SIKU YA HUKUMU ITAKUWAJE?

SIKU YA HUKUMU ITAKUWAJE?

Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze Maandiko..Biblia inatuasa tuwe tunajikumbusha kila siku yale ambayo tumeshajifunza ( 2 Petro 1:12-13, Yuda 1:5), hiyo itatusaidia kutompa nafasi shetani kuziiba zile mbegu ambazo zilishapandwa ndani yetu tayari…Leo kwa Neema za Bwana tutajikumbusha ni kwa jinsi gani Ulimwengu utahukumiwa na watakatifu.

Ni jambo la kufurahisha kuona bado kuna watakatifu ulimwenguni, watu wanaojitunza na kumweshimu Mungu, kwa viwango vya juu…kuona bado kuna watu wanamcha Mungu, kuna wanawake na wanaume wanaojiheshimu, kuona kuwa bado kuna watu ni wapole, ni wasomaji na watendaji wa Neno, ni wavumilivu, wasikivu, wenye huruma, wasiolipiza kisasi, wenye mioyo ya Toba, na wenye kuwahurumia wengine n.k Haijalishi watakuwa ni wachache kiasi gani, lakini uwepo wao tayari ni Tiba kubwa kwa ulimwengu.

Jambo lisilojulikana na wengi ni kuwa Uwepo wa Watakatifu duniani leo hii, ndio unaosababisha ulimwengu usiangamizwe…Bwana akitazama katika mji mmoja na kuona maovu yaliyomo ndani ya huo mji, na akaona huko watakatifu watano, basi huo mji wote unaweza ukasalimika kwasababu tu ya hao watakatifu watano waliopo ndani ya Huo mji. Na siku maangamizi ya Huu ulimwengu yatakapokuja Bwana atakuwa ameshawaondoa watakatifu wake kwa kuwanyakua, haiwezekani kuwaangamiza watakatifu wake pamoja na waovu. Ndio maana utaona Bwana alitamani kuuhurumia mji wa Sodoma na Ghomora endapo tu angekuta huko watu kumi tu walio wakamilifu, lakini hawakuwepo hata hao kumi..Na zaidi ya yote, hata Lutu huyo mmoja aliyesalia walimdharau. Na hivyo kujisababishia maangamizi yao….Hiyo ndiyo Neema wanayoibeba watakatifu waliopo katika ulimwengu sasa…

Lakini katika upande wa pili wa shilingi, Uwepo wa Watakatifu mahali fulani pia ni Ishara mbaya kwa ulimwengu…Kwasababu hao hao watakatifu ambao kwa kupitia wao Mungu anairehemu dunia, hao hao siku ya Hukumu watauhukumu Ulimwengu. Biblia inasema hivyo katika

1 Wakorintho 6:2 “Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu?……”

Sasa utauliza Watakatifu wataihukumu vipi dunia?..Na nafasi ya Bwana Yesu ya kuhukumu itakuwa ni ipi Kama watakatifu wataihukumu dunia?, Na pia inawezekanikaje siku ile mtu amhukumu ndugu yake ambaye alikuwa anamfahamu?.

Kuelewa Hukumu itakuwaje siku ile, hebu tafakari mfano ufuatao.

Mwalimu alikuwa na darasa lake la wanafunzi 10 la wanafunzi wa Bweni, akawafundisha kwa mwaka mzima, kisha mwisho wa mwaka akawapa mtihani, wawili kati ya hao 10 walipata alama ‘A’ na nane kati yao wakapata alama ya mwisho kabisa ‘F’. Mwalimu akafurahi kuona amepata wanafunzi wawili waliofaulu vizuri, lakini akahuzunika kuona Zaidi ya robo tatu wamefeli na kupata alama ya mwisho kabisa ‘F’…tena miongoni mwa hao waliopata F kuna wengine wamepata sifuri kabisa. Akawapatia zawadi wale wawili, kwa kuwapandisha daraja la juu na wale 8 akawapa barua ya kuwafukuza shule.

Lakini wale waliofukuzwa wakaanza kumlalamikia kwanini tumefukuzwa…Mwalimu akawaambia ni kwasababu mmefeli mtihani, wakaanza kila mmoja kulalamika…oo ni kwasababu Umetoa kitu ambacho hujatufundisha, wengine wakasema oo ni kwasababu mazingira ya shule hayakuwa mazuri, wengine wakasema oo ni kwasababu chakula kilikuwa kibovu kila siku mlo ule ule tu! Ndio maana tukashindwa kula vizuri na kupelekea kufeli, wengine wakasema tunaomba utupe nafasi ya pili.

Mwalimu akawauliza swali moja wote! Je! Hao waliopata alama ‘A’ hawakuwa kwenye mazingira kama hayo hayo ya kwenu? Ndio mwalimu akaamua kumuita mmoja wa hao waliopata alama ‘A’ mbele yao na kuanza kumhoji na kumwuliza…

Je! Wewe ulikuwa unakula chakula kizuri sana tofuati na hawa ndio ikakusababishia kufaulu, yule akajibu hapana mwalimu, nilikula chakula kimoja na hao, isipokuwa mimi nilikuwa sio mnung’unikaji kama wao nilijua tu hapa shuleni napita hivyo nilivumilia tu shida za kitambo hizi na nikaweka jitihada yangu yote kwenye masomo…akaulizwa tena je! Ulikuwa unalala kwenye kitanda kizuri Zaidi ya wengine, akasema hapana!..akaulizwa na swali la mwisho je! Katika mtihani uliofanya ulikutana na swali ambalo mimi sikuwahi kuwafundisha darasani?…akasema hapana! Maswali yote uliyoyatoa uliyafundisha darasani ndio maana mimi nimeweza kuyajibu mengi ya hayo kifasaha..

Baada ya mwalimu kumwuliza hayo maswali, akawageukia wale wanafunzi 8 waliofeli akawaambia..mnasikia anachosema mwenzenu?..Huyo ndiye anayewahukumu sio mimi…mlilala wote pamoja, mlikula wote chakula kimoja, wote mlikuwa darasa moja…lakini tofauti yenu ni kwamba ninyi hamkuwa makini na shule, na pia hamkujua kilichowapeleka shuleni ndio maana mkafeli kwahiyo ni haki yenu kufukuzwa shule. Kwasababu mlipitia mazingira sawasawa na ya wenzenu waliofaulu lakini nyinyi hamkuzingatia, mlipaswa mvumilie na kujituma kama wenzenu hata kama chakula kilikuwa ni mlo mmoja kila siku. Wale wanafunzi walikosa cha kujitetea na wakaondoshwa shuleni.

Ndugu yangu ndivyo itakavyokuwa siku ile ya Hukumu, Bwana atawahukumu wenye dhambi wote kulingana na matendo yao mbele ya kile kiti cheupe! Atawaambia wamefeli mtihani wa haya Maisha, na hivyo watashushwa daraja la chini (ambalo ni ziwa la Moto), Majina yao hayataonekana katika Kitabu cha uzima hivyo wataondolewa mbele yake, Kwasababu kila mtu sasahivi anafanya mtihani wake na kuandika kitabu chake…Na wengi watakaosikia hiyo hukumu wataanza kulalamika kuwa wanaonewa, wengine watasema Ulimwengu ulikuwa umejaa vishawishi tungewezaje kushinda! Wakubwa kwa wadogo, matajiri kwa maskini, kila mtu ataanza kutoa malalamiko yake..Ndipo yule aliyeketi katika kile kiti cha hukumu, atawaita watakatifu walioshinda ulimwenguni na kuwahoji mbele yao. Na hao waliohukumiwa watakosa cha kujitetea mbele yao, Kwahiyo wataenda kwenye lile ziwa la moto kwa huzuni na majuto makubwa, wakijua kuwa ni kweli wamestahili.

Ndugu wakati leo hii unaona wapo watakatifu wanaojituma kweli katika Mungu, hao sio ishara nzuri kwako, siku ile ya Hukumu watakuhukumu…Utasema Bwana mbona ilikuwa ni ngumu sana mimi kuacha uasherati kwenye kizazi changu ambacho kila kona ya barabara nilipishana na wanawake wapo nusu uchi? Nikifungua tv, internet, radio nakutana na mambo yavishawishi vya uasherati? Bwana atamleta mmoja ambaye alikuwepo kwenye hicho hicho kizazi chako, ambaye naye pia alikuwa anapitia majaribu kama ya kwako na hata pengine Zaidi hata na hayo yako kama vile Yusufu na akashinda uasherati na wewe utakosa cha kujitetea siku hiyo..

Utasema mbona mimi nilikuwa mzuri sana ningewezaje kushinda vishawishi mahali ambapo kila kona watu walikuwa wananitaka?..simalizi hatua mbili kila mwanamume ananijaribu? Siku ile watasimamishwa waliokuwa wazuri kuliko wewe mfano wa Sara katika kizazi chako, na pamoja na kwamba walikuwa ni wazuri sana, lakini walishinda vishawishi, na kujihadhari na ulimwengu, utakosa cha kujitetea siku ile.

Utasema nitawezaje kutubu na kumgeukia Kristo ninaposikia injili, si kila mtu atanicheka na kuniona mwendawazimu, nitawezaje kuacha Imani yangu na dini yangu, na dhehebu langu nililolizoea? Na kutubu na kumgeukia Kristo kikamilifu?…Biblia inasema katika Mathayo 12: 41 “Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona”

Utasema tena Bwana mimi nilikuwa ni Tajiri sana, nilikuwa ni Mkuu wa Wilaya, ningewezaje kupata muda wa kukutafuta wewe?..Siku ile watasimamishwa waliokuwa matajiri kuliko wewe katika wakati wako na katika utajiri wao wote walimtafuta Mungu na kujiepusha na ulimwengu. Biblia inasema katika..

Mathayo 12: 42 “Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani”

..Malkia anasafiri maelfu ya Maili…kwenda kuitafuta Hekima ya Mungu, wewe Balozi wa nyumba kumi huna muda! Siku ile hutakuwa na la kujibu.

Kwahiyo uonapo! Mtu mwema anafanya wema katika mazingira yasiyostahili wema..usiishie kufurahia tu! Bali pia Ujiulize nawe pia unafanya wema kama yeye katika mazingira kama yake?..Kwasababu kama hufanyi hivyo siku ile hutakuwa na cha kujitetea, na wala hutapata mtetezi…Dada uonapo kuna mwanamke mzuri kuliko wewe anavaa kwa kujisitiri pamoja na uzuri wake wote..usifikiri utakuwa na cha kujitetea siku ile ya hukumu mbele za Mungu, utaelekea kwenye Ziwa la Moto, na utasema ni kweli umestahili.

Unapoona kuna watu wanamtafuta Mungu katika kizazi chako cha uovu..Usiishie kufurahia tu! Na kusema nakushukuru Mungu!…Tambua kuwa kitendo wafanyacho huko mbeleni kitakuja kugeuka kuwa mashitaka kwa wasiomtafuta Mungu katika kizazi hicho hicho kigumu.

Bwana akubariki sana. Ni matumaini yangu kuwa umepata kitu, kama hujampa Kristo Maisha yako, mlango wa Neema haujafungwa, lakini siku si nyingi utafungwa, watakatifu wataondolewa duniani na kunyakuliwa juu mbinguni, na dhiki kuu kuanza duniani. Je! Bado ni vuguvugu?..bado unaupenda ulimwengu na anasa zake! Shetani anakudanganya kuwa hakuna watu wanaomcha Mungu duniani leo?…usidanganyike Mungu ana watu wake kila mahali, shetani anachotaka ni wewe uendelee kufikiri hivyo ili siku ile ya hukumu, uhukumiwe vizuri na Maisha ya watakatifu waliopo leo duniani.

Baada ya kutubu kama ulikuwa hujatubu, ni Ubatizo, ubatizo sahihi ni ule wa kuzama mwili wote katika maji mengi na kwa jina la Bwana Yesu.


 

Mada Nyinginezo:

KUNA HUKUMU ZA AINA NGAPI?

KUNA UFUFUO WA AINA NGAPI?

UTAWALA WA MIAKA 1000.

KARAMU YA MWANA-KONDOO.

WAFALME WATOKAO MAWIO YA JUA.

NYOTA ZIPOTEAZO.


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
John Siuhi
John Siuhi
2 years ago

A wonderful preachings

George kalama
George kalama
3 years ago

Mimi najaribu kuweza kufanya lolote q