KAZI YA UZURURAJI WA SHETANI.

KAZI YA UZURURAJI WA SHETANI.

Biblia inatuambia tabia mojawapo ya shetani ni “kuzunguka zunguka”, na sikuzote tunajua mzungukaji huwa na tabia Fulani ya udadisi na hiyo inafanya mwisho wa siku kuwa na tabia ya kupenda kuteka pia, kwasababu mahali alipo anaona hapamtoshi na hivyo anaamua kutoka na kwenda kuchunguza chunguza maeneo mengine na huko huko akiona upenyo mdogo tu au fursa fulani huwa anaitumia ipasavyo kutimiza matakwa yake mwenyewe..Na ndio maana jina Mzungu, limetokana na Neno mzungukaji, watu waliotoka bara la ulaya zamani walikuwa wakizunguka zunguka nchi mbalimbali na mabara mbalimbali duniani ili kutafuta rasilimali kwa ajili ya nchi zao, Na walipofika maeneo kama Afrika, na kuona kuna kila kitu na vile vitu walivyokuwa wanavitafuta ndipo wakatua hapo, na kufanya yaliyo yao na hata kutumia fursa hiyo kuteka watu na kuwatawala…

Vivyo hivyo na shetani naye, ni mzungukaji kufanikiwa kwake kunategemea kuzunguka zunguka huku na huko duniani, anajua asipofanya hivyo kabisa hawezi kufanikiwa kuuimarisha ufalme wake, Tukisoma kwenye maandiko katika kitabu cha Ayubu tunaona wakati Fulani malaika wa Bwana walipokwenda kujihudhurisha mbele za Mungu, shetani naye alikwenda katikati yao, ndipo Mungu akamuuliza maneno haya..

Ayubu 1:7 “Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo”.

Unaona hapo, anasema duniani, ikiwa na maana kila kona ya dunia alikuwa anazunguka zunguka, inamaana hata katika kila taasisi, kila shirika, kila dini, na katika kila nchi, na ndio maana hatushangai kumwona shetani yupo hata katikati ya kanisa la Mungu. Na lengo lake kubwa sio kutalii, hapana bali ni kuchukua mateka, na kuharibu kile kinachoonesha dalili ya kuinuka na kufanikiwa kwa ajili ya Bwana..Ukitaka kujua ukali wa shetani na jinsi anavyomchukia mwanadamu kwa namna isiyokuwa ya kawaida angali tu kitu alichomfanyia Ayubu baada ya Mungu kuuondoa ule ulinzi wake kwake..

Utaona bila kupoteza muda alimletea radi, ikawapiga wale kondoo wake wote, akanusurika Yule mtu mmoja aliyemletea taarifa ambaye alimwambia nimeona moto wa Mungu umeshuka, ilikuwa ni radii ile, sio moto tu kama moto, Hata wewe vile vile anaweza kukutengenezea radi ikiwa tu upo nje ya ulinzi wa Mungu, yaani nje ya wokovu, hiyo ndio kazi inayomfanya azungukezunguke duniani.

Utaona tena Muda huo huo akaandaa majeshi ya maadui, yakawavamia wafugaji wake yakawaua wote, halafu yakaondoka na mifugo, vivyo hivyo hata wewe anaweza akakuundia tu kikundi cha vibaka wakati unakatiza usiku umetoka labda kwenye shughuli zako, wakakuvamia na kukuchoma visu wakaondoka na fedha zako na wewe ukafa saa hiyo hiyo ikiwa tu haupo ndani ya wokovu..

Wakati huo huo tena Shetani akamletea upepo wenye nguvu ukaipiga ile nyumba ikawaangukia watoto wake wote wakafa, hashindwi kukuletea kipunga hapo ulipo umekaa kwa amani, au mafuriko, na kukusababishia tu ajali ambayo chanzo chake hakieleweki, hata gesi tu kukulipukia nyumbani, hashindwi kukufanyia hivyo au shoti kutokea nyumbani au kung’atwa na nyoka tu njiani na habari yako ikawa imeishia hapo,..hashindwi kufanya hivyo vyote kwa mtu ambaye ulinzi wa Mungu haupo juu yake.

Utaona tena Shetani akimeletea Ayubu mpaka magonjwa ambayo hajawahi kuumwa, Leo hii usijione unayo afya na bado upo nje ya wokovu ukadhani wewe unayo kinga kubwa zaidi ya wengine waliopo mahospitalini ndio maana huugui ugui ovyo, shetani anao uwezo wa kukutupia hapo hata kansa usijue imetokea wapi, au ugonjwa wa ajabu ajabu usiojulikana, na ukafa ndani ya siku tatu tu…

Hayo ndio matunda ya shetani ya kuzunguka zunguka kwake ni ili tu kutafuta mtu wa kummeza basi.. Na kumbuka lengo lake sio kukuangamiza tu halafu basi hapana bali ni anataka ufe haraka katika hiyo hali hiyo hiyo ya dhambi uliyonayo sasa ili uende kuzimu moja kwa moja hilo ndio lengo lake…kwasababu anajua akizidi kuchelewa pengine neema ya Mungu inaweza kukupitia ukatubu siku moja.

Na ndio maana Biblia inazidi kutuhimiza maneno haya..

1Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.

9 Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani.’’

Unaona ni jinsi gani shetani anavyokuchukia wewe uliye kwenye dhambi, kama sio huruma za Mungu tu kumzuia shetani tayari angeshakuangamiza siku nyingi…

Hivyo kama unahitaji kumruhusu leo Bwana aingie maishani mwako, utakuwa umefanya uamuzi wa busara, hapo ulipo tubu kwa kumaanisha kabisa kuacha dhambi zako zote, na kwamba unamaanisha kutokurudia yale yote maovu uliyokuwa unayafanya huko nyuma, Kisha mwambie Bwana Yesu nisamehe na nakukaribisha uje katika maisha yangu….Na ukishamaliza kumweleza mambo hayo yote kwa kumaanisha kabisa, hatua inayofuata tafuta mahali ukabatizwe ili kukamilisha wokovu wako, kumbuka ubatizo ni muhimu, na ni maagizo ya msingi kwa yeyote aliyempokea Bwana, Usipuuzie, ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi ni wa kuzingatia na uwe ni kwa jina la BWANA YESU KRISTO sawasawa na maandiko haya (Matendo 2:38, 8:16, 10:48, 19:5).

Hivyo ukikamilisha hayo, Bwana mwenyewe atakupa Roho wake Mtakatifu, naye atakaa na wewe milele kukulinda dhidi ya Yule adui azururaye huko na huko, mpaka ile siku ya mwisho ya kwenda mbinguni itakapofika.

Bwana akubariki.


Mada Nyinginezo:

ANGUKO LA UFALME WA SHETANI:

ZIFAHAMU HUDUMA KUU (10) ZA SHETANI DUNIANI.

VIFUNGO VYA GIZA VYA MILELE.

UNALITUMIA KWA HALALI NENO LA KWELI?.

NJAA ILIYOPO SASA.

CHUKIZO LA UHARIBIFU


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
my name is mr dude!!
my name is mr dude!!
2 years ago

nimefurah sana sababu nimepata neno zur laMungu wetu najina lake litukuzweee milele mbarikiwe!! BY H,DUDE S