NI KIPI MUNGU ANACHOKITAZAMA ZAIDI, MOYO AU MWILI?

NI KIPI MUNGU ANACHOKITAZAMA ZAIDI, MOYO AU MWILI?

Je! ni kipi Mungu anachokitazama zaidi, moyo au mwili?

Shalom. Jina la Bwana Yesu libarikiwe.

Karibu tujifunze Biblia. Neno la Mungu linasema katika..Waefeso 5:9-10 “kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; mkihakiki ni nini impendezayo Bwana”.

Hivyo kila siku ni wajibu wetu kuhakiki ni nini impendezayo Bwana. Kila tunachokifanya, kila tunachokisema na kila tunalichopanga kukifanya. Ni lazima tuwe na uhakika kwamba Je! kinampendeza Mungu.

Leo tutajifunza kuhusu mambo Mungu anayoyaangalia ndani ya mtu. Kama wengi wetu tunavyofahamu kuwa kuna usemi ambao upo kila mahali miongoni mwa wakristo wengi usemao kwamba “Mungu haangalii mambo ya nje kama mavazi bali anaangalia moyo”. Usemi huo upo kila mahali kama hujawahi kuusikia jaribu kufanya mahojiano na watu 5 au 10 hususani mabinti utalisikia Neno hilo likitoka vinywani mwao.

Kwanza kabisa ni muhimu kufahamu kuwa Mwanadamu kaumbwa katika sehemu kuu mbili ambazo ni UTU WA NDANI na UTU WA NJE. Utu wa ndani ndio unajumuisha Nafsi na Roho ya mtu. Na utu wa Nje ndio hii miili tuliyonayo. Hivyo kuna utu wa ndani na utu wa nje. Soma (Warumi 7:22, Waefeso 3:16),

Sasa aliyeufanya utu wa ndani ndio huyo huyo aliyeufanya utu wa nje. Hivyo vyote viwili kwake anavitazama. Lakini tukija katika suala la Ibada zetu sisi binafsi na Mungu ni ukweli usiopingika kwamba Mungu anatazama utu wetu wa ndani, na si nje. Ingekuwa anatazama miili yetu basi asingesikiliza sala zetu tunapojifungia vyumbani mwetu na kuomba tukiwa kifua wazi, au asingesikia sala zetu au sifa zetu tuwapo bafuni tunaoga. Hivyo hiyo ni wazi kuwa Mungu anaitazama mioyo yetu zaidi ya miili yetu.

Lakini linapokuja suala la kuwepo nje mahali ambapo pana mkusanyiko wa watu wengi. Kama kanisani au barabarani. Ni lazima ujifunike kwasababu haupo wewe na Mungu hapo..Bali upo wewe, Mungu pamoja na watu wengine. Mungu anatazama kweli moyo wako lakini hao wengine hawaoni moyo wako bali mwili wako, na wanapokuona upo nusu-uchi, au umevaa mavazi yasiyostahili au yasiyo na heshima, mioyoni mwao kutatokea tamaa, kutatoka shuku mbaya, kutatoka aibu, kutatokea kukwazika na wakati mwingine hasira na matusi.

Sasa mambo hayo ndiyo yanayomchukiza Mungu kwasababu unawakosesha wengine. Na ndio maana katuambia tuvae mavazi ya kujisitiri kila mahali tunapokwenda. 1Timotheo 2:9 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi;”

Usipofanya hivyo, utakuwa unatenda dhambi kwa kuwakosesha wengine. Na Biblia inasema katika..

Marko 9.42 “Na ye yote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini.”..

Wewe hujali mwingine anatenda dhambi kwaajili yako. Lakini Mungu anajali sana, adhabu yake ndio hiyo hapo kwamba ni afadhali “kufungiwa jiwe la kusagia na kutupwa baharini”, kuliko kumfanya mtu mmoja akutamani kutokana na uvaaji wako.Kuliko kumfanya mtu mmoja aige uvaaji wako utahukumiwa kwaajili ya hayo.

Kama unasikia joto na unataka kuomba au kuabudu huku umevaa nguo fupi, basi nenda nyumbani kwako peke yako, vaa nguo zako fupi. Jifungie peke yako mahali asipoweza mtu hata mmoja kukuona omba unavyotaka na Sali unavyotaka. Hapo Mungu kweli hataangalia mavazi yako bali roho yako. Lakini unapotoka nje! Hiyo ni habari nyingine kabisa. Mavazi yako na mwonekano wako unajalisha sana. Bwana Yesu alisema..

Mathayo 5:16 “Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni”.

Sasa Ikiwa kuangaza kwako ni nusu-uchi barabarani, ni nani atayayatazama matendo yako na kumtukuza Mungu mbinguni?

Mtu mmoja tu unapomkosesha! Kumbuka sio watu 20, biblia inasema mmoja tu!! Ni huzuni kubwa sana kwa Mungu. Hakuna mtu anayeweza kukutamani ukivaa nguo za kujisitiri mwili wako wote. Usidanganyike na Semi za kishetani zinazokwambia na kukufundisha utembee nusu uchi barabarani au uingie ibadani na vimini hakuna shida. Huo ni uongo wa shetani 100%, ambao unatokana na upambanuzi mbaya wa maandiko…maswali ya moyo au mwili kwamba Mungu anaangalia moyo zaidi ya mwili yakatae.

Na tunapozungumzia uvaaji, tunalenga mavazi..sio mapambo!. Mapambo kama lipstick, wigi, hereni, make-up zote kama kujipaka hina, kuchora tattoo,kupaka wanja.kuchonga nyusi, kujichubua… hayo ni machukizo kabisa ambayo biblia imeyakataza (Soma 1Timotheo 2:9-10, Walawi 19:28). Hupaswi hata kujipamba na kumwomba Mungu ukiwa chumbani mwako peke yako. Kwasababu ni sanamu umeziweka juu ya mwili wako, na hivyo huwezi kumwomba Mungu na huku kuna sanamu kichwani mwako au mwilini mwako.

2Wakoritho 6:16 “Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.

17 Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha”.

Bwana akubariki sana.

Kama hujaokoka! Mlango wa Neema upo wazi, ila si karibuni, na ile njia ya uzima inazidi kuwa nyembamba. Kuokoka kesho ni ngumu kuliko leo, hivyo ni vyema ukafanya uamuzi leo, kwasababu biblia inasema saa ya wokovu ni sasa. Amua kwa dhati kutubu dhambi zako zote huku ukimaanisha kuziacha kabisa, na kisha baada ya kutubu tafuta ubatizo sahihi, ambao huo utakufanya ukamilishe wokovu wako. Ubatizo sahihi ni wa maji mengi na kwa Jina la Yesu kulingana na Matendo 2:38. Na kwa kufanya hivyo Roho Mtakatifu atakutia muhuri na kuwa wake milele, na kukupa uwezo wa kushinda dhambi.

Maran atha!jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

SAMEHE KUTOKA NDANI YA MOYO WAKO.

TOBA IGUSAYO MOYO WA BWANA.

KAMA MUNGU ANABORESHA KAZI ZAKE, KWANINI WEWE USIBORESHE ZA KWAKO?.

Mpagani ni nani?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments