Ukiona Mungu kakuahidi mambo mazuri huko mbeleni, fahamu kuwa kuna uwezekano wa kupitia mabaya kabla ya hayo mazuri kuja…Na ukiona Mungu kakuahidia kuwa atakufunika na kukulinda na kukuokoa ujue kuwa unaweza ukapitia kwanza hali ngumu karibia na kupotea…Wengi tunazipenda faraja, hususani zinazotoka kwa Mungu lakini hatujui kuwa “huwezi kufarijiwa kama hujapitia kukatishwa tamaa au msiba fulani”..Hiyo ndio nguvu ya faraja iliyopo…Kadhalika Mungu anapotupa maneno ya faraja tufahamu kuwa kuna kukatishwa tamaa kutakuja kabla ya hiyo faraja.
Kwamfano Bwana anaweza kumwambia mtu “nitakuwa na wewe, na nitakubariki na kukuokoa na kukuweka juu”…na wakati anakwambia hayo pengine haupo kwenye shida sana, au tabu sana…Sentensi hiyo ni nzuri na ya faraja, lakini pia kwa upande wa pili ni ya Huzuni…Kwasababu kabla ya Mungu kuwa na wewe ni lazima utapitia hali Fulani ya kuona kama umeachwa, kabla ya kupata hiyo raha aliyokuahidia ni lazima upitie shida kwanza ili raha iwe na maana, kabla ya kukuinua juu sana ni lazima atakushusha kwanza chini sana, na kabla ya kukuokoa ni lazima ataruhusu upotee au uingie kwanza matatizoni..vinginevyo wokovu hautakuwa wokovu kama hakuna kilichopotea.
Kwasababu hakuna kuokolewa bila kupotea kwanza, wala kufarijiwa bila huzuni, wala kuinuliwa juu bila kushushwa chini kwanza. Ndivyo ilivyokuwa kwa Ibrahimu, Ili apewe Taifa lake mwenyewe ilimpasa anyanganywe Taila la Asili yake…ilimpasa aiache nchi yake, na aondoke aende mahali hata asipopajua…Biblia inasema hivyo katika..
Waebrania 11:8 “Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako. 9 Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile”
Waebrania 11:8 “Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako.
9 Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile”
Hizo ndio gharama za kuambiwa “Nitakufanya kuwa Taifa kubwa”… Unafikiri ni jambo jepesi kutoka nchi uliyozaliwa na kuacha ndugu zako wote, na mashamba yako na mali zako na kwenda nchi nyingine maelfu ya maili mbali na kwenu ambayo hata huijui?…Hivyo Baraka za Ibrahimu kufanywa Taifa kubwa hazikuwa ni nyepesi nyepesi kama zinavyodhaniwa…Alinyanganywa urai wa Taifa lake na Mungu ili apewe urai wa Taifa lake binafsi na Mungu.
Yusufu naye baada ya Mungu kumwonesha maono makubwa kama yale kwamba ndugu zake watakuja kumsujudia, alifurahi na kujua ni jambo la kesho na kesho kutwa, kwamba hatapitia lolote, mambo yatakuwa mteremko, mpaka atakapokuwa mtu mzima Mungu atakuwa kamnyanyua tu lakini badala yake miaka michache baadaye alifungwa kwenye Taifa lingine, katika gereza la kifalme kwa kosa la uzalilishaji wa kijinsia na jaribio la ubakaji..Ilimpasa achafuliwe kwanza kabla ya kusafishika..hauwezi kunyanyuliwa bila kushushwa kwanza.
Kadhalika Musa naye kabla hajawa mungu kwa Farao kama biblia inavyosema katika (Kutoka 7:1) ilimbidi aache ufalme wote, na enzi yote na mali zake zote aondoke aende jangwani kukaa huko miaka 40 akishushwa na kunyenyekezwa na Mungu, mpaka kufikia kiwango cha kuwa mtu mpole kuliko watu wote duniani waliokuwa kipindi kile..Na baada ya kushushwa hivyo ndipo ukaja wakati wa kunyanyuliwa kwake ambapo Mungu alimweka juu ya Taifa zima la Israeli. Biblia inasema Musa alipewa wana wa Israeli wote wawe wake.
Waebrania 11:24 “Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; 25 akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo; 26 akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo. 27 Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana”.
Waebrania 11:24 “Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao;
25 akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;
26 akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo.
27 Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana”.
