UMEPATANISHWA NA MAADUI ZAKO?

UMEPATANISHWA NA MAADUI ZAKO?

Je unawajua Wasamaria walikuwa ni watu gani?…Wasamari ni watu wanaotokea mahali panapoitwa SAMARIA, ulikuwa ni mji uliokuwepo katikati ya Taifa la Israeli. Zamani za wafalme Israeli ilipogawanyika sehemu mbili, yaani kaskazini na kusini, Eneo la Samaria lilibaki sehemu ya Kaskazini mwa Israeli na Yerusalemu ilibaki sehemu ya Kusini… kukawa na mataifa mawili ndani ya Taifa moja, sehemu ya kaskazini ikabakia na jina lile lile Israeli, ambayo mji wake mkuu ulikuwa ndio huo Samaria na sehemu ya kusini ikaitwa Yuda ambayo mji wake mkuu ndio uliokuwa Yerusalemu…

Lakini Israeli ilipokuja kuchukuliwa tena utumwani, wale waliokuwa kaskazini walipelekwa Ashuru wakabaki watu wachache sana ambao waliwekwa ili kuyatunza mashamba, na wale waliokuwa upande wa kusini walipelekwa Babeli, lakini baada ya miaka 70 Mungu aliwarudisha tena baadhi yao katika nchi yao ya ahadi, lakini wale waliopelekwa Ashuru hawakurudi tena, walidumu huko huko kwenye mataifa mengine, lakini Yule mfalme wa Ashuru alitoa watu baadhi kutoka katika taifa lake, na kuwaleta Israeli ili wakae Samaria, Hivyo kwa jinsi siku zilivyokuwa zinazidi kwenda hawa Wasamaria wakawa ni watu waliochanganyika, nusu wapagani nusu wanaishika sheria ya MUSA.

Sasa Wasamaria wao hawakuamini katika kuabudu katika lile Hekalu la Mfalme Sulemani kama wale wayahudi waliokuwepo Yerusalemu wakati huo….Hivyo ikasababisha kuwepo na matengano na kutokuelewana kwa muda mrefu…Waliokuwa wanaishi Yerusalemu yaani Yuda, waliwaona wasamari ni kama watu wa mataifa na hawajui sana dini. Na walikuwa hawachangamani, wakati mwingine hata kuzungumza walikuwa hawazungumzi. Waliendelea kuwa hivyo hadi wakati wa kutokea kwa Bwana wetu Yesu Kristo.

Bwana Yesu alikuwa yeye ni kutoka Uzao wa Daudi…Hivyo alikuwa ni myahudi ambaye ni wa upande wa Yerusalemu, yaani Yuda, na si msamaria. Siku moja alikuwa anapita kwenda Yerusalemu kutoka Galilaya na katika njia yake ilikuwa ni lazima akatize Samaria ili afike, kulikuwa hakuna njia nyingine, lakini alipofika Samaria wenyeji wakagundua kuwa anakwenda Yerusalemu kwa watu ambao hawaelewani kiimani..hivyo kwa jambo hilo tu, wakakataa asikae kwao wakamfukuza! Kwasababu walikuwa hawapatani.

Luka 9:52 “akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali.

53 Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu.

54 Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?

55 Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.]

56 Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine”.

Je! Ingekuwa ni wewe ungejisikiaje labda unakwenda mahali fulani unazuiliwa kwasababu tu ya Imani yako?..labda unakwenda nchi fulani tuseme ya kiislamu, na kitendo cha kufika tu pale wenyeji wanagundua kuwa wewe ni mfuasi wa Imani ya kikristo, na wakakuzuilia hata kulala kwenye hoteli zao na kukwambia uondoke?..ungejisikiaje? bila shaka ungehuzunika sana, na kama si mkristo uliyesimama vizuri ungeweza hata kulaani..Ndicho kilichotokea kwa hawa wanafunzi waliwalaani Wasamaria, wakaona ni heri hata waangamizwe, hawana maana, wala roho nzuri…

Lakini Bwana Yesu alikuwa na moyo mwingine…akawaambia hamjui ni roho ya namna gani mliyonayo, Mwana wa Adamu hakuja kuangamiza roho bali kuokoa! Haleluya!..Tafsiri yake ni kwamba “yeye bado anawapenda hata kama wao wanamchukia”

Na kama ni msomaji wa Biblia ulishawahi kukutana na hili Neno..

“Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye (Mithali 16:7)”.

Sasa Bwana Yesu bila shaka njia zake zilimpendeza sana Mungu, na kama ni hivyo basi ni lazima maadui zake wangekuja kupatanishwa naye tu!..Na maadui wake wa kwanza ni hawa Wasamaria, hebu tuone ni wapi walikuja kupatanishwa naye…

Baada ya Wasamaria kumkataa Bwana hata kukataa alale nchini mwao, tunaona kipindi kifupi tu baadaye baada ya wao kumkataa labda miezi miachache tu mbeleni au wiki chache tu mbele, alikuwa anarudi tena Galilaya, na ikambidi apite tena pale pale Samaria walipomkataa kwanza…na kuna tukio la Ajabu sana liliotokea pale ambalo liliubadilisha mji wote wa Samaria kumpenda Bwana.

Tunasoma katika:

Yohana 4:3 “ aliacha Uyahudi, akaenda zake tena mpaka Galilaya.

4 Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria.

5 Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe.

6 Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita.

7 Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe.

8 Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula.

9 Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.)

10 Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai.

11 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai?

12 Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake?

13 Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena;

14 walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.

15 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka.

16 Yesu akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa.

17 Yule mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume; 18 kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli.

19 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii!

20 Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.

21 Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu.

22 Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.

23 Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.

24 Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.

25 Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote.

26 Yesu akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye……………..

28 Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu,

29 Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?

30 Basi wakatoka mjini, wakamwendea………………39 Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda.

40 Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; naye akakaa huko siku mbili.

41 Watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake.

42 Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu”

Watu waliomkataa akae kwao sasa wanamwomba kwa kumsihi sana akae kwao angalau siku mbili…Hili Neno likatimia: Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye (Mithali 16: 7)” Mji mzima Samaria ulimgeukia Bwana…Na utaona hata baadaye walitaka kuja kumfanya kuwa mfalme wao, lakini Bwana akakataa.

Hakuna mahali ambapo Bwana Yesu alipokelewa vizuri kama kwa wasamaria ambao hapo kabla walimkataa.

Bwana wetu Yesu Kristo ni mfano kamili wa sisi kujifunza?..Alikuwa na maadui lakini waligeuzwa wote kuwa Rafiki zake, Hata wale waliomsulubisha msalabani aliwaombea msamaha na kwa kupitia damu yake kwa yeye ulimwengu umepatanishwa na yeye…Ndio maana mpaka leo Rafiki wa kweli amebakia kuwa Yesu tu!

Lakini maandiko yanatuambia katika:

Wafilipi 2:5 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu”

Je! Waislamu ni maadui zako?”

Jifunze kwa Bwana Yesu hapo juu, je! Majirani zako ni maadui zako kiasi cha kutaka hata moto ushuke uwateketeze? Kama ndivyo basi Bwana Yesu anakuambia “hamjui ni roho ya namna gani mliyonayo!..Jifunze kwa Bwana Yesu hapo juu Paulo anasema Iweni na nia iyo hiyo …Je! Wafanyakazi wenzako ni maadui zako kiasi kwamba hawataki hata kukuona upo karibu nao?..Jifunze kwa Bwana Yesu hapo juu…Na likumbuke hili neno : Njia za mtu zikimpendeza Bwana hata adui zake hupatanishwa naye!…Tafuta kupatanishwa na maadui zako na si kugombanishwa nao. Kwasababu hiyo ndio Nia ya Kristo kwetu.

Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu

Kwa Maombezi/Ushauri/Maswali/Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba hizi

+225693036618/+225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..

UCHUNGU WA KUIBIWA.

ROHO MBAYA KUTOKA KWA BWANA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments