HATARI YA KUHUBIRI INJILI TOFAUTI NA ILIYOANDIKWA KWENYE BIBLIA.

HATARI YA KUHUBIRI INJILI TOFAUTI NA ILIYOANDIKWA KWENYE BIBLIA.

Shalom! Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima!

Karibu tujifunze Biblia, kwa Neema Bwana aliyotupa.

Biblia inasema katika Wagalatia 1:7b

“…. lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo.

8 Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe.

9 Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe”.

Maneno hayo aliyazungumza Mtume Paulo kwa Uweza wa Roho, na Roho Mtakatifu mwenyewe akayatia Muhuri yafae kwaajili ya kutuonya na kututahadharisha sisi watu wa vizazi vyote. Ni maneno ambayo huwezi kuamini kama yapo kwenye Biblia Takatifu hususani katika agano jipya, lakini yapo!

Kuna hatari kubwa sana ya kuigeuza Injili ya Yesu Kristo kwa makusudi..ili tu mtu upendwe, au upate wafuasi wengi, au ujulikane…Kufundisha Injili nyingine tofauti na hiyo iliyohubiriwa na Mitume ndio “kuongeza Neno la Mungu” kunakozungumziwa katika biblia….ambapo Biblia imesema mtu wa namna hiyo ataongezewa mapigo katika siku ile.

Ufunuo 22: 18 “Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki”.

Biblia inaposema wazi kuwa waasherati na waabudu sanamu pamoja na walevi watakwenda kwenye ziwa la moto, na wewe unasema “si kweli acha kuhukumu”..unaposema biblia imeruhusu pombe!! hapo ni sawa na unahubiri Injili nyingine tofauti na ile Iliyohubiriwa na hivyo “Umelaaniwa”

1Wakorintho 6:9 “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,

10 wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi”

Biblia inaposema wazi katika Agano jipya kwamba Wanawake wavae mavazi ya kujisitiri, si kwa kusuka nywele!..

1Timotheo 2: 9 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;

10 bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu”.

Wewe unasema “Mungu haangalii mavazi anaangalia roho” sentensi ambayo haipo kwenye Biblia nzima…uliisikia kutoka kwa mtu fulani asiyefahamu maandiko nawe ukai-copy bila kuchunguza imetoka wapi!…..fahamu kuwa unahubiri Injili nyingine ambayo haipo kwenye Biblia…Na hakuna mtu yoyote anakuhukumu hapo..bali biblia yenyewe ndio inayokuhukumu kwamba UMELAANIWA!

Biblia inaposema katika Marko 16:16 “Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa”. Wewe unasema kuwa ubatizo haujalishi sana! Si lazima ubatizwe, Hapo unahubiri Injili ya Laana!

Pengine ulikuwa hujui kwamba hizo injili ni za laana! Na ulikuwa unazihubiri, Lakini leo umejua..Tubu mlipize shetani kwa uongo aliokudanganya kwa muda mrefu! Tubu nenda kachome vimini vyote ulivyokuwa unavaa,(na nguo zote zinazochora maungo yako) na kamwe usihubiri Injili hiyo uliyokuwa unaihubiri ya Laana kwamba Mungu haangalii mavazi…Ulikuwa unasuka nywele!, kafumue ziweke katika hali yake ya asilia Mungu alizokuumbia, ulikuwa unavaa mawigi, na kupaka lipstick pamoja na mapambopambo ya kidunia..jirudishe katika hali yako ya asili..Umesoma haya kwa macho yako! Hutasema siku ile hujaambiwa, wala hukusikia, au haujafafanuliwa vizuri!..

Ukikubali maonyo na kugeuka ni vizuri! Utakuwa umeisalimisha roho yako, lakini ukikataa pia ni vizuri, kwasababu Injili sio kitu cha kulazimishwa……isipokuwa hakikisha kama unajipamba jipambe kikweli kweli, Kama unavaa vimini tafuta vile vikali kabisa, kama unasuka, suka mitindo yote na ya kila namna…unapaka poda, uwanja, weka mwingi wa kutosha unavaa wigi tafuta za kila mtindo….usiwe nusu nusu, ili siku ile katika ziwa la moto usije ukajuta kwanini hukujipamba sana, utakapoona ulijipamba kidogo tu na bado umetupwa katika ziwa la moto!…usije ukajuta kwanini ulikuwa una nguo moja tu! Kimini ambacho ulikuwa unakivaa mara moja tu kwa mwezi katika tukio maalumu…na nguo nyingine ndefu za kujisitiri ulikuwa unazivaa kila siku na bado umetupwa kwenye ziwa la Moto!

Kama umechagua kwenda kuzimu usikubali kinguo kimoja tu kikupeleke kule! Tafuta madebe ya vimini na suruali zile zinazobana kabisa, pamoja na maboksi ya lipstick yatumie… kwasababu Bwana Yesu alisema mwenyewe katika Ufunuo.

Ufunuo 22:10 “ Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia.

11 Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa.

12 Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.

13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho”.

Bwana akubariki.

Maran atha.

Maran atha!

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

NGUVU YA UPOTEVU.

CHUKIZO LA UHARIBIFU.

LAANA YA YERIKO.

INJILI KULINGANA NA TEKNOLOJIA.

INJILI YA MILELE.

JE! KUBET NI DHAMBI?


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments