NINI TUNAJIFUNZA KWA MWANA MPOTEVU NA NDUGUYE?

NINI TUNAJIFUNZA KWA MWANA MPOTEVU NA NDUGUYE?

Wengi wetu, tunapoisoma habari ya mwana mpotevu, macho yetu yote yanamwelekea yule mwana wa mwisho..kwasababu sehemu kubwa ya mfano ule ulikuwa unamzungumzia yeye.

Lakini pia ipo siri nyingine imejifichwa kwa yule mwana mkubwa ambayo tukiijua basi, lile wazo la kufiria kumwacha Mungu ovyo ovyo tu litafutika katika vichwa vyetu..

Leo tutajifunza kwa ufupi ni nini tunapaswa tujifunze kwa watoto wote wawili..Sasa kabla hatujaanza nao, embu tuisome tena habari yenyewe jinsi ilivyo kisha tuendelee..

Luka 15:11  “Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili;

12  yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake.

13  Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati.

14  Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji.

15  Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.

16  Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu.

17  Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa.

18  Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako;

19  sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.

20  Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.

21  Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena.

22  Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni;

23  mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi;

24  kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia.

25  Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo.

26  Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini?

27  Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima.

28  Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi.

29  Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu;

30  lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona.

31  Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako.

32  Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana”.

Sasa ukisoma hapo kwa makini utagundua kuwa kila mmoja alikuwa tayari ameshaandaliwa urithi wake, na wote walikuwa wameshajua kuwa urithi wao utakuwa ni nini..Na ndio maana yule mdogo(ambaye ndiye mwana mpotevu) alikuwa na ujasiri wa kutosha wa kumwambia baba yake amgawie sehemu ya mali inayomuangukia…

Huyu Mwana mpotevu hakuwa mvumilivu..Mfano tu wa baadhi ya watoto wa Mungu leo hii, wakishaona urithi wao mbinguni unachelewa wanakuwa tayari, kuachana na habari za wokovu na kugeukia mambo ya kidunia, wanauuza  urithi wao kama vile Esau alivyouza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa ndugu yake..

Sasa huyu mwana mpotevu akagaiwa urithi wake kama alivyoomba akaenda zake, akawa hana sehemu yoyote ya urithi katika nyumba ya baba yake..Lakini hilo halikumfanya asiwe kabisa mtoto wa Baba.

Lakini yule mkubwa alikuwa mvumilivu, alistahimili yote baba yake aliyokuwa anamfanyia kwa kujibana bana, japokuwa baba yake alikuwa tajiri lakini hakuwahi hata sikumoja kumfanyia karamu yoyote…Na hivyo ndivyo Mungu anavyofanya kwa watoto wake wote anaowapenda  leo hii duniani…Wewe kama ni mwana wake ukiona maisha yako ni ya kawaida tu..usivunjike moyo hiyo haimaanishi kuwa urithi wako ni wa kawaida tu au wewe ni maskini au Mungu anakuchukia..bali fahamu kuwa sehemu yako ni kubwa mbinguni..

Sasa yule mwana mkubwa alipoona ndugu yake amezingatia kurudi kwa baba yao, baada ya ulimwengu kumshinda..Hilo halikumfanya ajisikie vibaya..Bali lililomfanya ajisikie vibaya ni kuona jinsi alivyopokelewa kwa shangwe nyingi na karamu kubwa aliyofanyiwa… Hata leo hii Mungu huwa anawafanyia karamu kubwa sana wale watoto wake ambao wanazingatia kurudi kwake.., Hivyo ikiwa umepotea leo hii mrudie Bwana kwasababu hajakuchukia bado anakupenda sana..

Sasa turudi kwa yule mwana mkubwa alipoona vile alipomwambia baba yake, maneno haya;

‘ mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu;   lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona’.

Sasa sikiliza kwa makini kitu Baba yake alichomjibu…

‘Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, NA VYOTE NILIVYO NAVYO NI VYAKO’.

Nataka uzingatie hilo Neno la mwisho. NA VYOTE NILIVYO NAVYO NI VYAKO… Hilo ndilo lililotuliza moyo wake..

Leo hii ukiwa mtiifu, usipokuwa na haraka ya kumkimbia Mungu, unakuwa mwaminifu hata kufa, unakuwa tayari kuonekana hupendi raha, hupendi maisha kama huyu mwana mkubwa alivyokuwa..anatumika tu kama mtumwa..lakini urithi wote ulikuwa ni wa kwake.

Na wewe ndivyo ilivyo baada ya maisha haya, ikiwa tangu siku ulipookoka hukuwahi kuwa  kiguu na njia, leo huku kesho kule..basi URITHI WOTE Mungu aliotuandalia katika huo ulimwengu unaokuja ni wa kwako..Usizimie tu moyo..Hiyo ndio thawabu yako.

Lakini kama wewe ni mfano wa mwana mpotevu, au bado upo katika dhambi na umenaswa katika mitego mibaya ya shetani, umeingia katika ushirikina na huku ulikuwa unajua kabisa ni makosa, umeua watu, umefanya uzinzi, umetoa mimba, umekula rushwa, umedhulumu watu, umetoka nje ya ndoa, umemkufu Mungu, umeiharibu kazi ya Mungu, ni msagaji, ni mfiraji, na muuzaji wa dawa za kulevya, ni mlevu, n.k. unajijua kabisa wewe ni mwenye dhambi..

Leo hii Mungu anakuita tena umrudie yeye..Anataka uanze upya tena naye. Anataka uwe na moyo wa kujiachilia kama wa mwana mpotevu.. Usiogope atakufikiriaje..Yeye hayupo hivyo..anakusamehe na kusahau unaanza upya tena kana kwamba hujawahi kutenda dhambi..Na urithi atakupa sawa sawa na yule mwana wake wa kwanza kwasababu ulifanya hivyo kwa kutokujua lakini kama utakuwa tayari kuanzia leo kumfuata kwa moyo wako wote..

Leo hii Amani ya Kristo itaingia ndani ya moyo wako kwa namna isiyokuwa ya kawaida, ikiwa upo tayari kuufungua moyo wako, na kudhamiria kutubu kweli kweli..

Na  umeamua saa hii maisha yako yaandikwe kwenye kitabu cha Uzima

Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU  MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, . NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Ubarikiwe sana

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

JE! NI KWELI UMEMFUATA YESU?

KUWA MAKINI NA MITANDAO, NI SHIMO REFU.

KUSUDI LA MIMI KUWEPO DUNIANI NI LIPI?

KISIMA CHA MAJI YA UZIMA NI KILE KILE CHA ZAMANI.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

NI NANI ALIYEWALOGA?

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Lucas mhula
Lucas mhula
1 year ago

Amina mtumishi asante sana kwa somo zuri