KILEMBA CHA NEEMA, JE! UMEMVIKA MWANAO?

KILEMBA CHA NEEMA, JE! UMEMVIKA MWANAO?

kilemba cha neema, Je! Umemvika mwanao ?


Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe..Karibu tujikumbushe mambo muhimu katika maisha yetu..Na hayo si mengine zaidi ya maonyo ya Neno la Mungu…Leo kwa Neema za Bwana tutajikumbusha majukumu machache ya wazazi juu ya watoto wetu..

Biblia inasema katika…

Kutoka 20: 12 “Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako”.

Neno hili ni Neno la Mungu kwa watoto wote ambao wanao wazazi…Na hata kama hawana wazazi labda wamefariki au hawaishi nao kwa namna moja au nyingine…Basi nafasi hiyo ya Baba na Mama itachukuliwa na walezi wao…Hao wanasimama kama Baba zao na Mama zao kihalali kabisa mbele za Mungu..hata kama wapo katika vituo vya malezi vya mayatima…hao walezi wao wanachukua nafasi hiyo ya Baba na Mama…wana amri kutoka kwa Mungu kuheshimiwa kama wazazi halisi…Kwasababu kuna Baraka kubwa sana katika kuwaheshimu wazazi na kuwasikiliza..

Kadhalika haijalishi mzazi ni mwovu kiasi gani lakini ni lazima kumheshimu, na kumtii haijalishi yeye hajiheshimu kiasi gani ni wajibu wa kila mtoto kumheshimu mzazi wake..Kwasababu ndio amri ya kwanza yenye ahadi…

Waefeso 6:1 “Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki.

2 Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi,

3 Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia”

Kupata heri na kuishi siku nyingi ni vitu viwili tofauti…Unaweza kuishi siku nyingi lakini maisha yasiwe ya heri..Hivyo, vyote viwili vinapaswa viende pamoja…

Jukumu la mzazi kwa mtoto.

Sasa Kitu cha Muhimu cha kufahamu kwa mzazi ni kwamba…Hatima ya mtoto, mzazi anaweza kuchangia kwa asilimia kubwa kuitengeneza au kuiharibu…Mzazi anaweza kukazana kweli kumpenda mwanawe, kumlipia karo, kumtafutia shule bora..kumpatia lishe bora, kumlinda..kumhakikishia bima ya afya n.k Lakini kama hatamtengenezea mwanawe mazingira ya kumheshimu au kumtii.. huyo mtoto hawezi kupata heri yoyote huko anakokwenda, wala hawezi kuishi maisha marefu…haijalishi atapatiwa elimu nzuri kiasi gani sasa…au atakuwa na afya nzuri kiasi gani sasa au maarufu kiasi gani…Maisha yake yatakatika katikati na yatakuwa ya tabu.

Hivyo mzazi ukilijua hilo utahakikisha mwanao anakuheshimu na kukutii…

Hayo ndio mambo ya kwanza ya kuzingatia kabla hata ya kwenda kuangalia ufaulu wake wa darasani…usifurahie anapofaulu sana na huku adabu yake inazidi kwenda chini..furahia pale heshima yake na utii wake unapozidi kupanda kwasababu unajua..hata kama atapepesuka kiafya sasa..hatakufa!..ataishi muda mrefu kwasababu Neno la Mungu linasema hivyo..hata kama hana heri sasa, lakini atakuja kuwa na heri baadaye katika kipindi cha maisha yake yote..

Hivyo kazana kumfundisha awe na tabia ya kukusikiliza…chochote utakachomwambia akutii na afanye kwa kupenda na si kwa kulazimishwa lazimishwa..mfunze tabia nzuri na heshima na utiii kwako na kwa watu wengine, mvishe mavazi ya adabu na mfundishe kuwa mtii….Mjaribu mara kwa mara kuangalia utii wake umefikia wapi ukiona umepungua tafuta namna ya kuurudisha…..mtume dukani mrudishe hata mara mbili au tatu, mpime..ujue kiwango cha utii alichonacho na heshima.

Mpime mwanao;

Mpime anapokuwa na wageni na watu wengine anakuwa na tabia gani zisizofaa na zile zinazofaa mpongeze…ukiona kasoro tumia fimbo kidogo, maana biblia inasema ukimpiga hatakufa…Wengi hawatumii fimbo wakidhani wanamharibia ujasiri mtoto, fimbo isiyokuwa na mafunzo sahihi ndiyo inayomharibia ujasiri..lakini fimbo yenye ujumbe wa kujenga ndiyo inayomjenga zaidi mtoto…

Na Mungu alivyowaumba watoto hawana kinyongo ili kwamba waweze kutengenezeka..ukimwadhibu sasahivi baada ya nusu saa mnacheka na kufurahi, ule upumbavu utakuwa umendoka lakini upendo wake kwako bado upo…..ukimwacha sasa bila kumfunza atakapokuwa mtu mzima hali za kuwa na vinyongo na uchungu zitakapomjia itakuwa ni ngumu kumtengeneza….kila utakalomwambia atakuwa anakwambia unamnyanyasa,..mara unaingilia uhuru wake..mara hujali hisia zake, mara wewe ni mkoloni, mara unamwaibisha n.k

Mfundishe biblia;

Pia katika utoto aliopo, mfundishe biblia..mpe mistari kadhaa ya kuikariri na kuishika kwasababu watoto wengi bado hawajaweza kuipambanua mistari..wape tu waikariri itawasaidia ukubwani..kuliko kukariri nyimbo za kidunia..pia wafundishe nyimbo za kuabudu, na kumsifu Mungu na wafundishe sala za kuomba muda wote na habari za Yesu ambazo ndizo za muhimu kuliko zote..Na wapime je hivyo unavyowafundisha au wanavyofundishwa na wengine wanavizingatia.??

Ukimpima mtoto vizuri na kujua kuwa anakutii na kukuheshimu na anaheshima kubwa ambayo mpaka watu wa nje wanaishuhudia na kusema Yule mtoto anaheshima na adabu…Basi, kuna Baraka ambazo Mungu anaziachia ambazo ulimwengu hauwezi ukaziona..hapo ndipo nyota njema ya mtoto inapoanzia..

Biblia inasema hayo mafunzo hatayaacha hata atakapokuwa mzee…

Mithali 22: 6 “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”…

Wengi wanaogopa kuwafundisha wanao adabu na heshima kwasababu wanahisi wakishafikisha umri Fulani labda wa kuvunja ungo au kubalehe watakengeuka..Huo ni uongo wa shetani!!…Watoto wengi wanakengeuka ukubwani kwasababu wazazi wao ambao hapo kwanza walikuwa wanawalea vizuri leo wamekengeuka!..sasa kama mzazi kakengeuka mtoto atasalimikaje?..Mzazi alikuwa anakwenda kanisani na mwombaji sasa hafanyi hivyo tena..mtoto ataendeleaje kwenda kanisani?…Mtoto alikuwa amezoea nyumbani ni mahali pa ibada sasa nyumbani kunapigwa kila siku kwenye TV, nyimbo za kidunia, mtoto ataendeleaje kuwa mtakatifu?….Lakini kama mzazi akibaki vile vile Yule mtoto kamwe hawezi kukengeuka hata atakapokuwa mzee..biblia sio kitabu cha Uongo!… Haiwezi kusema mtoto hataiacha ile njia halafu aje kuiacha!..sasa Mungu atakuwa ni mwongo.

Sasa faida nyingine ya mwisho na kuu ambayo mtoto anaweza kuipata kutoka kwako mzazi kwa kumfanya akutii na hata akusikilize na kukuheshimu katika viwango vya juu ni KUVIKWA KILEMBA CHA NEEMA KICHWANI PAKE?.

Faida hiyo ya kuvikwa KILEMBA CHA NEEMA KICHWANI PAKE.Biblia inaisema katika..

