UCHUNGU WA KUIBIWA.

UCHUNGU WA KUIBIWA.

Ufunuo 16:15 “ (Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.)”

Umewahi kujiuliza kwanini Bwana Yesu sehemu nyingi ujio wake anaufananisha na mwizi. Kwanini Bwana anajifananisha na wezi na sio watu watakatifu.. Tunafahamu wizi sio kitu kizuri, na moja ya Amri za Mungu ni “USIIBE”. Lakini hapa tunaona Bwana anajifananisha na mwizi. Kwanini anafanya hivyo?.

Ni wazi kuwa kuna hekima tunaweza kuiona hata katika waovu..Ndio maana Bwana alisema mahali pengine tuwe na “Busara kama nyoka”..Nyoka sio kiumbe chenye ishara nzuri, kuanzia Edeni mpaka sasa, shetani alikitumia kupenyeza dhambi ulimwenguni.. Lakini Bwana alituambia tuwe na Busara kama nyoka…Na zaidi ya yote yeye mwenyewe Bwana anajifananisha na Yule nyoka wa shaba Musa aliomnyanyua kule jangwani.

Yohana 3: 14 “Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa;

15 ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye”.

Na sehemu nyingine tena Bwana anajifananisha na yule Kadhi dhalimu:

Luka 18: 1 “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.

2 Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu.

3 Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu.

4 Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu,

5 lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.

6 Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu.

7 Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?

8 Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?”

Tena Sehemu nyingine Bwana anatufundisha kupitia mfano wa WAKILI DHALIMU aliyekuwa mwizi wa mali za Bwana wake na mwisho akatenda kwa Busara, Bwana akasema nasi pia tujifanyie rafiki kwa mali ya udhalimu ili itakapokosekana watukaribishe kwenye makao ya milele.

Luka 16: 1 “Tena, aliwaambia wanafunzi wake, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyekuwa na wakili wake; huyu alishitakiwa kwake kuwa anatapanya mali zake.

2 Akamwita, akamwambia, Ni habari gani hii ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena.

3 Yule wakili akasema moyoni mwake, Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya.

4 Najua nitakalotenda, ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao.

5 Akawaita wadeni wa bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, Wawiwani na bwana wangu?

6 Akasema, Vipimo mia vya mafuta. Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini.

7 Kisha akamwambia mwingine, Na wewe wawiwani? Akasema, Makanda mia ya ngano. Akamwambia, Twaa hati yako, andika themanini.

8 Yule bwana akamsifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru.

9 Nami nawaambia, Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele”.

Sehemu zote hizo Bwana hatumii watu wazuri au watakatifu kutufundisha Bali anatumia watu waovu, sio kwamba anataka tujifunze uovu wao, au tuige tabia zao hapana bali anataka tujifunze hekima yao. Kwasababu wana wa ulimwengu huu (wasiomjua Mungu biblia inasema wana hekima katika mambo yao).

Sasa tukirudi kwenye ule mfano wa Mwivi Bwana alioutuoa na kusema “Tazama naja kama mwivi”…Tunajua mwivi sio mtu mzuri, anakuja kwa lengo la kuiba…Lakini busara ya mwivi siku zote hapendi kusumbuliwa wala hapendi kumsumbua Yule anayemwibia..atafanya mambo yake kimya na taratibu na akishaiba anakwenda zake..Kwasababu hiyo basi anasubiria watu wakati wamelala na wamechoka usiku wa manane ndio anakuja na kuingia ndani na kuiba kisha kuondoka…Anakuja wakati ambao mali anayoitafuta na mwenye mali wamejitenga vizuri kabisa, anakuja wakati ambao nafasi ya matengano ni kati ya mali na mwenye mali ni kubwa sana..Hiyo ni hekima ya hali ya juu.

Na ndio Bwana Yesu naye ataitumia hekima hiyo hiyo wakati wa kuja kulichukua kanisa lake..atakachofanya kwanza ni kuja wakati ambao magugu na ngano vimeshajitenga..wakati ambao ulimwengu umelala usingizi na kumsahau Mungu, wakati ambao watakatifu wametengwa na ulimwengu wote, wakati ambao watakatifu wanaonekana ni watu wasiokuwa na maana, ulimwengu umewachoka, ulimwengu umeacha kuthamini mambo ya muhimu yahusuyo roho zao, Huo ndio wakati Bwana Yesu anakuja kuwaiba watu wake kutoka ulimwenguni.

Kama vile mwizi anapokuja, huwa anakuja wakati ambao watu hawaangalii tena tv zao ndani wamezichoka, wakati ambao watu hawatumii tena magari yao ya thamani wameyaacha yapumzike..wakati ambao simu zao za mikononi wamechoka kuzitumia n.k Huo ndio wakati mwizi anakuja kuzichukua.

Mteule wa Mungu hizi nyakati ni za hatari, nyakati ambazo ulimwengu haumtaki tena Kristo..Wakati ambao Watakatifu wanaonekana hawana thamani tena ulimwenguni, wakati ambao watakatifu wamechokwa na watu wa ulimwengu huu, ujue ni wakati wa matenganisho..vitu vya thamani vimechokwa kutumiwa, huo ndio wakati mwivi anakuja..wakati ambao usingizi wa anasa, na uasherati na ulevi umewavaa wengi huo ndio wakati Kristo anapoivamia nyumba.

 Na siku ya kuwanyakuwa watu wake hakuna mtu atakayejua siku hiyo..baada ya kipindi Fulani kupita ndipo hapo watakapojua kuwa kuna baadhi ya watu hawapo? Watu wetu wa muhimu na wa thamani waliokuwa wanatuhubiria habari njema za maisha ya umilele na utakatifu wametoweka.

Na kama vile mtu anavyopata uchungu wa kuibiwa mali yake ya thamani..ndivyo watu wengi siku hiyo watakavyopata uchungu wa kuachwa ulimwenguni na wapendwa wao wa thamani..watazidi kupata uchungu mwingi watakapoanza kupitia dhiki ya mpinga kristo na siku ya BWANA inayotisha. Watalia na kujuta na kuomboleza.. Kumbuka kitakachowaumiza sana sio mapigo yale bali ni “kwanini hawakukesha”..hicho ndicho kitakachowaumiza sana.. Ni kwanini wenzao wameondoka na wao wamebaki?? Na kwamba wenzao wapo utukufuni mbinguni milele na wao wataenda kwenye lile ziwa la moto, watasikia wivu uliochanganyikana na hasira mbaya sana.. Uchungu huo unafananishwa na uchungu wa mtu KUIBIWA MALI YAKE USIKU, na siku hiyo watu wote walioachwa watamchukia Bwana Yesu kuliko hapo kwanza. Watamchukia kwa ukomo wa chuki, Kama vile watu wanavyowachukia wezi baada ya kuibiwa. Watamkufuru na kumtukana, na dhiki watakazopitia zitaongeza hasira yao.

Ufunuo 16: 8 “Na huyo wa nne akakimimina kitasa chake juu ya jua, nalo likapewa kuwaunguza wanadamu kwa moto.

9 Wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa, NAO WAKALITUKANA JINA LA MUNGU ALIYE NA MAMLAKA JUU YA MAPIGO HAYO; WALA HAWAKUTUBU WALA KUMPA UTUKUFU.

10 Na huyo wa tano akakimimina kitasa chake juu ya kiti cha enzi cha yule mnyama; ufalme wake ukatiwa giza; wakatafuna ndimi zao kwa sababu ya maumivu,

11 WAKAMTUKANA MUNGU WA MBINGU KWA SABABU YA MAUMIVU YAO, NA KWA SABABU YA MAJIPU YAO; WALA HAWAKUYATUBIA MATENDO YAO”.

Watu wengi wanasema kutakuwa na nafasi ya kutubu wakati huo?? Ndugu yangu, ndugu yangu nataka nikuambie huo ni uongo wa shetani, siku hiyo hakutakuwa na nafasi ya kutubu. Utakuwa ni wakati wa maombolezo na vilio na hasira na uchungu..Wanadamu wote walioachwa watataka kufanya vita na mwanakondoo, watamchukia Yesu Kristo..

Kama ulishawahi kuibiwa unaweza ukaulewa uchungu wa kuibiwa..ni mbaya sana, wengi wasiomjua Mungu wanaishia kuwachukia wezi maisha yao yote… Ndio maana Bwana naye anatuonya kwasababu anauona UCHUNGU utakaokuja huko mbeleni kwa wanadamu wote watakaoachwa..anatuonya na kutuambia “KESHENI” naja upesi.

Luka 21:34 “ Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo;

35 kwa kuwa ndivyo ITAKAVYOWAJILIA WATU WOTE WAKAAO JUU YA USO WA DUNIA NZIMA.

36 BASI, KESHENI NINYI KILA WAKATI, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu.” 

Mathayo 24: 42 “Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu.

43 Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.

44 Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja”.

Kukesha hapo sio kukesha kwa mwili kutojizuia kulala, hapana bali ni kukesha katika roho,kwa kuishi maisha ya uangalifu, na utakatifu, kuishi kwa kuzisoma nyakati na kuyaelewa majira tunayoishi, kuishi kwa kuweka kando uasherati, ulevi, anasa, mavazi yasiyompendeza Mungu, matusi, rushwa, na mambo yote mabaya na kudumu katika kujifunza Neno la Mungu kila wakati. Hiyo ndio maana ya kukesha. Siku zinakuja hizi ni za hatari sana, tuwe macho wapendwa.

Maneno ya Mungu yaliyofunga kitabu cha biblia ni maneno ya Bwana Yesu na maneno hayo aliyoyasema ni haya..

Ufunuo 22:20 “Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana Yesu.

21 Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi nyote. Amina.”

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine, BWANA akubariki sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

KAMA MWIZI USIKU WA MANANE:

LUKA 12:20 INASEMA “USIKU HUU WA LEO WANATAKA ROHO YAKO!” NI WAKINA NANI HAWA WANAOITAKA ROHO YAKE?

NINI MAANA YA KUISHI KWA KUUKOMBOA WAKATI?.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments