hakumwacha…

Utaona wakati yupo nyumbani kwa Potifa..japokuwa alikuwa ni mtumwa ndani ya ile nyumba lakini Mungu alimfanikisha kila alilolifanya lilifanikiwa….Akiwa ndani ya nyumba ile pengine mifugo aliyopewa aisimamie na Bwana wake ilizaliana na kuwa na afya Zaidi kuliko ya wafanyakazi wengine…Pengine shamba alilopewa alisimamie lilikuwa linazaa Zaidi ya watumwa wengine…pengine kila alilotumwa na Bwana wake Potifa lilikuwa linafanikiwa..tofauti na wanapotumwa watumwa wengine n.k…Hivyo Potifa Bwana wake aliliona hilo ndipo akaamua kumweka juu ya kila kitu chake kwasababu aliona kijana ana Neema ya mafanikio.

Mwanzo 39:2 “Bwana akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri.

3 Bwana wake akaona ya kwamba Bwana yu pamoja naye, na ya kuwa Bwana anafanikisha mambo yote mkononi mwake.

4 Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake.

5 Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, Bwana akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa Bwana ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba.

6 Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote chake, ila hicho chakula alichokula tu”.

Vivyo hivyo…hata baada ya Yusufu kupachikiwa kesi ya jaribio la ubakaji…alipokuwa mule gerezani Mungu aliendelea kuwa naye…Na yale yale aliyoyaona Potifa kwa Yusufu..Mkuu wa gereza naye akayaona kwa Yusufu..akaona mbona tangu huyu kijana amekuja humu gerezani utaratibu wa gereza umebadilika…mambo yanakwenda vizuri…Na alipojaribu kumweka kuwa kiongozi wa wafungwa ndio mambo yalivyozidi kunyooka Zaidi, usumbufu wa wafungwa ulipungua…pengine alitamani hata Yusufu angeendelea kuwa mfungwa siku zote jinsi mambo yanavyokuwa yanakwenda vizuri mule gerezani.

Lakini ni nini tunaweza kujifunza hapo?…Hata katika hali ya utumwa na vifungo Mungu yupo na watu wake… Wengi hawalijui hilo?..wanadhani kama ni mkristo ukishapitia kwenye matatizo basi huo ni uthibitisho tayari Mungu kashakuacha…. Kitendo tu cha wewe kuwa mtumwa wa mwingine basi Mungu hayupo na wewe hivyo unahitaji maombi ya kufunguliwa…kitendo tu cha kufanya kazi ya kusafisha barabara basi upo chini ya laana na vifungo…Kuuza genge basi wewe ndio huna roho ya mafanikio Huo ni uongo wa shetani.

Hufanyi kazi wizarani lakini unafanya kazi katika nyumba ya mtu kama kijakazi…Kazi hiyo siyo uthibitisho kwamba Mungu hayupo na wewe…yupo na wewe huko huko kama alivyokuwa na Yusufu katika nyumba ya Potifa maadamu unajua umeokoka na unaishi kulingana na Maneno ya Yesu Kristo basi uwe na amani uwepo wa Bwana upo na wewe…Yusufu hakuwa na laana ya ukoo yeye kuuzwa utumwani…Alikuwa ni mwana wa Ibrahimu aliyebarikiwa….

Hivyo Kuwa tu mnyenyekevu usinung’unike ni suala la muda tu…utafika wakati utapelekwa hatua nyingine…lakini wewe tazama tu..kama kiongozi wako anapenda kuwa na wewe…na anaona anapata raha kuwa na wewe..na anafanikiwa sana anapokuwa na wewe kuliko alivyokuwa na wengine huko nyuma na hataki uondoke huo ni uthibitisho kwamba Mungu anafanikisha mambo yake kwaajili yako wewe…kama ilivyokuwa kwa Yusufu…Hivyo kuwa mnyenyekevu bado uwepo wa Bwana upo na wewe ni suala la muda tu…Usianze kusema anakutesa au anakutumia wewe kupata faida zake mwenyewe, wewe kuwa mtulivu endelea kuwa mwaminifu kama Yusufu.

Mungu hakushindwa kumtoa Yusufu nyumbani kwa Potifa na kwenda kumpa kwake binafsi na ambariki lakini alimbakisha pale pale kwa Potifa kwa kusudi maalumu.…Na Mungu hakuvifanikisha vitu vya Yusufu bali alivifanikisha vitu vya Potifa kwaajili ya Yusufu…Alifanikisha mifugo ya potifa na si ya Yusufu..ingawa chanzo cha baraka hizo ilikuwa ni Yusufu…Kadhalika aliistawisha kazi ya mkuu wa Gereza na si Yusufu..

Lakini ulipofika wakati, siku, tarehe, mwezi na Mwaka katika kalenda za kimbinguni…Njaa ilikuwa imekusudiwa duniani kote…na kwamba kwa kupitia mtu mmoja Yusufu dunia yote ilipaswa ipate Neema…Ndipo wakati wa Yusufu ulifika….Sasa hebu jaribu kufikiri endapo Mungu angemfungua Yusufu awe huru wakati wa Potifa na Mungu na kwenda kukaa kwake na kujenga nyumba nzuri na kumstawisha na kumbariki…je! huo wakati wa njaa ungefika na Yusufu na utajiri wake wote angekuwa wapi?..si na yeye angekufa na njaa tu kama wengine au angeuza kila kitu chake anunue chakula kama wengine?…manyumba yake yangekuwa wapi saahiyo?..mifugo yake ingekuwa wapi saahiyo?..Baba yake huko alikokuwa amemwacha Mungu alimbarikia katika mifugo na mali nyingi lakini pamoja na baraka zote hizo kutoka kwa Mungu walifunga safari kwenda Misri kutafuta chakula…unadhani endapo na Yusufu asingepitia hatua hizo angesalimika vipi na hiyo njaa ambayo imeikumbwa dunia?.

Kwahiyo wakati wa Mungu ni bora kuliko wakati mwingine wowote!..Na huo si mwanadamu anauamua..bali ni Mungu mwenyewe anaupanga mbinguni…tunachopaswa sisi kufanya ni kujinyenyekeza kila siku chini ya kusudi lake na kuishi Maisha yasiyo ya manungu’uniko tukijua kuwa uwepo wa Bwana bado upo na sisi…Usiseme mimi sasa nauza hiki au kile ningepaswa niwe kule au kama yule…Usiseme hivyo, jiangalie je! Unakwenda sawa na Mungu katika unachokifanya kama Yusufu?.. huku ukifahamu kuwa hata katikati ya dhiki, au katikati ya shida, au katikati ya misiba, au katikati ya utumwa mgumu, au katika ya kukandamizwa…Mungu yupo pamoja na sisi na anatuwazia yaliyo mema…

Endao tukiwa waaminifu kuishi katika Neno lake Kila mahali Mkono wa Mungu upo na sisi kutuongoza..hakuna tutakapopitia yeye asiwe pamoja na sisi biblia inasema hivyo…

Zaburi 139:5 “Umenizingira nyuma na mbele, Ukaniwekea mkono wako.…….7 Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako?

8 Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.

9 Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari;

10 HUKO NAKO MKONO WAKO UTANIONGOZA, Na mkono wako wa kuume utanishika.

11 Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku;

12 Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa.”.

Hivyo nakutia moyo wewe uliyeamua kujikana nafsi na kuukataa ulimwengu na kumfuata Yesu Kristo kwa gharama zozote, amesema yupo na wewe ni kweli yupo na wewe Neno lake si uongo Uwepo wa Bwana utakuwa nawe siku zote….Zidi kumtegemea, zidi kumwamini, ishi Maisha ya furaha, usijifananishe na wengine..Bali mtazame Mungu katika mambo yako yote. Na mambo yote Mungu atayafanikisha mbele zako kwa wakati wake.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Bwana akubariki.

Mada Nyinginezo:

TWEKA MPAKA VILINDINI.

KAMA MUNGU ANABORESHA KAZI ZAKE, KWANINI WEWE USIBORESHE ZA KWAKO?.

UTHABITI WA AGANO LA MUNGU KWA MKRISTO.

UPAKO NI NINI?

Nini maana ya maneno haya ya Bwana? “Nami nikiinuliwa juu ya nchi,NITAWAVUTA WOTE KWANGU”(Yohana12:32).

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Shalom masehe
Shalom masehe
1 year ago

Mungu awabariki sana Kwa mafundisho haya ya Neno la Mungu Kwa kweli Kwa upande wangu Mimi mafundisho haya yamefanyika msaada mkubwa Sanaa maana toka nilipoanza kufuatilia masomo yenu kweli Kuna mambo mengi nimejifunza na ninaendelea kujifunza na zaidi ninazidi kumfahamu zaidi Mungu na kuwa karibun nae. Mungu awabariki sana na Mungu azidi kuwapa mafunuo Zaid watumishi wa Mungu 🙏👋

ANICETH DAVID
ANICETH DAVID
3 years ago

MTUMISHI MIMI NAITWA ANISETH NINA MIAKA 29 NIPO MWANZA NAPENDA KUULIZA SWALI MIMI NILIFANYA KOSA KAZINI LA WIZ MARA YA KWANZA NKAKIMBIA KABISA KAMA MIEZ MITATU NIKARUDI KAZIN WAKANIIITA TENA BADO SIKUBADILIKA NIKARUDIA TENA WAKANIFUKUZA ILA NATAMAN NIOMBE MSAMAHA LAKIN NAONA AIBU ATA KUMSOGELEA BOSS WANGU ATA NISIPO RUDI KAZN ILA ANISAMEE TU MAANA KILA NIKIKAA NAONA KAMA NAMAKOSA SANA NINA TUBU ZAMBI ILA BADO NAKUWA CJIAMN KAMA YULE MTU ATAKUWA KANISAMEE MAANA BIBLIA INASEMA UNAPO KOSA MFATE ULIE MKOSEA UMUOMBE LADHI UTAKUWA UMESAMEEWA DUNIAN MPKA MBINGUN EBU NISHAURI MAANA NIMEANZA KUSALI LAKN NAITAJ USHAUR KWA HILI