USILETE UJIRA WA KAHABA, NYUMBANI KWA MUNGU.

USILETE UJIRA WA KAHABA, NYUMBANI KWA MUNGU.

Usilete ujira wa kahaba, nyumbani kwa Mungu.


Shalom, Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze Maandiko..

Kuna mambo ambayo unaweza kuyasema ukadhani hayapo kabisa kwenye biblia..Lakini yapo!…Na kuna mambo machache yanayopuuziwa na wengi..lakini ni ya kuzingatia sana tunapomkaribia Mungu..Kitu kimoja ambacho wengi hawajui ni kwamba Mungu wetu tunayemwabudu hachangamani na uchafu…Mtu yeyote Yule aliye mchafu awe mchungaji, au mwalimu, au mwinjisti, au nabii, au muumini wa kawaida..

Mungu hawezi kutembea naye akiwa katika hali ya uchafu, hastahili hata kushiriki meza ya Bwana wala kumtolea Mungu sadaka!!…wala maombi yake hayasikilizwi wala dua zake hazimfikii…Kwa ufupi mtu huyo tayari ameshafarakana na Mungu na ni Adui wa Mungu (Soma Isaya 59:1-5)..Na endapo akilazimisha kumfanyia Mungu ibada katika hali hiyo huku anajijua kuwa yeye ni mchafu na hataki kubadilika…Mtu huyo anajitafutia laana badala ya Baraka…

Asilimia kubwa ya wahubiri wanalijua hilo, isipokuwa hawapendi kuwaambia watu ukweli..kutokana na kwamba mapato yao kanisani yatashuka…watawezaje kumwambia kahaba asitoe kwanza sadaka zake mpaka atakapomgeukia Mungu kwa moyo wake wote kwanza, kwa kuacha uasherati wake??..Hawawezi kufanya hivyo kwasababu ndio ulaji wao upo hapo! akimwambia hivyo anaogopa atakasirika na hivyo kuondoka…Lakini matokeo ya kutokufanya hivyo ni kumtafutia laana Yule anayetoa sadaka hizo haramu mbele za Mungu…

Leo tutajifunza mistari kadhaa ihusuyo habari hizo..Ambapo tukishajifunza itatusaidia kudhamiria kuokoka kwanza kwa kumaanisha kuziacha dhambi ndipo tumkaribie Mungu.

Kwanza kabisa kama hujaokoka, na unajua kabisa unastahili kuokoka lakini hutaki na unaendelea kuwa vuguvugu..Bado unaendelea kufanya kazi yako ya kujiuza kisirisiri, bado unaendelea kula rushwa kisirisiri, unaendelea kutapeli kisirisiri..Na Jumapili unakwenda kanisani kuabudu na kutoa sadaka yako kwa Mungu..NATAKA NIKUAMBIE UNAFANYA DHAMBI!!..Inawezekana hujawahi kabisa kuhubiriwa hivi kanisani kwako..lakini leo hii sikia Neno la Mungu…Acha kabisa usimtolee Mungu, sadaka hizo kwasababu ni unamdharau..unajitafutia laana badala ya Baraka…

Biblia inasema…

Kumbukumbu 23: 18 “Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya Bwana, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; kwani haya ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako, yote mawili”.

Lengo la Mungu kutuagiza kumtolea, sio kwamba anashida ya Hela,.au anatafuta kuwatajirisha watumishi wake…hapana hilo sio lengo lake..Yeye ana njia zaidi ya milioni moja ya kuwalisha watumishi wake wa kweli, tofauti na hata hiyo ya madhabahuni…Lengo lake kuu ni kutuumbia sisi moyo wa utoaji ndani yetu kama yeye alivyo mtoaji..kwamba hata ikitokea yupo mtu mwenye uhitaji katokea mbele yetu tuwe na moyo wa kutoa sehemu ya vitu vyetu na muda wetu kumsaidia…jambo ambalo linampendeza na lituletealo Baraka kutoka kwake…

Anataka tuwe wakamilifu na watakatifu kama yeye alivyo…Lakini unapokwenda kanisani na lengo la kwamba Mungu anahitaji fedha kutoka kwako au unakwenda kumpa mchungaji fedha,..Na hivyo fedha yoyote tu itakayokuja mkononi mwako hata ya rushwa ni ruksa kuipeleka nyumbani kwa Mungu…Kanisa sio benki ya madanguro wala mafisadi kwamba mafedha yote haramu ndiyo yanakwenda kuhifadhiwa huko…..Ni kujitafutia laana badala ya Baraka.

Soma tena mstari huu..

Mhubiri 5: 1 “Jitunze mguu wako uendapo nyumbani kwa Mungu; Maana ni heri kukaribia ili usikie, Kuliko kutoa kafara ya wapumbavu; Ambao hawajui kuwa wafanya mabaya”.

