Yapo mengi ya muhimu mtu anapaswa kufahamu pindi tu anapozaliwa mara ya pili, vinginevyo shetani atatumia nafasi hiyo kumtesa na kumwangaisha mtu huyo kwa lengo tu la kumfanya auache wokovu mara: na moja ya mambo hayo, ni kumfanya mtu KULIHISI LILE DENI LA DHAMBI BADO LIPO NDANI YA MOYO WAKE.
Sasa mtu anapozaliwa mara ya pili [kumbuka, tunaposema kuzaliwa mara ya pili Neno linamaanisha mtu aliyekusudia kutubu kutoka moyoni mwake na kudhamiria kabisa kuacha dhambi zake, kisha akabatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa Jina la YESU KRISTO, kisha akapokea Roho Mtakatifu]. Mtu wa dizaini hiyo anakuwa kuanzia huo wakati amefanyika kiumbe kipya, na deni lote la dhambi liliokuwa juu yake, Mungu anakuwa ameshaliondoa, na anafanyika kuwa mtoto halali wa Mungu.
Lakini tatizo linakuja tu ni pale mara baada ya kuzaliwa mara ya pili vita vya kifikra vinaanza kuibuka ndani, shetani akishajua wewe umeshahesabiwa haki mbele za Mungu, na ile hatia ya dhambi zako haipo tena, kitu atakachofanya baada ya yeye kujua uchanga wako ataanza kuangalia sehemu zilizokuwa dhaifu katika maisha yako ulizokuwa unamwasia Mungu na kwa kupitia hizo atazigeuza kama mwiba wa kukushambulia wewe ujione kama haufai mbele za Mungu.
Jambo la muhimu la kufahamu kwa kila mtu, ni kwamba unapozaliwa mara ya pili hauwi kama robot, ambaye anaweza akaondolewa taarifa zake zote za kumbukumbuku na kuwekewa nyingine mpya (kuwa- formated), na kusahau vyote vya nyuma, pasipo kukumbuka hata kimoja. Hapana haiwi hivyo kwa mkristo pale anapozaliwa mara ya pili.
Mtu anapozaliwa mara ya pili kitu anachokifanya Roho Mtakatifu baada ya kumsamehe dhambi zake ni kuondoa ile kiu ya kutenda dhambi ndani ya mtu [anampa kila sababu ya kuona madhara ya dhambi], ndio hapo unakuta kama mtu alikuwa anakunywa pombe anaacha, alikuwa mvutaji sigara anaacha, alikuwa mwasherati hataki kufanya tena vile, alikuwa mwizi hofu ya Mungu inamwingia haibi tena, alikuwa mtukanaji ile kiu ya kutukana inakufa…
Lakini tatizo linalojitokeza ni pale anafanikiwa kweli kufanya hivyo lakini bado anaona kuna vitu havijaisha vizuri ndani yake..Kwamfano wapo watu wengi wanasema nimeacha uasherati lakini ndoto za uasherati zinanisumbua, mwingine anasema nimeacha uzinzi lakini na mawazo machafu yananisumbua, nashindwa kutawala mawazo yangu, kila ninapojaribu ninajikuta nimezama huko tena jambo ambalo linanikosesha raha, mwingine anasema nimeacha usengenyaji lakini kuna muda ninajikuta nimesengenya jambo ambalo baada ya hapo ninajisikia vibaya sana.
Mwingine anasema nimeacha kusikiliza miziki ya kidunia lakini zile nyimbo bado zinajirudia rudia kichwani mwangu, zinajiimba na sipendi zijirudie kwasababu nafahamu MUNGU hapendezwi nazo,,nifanyeje?. Mwingine atakwambia niliwahi kutoa mimba, nikatubu lakini ndani bado kuna kitu kinaniambia sijasamehewa jambo ambalo linanifanya nijihisi kama Mungu ananichukia,
mwingine anasikia wazo linamwambia amemkufuru Roho Mtakatifu hivyo dhambi yako hata atubuje hatasemehewa kwasababu alifanya dhambi Fulani zamani kwa makusudi.
Mwingine atakwambia baada ya kumpa Bwana maisha yangu na kuacha ushirikina, bado wachawi wananijia usiku, n.k.
Kumbuka hawa wote ndani ya mioyo yao wanatumaini na wana dhamira safi ya kuwa wasafi na watakatifu lakini wanashindwa. Kwa Nje wanajitahidi kweli kuishinda dhambi lakini ndani ni vita vikali kweli vya kimawazo, n.k.
Sasa hawa wote kazi anayoifanya shetani ni kuzidi kuwakandamiza na kuwakandamiza kwasababu ya uchanga wao. Kwasababu hawajui kuwa tangu siku ile ya kwanza walipoamua kutubu na kufuata hatua zote za wokovu, Mungu alishawasamehe dhambi zao pasipo matendo yoyote. Mungu hakuangalia uelekevu wao, au utakatifu wao ndipo awasamehe, hapana aliwasamehe bure tu kwa neema yake. Hivyo walipofanyika kuwa wana wa Mungu tu, walihesabiwa kama watakatifu wa Mungu..
Lakini sasa jambo linaloendelea katikati yao ni kama vile gari lilokuwa katika mwendo kasi lililopigwa breki ghafla, haliwezi likasimama hapo hapo, hapana bali litaendelea na mwendo kidogo, japo kuwa matairi yatakuwa hayazunguki, vivyo hivyo hali yake mtu anayezaliwa mara ya pili,.Anakuwa ametoka kwenye dhambi fresh, ametoka kwenye dunia fresh, anatoka kwenye uasherati, anatoka kwenye matusi n.k.
Sasa Roho Mtakatifu anapopiga breki ghafla kwenye maisha yake ya dhambi, na kukata kiu yote ya dhambi ndani yake, kweli matairi yatasimama, ndio hapo yule mtu utakuta hataki kuendelea mbele na maisha ya dhambi tena, lakini kwasababu alikuwa kwenye mwendo kuna nguvu ya zamani iliyokuwa ndani yake iliyokuwa ikimsukuma kufanya zile dhambi haiwezi kusimama saa hiyo hiyo, itachukua muda kidogo ndio iondoke kabisa.. Na ndio maana Biblia inasema “kile apandacho mtu ndicho atakachovuna”, hapo ndipo utakapojua kuwa dhambi ina madhara makubwa, ina maumivu makali, inalipiza kisasi, na kuindoa itampasa mtu aingie gharama yake binafsi mbali na ile breki ya Roho Mtakatifu..
Ushahidi utakaokuonyesha kuwa wewe ni mtoto wa Mungu ni kwamba utaona unayachukia yale mambo ya kale lakini baadhi bado utayaona unayatenda pasipo wewe mwenyewe kupenda. Tofauti na hapo mwanzo ulipokuwa kwenye dunia, uliyatenda wala hakukuwa na kitu ndani kikikuhukumu, Na ndio maana Mtume Paulo aliandika..
Warumi 7: 14 “Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi. 15 MAANA SIJUI NIFANYALO, KWA SABABU LILE NILIPENDALO, SILITENDI, BALI LILE NILICHUKIALO NDILO NINALOLITENDA. 16 Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema. 17 Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu 18 Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati. 19 Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo. 20 Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, SI MIMI NAFSI YANGU NILITENDAYE, BALI NI ILE DHAMBI IKAAYO NDANI YANGU.”
Warumi 7: 14 “Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi.
15 MAANA SIJUI NIFANYALO, KWA SABABU LILE NILIPENDALO, SILITENDI, BALI LILE NILICHUKIALO NDILO NINALOLITENDA.
16 Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema.
17 Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu
18 Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati.
19 Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo.
20 Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, SI MIMI NAFSI YANGU NILITENDAYE, BALI NI ILE DHAMBI IKAAYO NDANI YANGU.”
Unaona hapo? Ukiona hayo mambo yanakujia ujue kuna gharama ya kuziondoa hizo, hiyo ni kazi yako binafsi, na njia pekee ya kuviondoa ni kujitenga na kukaa mbali na vichocheo vya hizo dhambi, kwamfano, hapo mwanzo maisha yako yalikuwa ni ya uzinzi, ya kutazama pornography, na kufanya uasherati, na mustarbation zile picha na mawazo na kumbukumbu za yale matukio haziwezi kuisha mara, zitachukua muda kukutoka, unachotakiwa kufanya ni siku baada ya siku kuzidi kukaa mbali na mazingira yote yanayokupelekea wewe kuingia katika hayo mambo,
Kaa mbali na makundi yenye mazungumzo yasiyokuwa na maana muda wote yanazungumzia habari za uasherati, biblia inasema..
Waefeso 5: 3” Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; 4 wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. ”
Waefeso 5: 3” Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;
4 wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. ”
Kadhalika biblia inasema pia..1Wakorintho 15: 33”Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema”.
Sasa ukiendelea kudumu katika hali ya kuwa mbali navyo, kidogo kidogo vinaanza kuzikwa ndani yako na hatimaye kupotea kabisa, ile hali ya mawazo mabaya kukutumikisha inapotea, unakuwa na uwezo wa kutawala mawazo yako, zile ndoto ulizokuwa unaota kila siku unafanya uasherati hatimaye zinapotea kabisa.
Ulikuwa unasikiliza miziki ya kidunia, unachopaswa kufanya ili hayo mambo yazikwe kwenye akili yako, ni kufuta miziki yote kwenye simu yako au kompyuta yako, na wakati zile nyimbo zinapotaka kuanza kuja kichwani, weka nyimbo za injili za kumtukuza Mungu badala yake..jizoeshe kuzisikiliza hizo mpaka zenyewe zitakapochukua nafasi ya zile nyimbo za kidunia.
Kadhalika ulikuwa na tabia za kwenda kwa waganga wa kienyeji, na baada ya kumpa Kristo maisha yako bado zile nguvu za giza zinakujia jia, endelea kudumu katika maombi, na kujifunza Neno la Mungu, visikuogopeshe wewe tayari ni mwana wa Mungu haviwezi kukudhuru, ni vitisho tu vya shetani, kwa jinsi unavyoendelea kukaa katika kujifunza Neno la Mungu na kukusanyika na watakatifu wengine vile vitu vinaondoka vyenyewe kidogo kidogo mpaka kufikia kutoweka kabisa, hutakaa uone mambo hayo yote tena..
Unajikuta umeingia katika usengenyaji, na hali hupendi kufanya hivyo, unachopaswa kufanya ni kukaa mbali na mazingira yote yatakayokupelekea kumzungumzia mtu mwingine vibaya, vikao vya kwenye masaluni, marafiki wasio kujenga, vijiwe n.k. unakata, sasa ukiendelea kujizoesha hivyo ile hali ya kusengenya inaondoka yenyewe ndani yako, baada ya kipindi fulani hata ukija kukaa katikati ya hao watu, utajikuta huwezi kusengenya kwasababu hiyo tabia imeshakufa tayari ndani yako..
Na mambo mengi yote, unayoshindwa kufanya kwa nguvu zako, usianze kuwaza kushindana nayo, hutaweza kwa siku moja ,huo ni ukumbi wa shetani,utajikuta unatazama matendo kuhesabiwa haki mbele za Mungu, badala ya kusonga mbele katika Imani. wewe kimbilia chanzo cha hayo mambo kisha kaa nayo mbali, kwa muda Fulani utaona matokeo mazuri, hutajisikia kuhukumiwa, wala kujilaumu, mawazo yako yatakuwa safi, ndoto zako zitakuwa sio za uchafu kila wakati, n.k..
Kadhalika shetani anapokuletea mawazo ya kukuhukumu kwa madhaifu yako, unayakataa. Ukijua kuwa Mungu ndiye aliyekuchagua wewe, na sio wewe uliyemchagua Mungu. Na hatuhesabiwi haki kwa matendo bali kwa neema yake.
Pia ni jukumu la kila mtakatifu kujitakasa kila siku kama maandiko yanavyosema. (Ufunuo 22:10 )Na tutajitakasa tu pale tutakapozidi kukaa mbali na mambo yote yanayochochea uovu ndani yetu.
Lakini kumbuka mambo haya yote mtu hawezi kuyashinda kama hajazaliwa mara ya pili. Na kuzaliwa mara ya pili ni kwa njia ya kutubu, na kubatizwa katika ubatizo sahihi, na kupokea Roho mtakatifu. Hivyo kama haujafanya hivyo ni vema uchukue uamuzi sasa kwasababu majira haya sio ya kukawia tena..Bwana yu karibu kurudi.
Tafadhali “share/print” ujumbe huu na kwa wengine. Mungu atakubariki.
Ubarikiwe sana.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
VITA DHIDI YA MAADUI
MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA RUTHU:
“WOKOVU WETU U KARIBU NASI KULIKO TULIPOANZA KUAMINI”
NINI MAANA YA “NITAWAVUTA WOTE KWANGU” (YOHANA12:32)?
JE KUNA ANDIKO LINALOMRUHUSU MWANAMKE KUWA SISTER?
YOHANA MBATIZAJI ALIBATIZWA NA NANI?
Rudi Nyumbani
Print this post