Kwa mifano hiyo michache kati ya mingi, unaweza kuona kuwa ili unyanyuliwe huwezi kukwepa kushushwa chini..Kadhalika hata tunapomfuata Kristo, wengi wetu tumeweka shabaha na matumaini asilimia 100 katika Baraka za Mungu, kwasababu tu Mungu kaahidi kutubariki mashambani na mijini pindi tunapomfuata…..tunadhani pindi tu tunapomfuata Kristo basi mambo yetu hapo hapo tu yanaanza kukunyookea..Lakini tunapojikuta tunashuka chini katika hatua za awali ndio tunaanza kurudi nyuma na kulaani na kukufuru na kumwona Mungu ni mwongo.
Mambo hayaendi hivyo ndugu! Ulikuwa unafanya kazi za pombe haramu au kujiuza mwili wako na ulikuwa unapata pengine laki moja kwa siku kutokana na kazi hiyo, leo hii umeokoka na umeamua kuacha hiyo kazi, unategemea vipi uendelee kupata hiyo laki kwa siku kama ulivyokuwa unaipata?..Ni wazi kuwa huwezi kuipata hiyo tena kwasababu hiyo kazi umeacha,…hivyo kiuhalisia utapitia dhiki kwa kitambo Fulani kutokana na kwamba fedha uliyokuwa unaizalisha huipati tena, lakini pendo Kristo atakalokuwa amelimimina ndani yako litaifunika hiyo dhiki, hata kuona sio kitu….
Kitendo hicho cha kuacha hayo yote ndio KUJIKANA kwenyewe huko! na hivyo Mungu atakutengenezea chaneli nyingine ya kazi ambayo utaipata faida zaidi ya hizo kazi haramu ulizokuwa unazifanya, lakini hiyo inaweza isiwe leo au kesho, inaweza ikapita kipindi Fulani cha muda..kwasababu ni lazima Mungu akuweke chini ya madarasa yake ili Baraka za baadaye zisije zikakuharibu kama kwanza. Ndicho kilichomtokea Musa, ndicho kilichowatokea wana wa Israeli, ndicho kilichomtokea Yusufu na wengine wengi…
Bwana Yesu aliwaambia Mitume wake maneno yafuatayo..
Mathayo 19:27 “Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi? 28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli. 29 Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele”.
Mathayo 19:27 “Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?
28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.
29 Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele”.
Unataka kubarikiwa na Kristo leo unahitaji kupata mara mia? Kama ni ndio basi unahitaji kuingia gharama!..kwasababu Baraka hiyo haiji bila kuingia gharama..
Na gharama yenyewe ni kuacha vyote vilivyo viovu? unaacha ulevi wako, uasherati wako, upo kwenye mahusiano ambayo ni ya kizinzi unaachana na huyo uliye naye sasa, ulikuwa na bar! Unaifunga bila kujishauri shauri, umemtapeli mtu mali yake unamrudishia yote bila kujali umebakiwa na shilingi ngapi, ulikuwa unajiuza funga hiyo biashara na choma nguo zote za kikahaba, haijalishi zilikuwa zinakupa faida kiasi gani…tambua kuwa faida hiyo uliyokuwa unaipata sio kutoka kwa Mungu bali ni shetani ndiye aliyekuwa anakupa ili mwisho wa siku akupeleke kuzimu, kwahiyo mwachie shetani vilivyo vyake wewe tafuta vya Mungu, yeye anasema atakupa mara mia, na pamoja na hayo Uzima wa Milele?..Sasa ipi bora?…kupata pungufu pamoja na ziwa la moto au kupata mara mia pamoja na uzima wa milele?.
Na kumbuka unapoamua kuacha vyote leo na kumfuata Kristo, hatujapewa guarantee ya kupata mara mia kufumba na kufumbua, kwasababu lengo kuu na la kwanza la Mungu wetu ni kuziponya nafsi zetu zinazokwenda kuzimu sio kutufanya mabilionea!, hivyo katika hatua ya kututengeneza na kutupa mara mia..muda uliopo hapo katikati yeye ndio anayeujua mwenyewe….wengine miezi, wengine miaka, wengine miaka hata 30 au 40 ijayo, anajua yeye..kulingana na wito wa Mtu..Hivyo usiweke shabaha yako sana katika kupewa mara mia bali uweke katika kufanywa kiumbe kipya na kuyafanya mapenzi ya Mungu.
Mungu akubariki.
Maran atha!
Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali, au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba
+225693036618/ +225789001312
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
JE! NI KWELI UMEMFUATA YESU?
NINI KINATOKEA BAADA YA KIFO?
DANIELI: Mlango wa 1
HATARI YA KUHUBIRI INJILI TOFAUTI NA ILIYOANDIKWA KWENYE BIBLIA.
MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA RUTHU:
Rudi Nyumbani:
Print this post
Amen, Amen,Amen
Amen, ubarikiwe.