Unaona!..Biblia inasema ni heri ungeenda tu kusikiliza kuliko kwenda na kutoka kafara za wapumbavu ambao hawajui kuwa wanafanya dhambi…Usitie mkono wako kushiriki shughuli zozote za kanisa kama unajijua huna mpango na Mungu…Unafanya dhambi na utajitafutia laana badala ya Baraka.. Kadhalika usishiriki meza ya Bwana kama hujaokoka kikweli kweli na kupokea Roho Mtakatifu,.Kama ni mzinzi na mwasherati..pengine hukuhubiriwa kanisani, kwasababu Mhubiri wako pengine aliogopa angekwambia ukweli kwamba unatenda dhambi ungekwazika na kuhama kanisa na yeye akakosa mapato..lakini leo lisikie Neno la Mungu usiisogelee madhabahu kama hujaamua kumgeukia Yesu Kristo kikweli kweli…Usiule mwili wa Kristo, wala damu yake isivyopaswa kwasababu utajitafutia laana badala ya Baraka…

Usilete ujira wa kahaba, nyumbani kwa Mungu.

Soma…

1Wakorintho 11:27 “Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana.

28 Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe.

29 Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili.

30 Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala. Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu tusingehukumiwa”

Yuda hakujipambanua vizuri..akaenda kushiriki meza ya Bwana huku moyoni mwake kulikuwa na mawazo ya kumsaliti Bwana Yesu..kilichotokea ni shetani kumwingia saa hiyohiyo baada ya kupokea tonge na matokeo yake yaliishia ni kifo kasome Yohana 13:26-27 (Tonge linalozungumziwa hapo sio tonge la ugali bali mkate wa Bwana). Wakati wengine wamepokea Baraka kwa kushiriki ile meza ya Bwana, Yuda yeye kapokea laana kwa kushiriki kitendo hicho hicho…

Kadhalika Kabla ya kwenda kupokea ule mkate wala kupokea kile kikombe jiulize mara mbili mbili je!..umeokoka kweli kweli?..Kama hujaokoka na unakwenda kushiriki basi umeenda kujizolea laana badala ya Baraka.

Kadhalika kama Hujaamua kuacha dhambi na kugeuka na kukusudia kumfuata Yesu Kristo kwa moyo wako wote,..halafu unakwenda kubatizwa na huku moyoni mwako unajua kabisa hujaamua kuacha uasherati, ulevi au sigara au uchafu uliokuwa unaufanya..na hivyo ukaenda kuingia kwenye yale maji na kubatizwa nataka nikuambie utakuwa umekwenda kujitafutia laana badala ya Baraka..Kama hujaamua kumguekia Yesu kwa dhati..usiende kubatizwa kabisa..subiri mpaka wakati utakapoamua kama hiyo nafasi itakuwepo..

Usishiriki jambo lolote la kiimani kama hujaamua kweli kuwa upande wa Mungu.

Na mambo mengine yote hahusuyo madhabahu usiyafanye kama huna uhusiano wowote na Mungu…hata usimfuate Mtumishi wa Mungu kumwomba akutabirie wala kukuombea kama mwenyewe unajua moyoni huna mpango na msalaba..ni hatari kubwa sana kufanya hivyo nenda kasome kitabu cha (Ezekieli 14:3-4) na kilichomtokea mke wa mfalme Yeroboamu, uone ni nini kitamtokea mtu Yule ambaye kwa makusudi hana mpango na Mungu na bado anataka kwenda kuuliza kwa Mungu..

Usilete ujira wa kahaba, nyumbani kwa Mungu.

hata ya kuhubiri madhabahuni ni hatari,..kama hujatakaswa kwa Damu ya Yesu, usiisogelee kabisa madhabahu…

Kama ulikuwa unafanya hivyo na hujui kwamba ulikuwa unakosea..Ulikuwa hujui kwamba sadaka yako ya ukahaba ni machukizo mbele za Mungu..na sasa unataka kutubu na kujitakasa ili sadaka zako zikubaliwe mbele za Mungu..Mlango upo wazi leo..unachopaswa kufanya ni kudhamiria kwanza kuacha dhambi na kukiri kwamba ulikuwa mkosaji..kisha unatubu na kumwambia Bwana akusamehe na kukuosha tena kuwa mpya…

Ukifanya hivyo kwa kumaanisha kabisa kutoka moyoni, basi Bwana YESU atakuwa ameshakusamehe..Hivyo Baada ya hapo nenda kabatizwa kama hujabatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa Jina la Yesu, na kisha Roho Mtakatifu ataingia ndani yako na kukutia muhuri kuwa wake milele..

Na mwisho ni kusudia kuishi maisha ya usafi na utakatifu kuanzia huo wakati na kuendelea kulingana na maagizo ya Mungu..Hapo sadaka zako zitampendeza Mungu, na sala zako kwake zitakuwa kama manukato mazuri mbele zake, Maombi yako yatasikiwa, dua zako zitasikilizwa, sifa zako zitampendeza Mungu, kwasababu upo chini ya damu ya Emanueli, YESU KRISTO..

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

 

Bwana akubariki.

Mada Nyinginezo:

Je! ni vema kwa mkristo kwenda hospitali au kutumia miti shamba anapougua?

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

KAMA MUNGU ANABORESHA KAZI ZAKE, KWANINI WEWE USIBORESHE ZA KWAKO?.

NI KIPI MUNGU ANACHOKITAZAMA ZAIDI, MOYO AU MWILI?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments