NYIMBO ZA WOKOVU

NYIMBO ZA WOKOVU

Utauliza kuna nyimbo za wokovu?. Jibu ni Ndio! Uimbaji ni moja ya karama za Roho kama zilivyo karama nyingine, kama vile Uchungaji, Unabii, ualimu, uinjilisti n.k.

Na kama vile kulivyo na manabii wa uongo, na waalimu wa uongo na wainjilisti wa Uongo. Kadhalika pia kuna WAIMBAJI WA UONGO. Tabia zinazoonekana kwa manabii wa Uongo ndio zile zile zilizopo kwa waimbaji wa uongo.

Manabii  Uongo wanapenda fedha. Na ndivyo ilivyo kwa waaimbaji wa Uongo. Nabii wa uongo hatahubiri wokovu hata siku moja. Bali atahubiri anavyojua yeye ilimradi tu, asiwaudhi watu ili wawe wepesi kufungua pochi zao na kumpatia chochote. Hawataweza kuvumilia kamwe kufanya kazi ya Mungu bila kupata malipo yoyote kutoka kwa waumini. Na wanajua kitu pekee  kitakachomgeuza mtu na kuwa mkristo ni kumwambia kweli yote ya Biblia.

Waimbaji wa uongo nao ni hivyo hivyo. Kamwe hawataimba nyimbo za wokovu, za watu kutubia dhambi zao na maonyo ya siku za mwisho. Bali wataimba nyimbo za kuwafariji watu hata katika hali za dhambi walizopo. Lengo kuu na madhumuni ni ili wasiwaudhi mashabiki wao na hivyo wakakosa soko/fedha kwa nyimbo zao. Wanajua wakimhubiria mtu wokovu, mtu yule hatafikiria habari za kumpa yeye fedha. Bali atafikiria habari za kuyatakasa maisha yake. Mtu atatoka pale amechomwa moyo wake na mwenye moyo mzito, kitu ambacho wao hawakitaki. Kitawakoseshea mapato. Watakula nini??

Kadhalika Manabii wa uongo wanapenda UMAARUFU.

Na Waimbaji wa uongo ni hivyo hivyo. Leo utaona mtindo fulani umetoka nao pia wamo. Tofauti yao na watu wasanii wa ulimwengu huu haipo. NI WASANII, Kuimba kwao ni SANAA na sio Injili. Malengo yao ni kuwa waimbaji maarufu duniani na sio kitu kingine. Lakini muhubiri wa kweli au mwimbaji wa kweli lengo lake sio kuwa maarufu duniani. Au sio kujulikana duniani kote bali ni kuhakikisha injili inajulikana na watu wote, inawafikia watu wote duniani. Watu watubu na kuokoka na kuacha dhambi na kumgeukia Kristo na kwenda mbinguni. Hiyo ndiyo raha ya mhubiri au mwimbaji wa kweli wa nyimbo za wokovu.

Na kama uimbaji ni moja ya karama za Roho Mtakatifu. Viwango vya Roho ni vile vile. Bwana Yesu alisema mtu yeyote akitaka kuwa mwanafunzi wangu.. “ajikane mwenyewe ajitwike msalaba wake anifuate. (Mathayo 16:24)”. Uanafunzi sio tu uchungaji, au uinjilisti au ualimu..bali ni pamoja na uimbaji.

Na pia anasema katika Luka..

Luka 12:47 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana.

48 Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi.”

Umeijua Injili ya kweli. Lakini bado huimbi nyimbo za wokovu na badala yake unaimba tu nyimbo za kuwaburudisha watu. kiasi kwamba hata wakiwa bar! wanaona faraja tu kuipiga au kuisikiliza nyimbo yako. Fahamu kuwa kwako vitatakwa na vya ziada.

Na sifa nyingine ya mwisho ya Mwimbaji wa uongo, ni kufanya kazi kwa kutegemea malipo. Kwamfano utasikia mwimbaji fulani hataki kuimba mpaka ahakikishiwe kiwango fulani cha fedha. Akiahidiwa kiwango kidogo hasimami kuimba. Ukiona mwimbaji yupo hivyo basi fahamu kuwa ni mwimbaji wa uongo.

Ulishawahi kuona wapi, mchungaji anaalikwa kwenda kuhubiri kwa kuahidiwa kiwango fulani cha fedha?. Au mwinjilisti gani anakwenda kuhubiri huku tayari kashapambana na bei ya kupanda madhabahuni. Sasa kama wachungaji ambao karama zao zimewekwa wazi kwenye maandiko hawafanyi hivyo kwanini wewe unayejiita mwimbaji ufanye hivyo?. Huoni kama kutakuwa na kasoro kubwa sana kwako?.

Bwana atusaidie sana. Kama ulikuwa ni mmoja wapo wa wanaofanya hivyo, au wenye malengo ya kufanya hivyo. Na ulikuwa hujui kama ni makosa. Mlango wa kutubu bado upo wazi. Kutubu maana yake ni kugeuka kuacha kile ulichokuwa unakifanya kisicho sawa. Ukiamua tu kugeuka na kuamua kumwimbia Mungu NYIMBO ZA WOKOVU na sio NYIMBO ZA KUSAKA PESA. Bwana atakupokea, Kwasababu hizi ni siku za mwisho ambazo biblia imetabiri kuinuka kwa wimbi kubwa la manabii wa uongo, Ikijumuisha huko huko na waimbaji wa uongo na waalimu wa uongo na waachungaji wa uongo.  Bwana akusaidie usiwe miongoni mwao, Bwana atusaidie tusiwe miongoni mwao.

Maran atha!


Mada Nyinginezo:

YUDA ISKARIOTE! MTUME ALIYECHAGULIWA NA BWANA YESU.

INJILI NI NINI?

SIKU YA HUKUMU ITAKUWAJE?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments