Ili kufahamu vizuri ni kwanini hayo yote yalimpata Sauli, turudi nyuma kidogo tuitazame historia ya Mfalme Sauli jinsi ilivyokuwa. Kama tunavyosoma katika maandiko tunaambiwa kuwa Sauli alikuwa ni kijana mzuri sana, mrefu, mwenye haya ya uso, mlaini, hakuwa hata mtu aliyezaliwa katika mbari za kikuhani au za waamuzi walioamua Israeli wakati ule, hakuwahi hata kupigana vita yeyote, wala hakuwa na dalili ya kuonyesha kama ni mtu aliyeweza kusimama vitani, na ndio maana tunakuja kuona pindi tu siku ile alipokuja kutiwa mafuta na Nabii Samweli na kutangazwa kwa Israeli wote kama mfalme wao, baadhi ya watu walimkebehi kwa kumtazama tu mwonekano wake wa nje na uzoefu wake hafifu, alionekana kama ni mtoto tu, mtu mwenye tabia kama za kitoto, pengine walipomwona sura yake laini na uzuri aliokua nao au mazungumzo yake yasiyo na uzoefu wowote wa uongozi, watu wakamdharau na kumwona kama si kitu hawezi kuongoza taifa kubwa la kishujaa kama Israeli. Na ni kweli ndivyo alivyokuwa, alikuwa hana uwezo wowote ule Sauli.