UNALITUMIA KWA HALALI NENO LA KWELI?.

UNALITUMIA KWA HALALI NENO LA KWELI?.

Unaweza ukawa ni mchungaji mzuri,au mwalimu mzuri wa Neno la Mungu, unaweza ukawa una mafunuo mengi na kufahamu mambo mengi, lakini je! Katika huduma yako au utumishi wako unalitumia kwa halali Neno la kweli?. Mtume Paulo alimwambia Timotheo Hata mtu akishindana katika machezo hapewi taji, asiposhindana kwa halali.(2Timotheo 2:5). Unaona? tuchukulie mfano wanariadha, ikiwa mtu atatumia dawa za kusisimua misuli ili awe na pumzi zaidi ya wengine pale atakapokimbia, ni kweli anaweza akawa mshindi lakini hatapewa taji pale atakapobainika kafanya hila katika huo mchezo, kwasababu hajashiriki kwa halali katika michezo, au ikiwa mtu ataanza kukikimbia kabla ya kipenga kupigwa, huyo naye atatolewa katika mashindano kwasababu hajashiriki kihalali katika michezo, vilevile ikiwa waliagizwa wazunguke uwanja mara 10, lakini akatokea mmojawapo kakaidi amri na kukatisha katikati ya uwanja..Tunajua ni kitu gani kitakachofuata, bila shaka atapigwa Penalti na atatolewa katika mashindano hata kama ilikuwa imebaki mzunguko mmoja amalizie na ushindi, hiyo yote ni kwasababu hajashiriki kihalali.…

Vivyo hivyo katika mienendo yetu tunapolipeleka Neno la Mungu tusipojifunza Kulitumia kihalali, tunaweza tukajikuta katika hasara na tabu yetu mwisho wa siku inakuwa ni bure. 

Na ndio maana mbeleni kidogo Paulo aliendelea kumsisitiza Timotheo maneno haya:

2Timotheo 2:15 “Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, UKITUMIA KWA HALALI NENO LA KWELI”

Unaona, anamsihi ajionyeshe kuwa amekubaliwa na Mungu, ajionyeshe kuwa amekomaa katika mashindano ya wokovu, sio mtu atakayeleta aibu mbeleni kwa kushindwa kumaliza ungwe yake vizuri, na ndio tafsiri ya hilo Neno “mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari,” …kutahayari maana yake ni ‘kuabisha’

DALILI IPI ZITAKUTAMBULISHA KUWA HAUTUMII KWA HALALI NENO LA KWELI?

Sababu kuu Paulo ambayo aliitoa pale ni “Mashindano ya Maneno”.

2 Timotheo 2:14 “Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao.

15 Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, UKITUMIA KWA HALALI NENO LA KWELI.

16 Jiepushe na maneno yasiyo na maana, ambayo si ya dini; kwa kuwa wataendelea zaidi katika maovu,

17 na neno lao litaenea kama donda-ndugu. Miongoni mwa hao wamo Himenayo na Fileto,

18 walioikosa ile kweli, wakisema ya kwamba kiyama imekwisha kuwapo, hata kuipindua imani ya watu kadha wa kadha”.

Unaona?, sio hapo tu, sehemu nyingi sana Mtume Paulo alikuwa anamwonya Timotheo ajiepusha na mashindano ya maneno, ambayo madhara yake ni kama donda-ndugu. Donda-ndugu ni kidonda sugu kisichopona, kinakwenda miezi na miezi, miaka na miaka, hata kitibiweje hakitibiki, njia pekee ya kukiondoa ni kukata kile kiungo au lile Eneo. Sasa hiyo imefananishwa na mashindano ya maneno kwa watu wa Mungu, kwa jinsi mtu anavyojizoesha katika hali hiyo ndivyo anavyojiharibu nafsi yake kidogo kidogo, mpaka mwisho wa siku anajikuta anagota katika itikadi Fulani ya kidini ambayo hawezi tena kubadilika hata kama ni ya uongo, anabakia kuwa ni mtu wa mijibizano tu na mashindano ya itikadi zake siku zote, na ndio watu kama hao mwisho wa siku wanazama katika mafundisho potofu ambapo kuwatoa huko haiwezekani tena….

Mungu hakai katika mashindano, ikiwa mtu kakusudiwa kuamini ataamini, kama haamini, hawezi kuamini, pengine sio wakati wake huo. Ndugu ikiwa umepewa neema ya kuwa mhubiri wa injili basi usitumie karama yako kuwa mtu wa mashindano, hayo hayawezi kumjenga mtu zaidi yanamuharibu tu Yule asikiaye, ‘tutumie kwa halali Neno la kweli’,..Tudumu katika mfundisho ya Neno la Mungu..

Leo utaona kuna mijadala baina ya wa-kristo na waislamu, tazama kwa makini uone kama kuna mtu yeyote anajegwa au anavutwa kwa Kristo kwa malumbano yale..kinyume chake unazaliwa ugomvi, matusi na mizaha, hata wale ambao walikuwa wanaonyesha dalili za kuja kwa Kristo, wakiona machafuko yale ndio wana-kwenda mbali zaidi, hiyo yote ni kwasababu hatulitumii kwa halali Neno la Kweli, na hivyo mbele za Mungu tunatapanya badala ya kukusanya. 

Na ndio maana Mtume Paulo bado alikuwa anaendelea kumsihi Timotheo, tusome:

2Timotheo 2:23 “Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi.

24 Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu;

25 akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli;

26 wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.”

Hivyo Sisi ndio Timotheo wa sasa tukubali maonyo haya ya mitume, tukapokee taji bora lililowekwa mbele yetu.

Bwana akubariki sana.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

TUZO UTAPEWA KULINGANA NA NAFASI YAKO

TUNAPOSEMA TUISHI KWA NENO, INAMAANISHA TUISHI MAISHA YA NAMNA GANI?

MANENO YA MUNGU YANAPINDULIWAJE?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments