Siku moja nilimsikia mtumishi mmoja redioni akifundisha na kusema asilimia 60 ya mafundisho ya YESU yaliegemea katika fedha, na hivyo YESU alikuja hapa duniani ili sisi tujue kanuni za kufanikiwa kiuchumi..na ndio maana mimi hapa ninahubiri pesa.. alizungumza maneno hayo huku watu waliokuwa naye katika meza ya mazungumzo wakimsapoti kwa furaha kabisa..
Ni kweli, mifano mingi Bwana Yesu aliyokuwa anawafundisha makutano na wanafunzi wake, ni mifano aliyoitoa katika Maisha yetu ya kawaida tunayoishi kila siku, na mingine alitumia mifano ya fedha na wafanyabiasha pia, kwa mfano utaona ule mfano wa mfanyabiashara aliyekuwa anatafuta Lulu nzuri, baadaye alipoipata akaenda kuuza vyote alivyo navyo ili ainunue, mfano wa wale watu waliopewa talanta 10 wakaambiwa wafanyie biashara wazalishe, wengine wakazalisha wengine hawakuzalisha n.k.. Lakini ukiangalia mifano hiyo ilikuwa haimuelekezi mtu akawe bilionea au milionea, bali Bwana YESU aliitumia ile mifano ili kuwafundisha watu juu ya ufalme wa mbinguni..Kwamba kila mtu anapaswa akakizalie matunda kile anachopewa katika roho n.k.
Lakini Bwana YESU hakuja kwa lengo la sisi kuzijua kanuni za kuwa utajiri hapa duniani, hilo halikuwa lengo lake la msingi tangu mwanzo, kinyume chake wakati fulani maelfu kwa maelfu ya watu walipokusanyika ili kumsikiliza mpaka wakawa wanakanyagana, ukisoma Luka 12 pale utaona katikati ya mahubiri alitokea mtu mmoja ili kumwomba amsaidie kumwambia ndugu yake ampe sehemu ya urithi aliochiwa na baba yake.. Lakini saa hiyo hiyo Bwana alimjibu maneno haya.. “ Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu”?..
Unaona maneno hayo?, hakuishia hapo akaendelea na kusema..
“Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo”..
Kama wewe ni mtu wa kusoma maandiko kwa kuyatafakari vizuri, utaelewa hapo BWANA, alikuwa anamaanisha kuwa yeye amekuja ili kuwa mwamuzi wa uzima wa mtu, au mpatanishi wa dhambi za mtu, lakini yeye anataka kumfanya kuwa mwamuzi wa mali za ulimwengu huu..
Ndio sababu ya kuwambia maneno hayo “Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu”..Yeye kawekwa kuwa mwamuzi wa dhambi, sio mwamuzi wa mali.
Sasa ukiendelea kusoma utaona anawapa mfano huu..
Luka 12:16 “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; 17 akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. 18 Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. 19 Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. 20 Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? 21 Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu”.
Luka 12:16 “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana;
17 akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu.
18 Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu.
19 Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi.
20 Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?
21 Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu”.
Ndugu yangu, dunia ya sasa ya masumbufu imewafanya watu wengi wamkimbilie Mungu kwa lengo la kupata suluhisho la mali zao, na urithi wao, na biashara zao lakini hawataki kuambiwa habari za UZIMA wao, biblia inasema shina moja la mabaya ya kila namna ni kumpenda fedha (soma 1Timotheo 6:10), haimaanishi kuwa tusiwe na fedha au tusitafute fedha hapana, bali kuwa na tamaa ya fedha inatufanya tuangukie katika mambo mengi maovu, wengine wanawaua ndugu zao kikatili , kisa urithi tu, wengine wanakwenda kwa waganga, kisa urithi, wengine wanagombana mpaka kuwekeana visasi na vinyongo kisa mali tu, wengine wanatoa kafara za ndugu zao kisa mali, wengine wanawasaliti ndugu zao kisa mali na kuwatenga kisa fedha n.k..wengine wanaua watoto na watu wengine wasio na hatia kisa mali..
Hivyo kama wewe ni mkristo, pokea ushauri wa YESU anaotuambia jilindeni na choyo…usigombane na mtu kisa amekudhulumu, mtu akiichukua kanzu yako mwachie na joho pia, wala usimnyime mtu haki yake kwa tamaa ya mali..
Bwana akubariki sana.
Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba hizi
+225693036618/ + 225789001312
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
JE! UKRISTO UNAMPA MTU DHAMANA YA KUWA TAJIRI?
FIMBO YA HARUNI!
USIPIGE MATEKE MCHOKOO!
PEPETO LA MUNGU.
Rudi Nyumbani:
Print this post