Mithali 1: 8 “Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako,

9 Kwa maana hayo yatakuwa KILEMBA CHA NEEMA KICHWANI PAKO, Na mikufu shingoni mwako”.

Hii ni Baraka kubwa sana ambayo wazazi wengi hawaijui…Hapa duniani tunaishi kwa Neema,…Hivyo Neema ya Kristo inapokuwa nyingi juu yetu..ndipo tunapokuwa na nafasi zaidi ya kumkaribia Mungu, ndipo tunapokuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuwa watumishi wa Mungu…Na utumishi wa Mungu sio tu ule wa kuhubiri madhabahuni hapana! bali hata ule wa Danieli ni utumishi wa Mungu..Pale Mungu anapokuweka katika ngazi Fulani ya juu na huko anakutumia kuwatunza watu wake..Hivyo Neema kama hiyo ni njema kwa mtu yeyote…Mtu anayemtumikia Mungu,.. Mungu atamheshimu biblia inasema hivyo (katika Yohana 12:26).

Mfundishe kwa bidii kukutii;

Sasa ni nani asiyetaka kuheshimiwa na Mungu?..Je! unataka mwanao aheshimiwe na Mungu?…Kwa kuvikwa neema ya kuwa mtumishi wake?…Ni kwa kumfanya akutii na kukuheshimu..huku na wewe ukionyesha kielelezo cha kumcha Mungu maisha yako yote ili usimwangushe..

Kuwa na mtoto ni Baraka!..Hususani kama umemvisha kilemba hicho cha neema….Neno la Mungu linasema wapeni watu vitu nanyi mtapewa kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika ndivyo watu watakavyowapa kifuani mwenu…..Na wewe umempa mwanao hicho kipimo cha Neema ya Mungu juu ya kichwa chake kubwa namna hiyo…Bwana atamtumia huyo huyo kukulipa..kukurudishia kipimo cha kujaa na kushindiliwa nakusukwasukwa hata kumwagika katika siku za mbeleni..Na kwasababu mwanao au wanao watakuwa wanatembea na hiyo NEEMA kubwa sana kichwani mwao basi kila watakalomwomba Mungu, Mungu na kila watakalolifanya litafanikiwa katika maisha yao.

Bwana akubariki.

Kama wewe mzazi hujaokoka!..Tambua kuwa huwezi kuwavika wanao KILEMBA HICHO CHA NEEMA vichwani mwao..Wataharibikiwa na kuwa na maisha mabaya..kwasababu maisha yako wewe ni mabaya!..Hivyo ni vizuri leo hii ukamgeukia Kristo akuoshe dhambi zako kweli kweli kwa damu yake..Ili uwe mzazi/mlezi bora…Unachopaswa kufanya ni kutubu kuanzia leo na kumwambia Bwana akusamehe..akusamehe, uasherati wako kama ulikuwa unaufanya..akusamehe kwa kutowajali wanao,..akusamehe kwa kila uchafu uliokuwa unaufanya..na hivyo unamwahidi kwamba utafanya tena..

Baada ya kutubu kabatizwe katika ubatizo sahihi kwaajili ya ondoleo la dhambi (Matendo 2:38)..Kumbuka ubatizo sahihi ni ule wa kuzamishwa mwili wote kwenye maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo. Baada ya kufanya hivyo Roho Ambaye atakuwa ndani yako atakuongoza kufanya mengine yote yaliyosalia na kukupa uelewa wa ajabu wa kuyaelewa maandiko na kukusaidia kushinda dhambi ambazo kwa nguvu zako ulikuwa huwezi.

Kumbuka pia Yesu Kristo atarudi..Biblia inasema “Itatufaidia nini tuupate ulimwengu mzima na kisha tupate hasara za nafsi zetu’’..Hivyo uwe unalitafakari hilo kila siku.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Maran atha!..Shalom.

Mada Nyinginezo:

LENGO LA SHETANI KWA WATOTO WA KIZAZI HIKI.

MOTO HUFA KWA KUKOSA KUNI.HATA UASHERATI NAO

KIMBIA! KIMBIA! KIMBIA!

UNATAKA KUBARIKIWA? BASI USIKWEPE GHARAMA ZAKE.

BONDE LA KUKATA MANENO.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments